May 18, 2011

MAHMOUD JIBRIL: Kiongozi wa Baraza la mpito nchini Libya anayeandaa enzi mpya baada ya Gaddafi

 Mahmoud Jibril

Mahmoud Jibril akiwa na Rais wa Ufaransa, 
Nicolas Sarkozy


TRIPOLI
Libya

VITA vya Libya vimechukuwa sura ya vita vya kidiplomasia kwenye jamii ya kimataifa, huku Urusi na Umoja wa Afrika zikisimama upande mmoja na Umoja wa Mataifa na nchi za Magharibi zikisimama upande mwingine.
Ushindi wa waasi wa Libya mjini Misrata dhidi ya vikosi vya kiongozi wa nchi hiyo, Muammar Gaddafi, unaelezwa kuwa ni wa hatua moja mbele, moja nyuma, kutokana na vikosi vya Gaddafi kuendelea kuushambulia mji huo na kuongezeka kwa idadi ya waathirika.

Taarifa za Jumatano asubuhi ya wiki iliyopita zilithibitisha kuwa makombora kadhaa yamekuwa yakirushwa kutoka upande wa vikosi vya Gaddafi kuelekea bandari ya Misrata na kuilazimisha meli ya Shirika la Kimataifa la Wahamiaji ishindwe kutia nanga kuwaokoa wakimbizi.

Meli hiyo ilikusudiwa kuchukua wakimbizi 550 wa Kiafrika, kati ya 2,000 waliokwama katikati ya vita. Kwa mujibu wa madaktari, wakimbizi watatu wa Kiafrika wameuawa na 20 kujeruhiwa kutokana na mashambulizi hayo.

Katika mji wa Kabao, ripoti zilisema kuwa mapigano makali yalimalizika kwa ushindi wa waasi, ambapo wanajeshi 45 wa serikali waliuawa na wengine 17 kukamatwa mateka. Waasi pia walipoteza wapiganaji wawili na watatu kujeruhiwa.

Kimataifa, vita hivi vimeendelea kuigawa dunia mapande mawili. Umoja wa Afrika, kwa upande wake, umeyalaumu mataifa ya Magharibi kwa kuzihujumu kwa makusudi jitihada zake za kutafuta amani nchini Libya.

Kamishna wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja huo, Ramtane Lamamra, alisema mataifa hayo yanauchukulia mpango wa amani wa Umoja wake kama usio na maana, huku yakiendelea na mashambulizi yake dhidi ya Libya, akikusudia zaidi mashambulizi ya Nato dhidi ya makazi ya Gaddafi.

Kulikuwa na mazungumzo mjini Addis Ababa, kati ya pande mbili zinazozozana zilizoeleza maoni tafauti, ingawa pia zilielezea nia ya kuendelea na mazungumzo. Waziri wa Mambo ya Nje wa Libya, Abdelati Obeidi, alitaka jitihada za Umoja wa Afrika zipewe fursa, huku wawakilishi wa waasi wakiahidi kuendelea na mazungumzo, alimradi tu 'matakwa ya watu ya Libya' yanatimizwa. Kwa waasi, matakwa hayo ya watu wa Libya ni Gaddafi kuondoka madarakani.

Hata hivyo, Waziri Mkuu wa Urusi, Vladimir Putin, akiwa ziarani nchini Denmark, aliyaita mashambulizi ya ya Nato dhidi ya makazi ya Gaddafi kama kitendo kisichokubalika, kwani ni njama ya kumuua kiongozi wa nchi hiyo.

"Dunia ina mataifa mengi yenye hali kama ya Libya. Je, tutakwenda kote huko kupiga mabomu. Kimazungumzo, wanatekeleza azimio la kuzuia ndege kuruka, ambalo ni sawa. Lakini azimio hilo liko wapi ikiwa kila usiku nyumba anayoishi Gaddafi inapigwa kwa mabomu? Nani ameyaruhusu haya?" Aliuliza Putin.

Lugha kama hii pia imetumiwa na rais wa Venezuela, Hugo Chavez, ambaye ameyaita mashambulizi hayo kuwa ni "kuchanganyikiwa kwa mataifa ya Magharibi", aliyoyashutumu kumchukia Gaddafi ili yapate mafuta. Hata hivyo, iliripotiwa kuwa ujumbe wa serikali ya Libya ulikuwa Venezuela katika jitihada za kutafuta uungwaji mkono wa kimataifa.

Pamoja na lawama zote, mataifa wanachama wa Nato yanasema yataendelea na operesheni yao ya kuwalinda raia wa Libya, na kwamba yatafanya hivyo kwa kuviharibu vyanzo vyote vya mashambulizi ya Gaddafi.

Waziri wa Ulinzi wa Uingereza, Liam Fox, ameiita operesheni hiyo ya Nato kuwa ya mafanikio. Akizungumza kwenye Wizara ya Ulinzi ya Marekani, Pentagon, baada ya mazungumzo na waziri mwenzake wa ulinzi, Robert Gates, Fox alisema:
"Tumeshuhudia maendeleo yakipatikana katika siku chache zilizopita. Na ni wazi kwamba utawala wa Gaddafi umeshikwa pabaya. Na madhali serikali inawashambulia raia, nasi tutaendelea kuvichukulia vituo vyao vya kuendeshea mashambulizi hayo kuwa shabaha halali za makombora yetu."

Ndani ya Libya, milio ya mizinga na risasi inaendelea kuwa sehemu ya maisha ya kawaida. Nje ya Libya vita vya maneno vimekuwa mtindo wa sasa. Na tofauti na ilivyokuwa kwa Tunisia na Misri, ngoma ya Libya inaonekana kuwa na mpigaji zaidi ya mmoja na wachezaji wasio na idadi.

Kwa upande wao waasi wa Libya wametoa mwelekeo wa kisiasa kwa nchi hiyo iwapo Kanali Gaddafi ataondoka madarakani. Mwelekeo huo unaonesha kuanzishwa kwa serikali ya mpito wakati katiba mpya inaandikwa na uchaguzi kufanyika.

Kiongozi wa upinzani wa Baraza la Mpito la Taifa la Libya (NTC), Mahmoud Jibril alitoa pendekezo la Libya baada ya Kanali Gaddafi kuondoka katika mkutano wa wajumbe wa nchi zinazounga mkono waasi uliofanyika Rome Italia. Alifafanua kuwa serikali ya mpito itaanza kazi mara moja ili kutoa maelekezo ya utendaji wa siku kwa siku na kuweka ulinzi.

Mahmoud Jibril amekubaliana na mpango wa misaada uliopitishwa na nchi 22 zinazounga mkono waasi hao. Katika habari nyingine, Ufaransa iliwaamuru wanadiplomasia 14 wa Libya wanaomuunga mkono Kanali Gaddafi kuondoka nchini humo ndani ya siku mbili. Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa alisema maafisa hao wametajwa kuwa 'watu wasiotakiwa nchini humo.'

Pendekezo la Mahmoud Jibril limeungwa mkono na Mwenyekiti wa kamati ya Seneti ya Marekani ya masula ya kigeni, Seneta John Kerry aliposema kuwa wakati raia wa Libya wanalindwa na ushirika wa kijeshi unaoongozwa na Nato, mpango unafanyika wa kutayarisha enzi baada ya Moammar Gadhafi.

Seneta Kerry alizungumza na waandishi wa habari baada ya kukutana na kiongozi huyo wa upinzani wa Baraza la Mpito la Taifa la Libya, Mahmoud Jabril, aliyekuwa ziarani Marekani.

Historia ya Jibril

Mahmoud Jibril amezaliwa mwaka 1952, ni mwanasiasa wa Libya ambaye, tangu Machi 23, 2011, amekuwa Waziri Mkuu wa serikali ya mpito ya Jamhuri ya Libya, moja ya taasisi mbili zenye udhibiti wa Libya. Yeye pia ni Mtendaji mkuu wa Timu ya Baraza la Mpito la Taifa la Libya (NTC). Serikali yake inatambuliwa kama "mwakilishi pekee halali" wa Libya na Ufaransa, Ureno, Uingereza na Qatar, lakini, hadi sasa haijatambuliwa rasmi na idadi kubwa wanachama wa nchi za Umoja wa Mataifa.

Maisha yake ya awali

Jibril amefuzu shahada ya kwanza katika Uchumi na Sayansi ya Siasa kutoka Chuo Kikuu cha Cairo mwaka 1975, kisha akapata shahada ya uzamili katika sayansi ya siasa mwaka 1980 na udaktari katika strategic planning mwaka 1985, zote kutoka Chuo Kikuu cha Pittsburgh. Baada ya hapo alifundisha somo la strategic planning katika Chuo cha Pittsburgh kwa miaka kadhaa, na amechapisha vitabu 10 kuhusu strategic planning na maamuzi, ikiwa ni pamoja na Picha na Itikadi katika sera za Marekani kuelekea Libya, 1969-1982.

Jibril aliongoza timu ambayo iliandaa na kuunda Mwongozo wa Mafunzo ya Umoja wa Kiarabu. Pia ndiye alikuwa na jukumu la kuandaa na kuendesha mikutano miwili ya kwanza ya Mafunzo katika dunia ya Kiarabu katika miaka ya 1987 na 1988. Baadaye alichukua jukumu la usimamizi na utawala wa viongozi wengi wa programu za mafunzo kwa ajili ya usimamizi katika nchi za Kiarabu ikiwemo Misri, Saudi Arabia, Libya, UAE, Kuwait, Jordan, Bahrain, Morocco, Tunisia, Uturuki na Uingereza.

Tangu mwaka 2007 alikuwa katika serikali ya Gaddafi kama mkuu wa Bodi ya Maendeleo ya Uchumi wa Taifa, ambapo alihimiza sera za ubinafsishaji na soko huria.

Tarehe 23 Machi 2011, Baraza la Mpito la Taifa liliundwa rasmi kwa serikali ya mpito na yeye aliteuliwa rasmi kuwa Waziri Mkuu wa serikali ya mpito. Jibril anajulikana kwa kuongoza mkutano na mazungumzo na Rais wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy, mkutano ambao ulisababisha Ufaransa kulitambua rasmi Baraza la Mpito la Taifa kama mwakilishi pekee wa watu wa Libya.

Makala haya yameandaliwa na Bishop J. Hiluka kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari na mashirika ya habari ya kimataifa.


No comments:

Post a Comment