May 18, 2011

…Watuhumiwa kuandaa mwenyekiti wao UVCCM

 Kaimu Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, 
Benno Malisa

Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa UVCCM mkoa wa Dar es Salaam, Augustino Oscar Matefu
Sadifa Juma Khamis

BISHOP J. HILUKA
Dar es Salaam

KUTOKANA na kile kinachotafsiriwa kuwa ni juhudi za kuutaka urais wa nchi hii mwaka 2015 kwa gharama yoyote, watuhumiwa wa ufisadi, licha ya kutakiwa ‘kujivua gamba’ wanadaiwa kuanza mikakati ya kuhakikisha kuwa mtu wao waliyempandikiza anakuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa CCM Taifa (UVCCM).

Tuhuma hizi zimetolewa na Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa UVCCM mkoa wa Dar es Salaam, Augustino Oscar Matefu, wakati alipoongea kwenye ofisi za gazeti la KuliKoni wiki hii.

Matefu alidai anao ushahidi kuwa mtu aliyepandikizwa na mafisadi ili kujaza nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa Mwenyekiti UVCCM, Hamad Yusuf Masauni baada ya kujiuzulu wadhifa huo ni Mbunge wa Jimbo la Donge, Kaskazini Unguja, Sadifa Juma Khamis.

Hata hivyo, mbunge huyo alipoongea na KuliKoni kwa njia ya simu, kwanza alicheka sana kusikia tuhuma hizo kisha akasema hazina ukweli wowote na ndio kwanza anazisikia.

Kama utasoma gazeti la Uhuru, kadri nilivyojieleza, utagundua kwamba mimi nimeamua kugombea ili kuitoa jumuiya yetu katika makundi kama hayo. Ninataka tuwe na umoja wa vijana wa kujitegemea na si wa kutegemea wafadhili fulani,” alisema Sadifa.

Mbunge huyo alizidi kusema: “Kwanza mimi ni mbunge wa juzijuzi tu na umri wangu ni miaka 29, hiyo tu haikufanyi uone kwamba sijawa kwenye siasa kwa kipindi cha muda mrefu kiasi cha kuwa rafiki wa hao mnaowaita mafisadi kwa sababu wao nina hakika ni watu wazima sana.”

Sadifa alisema anaamini Matefu anataka kutumia jina lake kujitafutia umaarufu kwa sababu anachoongea si kweli. “Tafadhali mwambie huyo kijana asitumie jina langu kujitafutia umaarufu kwa kuninasibisha na kundi lolote. Mimi ni mtu huru, mwenye mawazo ya kujitegemea na kamwe sigombei nafasi kwa maslahi ya watu fulani bali kusaidia jamii yangu.”

Mbali na Sadifa, wengine waliochukua fomu ya kuwania uenyekiti wa UVCCM ni Hamidu Bilal Gharib ambaye ni mtoto wa kaka yake Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal, Thabiti Jecha Kombo, Bakar Bakar, Omar Mwadi Mwarabu, Asha Suleiman Shibu, Shinuna Kombo Juma, Mwanawewe Usi Yahya, Laila Burhan Ngozi na Innocent Melleck Shirima.

Kwa mujibu wa Matefu, vijana wa CCM mkoa wa Dar es Salaam wanasikitishwa sana na kitendo cha mafisadi kutumia pesa za wananchi ili kudhoofisha harakati za chama kujivua gamba na wanaipa serikali siku ishirini na moja kuwafikisha mahakamani watuhumiwa wote wa ufisadi ambao amedai wanafahamika, na kuuvunja uongozi wa UVCCM Taifa.

Jumuiya ya Vijana wa CCM hivi sasa haifanyi kile inachotakiwa kufanya kwa maslahi ya wananchi badala yake watuhumiwa wa ufisadi wanaitumia Jumuia yetu ili kukidhi mahitaji yao binafsi na siyo kwa maslahi ya chama, Jumuia yenyewe ama Watanzania kwa ujumla,” anasema Matefu.

Bado nasisitiza kuwa idadi kubwa ya viongozi wa jumuiya yetu ni mapandikizi ya mafisadi wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti, Beno Malisa na Mjumbe wa Baraza kuu la jumuiya hiyo, Hussein Bashe. Na huyu Bashe siku za karibuni aliongea na waandishi wa habari kuzijibu tuhuma nilizotoa kwa niaba ya watuhumiwa wa ufisadi.”

Hata hivyo Malisa na Bashe walishakanusha tuhuma hizo zinazotolewa na Matefu.

Matefu pia amewatupia lawama Waziri Mkuu aliyejiuzulu kwa kashfa ya Richmond, Edward Lowassa ambaye ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Udhamini la Jumuiya hiyo na mkongwe mmoja wa siasa (jina tunalo) kuwa wameumega umoja wao kwa lengo la kuweka mikakati ya kuhakikisha kampeni ya Rais Kikwete ya kujivua gamba inashindikana.

Matefu amewataka wakongwe hao wa siasa waondolewe kwenye nyadhifa hizo ili wasivuruge maamuzi sahihi ya chama.

Pia huyu Rostam Aziz ndiye kinara na amekuwa akitoa pesa nyingi kwa ajili ya kuwanunua watu mbalimbali wakiwemo wanasiasa wa upinzani kwa lengo la kuhakikisha watuhumiwa akiwemo yeye mwenyewe wanasafishwa. Inasikitisha kuona akitumia rasilimali za nchi ku-invest kwenye makampuni yake na kuwanyonya wananchi kwa maslahi ya kundi dogo,” alidai Matefu.

Alipoulizwa na gazeti hili kuhusu wanasiasa wa upinzani wanaotumiwa na mafisadi, Matefu alisema kwa kujiamini kuwa wana ushahidi kwamba Rostam Aziz amekuwa na mawasiliano na Mwenyekiti wa chama kimoja cha upinzani na kwamba amekuwa akitoa pesa nyingi sana kuhakikisha chama hicho wanawasafisha mafisadi na kushusha lawama kwa Chama Cha Mapinduzi na viongozi wapambanaji wa ufisadi nchini ili kupotosha ukweli.

Kuna kijana mmoja anaitwa Deo alikuwa msaidizi wa mwenyekiti huyo, huyu aliona nyaraka za kifedha zilizotumwa kutoka kwa Rostam Aziz kwenda kwa mwenyekiti huyo, baada ya kujulikana ilibidi akimbie kabla hajashughulikiwa ili asitoe siri. Ushahidi wa kuwa Rostam anawapa wapinzani hawa fedha tunao, wakitaka kwenda mahakamani waende tutauonesha,” alibainisha Matefu.

Inashangaza sana baada ya kuandikwa kwenye vyombo vya habari kuwa, watuhumiwa wa ufisadi watawatumia viongozi wa vyama vya upinzani kumtukana Kikwete na familia yake, haupiti muda wapinzani wanaanzisha madai ya Ridhiwani! Kwa nini haya yafanywe sasa wakati inatangazwa kuwa maadui wa Kikwete watakitumia chama cha upinzani?” Alihoji Matefu.

Hili la kukubali kutumiwa na mafisadi ili kuipaka matope familia ya Rais Kikwete na baadhi ya viongozi waadilifu wa CCM waliojipambanua kupiga vita ufisadi lazima Watanzania wahoji, kulikoni!,” alidai Matefu.

Mwanasiasa huyo kijana aliongeza: “Mwandishi hushangai wanapoacha ajenda zao na kuamua kujibizana na watu wa CCM, hasa suala la kujivua gamba? Kwani wakizungumzia namna ya kupunguza gharama za maisha zinazopanda, na namna ya kuwafaidisha Watanzania na zoezi la mjadala wa katiba mpya hawataeleweka? Kwa nini wasizungumze ni vipi katiba mpya itawasaidia Watanzania kupambana na rushwa, ufisadi na matatizo mengine badala ya kukimbilia kujibizana na watu kama Nape Nnauye, na sasa wameingia kwenye ugomvi na Samuel Sitta, Dk. (Harrison) Mwakyembe na wengine?” Alihoji.

Matefu alidai kuwa mzozo unaoendelea baina ya Chadema na baadhi ya viongozi wa CCM kuhusu nani alitaka kuanzisha chama gani hauwanufaishi Watanzania bali watuhumiwa wa ufisadi, maana sasa hawazungumzwi wao na ajenda ya ufisadi imehama kutoka kwao.

“Hata kama kina Sitta walitaka kujiunga CCJ au Chadema, kuwaumbua huko kunaleta faida au hasara kwa Chadema? Je, kama watu wengine walio ndani ya CCM nao wangependa kuondoka, wataonaje? Hivi Chadema hawawezi kuzungumza kuhusu mustakabali wa Tanzania bila kuizungumzia CCM kwa jazba?” alihoji.

Matefu pia alidai kuwa kama serikali itasita kuwachukulia hatua mafisadi ndani ya siku ishirini na moja, vijana wamepanga kuandamana ili kushinikiza, na tayari baadhi ya mikoa imeshathibitisha kushiriki maandamano hayo ikiwemo mikoa ya Arusha, Mwanza na Tabora.

No comments:

Post a Comment