Oct 7, 2011

DK. GUY SCOTT: Mzungu wa Zambia na msomi aliyeukwaa umakamu wa Rais

 Dk. Guy Scott

LUSAKA
Zambia

RAIS wa Zambia, Michael Sata, amefanya kile ambacho mtu yeyote mpenda maendeleo anapaswa kukiunga mkono, hasa pale alipoteua mawaziri sita katika baraza lake la mawaziri wenye sifa bila kujali itikadi zao, wanaotoka chama kilichokuwa kikitawala cha MMD ambacho ni chama pinzani kwa sasa. Kadhalika amempa cheo cha umakamu wa Rais kada wa chama chake cha Patriotic Front (PF), Dk. Guy Scott, mwenye asili ya Uingereza.

Hakika Rais Sata ametoa funzo kubwa kwa wanaodhani kuwa Ikulu ni ya wateule fulani tu na kwamba, haiwezekani hata siku moja watu wengine kuingia au kufanya kazi na watu wenye itikadi tofauti na wao, kuwa sasa inawezekana.

Mawaziri hao kutoka MMD ni pamoja na E. C. Lungu, aliyeteuliwa kuwa Naibu Waziri katika ofisi ya Makamu wa Rais, S.S Zulu aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Sheria, G. B. Mwamba, anayekuwa Waziri wa Ulinzi na A. B. Chikwanda, Waziri wa Fedha.

Wengine ni C. Kambwili, aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na K. Sakeni aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani. Baraza hilo lilitangazwa siku 63 toka baraza lililopita kuvunjwa na rais wa zamani, Rupia Banda, alipotangaza tarehe ya uchaguzi mkuu.

Historia ya Scott

Dk. Guy Scott amezaliwa 1 Juni 1944, katika eneo la Livingstone. Amepata elimu yake katika eneo la Rhodesia ya Kusini (sasa Zimbabwe) na Uingereza katika Chuo Kikuu cha Cambridge na Chuo Kikuu cha Sussex, ambako alipata shahada ya uchumi na PhD katika utambuzi sayansi.

Dk. Scott ni mwanasiasa wa Zambia ambaye ameoa na anaishi jijini Lusaka.

Mafanikio katika taaluma
Baada ya kufuzu katika Chuo Kikuu cha Cambridge mwaka 1965, alijiunga na serikali ya Jamhuri ya Zambia ambapo aliajiriwa katika Wizara ya Fedha kama afisa mipango. Pia alikuwa naibu mhariri wa Biashara na Uchumi wa Afrika Mashariki na Kati katika kipindi hiki.
Mwaka 1970, Scott aliacha kazi ya serikali na kuwa mjasiriamali ambapo alianzisha mashamba, mradi wa kilimo cha biashara, ambayo aliwekeza katika mazao ya thamani kubwa kama vile umwagiliaji wa ngano, stroberi, na aina mbalimbali ya mboga mboga za msimu.

Mwaka 1978, alishiriki katika kuanzisha kampuni ya Mpongwe Development pamoja na Shirika la Maendeleo ya Jumuiya ya Madola. Baada ya hapo aliendelea kushiriki katika kutoa elimu na utafiti katika Chuo Kikuu cha Oxford katika miaka ya 1980.

Kazi ya siasa

Mwaka 1990, Scott alijiunga na kazi ya siasa kwa kujiunga na chama cha Movement for Multi-Party Democracy (MMD), ambapo alichaguliwa kutumikia nafasi ya Mwenyekiti wa kamati ya kilimo katika mkataba wa kwanza. Ushiriki wake katika siasa za Zambia ulitokana na marehemu baba yake ambaye alikuwa mshirika wa uanzishwaji wa taifa la Zambia na mwanzilishi wa magazeti yaliyopinga serikali ya kikoloni ikiwa ni pamoja na African Mail, ambalo sasa linajulikana kama Zambia Daily Mail. Katika miaka ya 1950, baba yake alikuwa mbunge wa kujitegemea wa shirikisho kupitia jimbo la Lusaka.

Scott aliteuliwa kuwa mgombea wa MMD wa jimbo la Mpika katika Bunge wakati wa uchaguzi mkuu wa 1991. Alichaguliwa na baadaye kuteuliwa kuwa Waziri wa Kilimo, Chakula na Uvuvi. Alifanya mageuzi kadhaa ya sera na alikuwa na jukumu la kusimamia hali ya maendeleo ya chakula baada ya "ukame wa karne" kati ya Januari na Februari 1992. Hakukuwa na hifadhi ya mahindi nchini Zambia wala kusini mwa Afrika, hivyo alikuwa na mipango ya dharura ya kuagiza kutoka nje ya nchi na kuyaleta Zambia kupitia reli na barabara.

Mwaka 1996, alijitoa MMD na kuunda chama cha Lima pamoja na Ben Kapita, aliyekuwa rais wa ZNFU. Aliandaa mpango wa muungano kati ya Chama cha Lima na vyama vingine ikiwa ni pamoja na ZADECO cha Dean Mungomba na kuunda ZAP.

Hata hivyo, baadaye alijitoa ZAP na kuelekeza nguvu zake kwenye kampuni yake ya ushauri wa kilimo. Mwaka 2001, alijiunga na Patriotic Front na kurejea kwenye siasa. Alirejea Bungeni alipochaguliwa kuwa mbunge wa Lusaka Kati katika uchaguzi mkuu wa 2006. Guy Scott pia alipanda hadi nafasi ya Makamu wa Rais wa Patriotic Front.

Na baada ya uchaguzi wa rais wa Zambia uliofanyika tarehe 20 Septemba 2011, na matokeo ya mwisho yaliyotolewa tarehe 23 Septemba kuonesha mgombea wa Patriotic Front, Michael Sata, kushinda kwa asilimia 43 ya kura dhidi ya asilimia 36 alizopata mgombea wa MMD na rais aliyemaliza muda wake, Rupiah Banda, Scott Guy aliapishwa kuwa Makamu wa Rais mnamo 29 Septemba 2011.

Makala imeandaliwa na Bishop Hiluka kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari vya kimataifa.


No comments:

Post a Comment