Oct 12, 2011

Uchaguzi wa Igunga na haja ya Katiba mpya, Tume huru

 Mbunge mteule wa Igunga, Dk. Kafumu akipongezwa

 Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya uchaguzi,
Rajabu Kiravu

BISHOP J. HILUKA
Dar es Salaam

UCHAGUZI mdogo wa hivi karibuni katika jimbo la Igunga, ambapo mgombea ubunge wa Chama Cha Mapinduzi, CCM, Dk. Dalaly Peter Kafumu, ameibuka mshindi wa kinyang’anyiro hicho umeendelea kuonesha kuwa mazingira ya uchaguzi hapa nchini bado si shirikishi kwa vyama visivyoshika dola, na kwamba vyama vya upinzani vilivyoshiriki uchaguzi huo na chaguzi nyingine, vinaingia kwenye uchaguzi kwa hofu tu ya kumsusia nguruwe shamba na wala sio kushinda, ingawa kwa baadhi ya vyama kama Chadema au CUF vilionesha kuwa na nafasi nzuri ya kushinda.

Uchaguzi wa Igunga ambao kwa kiasi kikubwa ulitawaliwa na vitisho na fujo huku viongozi wengine wakipanda jukwaani na bastola, umeendelea kuonesha kuwepo mapungufu mbalimbali katika mfumo mzima wa namna tunavyoendesha chaguzi zetu, hasa tangu tulipoingia kwenye mfumo wa vyama vingi mwaka 1992.

Mfumo unaotumika sasa kuendesha uchaguzi umekuwa ukilalamikiwa sana na vyama vya upinzani hasa uwepo wa wasimamizi wote wa uchaguzi, tangu mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), mpaka wasimamizi wa majimbo na kata ni watumishi wa serikali ama wateule wa rais ambaye wakati huohuo yeye mwenyewe na chama chake wanashiriki katika uchaguzi huo. Ndiyo maana, kwa mfano, kwenye uchaguzi wa Igunga watendaji wa vijiji wametuhumiwa kugawa mahindi kuwashawishi wapiga kura wamchague mgombea wa chama tawala, na tuhuma za ununuzi wa shahada.

Hapa naomba ieleweke kuwa siandiki makala hii kwa kuwa labda ninashabikia chama fulani hasha, mimi si mmoja wa wale ambao hudhani kuwa ili demokrasia ionekane imefanya kazi basi ni lazima chama cha upinzani kishinde. Nimeamua kuandika haya kutokana na mazingira ya chaguzi zetu (ambayo hayafichiki) tangu tulipoanza mfumo huu wa vyama vingi ambapo imekuwa ikionekana dhahiri kuwa chama tawala kimekuwa kikibebwa.

Mazingira haya ndiyo yanayosababisha watu wengi kukata tamaa na ndiyo sababu ya walio wengi kutokwenda kupiga kura, hasa pale wanapohisi kuwa mtu watakayemchagua (ambaye hatokani na chama tawala) hatapita kwa kuwa matokeo yatachakachuliwa, ingawa ukiangalia kwa undani utagundua kuwepo pia sababu nyingine inayowakatisha tamaa, kama kampeni za uchaguzi kutawaliwa na vitisho vya kila aina kwa washiriki wa uchaguzi na viongozi wa siasa.
Mfano hadi uchaguzi wa tatu tangu kuanza mfumo wa vyama vingi mwaka 2005, wananchi walio wengi walionekana kuwa bado wana imani na mfumo, lakini mwaka jana ikawa tofauti kabisa ambapo walionesha jinsi walivyokatishwa tamaa na mfumo uliopo, hasa serikali ya awamu ya nne.

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana ambao ni wa nne tangu mfumo wa vyama vingi, idadi ya wapiga kura ilipungua sana katika kiwango cha kushangaza mno, kwani hesabu za waliojiandikisha unapolinganisha na waliojitokeza kupiga kura, inaonekana kuna tatizo kubwa katika mfumo wetu ambalo linahitaji ufumbuzi wa haraka. Ufumbuzi huo si mwingine bali Katiba mpya na Tume huru ya uchaguzi.

Serikali ya awamu ya nne iliingia baada ya uchaguzi wa mwaka 2005, wananchi waliojiandikisha kupiga kura wakati huo walikuwa 16,407,318 na waliopiga kura walikuwa 11,365,477 ambao ni takriban asilimia 70 ya watu waliojiandikisha.

Lakini mwaka jana, kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ni watu 20,137,303 waliojiandikisha lakini waliopiga kura ni 8,398,394 tu ambao ni sawa na asilimia 42.64 tu ya watu wote waliostahili kupiga kura!

Kwa hali hii ni kwamba imani ya watu kwa serikali iliyopo madarakani imepungua mno, na hili si jambo la kishabiki kwani hata ukiangalia katika chaguzi zilizotangulia kabla na baada ya mfumo wa vyama vingi utagundua kuwa wananchi wengi walikuwa na imani na serikali yao. Mwaka 1965 waliopiga kura walikuwa asilimia 77.1 ya walioandikishwa. Mwaka 1970 walikuwa asilimia 72.2, mwaka 1975 asilimia 81.7. Mwaka 1980 asilimia 75, mwaka 1985 asilimia 75 na 1990 walikuwa asilimia 74.4.

Baada ya kuingia mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 na uchaguzi wa kwanza katika mfumo wa vyama vingi mwaka 1995, waliopiga kura walikuwa asilimia 76.7 ya waliojiandikisha, mwaka 2000 waliongezeka na kuwa asilimia 84.4, ambapo mwaka 2005 walipungua kidogo na kuwa asilimia 72.4.

Tatizo lilizidi mwaka 2010 kutokana na mfumo tulionao ambapo ni asilimia 42.64 tu ya waliojiandikisha ndiyo waliopiga kura. Na hapa panaonekana kuwepo tatizo kubwa ambalo linapaswa kuangaliwa kwa umakini sana bila ushabiki.

Hali hii imedhihirika hata katika uchaguzi mdogo wa Igunga kwa idadi ndogo ya watu walijitokeza kupiga kura, ambapo ni watu 53,672 tu ambao ni sawa na asilimia 31.3 tu ya watu 171,019 waliojiandikisha ndiyo waliopiga kura.

Katika chaguzi zote zilizotangulia kabla ya 2010 hatujawahi kuwa chini ya asilimia 70 ya wapiga kura waliojiandikisha. Je, kwa nini sasa hali hii inajitokeza tena kwa kiwango cha chini mno? Sababu hasa ni nini?

Je, si kweli kwamba mfumo uliopo ndiyo chanzo cha idadi ya watu wanaopaswa kupiga kura kupungua? Je, kwa nini serikali ambayo mwaka 2005 ilionekana kukubalika mno kwa kupata kura zaidi ya milioni 9, miaka mitano tu katika uchaguzi uliofuata ikaambulia kura milioni 5 tu ambazo ni tofauti ya kura takriban milioni nne wakati idadi ya waliojiandikisha kupiga kura ikiwa imeongezeka? Kwa kweli hili siyo jambo la kujivunia kabisa.


No comments:

Post a Comment