Oct 26, 2011

KUKITHIRI KWA RUSHWA: Rais Zuma awafukuza mawaziri waandamizi

Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma

PRETORIA
Afrika Kusini

KATIKA pekuapekua yangu nikitaka kujua mambo mbalimbali kupitia machapisho, hivi karibuni nilibahatika kuona kazi fulani ya waandishi wawili, Paul Holden na Hennie van Vuuren, walioandika na kuchapisha kazi yao: “The Devil in the Detail...”, wakimaanisha “Tazama kwa makini (serikali ya Mzee wa Afrika Kusini) ili umuone Shetani” na “...How the Arms Deal Changed Everything”.

Nilijitahidi kuperuzi lakini kuna kitu kimoja nikiri kuwa sikuwa nimekielewa au sikukitilia maanani wakati nikisoma; sikuweza kujua machapisho yao yalichapwa lini na walikuwa wakimmaanisha rais yupi kati ya huyu aliyepo sasa madarakani nchini humo (Jacob Zuma) au yule aliyepita (Thabo Mbeki). Hata hivyo, itoshe tu kusema kuwa ujumbe uliopo ni kuhusu kukithiri kwa rushwa nchini humo.

Maoni ya waandishi hao katika kitabu chao yanamaanisha kwamba vyombo vya dola vya nchi ya Afrika Kusini kwa sasa vinamilikiwa na watu binafsi walio karibu sana na rais wa nchi hiyo, watu hao wakijumuisha wafanyabiashara kadhaa wakubwa, wanasiasa na maofisa fulani wa jeshi.

Watu wote wamepewa vyeo vya juu na wote, kama kigezo cha kupewa vyeo hivyo wakiwa na historia tu ya ukaribu naye (Rais) binafsi, bila kuwa na uwezo maalum au ujuzi katika kazi husika.

Wakati wananchi wa kawaida, kwa maoni ya waandishi hao, wamekuwa hawanufaiki kabisa kadiri siku zinavyosonga mbele; na yote hii ilitokana na ununuzi wa silaha (Barani Ulaya) ulioambatana na madai ya kuwepo rushwa kwa viongozi wa ngazi za juu nchini humo. Yaani “vyombo vya dola ya Afrika Kusini vinazidi kugeuzwa kama viungo vya maiti anayeliwa na huyo (ibilisi wa wachache wenye kuendesha nchi kwa matakwa yao na ubinafsi)”.

Rushwa inazidi Afrika Kusini

Mnamo Julai 16, 2011, Chama kikuu cha wafanyakazi cha Afrika Kusini, kilionya kuwa rushwa nchini humo imezidi, na imefikia kiwango kikubwa cha kuweza hata kuigeuza nchi hiyo kuwa nchi isiyokuwa na nidhamu.

Msemaji wa Jumuiya ya wafanyakazi, COSATU, Patrick Cravan, alisema kuwa madai ya ufisadi na matumizi mabaya ya fedha za umma yanazidi kuongezeka nchini humo na kufikia kiwango cha kutisha. Wakati huohuo mashirika mengine, ambayo yanamuunga mkono Rais Jacob Zuma, yalipokea vema uamuzi wa serikali yake, wa kuanzisha uchunguzi kuhusu tuhuma mbalimbali za ufisadi ndani ya jeshi la polisi.

Msemaji huyo wa COSATU alisema kuwa suala hilo lazima lipewe uzito mkubwa na wakuu wa nchi: “Ikiwa hatuchukui hatua kali dhidi ya vitendo hivi, basi tutafikia hali ambapo wahalifu katika nchi hii wataweza kuiba mali ya taifa watakavyo, bila woga wala kufikishwa mahakamani.”

Rais Zuma awafukuza mawaziri wawili

Taarifa za hivi karibuni zinasema kuwa kutokana na kukithiri kwa rushwa Rais Jacob Zuma amechukua hatua ya kuwafukuza kazi mawaziri wawili, Waziri wa Serikali za Mitaa, Sicelo Shiceka, anayeshutumiwa kutumia fedha ambazo hazijaidhinishwa kisheria, na Waziri wa Kazi za Umma, Gwen Mahlangu-Nkabinde.

Rais huyo pia amemsimaisha kazi mkuu wa Jeshi la Polisi nchini humo, Jenerali Bheki Cele, ambaye pamoja na Bi Mahlangu-Nkabinde, wamehusishwa na madai ya kuuza majengo kinyume cha sheria. Viongozi wote watatu waliosimamishwa kazi wamekana kuhusika na kufanya jambo lolote kinyume cha sheria za nchi.

Mchunguzi maalum wa Afrika Kusini, aliyeteuliwa kuchunguza malalamiko dhidi ya maafisa hao wa serikali, alitoa wito kwa Rais Zuma kuwachukulia hatua kali. Lakini, Thuli Madonsela, mchunguzi maalum anayejulikana Afrika Kusini kama mwendesha mashtaka mkuu aligundua kuwa Shiceka alitumia zaidi ya dola za Marekani 68,000 (sawa na shilingi milioni 115 za Kitanzania) za serikali ya nchi hiyo kwa safari za kifahari na malipo ya hoteli bila idhini.

Gharama hizo ni pamoja na safari za kumtembelea mpenzi wake aliyekuwa amefungwa katika gereza moja nchini Switzerland kwa makosa ya kufanya magendo ya dawa za kulevya. Katika ripoti iliyotolewa mwezi uliopita, Bi Madonsela alisema kuwa vitendo vya Shiceka vilikuwa "kinyume cha sheria na matumizi mabaya ya madaraka, kukosa uaminifu kwa fedha za umma."

Alimshutumu pia kwa kusafiri nchi ya jirani ya Lesotho wakati akiwa likizo kutokana na kuumwa kwa gharama za walipa kodi wa nchi hiyo huku akitumia jina la uongo. Kwa wakati huo, Shiceka alikana madai hayo akisema "hayana msingi" na kuahidi kusafisha jina lake mahakamani. Alielezea kuwa baadhi ya gharama zake za hoteli ni kutokana na nyumba aliyopewa kuishi kutokana na wadhifa wake kujaa mbu.

Katika uchunguzi tofauti, Bi. Madonsela alibainisha kwamba Bi Mahlangu-Nkabinde na Jenerali Cele, mshirika mkuu wa Zuma, waliidhinisha mpango wa majengo yenye thamani ya mamilioni ya dola za Marekani kifisadi.

Rais Zuma alisema kuwa Jenerali Cele atasimamishwa kazi huku akilipwa mshahara wake wote, na uchunguzi ukiendelea dhidi yake. Rais huyo alisema kuwa uchunguzi huo utaongozwa na Jaji wa Mahakama ya Katiba, Yvonne Mokgoro.

Hata hivyo, Rais Zuma mwenyewe amewahi kukabiliwa na madai ya rushwa wakati alipokuwa makamu wa rais wa nchi hiyo, chini ya serikali ya Thabo Mbeki, lakini baadaye mashitaka dhidi yake yakatupiliwa mbali na mahakama. Sifa kubwa ya Rais Zuma ni kuaminika kwake kuwa msikilizaji zaidi wa matatizo ya masikini kuliko ilivyokuwa kwa rais aliyemtangulia, Thabo Mbeki, ambaye alikosolewa sana kutokana na kuhusudu zaidi biashara, sera za kiuchumi za kihafidhina – na kutumia mfumo wa kutoa maamuzi kutoka serikali kuu.

Baada ya kesi ya Zuma kufutwa na Mahakama Kuu katika mji wa Kusini-Mashariki wa Pietermaritzburg, alisafiri hadi Midrand, karibu na Johannesburg, ambako alipokelewa na wajumbe wa mkutano wa mwaka wa COSATU.

Lakini Jake Moloi, mtafiti mwandamizi katika Taasisi ya Mafunzo ya Usalama (ISS), yenye makao yake mjini Pretoria, alitoa taarifa yake ya kukumbusha kuwa matatizo ya kisheria ya makamu huyo wa rais wa zamani hayakuwa jambo la zamani.

"Ni mafanikio ya muda. Kuifuta kesi kutoka kwenye orodha ya mahakama kumeimarisha tu kibwagizo cha nyimbo za mashabiki wake," aliiambia IPS.

"Kwa upande wa Zuma, inaweza pia kuonekana kama tafu kubwa sana. Lakini bado wingu limetanda juu yake. Jaji mmoja tayari ameshamwelezea kama mwenye 'uhusiano wa rushwa' na mshauri wake wa zamani wa masuala ya fedha. Mtizamo huu una nafasi ya kubakia kwa muda mrefu," alisema Moloi.

Hata hivyo, uwezo wao wa kufuta madai ulitegemea nyaraka za dola zilizopatikana wakati wa upekuzi wa makazi ya Zuma na ofisi zake na mwanasheria wake – uhalali ambao ulipingwa mahakamani.

Kutokana na matokeo ya changamoto hizi, Jaji Herbert Msimang alitoa maamuzi kwamba waendesha mashitaka hawakutekeleza matakwa ya kisheria kwa wao kuonesha kuwa ushahidi muhimu ungepatikana hadi tarehe ya kuahirishwa kwa kesi hiyo.

Kwa upande wa kukosoa dola, alibainisha kuwa "uamuzi wa haraka" ulichukuliwa kumfungulia mashitaka Zuma, na pia kwamba "Utekelezaji wa uamuzi huo ulikuwa ni mwanzo wa mwisho… Hivyo kesi ya dola kuchechemea kutoka kwa janga moja hadi jingine."

Lakini, wakati uamuzi huo ulimwondoa Zuma kutoka kwenye mtego, bado haukuonesha mwisho wa mashitaka kumwandama katika siku zijazo: Waendesha mashitaka walitaka kumwingiza kwenye kitabu kuhusiana na jaribio la kutaka kupata rushwa ya mwaka ya dola za Marekani 70,000 kutoka kwa mshauri wake wa zamani wa masuala ya fedha, Schabir Shaik, kutoka kwa Kampuni ya silaha ya Kifaransa ya Thales – ili ailinde wakati wa mpango wa ununuzi wa silaha mwaka 1999.
Makala haya yameandaliwa na Bishop J. Hiluka kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari vya kimataifa.

No comments:

Post a Comment