Oct 26, 2011

WINSTON TUBMAN: Alihitilafiana na George Weah, sasa wanapeperusha bendera

 Winston Tubman

MONROVIA
Liberia

BAADA ya matokeo ya uchaguzi wa urais nchini Liberia duru ya kwanza kujulikana, vyama vya upinzani vya nchi hiyo viliwataka wafuasi wao wasiyatambue na wajumuike kwenye mhadhara mkubwa wa kupinga uchaguzi huo wa rais, ambao vyama hivyo vinasema kuwa umegubikwa na udanganyifu.

Wapinzani wa serikali wanasema kuwa wana ushahidi kuwa matokeo ya mwanzo ya uchaguzi huo yalibadilishwa wakati wa kuhesabu kura, ili kumpendelea rais wa sasa, Bibi Ellen Johnson Sirleaf. Hata hivyo, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya nchi hiyo, James Fromayan, alikanusha tuhuma hizo.

Matokeo hayo yalionesha kuwa rais wa nchi hiyo anayetetea kiti chake kwa mara ya pili, Ellen Johnson Sirleaf, aliongoza kwa kura chache, lakini hazikuwa zimetosha kumfanya Sirleaf aepuke duru ya pili ya upigaji kura, ambapo mgombea aliyeshika nafasi ya pili, Winston Tubman, ni kati ya wagombea waliodai kuwa kumepita udanganyifu kwenye uchaguzi huo.

Habari nyingine zenye utata zinaonesha kuwa kiongozi wa upinzani na mgombea urais nchini Liberia, Winston Tubman, wiki iliyopita alisafirishwa hadi nchini Ghana kwa ajili ya matibabu baada ya afya yake kuwa mbaya na kuanguka. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Ijumaa ya Oktoba 21, 2011 ilisema kuwa afya ya kiongozi huyo sio nzuri.

Chanzo kimoja kutoka katika Hospitali ya Umoja wa Mataifa ya nchini Liberia ambapo Tubman alikimbizwa mara baada ya kuanguka kwa sababu iliyosemwa kuwa alikuwa akisumbuliwa na malaria, kilisema kwamba kiongozi huyo wa upinzani alipelekwa nchini Ghana hasa kutokana na hali yake ya afya kuwa mbaya zaidi.

Tubman, ambaye anatarajiwa kushiriki katika uchaguzi wa marudio wa urais nchini Liberia akichuana na rais aliyeko madarakani, Ellen Johnson Sirleaf, katika uchaguzi utakaofanyika tena Novemba 8, 2011 kulingana na vyanzo mbalimbali vya habari, inasemekana kuwa alipelekwa mjini Accra, Ghana, Oktoba 20, 2011 mchana kwa kuzingatia ushauri kutoka kwa madaktari wake.

Lakini vyanzo vingine vya habari vinasema kuwa mgombea huyo wa CDC ana tatizo la shinikizo la damu linalomfanya ahitaji matibabu ya dharura.

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa CDC, Acarous Musa Gray, alisema kwamba Tubman amekwenda nchini Ghana kwa ajili ya kufanya mashauriano na viongozi katika kanda hiyo ya Afrika Magharibi hasa kuhusiana na uchaguzi mkuu nchini Liberia.
“Tubman alikuwa akiumwa malaria tu kama mtu mwingine yeyote. Kwa sasa yupo katika nchi fulani katika kanda yetu ya Afrika Magharibi, akifanya mazungumzo juu ya hatma ya uchaguzi wa Liberia,” alisema Gray.

Wakati huohuo, habari kutoka gazeti moja la mjini Monrovia la New Dawn, ambalo lina tetesi kuwa kutokana na hali mbaya ya afya ya Tubman, chama chake cha CDC kinaangalia uwezekano wa kumsimamisha mgombea mwenza, George Weah Manneh, kuchukua nafasi yake katika uchaguzi huo unaosubiriwa kurudiwa wa rais.

Hata hivyo, waangalizi wa uchaguzi huo wanasema kuwa uwezekano huo wa George Weah kuchukua nafasi ya Tubman katika kinyang’anyiro hicho ni mdogo sana kwani kuna taarifa kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi tayari imeanza uchapishaji wa karatasi za kupigia kura.

Kabla ya kinyang’anyiro hicho, kulikuwa na tetesi za kutoelewana kati ya Tubman na George Weah kufuatia mzozo wa nani atakayebeba bendera ya CDC katika kinyang’anyiro cha urais, hata hivyo, Tubman alipitishwa na CDC kwa kura 111 kati ya 118 na kumuengua George Weah katika uwezekano wa kugombea nafasi hiyo.

Historia ya nchi ya Liberia

Nchi ya Liberia ni nchi iliyoko Afrika ya Magharibi ikiwa imepakana na nchi za Ivory Coast, Guinea, na Sierra Leone.

Liberia ni nchi iliyoundwa na makabila mbalimbali ya asili nchini humo na wahamiaji weusi toka Marekani. Wamarekani Weusi hawa walikuwa ni watumwa waliopata uhuru ambao kwa kushirikiana na chama cha American Colonization Society waliunda taifa hili na kutangaza uhuru wa nchi hiyo Julai 26, 1847.

Wamarekani Weusi hawa waliichukulia nchi hiyo kama nchi ya ahadi kutokana na asili yao kuwa ni Afrika ambako ndiko mababu zao walikotokea kabla ya kupelekwa utumwani Marekani. Hata hivyo, wahamiaji hawa waliendelea kujitambulisha kama Wamarekani na hawakujenga mahusiano ya karibu na wenyeji.

Alama za taifa hili (bendera, kaulimbiu, na nembo ya taifa) na hata muundo wa serikali vilikuwa vikionesha mahusiano ya karibu kati ya nchi hizi mbili; Liberia na Marekani. Liberia imekuwa katika vita ya wenyewe kwa wenyewe kati ya mwaka 1989-1996 na 1999-2003.

Historia ya Tubman

Winston A. Tubman amezaliwa mwaka 1941 nchini Liberia, ni mwanadiplomasia na mwanasiasa wa Liberia akiwa mmojawapo wa wahamiaji weusi toka Marekani, walioletwa nchini Liberia (Americo-Liberia descent). Tubman ni waziri wa zamani wa sheria wa Liberia na mwanadiplomasia wa taifa hilo ambaye kwa sasa ndiye kiongozi wa chama hicho kikuu cha upinzani cha Congress for Democratic Change (CDC).

Tubman alizaliwa katika eneo la kata ya Maryland katika mji wa Pleebo, ni mpwa wa William VS Tubman, aliyekuwa rais wa Liberia na aliyeitumikia nchi hiyo kwa muda mrefu zaidi kuliko marais wote wa nchi hiyo. Tubman ana shahada kutoka Shule ya Uchumi ya jijini London, Chuo Kikuu cha Cambridge kilichoko Uingereza na Chuo Kikuu cha Harvard cha nchini Marekani.

Tubman alianzisha kampuni yake ya sheria mwaka 1968 na aliwahi kuwa mshauri wa kisheria wa Wizara ya Mipango na Uchumi wakati wa serikali ya mjomba wake, William VS Tubman. Pia Tubman anasemekana kuwa na uzoefu mkubwa sana wa kazi katika Umoja wa Mataifa. Kazi yake ya kwanza kabisa ilikuwa ni katika Ofisi ya Sheria mwaka 1973.

Aliwahi kufanya kazi chini ya Rais Samuel Doe, akiwa Waziri wa Sheria kati ya mwaka 1982 hadi 1983. Tubman alisafiri kwenda Marekani mwaka 1990 kwa niaba ya Samuel Doe kwenda kujaribu kuishawishi serikali ya Marekani ikubali kuingilia kati katika vita vya kwanza vya Liberia vya wenyewe kwa wenyewe lakini hakufanikiwa. Na baadaye katika miaka ya karibuni alifanya kazi kama mwakilishi wa Katibu Mkuu na mkuu wa kisiasa katika Ofisi ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Somalia, kuanzia mwaka 2002 hadi 2005.

Kabla ya mwaka huu kupitishwa kuwa mgombea urais kupitia CDC, Tubman alishiriki katika uchaguzi wa Oktoba 11, 2005, akiwa mgombea wa urais kupitia chama chake cha zamamni cha National Democratic Party of Liberia (NDPL). Katika uchaguzi huo alishindwa kufurukuta ambapo alijikuta akiangukia pua katika duru ya kwanza tu, kwa kushika nafasi ya nne kwa kuambulia asilimia 9.2 ya kura zote zilizopigwa.

Mnamo tarehe 1 Mei, 2011, ndipo Tubman alichaguliwa kuwa mgombea urais kupitia Congress for Democratic Change katika uchaguzi wa mwaka huu ambao unatarajiwa kurudiwa katika duru ya pili mwezi Novemba, uchaguzi unaolalamikiwa na wagombea urais wa vyama vya upinzani akiwemo Tubman.

Katika uchaguzi wa mwaka huu, Tubman anagombea urais huku mgombea mwenza wake kupitia CDC akiwa ni George Weah, ambaye alishika nafasi ya pili katika uchaguzi wa mwaka 2005.

Makala haya yameandaliwa na Bishop Hiluka kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari vya kimataifa.

No comments:

Post a Comment