Nov 2, 2011

ANDERS RASMUSSEN: Mkuu wa Nato aliyepata msukosuko kutokana na katuni ya Muhammad

 Anders Fogh Rasmussen

TRIPOLI
Libya

MKUU wa Umoja wa Kujihami wa nchi za Mharibi (Nato), Anders Fogh Rasmussen, amesema majeshi yake yamefanya kazi nzuri kusaidia Libya wakati wa mapinduzi anayoita ya kiraia dhidi ya hayati Kanali Muammar Gaddafi.

Rasmussen ameyasema hayo akiwa katika jiji la Tripoli kuhitimisha rasmi ujumbe wa Nato nchini Libya. Amesema Nato ingeweza kusaidia utawala mpya wa Libya kwa ulinzi na mageuzi kuelekea demokrasia iwapo wangeombwa.

Vikosi vya Nato vikifanya kazi chini ya amri ya Baraza la Umoja wa Mataifa kuwalinda raia vilianza harakati zake mwezi Machi wakati vikosi vya Gaddafi vilipoamua kupambana na waandamanaji. Ujumbe wa Nato umekamilisha rasmi kazi zake Libya dakika moja kabla ya kuingia saa sita usiku ya Jumatatu kwa saa za Libya.

Rasmussen alisema wamefanya mazungumzo na viongozi wa NTC akiwemo mwenyekiti Mustafa Abdul Jalil, kuhusu hatma ya Libya katika siku zijazo na mwelekeo wa mageuzi ya kidemokrasia.

"Mmechukua hatua kubadilisha historia na hatma yenu. Nasi tumewalinda. Pamoja tumefanikiwa. Libya hatimaye iko huru, kuanzia Benghazi hadi Brega, Misrata hadi kwenye milima ya Nafusa na Tripoli.

"Nchi nyingi za Kiarabu watatufahamu na kutuamini, wengi walifanya kazi pamoja kuwalinda ninyi. Ni matumaini yangu kuwa Libya yenye uhuru, demokrasia itajiunga nasi kama washirika siku moja lakini hilo ni uamuzi wenu. Hatma ya Libya sasa iko mikononi mwenu,” alisema.

Historia yake

Anders Fogh Rasmussen alizaliwa Januari 26, 1953, katika eneo la Ginnerup, Jutland, kwa mkulima Soren Rasmussen na Marie Rasmussen (nee Fogh). Ni mwanasiasa wa Denmark, na Katibu Mkuu wa 12 na wa sasa wa Nato. Rasmussen aliwahi kuwa Waziri Mkuu wa Denmark kuanzia Novemba 27, 2001 hadi 5 Aprili 2009.

Rasmussen alikuwa kiongozi wa chama cha Liberal (Venstre), na aliongoza muungano wa mrengo wa kulia na chama cha Conservative ambacho kilichukua madaraka mwaka 2001, na kushinda mara ya pili na ya tatu mnamo Februari 2005 na Novemba 2007. Serikali ya Rasmussen ilitegemea kuungwa mkono na Chama cha Watu wa Denmark (Danish People's Party), kufuatana na mapokeo ya serikali ya Wadanish wachache.

Katika kazi yake ya mwanzo, Rasmussen alikuwa mkosoaji wa hali ya ustawi, akiandika kitabu; Kutoka Serikali ya Jamii Hadi Serikali Ndogo mwaka 1993, ambapo alitetea mageuzi ya kina ya Denmark na mfumo wa ustawi wa jamii pamoja na uliberali. Hata hivyo, miaka ya 1990, maoni yake yalibadilika. Chini ya serikali ya Rasmussen, baadhi ya kodi zilipunguzwa, lakini muungano wa washirika wa Conservative ulirudia kudai punguzo la zaidi kwa ushuru na kodi ya kiwango kisichozidi asilimia 50.

Rasmussen alitekeleza mageuzi ya kiutawala kupunguza idadi ya manispaa (kommuner) na badala yake kuanzisha wilaya kumi na tatu (amter) na mikoa mitano. Rasmussen alitambua jambo hili kama “mageuzi makubwa katika miaka thelathini”. Hana uhusiano wowote na mtangulizi wake, Poul Nyrup Rasmussen, au mrithi wake, Lars Lokke Rasmussen; kufanana kwa majina yao ya mwisho ni jambo la kawaida nchini Denmark.

Amesomea lugha na masomo ya kijamii kutoka Shule ya Viborg Cathedral, 1969 – 1972, na Uchumi katika Chuo Kikuu cha Aarhus ambapo alifuzu mwaka 1978. Amekuwa akishiriki katika siasa karibu maisha yake yote na ameandika vitabu kadhaa kuhusu kodi na muundo wa serikali. Rasmussen na mkewe, Anne-Mette, aliyezaliwa 1958, wameoana mwaka 1978 na wana watoto watatu: Henrik (amezaliwa 1979), Maria (amezaliwa 1981) na Christina (amezaliwa 1984).

Alishikilia nafasi mbalimbali katika serikali na upinzani katika kazi yake, alishinda kwa mara ya kwanza kuingia katika bunge la Denmark kupitia Folketing mwaka 1978. Kwa ujumla, Rasmussen anapendelea katika ubinafsishaji na kupunguza ukubwa wa serikali. Hasa, hupenda kupunguza kodi na serikali kutoingilia katika ushirika na masuala ya mtu binafsi nk. Mwaka 1993 alipewa tuzo ya Adam Smith, na jamii ya Libertas, kutokana na yeye kuandika 'Kutoka Serikali ya Jamii Hadi Serikali Ndogo'.
Kuanzia 1987 hadi 1990 alikuwa Waziri wa Kodi na kuanzia 1990 akawa Waziri wa Uchumi na Kodi katika serikali ya Conservative iliyoongozwa na Poul Schlüter. Mwaka 1992 alijiuzulu nafasi yake ya uwaziri baada ya ripoti kutoka tume ya uchunguzi iliyoamua kwamba aliitolea Folketing (Bunge) taarifa zisizo sahihi na kamilifu kuhusu uamuzi wake wa kuahirisha malipo ya bili kadhaa za Regnecentralen na Kommunedata kutoka kwenye mahesabu ya mwaka. Rasmussen hakukubaliana na matokeo ya tume, lakini alikabiliwa na tishio la hoja ya kutokuwa na imani, aliamua kujiuzulu kwa hiari yake.

Uchaguzi wa 2001
Chama chake cha Kiliberali kilishinda katika uchaguzi wa Novemba 2001, kikiishinda serikali ya chama cha Social Democratic ya Poul Nyrup Rasmussen, na kumuwezesha kuunda Baraza lake la Mawaziri la kwanza. Uchaguzi huo ulileta mabadiliko makubwa katika siasa za Denmark. Ilikuwa ni mara ya kwanza tangu 1920 kwa Chama cha Social Democratic kupoteza nafasi yake kama chama kikuu katika Bunge.

Waziri Mkuu wa Denmark

Baada ya kuwa Waziri Mkuu, Rasmussen alijiweka mbali na maandiko yake ya awali na kutangaza kifo cha uliberali wa kisasa wakati wa uchaguzi wa kitaifa wa 2005. Alionekana kuvutiwa na mafanikio ya awali ya Tony Blair, Rasmussen sasa alionekana zaidi kupendelea nadharia ya Anthony Giddens na njia yake ya tatu. Kulikuwa na majadiliano katika jamii ya Libertas ya kutangua tuzo ya Rasmussen kama matokeo ya hili, ingawa haikutokea.

Serikali yake pia ilitunga hatua ngumu iliyoundwa kupunguza idadi ya wahamiaji kuingia Denmark, hasa wanaokimbilia kumo kutafuta makazi au kwa njia ya kupanga ndoa. Hata hivyo, serikali ya Rasmussen ilitegemea msaada wa Dansk Folkeparti, na ilikuwa vigumu kuchora mstari ulio sawa wa kugawa kati ya itikadi ya Rasmussen na siasa za serikali yake kutokana na maafikiano na Dansk Folkeparti.

Urais wa EU 2002

Rasmussen alishikilia nafasi ya urais wa kupokezana wa Umoja wa Ulaya kuanzia Julai hadi Desemba 2002, wakati ambao alijitolea kuunga mkono ajenda ya EU na kanuni elekezi ya mafundisho ya Ellemann-Jensen.

Wakati wa urais wa EU, alihusika katika tukio la kichunguzi na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Italia, Silvio Berlusconi. Katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari Oktoba 4, 2002, Silvio Berlusconi alisema: “Rasmussen ni waziri mkuu handsome kuliko wote barani Ulaya. Nadhani nitamtambulisha kwa mke wangu kwa sababu yeye ni mzuri zaidi kuliko Cacciari”. Massimo Cacciari ni mwanafalsafa wa Italia na mwanasiasa mpinzani wa Berlusconi, na baadhi ya magazeti ya udaku yamewahi kuandika uvumi kuhusu madai ya uhusiano kati yake na mke wa pili wa Berlusconi, Veronica Lario. Rasmussen alishangazwa na kauli hii na Berlusconi haraka akamwambia angemwelewesha baadaye.

Ndoa za mashoga

Vyama vya wanandoa mashoga vimekuwepo kisheria nchini Denmark tangu 1989. Januari 2004, Rasmussen alisema imani yake kwamba mashoga wanapaswa kuoana katika sherehe za kidini, ambazo kwa sasa haziruhusiwi katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri la Denmark, lakini alisema ni lazima jumuiya za kidini ziamue kama kufanya sherehe kwa ajili ya wapenzi mashoga.

Uchaguzi wa 2005
Januari 18, 2005 Rasmussen aliitisha uchaguzi wa Februari 8, 2005. Alichelewesha wito huo kwa wiki kadhaa kwa sababu ya tetemeko la Bahari ya Hindi 2004 lililoua Wadanish kadhaa. Serikali yake imekuwa ikikosolewa na Wadanish wachache kwa kile walichodhani yalikuwa majibu mepesi ya mgogoro huo, ingawa walio wengi waliipongeza serikali kwa kukabiliana na maafa.

Ingawa waliounga mkono chama chake walipungua kutoka uchaguzi wa 2001, na kusababisha kupoteza viti vinne, Venstre ilikuwa na uwezo wa kudumisha umoja wake baada ya uchaguzi kwa njia ya mafanikio na vyama vingine, na 18 Februari, Rasmussen aliunda Baraza lake la Mawaziri la pili. Rasmussen ndiye mwanasiasa aliyewahi kupata "kura binafsi" nyingi kuliko mwanasiasa yeyote katika Bunge la Denmark, (kura 61,792).

Katuni ya Muhammad
Mgogoro mkubwa katika kipindi cha siasa za Rasmussen kinahusiana na katuni iliyochapishwa katika Jyllands-Poste, gazeti kubwa la Denmark. Septemba 2005, gazeti lilichapisha ukurasa mzima katuni 12 zikionesha tafsiri mbalimbali ya Muhammad, ikiwa ni pamoja na moja ambayo Muhammad alionekana na bomu katika kilemba chake. Baadhi ya shule za dini ya Kiislamu hazikuruhusu picha ya tafsiri ya Muhammad. Baadhi ya Waislamu waliiona katuni hiyo ni ya kukera.

Rasmussen alikataa ombi la mabalozi 11 wa nchi za Mashariki ya Kati kujadili suala hilo. Rasmussen ameuelezea utata huo kama mgogoro mkubwa zaidi wa kimataifa kwa Denmark tangu Vita Kuu ya Pili. Alinukuliwa baadaye akisema, “alikuwa na mashaka kwamba katuni ilionekana kwa baadhi ya Waislamu kama jaribio la Denmark kuwatusi au kukosa heshima dhidi ya Uislamu au Muhammad.”

Baada ya kuthibitishwa kama Katibu Mkuu wa Nato, Rasmussen alitangaza kujiuzulu uwaziri Mkuu wa Denmark tarehe 5 Aprili 2009.

Makala haya yameandaliwa na Bishop Hiluka kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari vya kimataifa.

No comments:

Post a Comment