Mar 9, 2011

Serikali iwe makini sana kuhusu dawa ya Loliondo

 Mchungaji Ambilikile Mwasapile (kulia), akigawa dozi kwa wateja wake

 Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Haji Mponda


BISHOP J. HILUKA
Dar es Salaam

KWA zaidi ya wiki sasa vyombo vya habari vimetawaliwa na habari moja kubwa kuhusu uvumbuzi wa dawa ya kienyeji inayoitwa Mugariga iliyovumbuliwa na Mchungaji mstaafu, Ambilikile Mwasapile wa kijiji cha Samunge, kata ya Digodigo Wilaya ya Ngorongoro, inayodaiwa kutibu magonjwa sugu kama Pumu, Ukimwi, Kansa, Kisukari na Kifua Kikuu.

Taarifa kwenye vyombo vya habari zimekuwa zikiambatana na picha zinazoonesha maelfu kwa maelfu ya watu wakizidi kumiminika katika kijiji hicho kupata tiba ya magonjwa hayo sugu, huku taarifa zikionesha kwamba Serikali imeamua kusitisha safari hizo kwa wiki moja kutokana na mrundikano mkubwa wa watu na magari.

Taarifa zinasema hatua hiyo imechukuliwa kutokana na zogo la foleni ya magari na watu kutoka kijiji cha Samunge anakoishi mchungaji huyo hadi katika kona ya kwenda kijiji cha Sale, zaidi ya kilomita 20.

Bahati mbaya sana mimi nipo mbali na eneo hilo na sijaweza kufika huko kuthibitisha, na sijapata nafasi ya kukutana na mtu yeyote ambaye angenishuhudia kupona baada ya kupata tiba kutoka kwa mchungaji huyo. Si hivyo tu bali kati ya wanaodaiwa kupona simfahamu yeyote kiasi cha kuthibitisha kuwa kweli hiyo dawa inaponesha.

Baadhi ya niliowasiliana nao kama wana uthibitisho wa kupona kwa kutumia dawa hiyo, waliishia kusema: “Hata mimi nina ndugu yangu kaenda huko, nasubiri aje anieleze kama kapona ama la”.

Lakini tukio la Loliondo linatupa picha moja kubwa, kwamba magonjwa tajwa hapo juu yanawaumiza sana wananchi wetu na serikali inapaswa sasa kuyashughulikia kwa bidii kubwa zaidi.

Waswahili husema “lisemwalo lipo...” idadi kubwa ya watu wanaomiminika huko ni kielelezo cha kwamba huenda kuna ushuhuda fulani katika tiba za Mchungaji Mwasapile.

Sikumbuki ni wapi nilisoma habari kuhusu Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Elias Wawa Lali kusema kuwa ofisi yake imepeleka sampuli ya dawa hiyo ya ajabu inayodaiwa kutibu maradhi kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa uthibitisho zaidi.

Taarifa hiyo ilibainisha kuwa uongozi wa Wilaya pia ulipeleka kikosi cha askari ili kulinda usalama wa eneo la tiba ambalo lilikuwa limefurika watu wapatao 50,000 na magari yasiyopungua 200.

Hata kanisa ambalo Mchungaji Mwasapile aliwahi kulitumikia, Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), limethibitisha kutambua na kubariki dawa inayotolewa na Mchungaji wake mstaafu huku baadhi ya maaskofu wa kanisa hilo wakidai kwamba wamekunywa dawa hiyo na kuponywa.

Baadhi vyombo vya habari viliwakariri Maaskofu Thomas Laizer wa Dayosisi ya Mkoani Arusha na Dk. Martin Shao wa Dayosisi ya Kaskazini, wakisema huduma inayotolewa na Mchungaji Mwasapile ni sahihi na imeanza siku nyingi na kwamba wao ni miongoni mwa watu wa mwanzoni waliowahi kunywa dawa hiyo na kupona.

Kumekuwepo mitazamo tofauti juu ya tiba ya mchungaji huyo na uhakika wa tiba yenyewe. Nimebahatika 'kuchati' na baadhi ya wataalam wa tiba za kizungu ambao wameonekana kukataa au kupinga uwezo wa dawa ya mchungaji huyo kutibu.

Ikumbukwe kuwa mimi mwenyewe ni tabibu kitaaluma, lakini sitaki kubeza kuhusu tiba hiyo kwa kuwa naamini (kwani nimefundishwa hivyo chuoni) kuwa kuna baadhi ya magonjwa yasiyotibika hospitalini yana tiba zake za asili na mgonjwa hupona kabisa. Lakini nachelea kusema kitu kwenye hizi tiba za mchungaji.

Mmoja wa jamaa zangu ambaye ni daktari wa Hospitali ya Mwananyamala aliniambia akikariri moja ya vyombo vya habari kuwa dawa hiyo haina uhakika sana kwani wagojwa kumi wa ukimwi wamekunywa kikombe hicho lakini hawakupata nafuu na wanne kati ya hao wamekufa kwa hiyo watu wafikirie kwanza kabla ya kuacha dawa zao za hospitalini.

Nilipomweleza kuwa nakusudia kuandika makala kuhusu jambo hili alinisisitizia kuwakumbusha watu ambao wameshakunywa (kikombe) kwamba ni vyema waendelee kwenda kliniki kuangalia maendeleo ya afya zao badala ya kutegemea muujiza wa mtu aliyemuita “Babu wa Loliondo”.

Kwa wanaoishi na VVU (Virusi vinavyosababisha Ugonjwa wa Ukimwi) ni hatari kuacha kutumia dawa za Hospitali bila kuthibitisha kama kweli ugonjwa umeisha mwilini. Iwapo wenye VVU wataacha kutumia ARV na kinga za mwili (CD4) kushuka kuna hatari kubwa sana kwao,” alisema daktari huyo ambaye hakutaka niandike jina lake.

Ukitazama kwa makini hoja za wataalam wengi utakuta zinanafungwa na kauli moja ya kama hujafanya utafiti wa kina, huna haki ya kuzungumza (No research no right to speak). Serikali na wataalam wetu hata kama wamechukua 'sample' za dawa hiyo na kupeleka kwa Mkemia Mkuu lakini pia wanatakiwa kuitumia fursa iliyopo ya wagonjwa wenyewe kuamua kwa utashi wao kutumika kama “testa” bila hata ya kudai malipo.

Wizara ya Afya wanapaswa kuanzia kwa wale wanaodai kuponeshwa na tiba za Babu wa Loliondo, kisha kufuatilia (monitoring) ili kujua maendeleo yao ukilinganisha na hali waliyokuwa nayo kabla ya kupewa dawa, wakati ikisubiri utaratibu mwingine.

Hata hivyo, wakati makala hii inaandikwa kulikuwa na taarifa za Wizara ya Afya kutuma wataalam wake Loliondo kuangalia kama mazingira ya eneo hilo ni hatarishi kwa wagonjwa na kumshauri mchungaji asajili dawa yake kwenye Mamlaka husika ya Dawa na Vyakula (TFDA) ili iweze kuthibitishwa kama haina madhala yoyote, kwa maana ya sumu.

Binafsi ninashindwa nisimame upande upi kati ya ule wa kuipinga tiba hii au kuikubali kwa kuwa hapa kuna kitu kimoja kinachonitia kigugumizi kidogo, naambiwa kuwa mchungaji huyo kumbe alioteshwa kuhusu dawa hiyo.

Swali la kujiuliza, kama serikali imeamua kuipima dawa ya Mugariga ni vipi imani ya kiroho aliyonayo mtu iweze kufanyiwa utafiti wa kisayansi? Mchungaji huyo anasema wazi kuwa dawa anayotumia kutibu wagonjwa ameoteshwa na Mungu, iweje wataalam wetu wapate shaka juu ya imani? Je wakipima wakakuta ni maji tu yasiyo na chochote watamzuia kutibu kwa sababu yapo madai pia kwamba tiba hiyo huandamana na sala au watafanya nini?

Nilifundishwa kuwa kuna aina kuu mbili ya magonjwa; ya kimwili (physical illness) na ya kisaikolojia (psychological illness). Lakini katika aina zote za magonjwa hata kwa tiba ya hospitali bado unapaswa kuwa na imani na dawa ndipo upone.

Sasa sampuli iliyochukuliwa kupelekwa kwa mkemia mkuu, je nadharia yake (hypothesis) ni ipi ili katika majibu tulinganishe na uhalisia wa dawa?

Mimi si mtu wa imani ya kiroho ingawa naamini kuwa Mungu yupo, lakini nimewahi kushuhudia kwa baadhi ya watu waliokuwa wagonjwa kuponywa kwa imani, imani huponya, aaminiye kikombe kimoja cha maji ya 'mugariga' ya Babu wa Loliondo yanaweza kutenda kile kilichokusudiwa, yaani uponyaji.

Pia mimi si mtaalamu wa ndoto wala huwa siamini sana katika ndoto lakini ndoto bado ina maana sana. Nimewahi kusoma sehemu kuhusu habari za Kekule alivyooteshwa ndoto ya “structure ya Benzene”: Benzene ina Carbon sita ambazo electron zake zimekaa kiajabu, zinazunguka na kuifanya structure kuwa imara (stable).

Kekule aliamka usiku na kujaribu kuichora, na huu ni msingi wa Organic Chemistry (Zilizo chini ya kundi la Aromatic Compounds) ambalo limepelekea kutengeneza dawa nyingi ambazo tunazitumia. Ndiyo maana nikasema napata kigugumizi kuhusu ndoto ya mchungaji na hata kama siziamini ndoto lakini bado siwezi kupinga wazo la ndoto.

Pamoja na yote, naamini kuwa nafasi ya wataalam ipo palepale, tunaweza kupata mahali pazuri pa kuanzia utafiti badala ya kutaka kukurupuka katika jambo hili.

No comments:

Post a Comment