Mar 30, 2011

UVCCM vs Baba zao Hii ni 'Part 2' ya filamu ya Dowans?

 Kaimu Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM, Beno Malisa

 Waziri Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye

BISHOP J. HILUKA
Dar es Salaam

FILAMU (kwa Kiingereza huitwa Movie au Motion pictures). Ni mfululizo wa picha zinazoonesha mwendo wa watu au vitu na kuonekana mbele ya watazamaji kwenye skrini. Ni aina ya mawasiliano yanayotumiwa kutolea hadithi au kuwaelezea watu kuhusiana na kujifunza fikra au mitazamo mipya katika jamii.

Wafuatiliaji wa filamu sehemu mbalimbali duniani huangalia filamu ambazo zinaelezea hadithi fulani kama sehemu ya burudani, au njia mojawapo ya upenzi. Filamu nyingi zinatengenezwa zikitegemewa kuoneshwa katika kumbi za video au majumba ya sinema.

Mtu wa kwanza anayeiona filamu ni mwandishi wa muswaada andishi (scriptwriter) ambaye huiona filamu hiyo mawazoni mwake kisha huandika muswaada utakaotumika katika filamu (script), kabla waigizaji hawajapewa muswaada huo kwa ajili ya kuigiza. Kisha mtayarishaji hutafuta watu watakaoshiriki kuitengeneza filamu baada ya kuwa na pesa zitakazohitajika kuwalipa waigizaji na vyombo vya utenegezaji wa filamu.

Zipo njia nyingi ambazo mtayarishaji anaweza kuzitumia kupata pesa za kuandaa filamu yake zikiwemo zile za kupitia mikopo ya benki au kupitia wawekezaji. Watayarishaji katika tasnia ya filamu wamegawanyika katika aina kuu mbili; watayarishaji wanaofanya kazi katika studio kubwa za utengenezaji wa filamu (mainstream), na wengine wa kujitegemea (independent).

Kuna aina kadhaa za filamu ambazo hugawanyika katika makundi yafuatayo; Maigizo, Uzushi wa kisayansi, Vichekesho na Filamu za mapigano.

Pindi filamu inapokamilika, nakala nyingi za filamu hutengenezwa na kusambazwa kupitia diski (DVD na VCD) au mikanda maalum ya kuhifadhia filamu (VHS) na kusambazwa katika majumba ya sinema kwa ajili ya kuzinduliwa na kisha kuingizwa sokoni.

Tangu kumalizikika uchaguzi mkuu wa mwaka jana, 2010, nimekuwa nikishuhudia vituko kadha wa kadha ambavyo kwangu ni kama filamu ya vichekesho (comedy). Kwanza ilianzia kwenye filamu ya Dowans, ambayo hadi sasa simjui steringi wala muongozaji wake.

Hili la Dowans ni kisa kilichoandaliwa siku nyingi kidogo; tatizo lilianzia ndani ya CCM kufuatia makundi yaliyozaliwa mwaka 1995, na baadaye kufuatiwa na mgawanyiko mkubwa ulioanzisha kundi la wanaharakati maarufu kama “Mtandao” mwaka 2005.

Bahati mbaya mtandao haukudumu muda mrefu kutokana na wajumbe wake kuhitilafiana katika masuala kadhaa, na hivyo kuufanya usambaratike miezi michache tu baada ya uchaguzi wa 2005 na kutokea makundi matatu. Mgawanyiko huo ndiyo umepelekea makundi yake kufikia kiwango ambacho si rahisi sana kuyaunganisha au kuyamaliza, na wala hayawezi kuzikwa kama watu wengine wanavyojidanganya. Kuyaunganisha makundi haya ni kama kuwaunganisha wana wa Israel na Wapalestina. Na kulazimisha kuyazika makundi haya watajikuta wakiyazika pamoja na chama.

Katika filamu hii mpya “UVCCM vs Baba zao”, ambayo kwa mtazamo wangu ni muendelezo (part two) wa filamu ya kwanza (Dowans), imejengwa katika maudhui (concept) yaleyale japo kisa chake kinaonekana kuwa tofauti kidogo. Kabla ya yote ningependa kuwapongeza sana waongozaji wa filamu hizi kwa kuwa wanafanya kazi yao kwa umakini mkubwa sana. Kwani ni wao pekee wanaojua kwa nini filamu hizi zinapaswa kuandaliwa kipindi hiki cha sasa.

Katika filamu yoyote, mwandishi anayeandika mwongozo anapaswa kuzingatia sana kitu kimoja muhimu ambacho endapo kitakosekana sinema itakwenda shaghalabaghala; PLOT. Plot ni kisa halisi kinachoendelea kwenye hadithi, kisa hiki huwa na hatua muhimu tano ambazo kitaalam hujulikana kama; Introduction, Rising action, Climax, Falling action na Conclusion.

Katika filamu zinazoendelea sasa plot yake imebebwa na hoja za viongozi wa Umoja wa Vijana wa CCM tangu tamko lao zito kuhusu sakata la kampuni ya kufua umeme ya Dowans, wakipendekeza kuwa hoja kuhusu sakata hilo irudishwe bungeni ili Watanzania wajue nani kaifikisha serikali ilipo, na hatua zichukuliwe dhidi ya wahusika! Kwangu mimi hii ilikuwa ni hatua (stage) ya kwanza kabisa ya plot ya filamu hii, 'introduction'.

Kwa mtazamo wa juujuu unaweza kudhani tamko lililotolewa katika mkutano wa wajumbe wa Kamati ya Utekelezaji ya Baraza Kuu la Umoja huo na Jukwaa la Wahariri Tanzania, kwenye hoteli ya Peacock, mjini Dar es Salaam lilikuwa na nia njema ya kutaka kuokoa fedha za Watanzania zisichukuliwe na mafisadi, lakini ukitazama kwa undani utagundua kuwa lililenga kutaka kuwasaidia baadhi ya viongozi waliokumbwa na kashfa ili kuwasafishia njia ya ikulu 2015.

Hatua ya pili ya plot 'rising action', ilianzia kwenye kulaani kitendo cha mawaziri (si wote waliolengwa) kupingana hadharani na kutokuwa na uwajibikaji wa pamoja, na kuwataka kama wamechoka kuziongoza wizara waachie ngazi, wawapishe vijana wengine wenye nia njema ya kuongoza na kufuata maadili ya taifa.

Kauli ya Umoja huo kuapa kuwa utafanya kampeni za kuhakikisha viongozi fulani, uliodai kuwa wana malengo ya kupata Urais mwaka 2015, hawapati nafasi yoyote ya uongozi ni hatua ya tatu “climax” ya plot, na hapa ndo' filamu ilipoanza kunoga zaidi kwani iliwaibua baadhi ya wastaafu, wanaopaswa kuwa baba wa vijana hawa waliolazimika kujibu hoja hizo.

Kutishana huku hata kama wenyewe wanajaribu kukanusha kunaonekana wazi kuwa na agenda iliyojificha kuelekea uchaguzi wa 2015, kupitia uchaguzi ndani ya CCM unaotarajiwa kufanyika mwaka 2012. Kauli ya kwamba wanaokikosoa chama hadharani wasipewe nafasi za uongozi wa chama kwenye uchaguzi wa chama wa mwaka 2012 ni dalili za maandalizi ya mbio za kuelekea Ikulu 2015.

Eti wenyewe wanadai kuwa wanajivua gamba la zamani na kukivika chama gamba jipya! Nawashauri wajaribu kuwa na tahadhari kwani wasije wakadhani kwamba wanajivua gamba kama nyoka kumbe wanavua nguo na kubaki watupu!

Wadadisi wamekuwa wakijiuliza maswali yasiyopata majibu; inakuwaje kiongozi mwandamizi wa jumuiya ya chama tena nyeti ya vijana kuwachambua na hata kuwatusi baadhi ya viongozi wastaafu na hata waliopo serikalini kiasi hicho kama siyo 'picha' au hana baraka za wakubwa fulani?

Kwa upande mwingine, wananchi walio wengi sasa wanaamini kwamba chama kikongwe kimeanza kupauka na kama juhudi za makusudi hazitachukuliwa kurekebisha hali hii, basi kitakosa sifa za kuongoza nchi yetu kuelekea kwenye maendeleo. Wananchi wanaanza kukosa imani, wakidhani kuwa vijana wanatumiwa na kundi fulani ili waliaibishe kundi jingine kwa manufaa ya kundi wanalolitetea.

Bila kuweka wazi dira katika masuala haya nyeti kwa maslahi ya taifa, matokeo yataendelea kuwa ni malumbano endelevu, na kila kukicha mafisadi, ambao mimi nadhani ndiyo waandishi na waongozaji wa filamu hizi, watazidi kubuni mbinu mpya za kuendelea kulididimiza na hatimaye kuliteka na kulitawala taifa hili!

Kama ilivyo kwa filamu yoyote ile, lazima kuwe na muongozaji wa filamu na hadithi lazima iwe na mchezaji kinara 'steringi' anayeinogesha, hivi katika sakata hili kuna mtu anaweza kuniambia nani hasa kinara aliye nyuma ya sakata zima, ambalo linalitikisa taifa hili?

Kama haya yanafanyika kwa nia njema au kwa kutumiwa na watu fulani, bora kwanza wahusika wangejiuliza maswali kuhusu faida na hasara ya mchezo huu, isije ikawa ni mchezo wa paka na panya kwani siku zote majuto ni mjukuu!

Nawasihi wasomaji wangu wasiwe na haraka, hivi karibuni tutazishuhudia hatua mbili (falling action na conclusion) zilizobakia za plot yetu katika kukamilisha filamu hii.

Mungu ibariki Tanzania.

No comments:

Post a Comment