Apr 5, 2011

MOUSSA KOUSSA: Mshirika wa Gaddafi aliyesoma alama za nyakati

Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Libya, 
Moussa Koussa


TRIPOLI / LONDON

WIKI iliyopita vyombo vya habari vya kimataifa na hata vya ndani vilipambwa na tukio la Waziri wa Mambo ya Nje wa Libya, Moussa Koussa kukimbilia uhamishoni nchini Uingereza na kutangaza kwamba amejiuzulu wadhifa huo.

Mapambano bado yanaendelea nchini Libya, huku kujiuzulu kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Libya, Moussa Koussa kukielezwa kuwa siku za utawala wa Muammar Gaddafi zinahesabiwa. Moussa Koussa hivi sasa yupo Uingereza wakati huu vikosi vya Gaddafi vikiongoza mashambulizi ya ardhini dhidi ya Waasi.

Akizungumza na kituo cha televisheni cha France 24, Waziri wa zamani wa Uhamiaji wa Libya ambaye naye kwa hivi sasa anaishi uhamishoni, Ali Errishi alisema kuwa hatua hiyo inaashira sasa watu wengine watapata fursa ya kuiongoza nchi hiyo.

Waziri huyo alisisitiza kwamba mara nyingi amekuwa akieleza kwamba, yeye na kiongozi huyo waliwekwa kizuizini mjini Tripoli na inashangaza kuona amewezaje kutoroka nchini humo.

Aidha alisema kuondoka kwa Moussa Koussa kuna maana kwamba Gaddafi kwa hivi sasa hana mtu wa kuaminika zaidi ya yeye mwenyewe na watoto wake.

Waziri huyo wa zamani, Ali Errishi aliondoka mapema mwezi Februari nchini Libya baada ya kuanza kwa vuguvugu la kutaka kumuondoa madarakani Kanali Gaddafi. Ofisi ya Mambo ya Nje ya Uingereza ilithibitisha uwepo wa Moussa Koussa nchini humo kwa kusema kuwa aliingia kwa ridhaa yake akitokea nchini Tunisia.

Kiongozi huyo anatajwa kuwa ni nguzo muhimu katika serikali ya Gaddafi kwa kuwa ndiye alikuwa akishughulikia masuala muhimu ya kidemokrasia kabla ya kuanza kwa machafuko.

Moussa Koussa mwenye umri wa miaka 59, amekuwa Waziri wa Mambo ya nje tangu mwaka 2009, baada ya kuwa mkuu wa usalama wa taifa wa nchi hiyo tangu 1994.

Wakati hayo yakitokea, jumuiya ya kujihami ya NATO wiki iliyopita ilichukua mamlaka yote ya kutekeleza operesheni ya kuzuia ndege kuruka nchini Libya iliyoidhinishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Machi 19 mwaka huu. Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa NATO, Anders Fogh Rasmussen, jumuiya hiyo inayojumuisha nchi 28, itaratibu operesheni yote ya anga nchini humo.

Mapambano yanaendelea katika maeneo tofauti nchini Libya huku Gaddafi akitajwa kuyadhibiti karibu maeneo yote yaliyochukuliwa na waasi wiki mbili zilizopita yakiwemo, Ras Lanuf, Uqayla na Brega huku waasi wakiwa wametawanyika tawanyika katika maeneo tofauti.

Vyombo vya habari vilisema Gaddafi amekuwa akiwatawanya kwa kutumia vifaru pamoja na mizinga ya masafa marefu.

Mmoja kati ya wapiganaji waasi ambaye hakuweza kufahamika jina lake alisema “Tulikuwa Ras Lanuf, Vikosi vya Gaddafi vikatushambulia kwa mabomu, kwa hiyo tukalazimika kurejea nyuma ya Ras Lanuf”.

Hata hivyo waasi hao waliopoteza nguvu wakati wote wamekuwa wakihimiza vikosi vya anga vya Muungano vifanye mashambulizi dhidi ya vikosi vya Gaddafi ili waweze kurejea katika maeneo walikofurushwa na hatimaye kushika hatamu ya uongozi wa Libya.

Moussa Koussa ni nani hasa?

Moussa Muhammad Koussa (jina la Kiarabu linalotamkwa Musa Kusa ambaye anaaminika kuzaliwa mwaka 1949, ingawa hakuna taarifa rasmi za kuzaliwa mwaka huo, hadi anakimbilia Uingereza alikuwa mwanasiasa na mwanadiplomasia wa Libya, ambaye aliitumikia serikali ya Libya katika wadhifa wa Waziri wa Mambo ya Nje kuanzia Machi 2009 hadi 2011 wakati alipoamua kujiuzulu nafasi yake katika serikali ya Libya kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Koussa awali alikuwa akiliongoza shirika la usalama wa taifa nchini Libya kuanzia mwaka 1994 hadi 2009, na alikuwa akichukuliwa kama mmoja wa watu yenye nguvu zaidi nchini humo. Aliwasili nchini Uingereza tarehe 30 Machi 2011, na baadaye Ofisi ya Mambo ya Nje ya Uingereza na Jumuia ya Madola ikatoa taarifa rasmi kwamba Koussa si mwakilishi tena wa serikali ya Libya na ana nia ya kujiuzulu.

Elimu yake:

Alihudhuria masomo katika Chuo Kikuu cha Michigan eneo la Lansing Mashariki, Michigan, na kupata shahada ya kwanza katika elimu ya jamii mwaka 1978.

Mwanadiplomasia na mkuu wa Usalama wa Taifa:

Koussa alifanya kazi kama mtaalamu wa usalama katika balozi za Libya zilizopo barani Ulaya kabla ya kuteuliwa kuwa Balozi wa Libya akiiwakilisha nchi yake nchini Uingereza mwaka 1980. Alifukuzwa kutoka Uingereza mwaka 1980, baada ya kusema katika mahojiano na gazeti la The Times kwamba serikali yake ilikuwa na nia ya kuwaondoa wapinzani wawili wa kisiasa wa serikali ya Libya, ambao walikuwa wakiishi nchini Uingereza.

Baadaye alifanya kazi kama Naibu Waziri wa Mambo ya Nje kuanzia mwaka 1992 hadi 1994, na baadaye kama mkuu wa shirika la usalama wa taifa la Libya kuanzia mwaka 1994 hadi 2009. Alikuwa ni mtu muhimu sana katika kurejesha hali ya kawaida ya uhusiano kati ya Libya na mataifa mengi wanachama wa kujihami ya NATO, ikiwa ni pamoja na Marekani na Uingereza.

Koussa alikuwa chanzo muhimu katika kutolewa kwa mtuhumiwa wa milipuko iliyoteketeza ndege ya Pan Am, Abdelbaset al-Megrahi. Mwezi Oktoba 2008, alikutana na viongozi wa serikali zote mbili za Uingereza na Scotland, akitajwa kama mkalimani. Katika ziara yake ya mara ya pili mwezi Januari 2009, alitajwa kama Waziri wa Usalama.

Waziri wa Mambo ya kigeni:

Tarehe 4 Machi 2009, Koussa aliteuliwa kushika nafasi ya Waziri wa Mambo ya Nje, nafasi iliyoachwa na Abdel Rahman Shalgham, katika mabadiliko ya baraza la mawaziri la Libya yaliyotangazwa na bunge.

Mwezi Aprili, 2009, aliongoza mkutano wa 28 wa Baraza la Nchi za Kiarabu zilizopo Magharibi mwa Afrika (Arab Maghreb Union), nchi hizo ni pamoja na Algeria, Libya, Morocco, Mauritania na Tunisia katika mji mkuu wa Libya, Tripoli.

Katika mahojiano yaliyochapishwa na jarida la Asharq Al-Awsat tarehe 10 Novemba 2009, Koussa alikosoa vikali baadhi ya nyanja za uwekezaji wa China katika Bara la Afrika. Kwa mujibu wa Koussa, ilikuwa haikubaliki kwa China kutuletea “maelfu ya wafanyakazi wa Kichina barani Afrika” wakati Waafrika wenyewe wanahitaji ajira, na alizungumzia “uvamizi wa China kwa bara la Afrika” akisema kwamba “inaashiria kwamba madhara ambayo ukoloni aliyaacha katika bara la Afrika.”

Koussa pia alikosoa sana tabia ya China kutokuwa tayari kufanya kazi na Umoja wa Afrika na upendeleo wake wa kushughulika na taifa moja moja la Afrika, kitu ambacho alisema kilikuwa ni sawa na sera ya kuwagawa na kuwatalawa.

Aidha, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kisiasa pamoja na ushirikiano wa kiuchumi, akisema kwamba zamani kulikosekana uhusiano wa China na Afrika. Alisema kuwa China inajishughulisha tu katika mahusiano ya kibiashara, na kamwe haitaki kushiriki katika msaada wa kisiasa, ili kukidhi pande zote katika mgogoro.

Tarehe 29 Machi 2011, Koussa aliandika kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, akielezea kuteuliwa kwa waziri wa kigeni wa zamani wa Nicaragua wa serikali ya kijamaa ya Sandinista na rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Miguel d'Escoto Brockmann, kuwa balozi mpya wa Libya katika Umoja wa Mataifa. Barua iliyoelezea kuwa Brockmann alikuwa ameteuliwa, kama Ali Treki, pia rais wa zamani wa Mkutano Mkuu aliyekuwa chaguo lao la kwanza, kukataliwa visa ya kuingia nchini Marekani chini ya kifungu cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ya mwaka 1973.

Kuondoka na kujiuzulu:
Baada ya kuondoka kwa gari jijini Tripoli na kuwasili jijini Tunis, Tunisia, tarehe 28 Machi 2011, kupitia mpaka wa Ras Ejder, Msemaji wa serikali ya Tunisia alisema kwamba Koussa aliwasili nchini humo kwa “ziara binafsi.” Tarehe 30 Machi 2,011, alitoka Djerba kwa ndege binafsi iliyosajiliwa Uswisi na kuwasili Uwanja wa ndege wa Farnborough, Uingereza, kwa mujibu wa vyanzo vya kidiplomasia vya Libya.

Ofisi ya Mambo ya Nje na Jumuia ya Madola baadaye ikatoa taarifa rasmi kwa waandishi wa habari, na kusema kuwa Koussa hakutaka tena kuwakilisha serikali ya Libya na ana nia ya kujiuzulu, akiwa anahuzunishwa kutokana na Jeshi la Libya kufanya mashambulizi dhidi ya raia.

Makala haya yameandaliwa na Bishop J. Hiluka kwa msaada wa vyombo mbalimbali vya habari vya kimataifa.

No comments:

Post a Comment