Apr 13, 2011

KATIBA MPYA: Tusiwafanye Watanzania mbumbumbu

 Rais Jakaya Mrisho Kikwete, amepewa madaraka makubwa sana katika mchakato wa kutafuta katiba mpya

 Tambwe Hiza, kada wa CCM anayedai wananchi hawahitaji katiba mpya

BISHOP J. HILUKA
Dar es Salaam

MNAJADILI Katiba kwa kuwa nyie mmeshiba, kuna matatizo mengi ya msingi, vyakula vinapanda bei kila kukicha, wanafunzi wanakosa mikopo, wazazi wetu vijijini wana maisha magumu, mbona hayo hamjadili?...”
Maneno ninayoyakumbuka yaliyosemwa na kijana mmoja mwenye jazba (bahati mbaya silijui jina lake) wakati akichangia mjadala wa rasimu ya muswada wa kuanzisha mchakato wa kuandika katiba kwenye ukumbi wa Nkrumah, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, hivi karibuni.

Nimekuwa nikifuatilia kwa ukaribu sana mchakato unaoendelea wa kutafuta maoni ya wananchi kuhusu rasimu ya muswada wa kuanzisha mchakato wa kuandika katiba mpya na kugundua jambo moja kubwa, mijadala hii imejikita katika pande mbili kubwa.

Wanaodai katiba mpya wamekuwa na sababu zao ikiwemo ile ya kukosekana uhalali wa kisiasa kwa katiba iliyopo ambayo haikuwashirikisha wananchi, kuonekana kama ni ya chama kimoja, kumpa madaraka makubwa rais, kuhisi kwamba haihamasishi uwajibikaji, kujaa viraka vingi mno na kadhalika. Upande wa wanaopinga katiba mpya pia wana madai kuwa hakuna haja ya kuwa na Katiba mpya kwa kuwa wananchi walio wengi bado hawana elimu ya kutosha kuhusu uraia na hawahitaji katiba mpya kwa sasa.

Mara kwa mara nimekuwa nikisikia lugha ya dharau ya aina fulani kutoka kwa watu wasiolitakia mema taifa letu kuwa “Watanzania hawaijui katiba iliyopo” na kuwa hakuna umuhimu wa kujadili katiba mpya wakati iliyopo hawaijui ndiyo maana wanaishia kushabikia katiba mpya bila kuelewa.

Kama hiyo haitoshi, wiki hii nimesikia taarifa za baadhi ya viongozi wa asasi fulani kuishauri serikali isitishe mchakato wa katiba mpya kwa kuwa wananchi hawana elimu ya kutosha ya uraia, isitishwe hadi pale watakapopata elimu hiyo na kuielewa katiba ya zamani kwanza kabla ya kutaka mpya!

Nadhani tunakosea sana kutaka kuwasemea wananchi bila kujua nini mtazamo wao, kama wanaona haja ya kuwa na katiba mpya au la.

Nimewahi kuandika katika makala zangu zilizopita kuwa ipo haja ya kuiangalia upya katiba tuliyonayo ili kurekebisha mambo yaliyopitwa na wakati na naamini kabisa kuwa viongozi wetu wanajua umuhimu wa Katiba ya nchi na mahitaji ya wananchi kuhusu Katiba. Ile hoja ya kwamba wananchi hawaijui Katiba iliyopo haimaanishi kuwa hawahitaji Katiba nzuri itakayowahakikishia kupata haki zao za msingi.

Kama ilivyojitokeza kwa kijana mwenye jazba pale Nkrumah Hall, Chuo Kikuu wakati wa mdahalo, wananchi wengi pia wanaponung'unikia vitendo vya matumizi ya nguvu vinavyofanywa na polisi, kuongezeka kwa rushwa, ukosefu wa miundo ya usawa ndani ya jamii, ubadhirifu wa mali ya umma pamoja na kukosekana maadili mema yanayozingatia tunu za msingi za maisha ya kifamilia inaonesha udhaifu wa katiba iliyopo na kuhimiza uwepo wa katiba mpya.

Kwa kutaja tu mambo haya ambayo yule kijana mwenye jazba na hata wananchi wanataka yarekebishwe ili kuwapa maisha bora inaonesha dhahiri kuwa wananchi wanayagusa mahitaji halisi ya kuwepo Katiba mpya.

Wananchi wanapolalamika kukosa viongozi waadilifu, wakweli na wenye kuelewa maana ya Uongozi na umuhimu wa kuhamasisha na kutetea haki za jamii zao na si kujifikiria wao kwanza, wanaonesha kuifahamu Katiba vizuri sana kuliko hata sisi tunaojifanya tumeisoma kwa kuwa naamini tumeishia kukariri vifungu tu lakini hatuielewi kwa kuwa haitugusi moja kwa moja.

Mara nyingi watu wanashtushwa wakisikia wanakijiji fulani wamembana waziri huko vijijini, hii inaonesha dhahiri kuwa Watanzania wana uelewa mkubwa. Uelewa kwamba uongozi mbaya haufai. Ndio maana utaona hata leo hii ni vijijini ndiko kuna mwamko mzuri zaidi wa kupokea demokrasia na sera mbadala kuliko mijini.

Haihitaji shahada au diploma kujua uongozi mbovu, siku zote wananchi wamewaelewa viongozi wabovu na kuwatimua. Tatizo liko kwa hawa wanaojidai wana uelewa na kuwasemea wananchi ambao kwa kweli wamezoea kuishi katika mfumo wa kitawala wa ufisadi, wamevuna matunda yake na wanayafurahia.

Kabla hatujarukia kusema kuwa wananchi hawaijui katiba iliyopo hivyo hakuna haja ya kutaka katiba mpya inabidi sisi wenyewe kukubali hoja kwa mtazamo wake kisha kupambanua ukweli.

Inashangaza kuona baadhi ya wasomi kudai eti hakuna haja ya katiba mpya, hali hii inaonesha kuwa bado wana fikra za kutawaliwa kiasi kwamba leo hii hata ukiwauliza wakupe tofauti baina ya kutawaliwa na mkoloni sidhani kama wengi wanafahamu.

Ingawa sioni sababu ya kusitisha mchakato wa kutafuta katiba mpya lakini bado sikubaliani na aina ya mchakato tunaoutumia katika kupata katiba mpya kwa kuwa aina hii hujulika kama Power-centred constitution (katiba kuandaliwa na viongozi), badala ya people-centred consitution (katiba kuandaliwa na wananchi).

Tusisahau kuwa ni vigumu kwa Power-centred constitution kutusaidia kupata katiba nzuri kwa kuwa miongoni mwa waandaaji wa katiba yupo mwenye nguvu kuliko wengine wote ya kukataa jambo bila kuhojiwa; rais.
Vilevile, ni vigumu kupatikana katiba nzuri iwapo mmoja wapo ana uwezo wa kulazimisha jambo fulani likubaliwe kinyume cha matakwa ya wengine. Na ni vigumu mno kupata katiba nzuri kama mmoja kati ya waandaaji ana uwezo peke yake wa kuteua wajumbe wa kuandaa katiba hiyo.

Katiba nzuri haiandaliwi na wajumbe walioteuliwa na mamlaka moja, bali makundi yanayoshiriki yakishatambuliwa na kujulikana, huteua wawakilishi kwenye kongamano la kuandaa katiba.

No comments:

Post a Comment