Apr 27, 2011

Tunapojadili Katiba tujadili pia hili la asilimia moja tu kumiliki uchumi wote!

 Mwananchi mjasiriamali kama huyu ana safari ndefu katika kumiliki uchumi

BISHOP J. HILUKA
Dar es Salaam

WIKI iliyopita niliona kipindi kimoja kilichoonesha vijana wawili ambao sikumbuki ni viongozi wa asasi gani, lakini walikuwa wakielezea mikakati yao kuhusu Mkukuta awamu ya pili na jinsi walivyopania kutoa elimu kwa vijana ili kujikwamua na umasikini.

Mkukuta ni neno maarufu katika jamii ya Tanzania toka ulipozinduliwa mwaka 2005. Kirefu chake ni Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini Tanzania, ukiwa umeboreshwa kutoka katika Mkakati wa kwanza wa kupunguza umaskini uliozinduliwa Oktoba mwaka 2000 na ulitekelezwa kuanzia 2005 hadi ulipoisha mwezi Juni 2010 kabla ya kuzinduliwa kwa awamu ya pili ya mpango huo.
Mojawapo ya eneo ambalo Mkukuta ulipaswa kujikita ni ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini wa kipato, ikisemwa kuwa eneo hili lina malengo sita likiwemo la kupunguza umaskini wa kipato kwa wanawake na wanaume wa maeneo ya vijijini. Ilidhamiriwa kuwa ifikapo mwaka 2010 wanaoishi chini ya mstari wa umaskini wangepungua toka asilimia 38.6 hadi asilimia 14.

Lakini taarifa iliyotolewa mwaka jana ya Utendaji ya Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, iliyowasilishwa katika kikao cha Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi, kuwa ni asilimia moja tu ya watu, tena wenye asili ya mabara ya nje ndiyo wanaomiliki uchumi wa Tanzania!

Ilielezwa kuwa zaidi ya asilimia 90 ya uchumi wa Tanzania unaendelea kumilikiwa na watu hao wenye asili ya Asia na Ulaya, huku kukiwa na kilio kikubwa cha Watanzania wazawa, kutaka wajengewe mazingira mazuri ya uwezeshaji ili kumiliki uchumi wa nchi yao kupitia migodi mikubwa ya madini na maeneo nyeti ya kiuchumi.

Taarifa imeeleza kuwa tangu uhuru Watanzania wengi hawajawahi kushiriki kikamilifu katika kumiliki uchumi wa nchi yao. Uchumi wa nchi umeendelea kutawaliwa na wageni wakishirikiana na Watanzania wachache.
Huwa ninashangaa sana pale ninaposikia hoja ya uchumi wa nchi unakuwa kwa kigezo cha wingi wa magari, na wengine kusifu uchumi wetu kwa sababu ya kuongezeka kwa ‘masupamaketi’ makubwa tena yenye bidhaa nzuri (japo nyingi ni za nje pia), ilihali wananchi wengi hawana uwezo wa kuingia na kununua kilichopo.

Tujaribu kutofautisha maendeleo yaliyopo Oysterbay na Masaki na yale unayoweza kuyaona Manzese au Vingunguti, maendeleo yatakuwa ni barabara za kupitisha mchanga wa kujenga nyumba za mapumziko ya wikiendi. Tutataendelea kupita huku watoto wadogo wenye kamasi vifua wazi wakiendelea kupungia magari yetu makubwa kama nyumba. Hatutasikia kelele zao kwani vioo vitakuwa vimefungwa ili hewa iliyochujwa isichanganyike

Kwa taarifa ya Utendaji ya Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi inanifanya nishindwe kuelewa tofauti ya ukoloni na sasa katika umilikaji wa uchumi. Hivi ina maana 'fact' ya maendeleo ni kumilikiwa na Wazungu na wale wenye asili ya kutoka Asia?

Ile dhana kwamba kipimo cha mafanikio ya Mkukuta ni wananchi kila mahali kuanzisha vyama vya kukopa na kuweka (SACCOS). Vyama hivi vinawasaidia wananchi wenye kipato cha chini kupata mikopo inayowasaidia kuendeleza kilimo au biashara zao ndogo ndogo lakini sidhani kama vitawawezesha kumiliki uchumi.

Inashangaza kuona kuwa tuna ardhi nzuri, tuna madini na rasilimali kibao lakini tunaendelea kuwa masikini wa kutupwa, tukitegemea misaada ya wahisani ili kuendesha maisha yetu.

Kwa sasa huduma za jamii hususan elimu na afya zimedorora mno, mashule ya serikali yamebaki majengo tu, walimu hawatoshi, vitendea kazi kwa walimu havitoshi na zana za kujifunzia kwa wanafunzi havikidhi mahitaji halisi, madawati hayatoshi na hivyo watoto wengi wanakaa chini wakati wakisoma, na michango na ada sasa ni kero na vikwazo kwa watoto wengi kupata elimu.

Kwa sasa shule za serikali zimekuwa kama biashara, ada na michango inaanzia shule za msingi mpaka Chuo Kikuu. Pia ubaguzi katika elimu kwa sasa umekuwa rasmi, kwani kuna shule za matajiri na zile za watoto wa masikini, shule za matajiri zina huduma zote muhimu na ni za kisasa, wakati zile za walalahoi ziko hoi bin taaban.

Watoto wengi wa masikini sasa hawaendi shule na hivyo kusababisha kuongezeka kwa idadi ya watu wasiojua kusoma na kuandika, jambo linaloongeza umasikini miongoni mwa Watanzania, ambapo sasa inakadiriwa kuwa wananchi karibu asilimia 30 hawajui kusoma wala kuandika.

Mahospitali na zahanati za serikali sasa si mahali pa kuokoa maisha ya watu bali ni mahali pa kufia ndiyo maana watu wameona tegemeo pekee la kupata tiba ni Loliondo kwa Babu, kwani mahospitalini hakuna dawa na huduma zingine muhimu za matibabu, watumishi wa afya hawana ari ya kufanya kazi kwa kuwa hawalipwi vizuri, imefikia hatua wagonjwa wanakufa mikononi mwa manesi na madaktari kwa kukosa huduma huku uchumi wetu tukiwa tumeukabidhi mikononi mwa wageni.

Serikali imekuwa tegemezi, bajeti ya serikali inategemea misaada na mikopo kutoka kwa wageni kwa asilimia 35, na hili limesababisha manyanyaso na kuingiliwa kwa uhuru wetu kwa kupangiwa mambo ya kufanya na hawa wanaojiita wawekezaji.
Ingawa Katiba yetu inatamka kuwa nchi ya kijamaa lakini ukweli ni kwamba Tanzania siyo nchi ya Kijamaa na wala siyo nchi ya Kibepari bali iko tu katika hatua za kusahau nasaha za ujamaa na kuuelekea ubepari.

Kilichofanyika hapa ni kuacha kuvaa kaunda suti na kuanza kuvaa suti za Kimagharibi. Kutokuwa na msimamo kamili ndo’ kunaleta utata juu ya faida na hasara za mifumo hii katika kuleta maendeleo yetu.

Mimi naamini kuwa mfumo tunaoufuata hivi sasa ni mfumo wa Ubepari ingawa serikali ya CCM haitaki kukubali, ambao utaweza kuleta maendeleo kwa watu wachache tu wanaojua kucheza katika anga za ubepari, walio wengi hawajui na hawatajua nini kinaendelea na wanaweza kuuzwa kwa bei ya jumla.

Kinachofanyika sasa hivi katika mfumo huu wa kibepari ni kwa wachache kulimbikiza mali na si rahisi kujenga uwiano – hapa ni rahisi kujenga jamii mbili za wazalishaji na walaji na mara nyingi masikini ambao ni asilimia 99 ya Watanzania ndiyo wazalishaji.


Hatuwezi kufanikiwa katika Mkukuta kwa mfumo huu, vinginevyo tutakuwa tunadanganyana. Kwa mtazamo wangu ubepari si njia bora ya kuwafanya wananchi kujikwamua kwenye lindi la umasikini.


Mungu ibariki Tanzania

No comments:

Post a Comment