Mar 7, 2011

WILLIAM RUTO: Shutuma hizi ni mbinu ya kumchafua kisiasa.

*Asisitiza kuwa nyota yake kisiasa itaendelea kung’aa.

William Ruto

NAIROBI
Kenya

WAZIRI wa Elimu aliyesimamishwa, William Ruto na Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Fedha wa nchi hiyo, Uhuru Kenyatta, ni miongoni mwa watuhumiwa sita waliotajwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kuhusika katika kupanga vurugu zilizotokea baada ya uchaguzi mkuu nchini humo mwaka 2007.

Majina hayo yaliwekwa hadharani mjini Hague nchini Uholanzi na Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), Luis Moreno Ocampo.

Katika vurugu hizo, zaidi ya watu 1,133 waliuawa huku wengine zaidi ya 500,000 wakiachwa bila makazi. Ocampo pia alimtaja Waziri wa Viwanda wa Kenya, Henry Kosgey kuwa mtuhumiwa mwingine katika suala hilo.

Kenya inakuwa nchi ya nne ya Afrika kwa watu wake kufikishwa kwenye Mahakama ya Uhalifu ya Kimataifa (ICC), iliyopo The Hague, Uholanzi. Nchi zingine zikiwa ni Uganda, Sudan, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) na Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Wengine waliotajwa kuhusika na vurugu za Kenya ni Mwandishi wa habari ambaye pia ni Mkuu wa uendeshaji wa Radio Kass FM, Joshua Arap Sang, Katibu wa Baraza la Mawaziri, Francis Kirimi Muthaura na Mkuu wa zamani wa Jeshi la Polisi la nchi hiyo, Mohammed Hussein Ali.

Kufuatia taarifa hiyo, Rais Barrack Obama wa Marekani ambaye ana asili ya Kenya ametoa kauli kuwataka viongozi wote na watu wa Kenya, kutoa ushirikiano kwa ICC. Obama anaamini kuwa njia ya kusonga mbele ni ngumu lakini Wakenya wanaweza kusonga mbele na kuwaondoa wanaotaka kulirudisha nyuma taifa hilo.

Rais wa Kenya, Mwai Kibaki alitangaza kuwa serikali yake itaendesha uchunguzi kuhusu suala hilo, hatua ambayo wapinzani wake wameiona kuwa ni sawa na jaribio la kuzuia watuhumiwa kupelekwa The Hague. Ghasia hizo zilizuka nchini Kenya baada ya wafuasi wa Kibaki kutuhumiwa kujaribu kuvuruga uchaguzi huo uliomwingiza madarakani kwa mara ya pili.

Uhasama huo ulimalizika baada ya Kibaki na mpinzani wake kisiasa, Raila Odinga, kukubaliana kuunda Serikali ya mseto na Odinga kuwa Waziri Mkuu. Taarifa kutoka The Hague zinaeleza kuwa watuhumiwa hao sita kila mmoja atatumiwa hati ya kuitwa mahakamani. Hata hivyo, Ocampo alisema kuwa iwapo watuhumiwa hao watagoma au kujaribu kuingilia uchunguzi na kuwatisha mashahidi, ataomba kibali cha kuwakamata.

Kenya imekuwa ikiingia katika machafuko karibu kila baada ya chaguzi lakini Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2007, nusura uliingize taifa hilo kwenye vita ya wenyewe kwa wenyewe. Mapigano hayo yalimalizika baada ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan, kuzipatanisha pande mbili zilizokuwa zinapingana.

Kama ilivyodokeza kuwa Kenya ni nchi ya nne; lakini tofauti ni kwamba nchi kama Uganda watuhumiwa wake ni waasi wa kundi Lord’s Resistance Army (LRA), linaloongozwa na Joseph Kony na Serikali ya Uganda ndiyo iliyowafungulia mashitaka Kony na wenzake wanne.

Kwa upande wa nchi ya Sudan, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliwafungulia kesi ya uhalifu wa kivita kwenye jimbo la Darfur, Sudan, raia wanane wa Sudan akiwemo Rais Omar al-Bashir.

Pia serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) iliwafungulia mashitaka ya uhalifu wa kivita katika mahakama hiyo watuhumiwa wa kikundi cha waasi, Thomas Lubanga, Germain Katanga na Mathieu Ngudjolo ambao wamekamatwa. Wengine ni Bosco Ntaganda na Callixte Mbarushinama ambao hawajakamatwa.

Serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati ilimfungulia mashtaka Jean-Pierre Bemba wa DRC aliyekuwa akiongoza kundi la Movement for the Liberation of Congo (MLC), kwa tuhuma za kuchochea vita Jamhuri ya Afrika ya Kati kwa kuwatumia wapiganaji wake.

Vurugu za Kenya zilimfanya William Ruto, hivi karibuni kwenda The Hague na kuomba kukutana na mwendesha mashitaka mkuu wa mahakama hiyo ya Kimataifa ya Mauaji (ICC), Luis Moreno Ocampo ili “kuweka rekodi sawa” kama alivyosema mwenyewe.

Ruto amekanusha kuhusika na vurugu hizo, ambazo zilijikita kwa kiasi kikubwa katika jimbo analotoka la Bonde la Ufa. Ruto pia amewashutumu Rais Mwai Kibaki na Waziri Mkuu Raila Odinga na kusema kuwa anaheshimu uamuzi wa rais na waziri mkuu wa kumsimamisha kazi japo hakubaliani nao. Aliyasema hayo alipokuwa akimkabidhi ofisi waziri Hellen Sambili.

Aidha Ruto amesema hababaishwi kamwe na shutuma dhidi yake akizitaja kama zilizoshinikizwa na mahasimu wake wa kisiasa. Alisisitiza kuwa nyota yake katika ulingo wa kisiasa itaendelea kung’aa.

William Samoei Ruto alizaliwa tarehe 21 Desemba, 1966 katika kijiji ya Kamagut, wilaya ya Uasin Gishu. Ni mwanasiasa maarufu wa Kenya ambaye amekuwa Waziri wa Kilimo tangu Aprili mwaka wa 2008.

Pia alikuwa Katibu Mkuu wa Kanu, chama tawala cha zamani, na amekuwa mbunge wa Eldoret Kaskazini tangu mwaka 1997. Pia alikuwa Waziri wa Mambo ya ndani mnamo Agosti 2002 lakini alipoteza nafasi hiyo baada ya uchaguzi wa Desemba 2002, ambapo Kanu ilipoteza madaraka dhidi ya muungano wa Narc.

MAISHA YAKE
Alipata elimu ya msingi katika shule ya Sambut kabla ya kujiunga na Sekondari ya Wareng alikomaliza masomo yake mwaka 1984.
Alichaguliwa kuchukua elimu ya juu katika shule ya Wavulana ya Kapabet mwaka 1985-86.
Kisha akaingia Chuo kikuu cha Nairobi mwaka 1987 kwa ajili ya masomo ya shahada ya kwanza ya sayansi.

Alipokuwa Chuo Kikuu, Ruto ambaye ni muumini wa Kanisa la AIC, alichaguliwa kuwa kiongozi wa kwaya ya umoja wa Kikristo ya Chuo Kikuu, nafasi iliyomfanya kukutana na mtu aliyemhusudu sana, Rais mstaafu Daniel Arap Moi, kwa kuwa kwaya hiyo ilikuwa ikialikwa mara kwa mara kumtumbuiza Mkuu huyo wa nchi.
Marafiki wa karibu wa Ruto wanasema kuwa hali hiyo ilimfanya Ruto kutamani sana awe rais wa nchi siku moja. Wakati akiwa bado chuo, Rais Moi alimuomba Ruto kuongozana naye katika safari mbalimbali za nje ya nchi. Ziara ya kwanza ilikuwa Indonesia.
Baada ya kuondoka chuoni na 'kuonja' utamu wa harufu ya madaraka, Ruto hakutaka kurudi nyuma pamoja na kuajiriwa kama mwalimu wa muda wa shule ya sekondari Sirgoi na baadaye shule ya sekondari Kamagut, zote zikiwa katika jimbo la Bonde la Kaskazini.
Aliachana na kazi ya kufundisha na kuamua kusajili kampuni ya biashara jijini Nairobi, akiitumia kama daraja la kumfikisha alikokutaka katika ulimwengu wa siasa na hapohapo kuwa na pesa nyingi. Wakati huohuo, alichukua shahada ya uzamili chuo cha Chiromo.

WASIFU WA KISIASA
Ruto alikuwa Katibu wa Vijana wa Kanu '92 (YK92), kikundi kilichoundwa kupigia debe kampeni za Rais Daniel Arap Moi katika uchaguzi wa mwaka 1992.

Januari 2006, Ruto alitangaza hadharani kuwa atawania urais katika uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Desemba 2007. Taarifa yake ilishutumiwa na baadhi ya wanachama wa Kanu, pamoja na rais wa zamani Daniel Arap Moi. Ruto alitaka ateuliwe na ODM kama mgombea urais, lakini katika kura za maoni za Septemba 2007, alikuwa wa tatu kwa kupata kura 368, nyuma ya mshindi, Raila Odinga (kura 2,656) na Musalia Mudavadi (kura 391).

Ruto aliunga mkono uteuzi wa Odinga baada ya kura. Alijiuzulu wadhifa wake kama Katibu Mkuu wa Kanu Oktoba 6, 2007.

Uchaguzi wa rais wa Desemba 2007 uliambatana na vurugu baada ya ushindi wenye utata wa Mwai Kibaki na kupelekea ODM kupinga matokeo hayo, wakidai ushindi kwa Odinga. Baada ya vurugu hizo za kupinga matokeo, Kibaki na Odinga walikubali kuunda serikali ya pamoja. Ruto aliteuliwa kuwa Waziri wa Kilimo.

William Ruto kwa sasa ana kesi akihusishwa kupora pesa nyingi kwenye kampuni ya Kenya pipeline kupitia mikataba isiyoeleweka. Mahakama ya katiba iliahirisha kesi kutokana na malalamiko ya Ruto kwamba mashtaka hayo yalikuwa na lengo la kummaliza kisiasa.

KASHFA LA MAHINDI
Mapema mwaka 2009 baada ya mjadala wa bunge juu ya kashfa ya mahindi, Waziri wa Kilimo William Ruto alishutumiwa kwa kashfa ya kuuza mahindi nje ya nchi wakati taifa likikabiliwa na njaa. William Ruto alidai kuwa madai ya kuhusika katika ufisadi wa kashfa ya mahindi ilikuwa mbinu ya maadui wake kisiasa.

No comments:

Post a Comment