Jun 1, 2012

Arumeru msichague chama bali mwadilifu

Joshua Nassari (Chadema) na Sioi Sumari (CCM)

BISHOP HILUKA
Dar es Salaam

KESHOKUTWA Jumapili, tarehe mosi, Watanzania wenzetu wa Jimbo la Arumeru watakuwa na zoezi muhimu la kisiasa, kumchagua Mbunge wao. Hivyo huu ni wakati muhimu na muafaka kwa wananchi wa Arumeru kutafakari kwa makini tunu na maadili ya kiongozi bora kabla ya kuingia kwenye chumba cha upigaji kura.

Natoa wito kwa wana-Arumeru kuchagua kiongozi ‘muadilifu’ bila kujali anatoka chama gani au kina nani wanampigia debe, kwani mwisho wa siku wananchi watabaki na mbunge wao huku chama na wapiga debe (ambao wanatoka nje ya jimbo) watakuwa wameondoka zao na kuwaachia matatizo yao.

Kabla hatujasonga mbele kwanza tujiulize dhana ya maadili, maana yake ni nini? Kwa mujibu wa Padre Hurbert Akhweso, Mtalaam katika masuala ya Maadili, katika moja ya machapisho yake amewahi kuandika kuwa: maadili ni wema wa mwenendo au tendo la mtu; ni kule kuhukumiwa kwa mwenendo wa mtu kuwa ni mwema, au tendo la kibinadamu kuwa ni jema. Mwenendo au tendo la mtu ni jema vinapolingana na hadhi yake kibinadamu, yaani vinapoakisi utu wake. Hapa tunasema mtu huyu ni mwadilifu, au tendo hili ni adilifu.

Na mwenendo wa mtu au matendo yake vinapokuwa kinyume na hadhi yake ya kibinadamu, yaani kinyume cha utu wake, tunahukumu kuwa ni mabaya, na huo ni ukosefu wa uadilifu. Kwa kifupi, uadilifu ni wema wa mwenendo au tendo la kibinadamu, na ukosefu wa uadilifu ni ubaya wa mwenendo au tendo la kibinadamu. Maadili pia ni taaluma juu ya kanuni zinazohukumu mwenendo na matendo ya mtu kulingana na UTU wake.

Hivyo kwa kutumia kipawa cha akili binadamu hutafuta, kung’amua na kufahamu ukweli, naamini wananchi wa Arumeru wataweza kufahamu au kujua ni kiongozi yupi anayewafaa, na watawaweza kufahamu au kujua jambo lililo la kweli wakati huu wa kampeni zilizotawaliwa na porojo, kashfa kwa watu binafsi badala ya sera na ahadi zisizotekelezeka jambo ambalo haliwasaidii wana Arumeru kutatua matatizo yao.

Ieleweke kuwa mtu anapojiuliza kama jambo fulani ni la ‘kweli au la,’ au kama ‘lipo au halipo,’ anatumia kipawa cha akili, na akili inapokosa ukweli, huwa na mahangaiko makubwa na maswali mengi; lakini inapopata ukweli, hutulia kwa kuwa imeridhika.

Chakula kikuu cha akili ni ukweli, hivyo kila mmoja anao wajibu wa kuilisha akili yake kwa kutafuta ukweli daima, yaani, kujifunza na kuzitafakari hoja za wagombea na wapiga debe wao kabla ya keshokutwa kupiga kura.

Wananchi wa Arumeru ni vyema wakaongozwa na utashi katika kupiga kura. Utashi ni kipawa kinachotuwezesha kuona jambo fulani kuwa ni jema. Na jambo lililo jema ni lile ambalo akili imethibitisha kuwa ni la kweli.

Kinachonishangaza hadi sasa wakati huu wa kuelekea mwisho wa kampeni kabla ya uchaguzi jimboni Arumeru ni malumbano yasiyo na tija kwa wananchi wa jimbo hilo, tena yakiwahusisha viongozi wenye heshima kubwa katika taifa hili lakini wanaotoka nje ya jimbo hilo, kitendo ninachokitafsiri kama kufirisika kisiasa.

Huu ndiyo ulikuwa wakati muafaka kwa wananchi kutafakari kwa kina na kujua ni nani anayewafaa, mwenye maadili ya kweli, mwenye dhamira ya kweli kuwaondoa katika matatizo yao, bila kujali propaganda za wakubwa fulani ambao baada ya uchaguzi wataondoka zao na kuwaachia wananchi mbunge ambaye kama atakuwa ‘garasa’ watoto wa mjini wanasema kuwa itakuwa “imekula kwao”.

Jambo la msingi la kuangalia hapo ni kiongozi mwadilifu na mwenye maadili. Tukumbuke kuwa kule kuumbwa na utu (yaani, kuwa mtu), ndiko kunakomdai mtu kuwa mwadilifu, madai ambayo hawezi kuyakataa maadam ni mtu. Kuwa au kutenda kinyume na utu ni kujishusha hadhi na kuwa sawa na, au hata kuwa chini ya wanyama.

Hivyo keshokutwa wagombea (na vyama vyao) baada ya kunadi sera zao na kuahidi mambo mengi, itakuwa ni zamu ya Mpiga kura mwadilifu ambaye ameshasikiliza kwa makini na kupima hoja za wagombea wote kwa kadiri ya ufahamu wake na kubaini ukweli na kuridhisha utashi wake, kupiga kura.

Wananchi wa Arumeru wasifanye makosa kumchagua kiongozi asiye mwadilifu kwa kuwa anatoka chama fulani au wakubwa fulani waliwaambia eti huyo ndiye anayefaa. Wachague kwa kuzingatia sheria ya maumbile ya kimaadili ili baadaye wasije wakajutia kwa hii miaka mitatu iliyobakia kabla ya uchaguzi mkuu hapo 2015.

Kwa luga nyingine, ninawaasa wana-Arumeru keshokutwa msichague Chama bali mtu ambaye ni mwadilifu na mwenye uwezo wa kushirikiana nanyi katika kutatua ama kupunguza kero zenu ambazo kubwa tumeambiwa ni suala la ardhi inayokaliwa na ‘wawekezaji’ wachache, maji safi na salama na kupanda kwa gharama za maisha.

Alamsiki...

No comments:

Post a Comment