Jun 1, 2012

AUNG SAN SUU KYI: Mwanaharakati aliyelegeza masharti ili kuwatumikia wananchi

Aung San Suu Kyi

MYANMAR

KIONGOZI anayetetea sera za kidemokrasia nchini Myanmar (zamani ilijulikana kama Burma), Aung San Suu Kyi, amekubali kuapishwa pamoja na wabunge wa chama chake na hivyo kumaliza mzozo wa kisiasa uliokuwepo. Suu Kyi amesema uamuzi wake umetokana na matakwa ya raia ambao wanamtaka kuingia bungeni.

Chama chake cha NLD kilisusia kuapishwa kutokana na maandishi kwenye kiapo hicho. Kiapo kilichozua utata kinawataka wabunge kuapa kulinda katiba ambayo iliandikwa chini ya utawala wa kijeshi. Wabunge wapya wanatarajiwa kuanza vikao vyao wiki hii.

Hali hiyo imemfanya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon kuyataka mataifa ya Magharibi kulegeza zaidi vikwazo vyao dhidi ya Myanmar ikiwa njia bora ya kuunga mkono mabadiliko ya kidemokrasia katika taifa hilo la kusini mwa Asia.

Katibu Mkuu huyo amezungumza hayo alipolihutubia bunge la nchi hiyo wiki hii, sehemu ya ziara yake ya siku tatu nchini Myanmar. Hotuba hiyo aliitoa baada ya mazungumzo yake na Rais Thein Sein.

Pamoja na Umoja wa Mataifa kufanikiwa kutuma ujumbe wake wa usaidizi katika eneo hilo hivi karibuni lakini bado watu wengi wameendelea kuishi katika mkwamo mkubwa huku hali hiyo ikitabiriwa huenda ikawa mbaya zaidi.

Sambamba na yanayotokea sasa Mwanadiplomasia wa ngazi ya juu kabisa katika Umoja wa Ulaya Catherine Ashton nae yupo Myanmar kwa ajili ya mazungumzo na rais wa taifa hilo baada ya umoja huo kusimamisha vikwazo vyake dhidi ya taifa hilo .

Historia yake

Aung San Suu Kyi alizaliwa Juni 19, 1945, ni mwanasiasa, kiongozi wa upinzani na Katibu Mkuu wa National League for Democracy (NLD) nchini Myanmar. Katika uchaguzi mkuu wa 1990, NLD kilishinda kwa asilimia 59 ya kura za kitaifa na asilimia 81 (392 kati ya 485) za viti katika Bunge. Hata hivyo, tayari alikuwa kawekwa kizuizini nyumbani kabla ya uchaguzi.  Alibaki kizuizini nchini Myanmar kwa karibu miaka 15 kati ya 21 kuanzia 20 Julai 1989 hadi kutolewa kwake miaka ya karibuni mnamo Novemba 13, 2010, na kuwa mmoja wa wafungwa wa kisiasa maarufu zaidi.

Suu Kyi alipokea Tuzo ya Rafto na Tuzo ya Sakharov mwaka 1990 na Tuzo ya Amani ya Nobel mwaka 1991. Mwaka 1992 alituzwa Tuzo ya Jawaharlal Nehru na serikali ya India na Tuzo ya Kimataifa ya Simón Bolívar kutoka serikali ya Venezuela. Mwaka 2007, Serikali ya Canada ilimfanya kuwa raia wa heshima wa nchi hiyo, kwa wakati huo, alikuwa mmoja wa watu wanne tu waliopokea heshima hiyo. Mwaka 2011, alitunukiwa tuzo ya medali ya Wallenberg.

Aprili 1, 2012, chame chake cha upinzani, NLD, kilitangaza kuwa alichaguliwa kwenye Pyithu Hluttaw, bunge la Myanmar, kuwakilisha jimbo la Kawhmu; chama chake pia kilishinda viti 43 kati ya 45 katika bunge hilo. Matokeo ya uchaguzi yalithibitishwa na tume rasmi ya uchaguzi siku iliyofuata.

Suu Kyi ni mtoto wa tatu na wa kike pekee wa Aung San, anayeonekana kuwa baba wa kisasa wa Myanmar.

Aung San Suu Kyi alipata jina lake kutoka kwa ndugu watatu: "Aung San" kutoka kwa baba yake, "Suu" kutoka kwa bibi yake upande wa baba na "Kyi" kutoka kwa mama yake, Khin Kyi. Mara nyingi huitwa Daw Aung San Suu Kyi. Daw si sehemu ya jina lake, lakini ni jina la kiheshima, sawa na madame, kwa ajili ya wanawake watu wazima, wanaoheshimiwa, maana halisi ya "shangazi."

Suu Kyi alizaliwa eneo la Rangoon (sasa linaitwa Yangon). Baba yake, Aung San, alianzisha jeshi la kisasa la Myanmar na aliongoza mazungumzo ya uhuru wa Burma (sasa Myanmar) kutoka milki ya Uingereza mwaka 1947; aliuawa na wapinzani wake mwaka huo. Suu Kyi alikulia kwa mama yake, Khin Kyi, akiwa na kaka zake wawili, Aung San Lin na Aung San Oo, eneo la Rangoon. Aung San Lin alikufa akiwa na umri wa miaka nane, alipozama ziwani. Kaka yake mkubwa alihamia San Diego, California, na kuwa raia wa Marekani. Baada ya kifo cha Aung San Lin, familia ilihamia nyumba ya Ziwa Inya ambapo Suu Kyi alikutana na watu wa asili tofauti sana, wenye maoni ya kisiasa na dini. Alipata elimu katika Shule ya Kiingereza ya Methodist kwa muda mwingi wa utoto wake nchini Burma, ambako alibainisha kuwa na kipaji cha kujifunza lugha. Ni Mbuddha. .

Mama yake, Khin Kyi, alipata umaarufu kama mtu muhimu wa kisiasa katika serikali mpya ya Burma. Aliteuliwa kuwa balozi wa Burma nchini India na Nepal mwaka 1960, na Suu Kyi alimfuata huko, alisoma katika Shule ya Convent ya Yesu na Maria, New Delhi na kuhitimu shahada ya siasa katika Chuo cha Lady Shri Ram mjini New Delhi mwaka 1964. Suu Kyi aliendelea na elimu yake katika Chuo cha St Hugh, Oxford, na kupata shahada katika Falsafa, Siasa na Uchumi mwaka 1969. Baada ya kufuzu, aliishi mjini New York kwenye familia rafiki na kufanya kazi katika Umoja wa Mataifa kwa miaka mitatu, hasa juu ya masuala ya bajeti. Mwaka wa 1972, Aung San Suu Kyi alifunga ndoa na Dr Michael Aris, msomi wa utamaduni wa Tibet, aliyeishi nje ya nchi huko Bhutan. Mwaka uliofuata alijifungua mtoto wao wa kwanza, Alexander Aris, jijini London; mtoto wao wa pili, Kim, alizaliwa mwaka 1977. Baadaye Suu Kyi alipata shahada ya uzamivu (PhD) katika Shule ya Oriental and African Studies, Chuo Kikuu cha London mwaka 1985.

Mwaka 1988 Suu Kyi alirudi Burma, kwa mara ya kwanza na kwa mama yake aliyekuwa mgonjwa lakini baadaye akaongoza harakati za demokrasia. Ziara ya Aris kwenye Krismasi 1995 iligeuka kuwa mara ya mwisho kwake na Suu Kyi kuonana, Suu Kyi alibakia Burma na uongozi wa kidikteta wa Burma ulikataa kumpa Aris hati ya kuingia tena nchini humo. Aris aligundulika kuwa na saratani ya kibofu mwaka 1997 iliyoonekana baadaye kuwa mwisho. Licha ya kuomba msaada kutoka watu maarufu na mashirika, ikiwa ni pamoja na Marekani, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan na Papa Yohane Paulo II, serikali ya Burma haikumpatia Aris hati ya kuingia nchini humo, ikisema kuwa hawakuwa na vifaa vya kumhudumia, na badala yake ilimtaka Aung San Suu Kyi kuondoka nchini akamtembelee. Kwa wakati huo alikuwa huru kwa muda kutoka kizuizi cha nyumbani lakini alishindwa kuondoka kwa kuogopa angeweza kukataliwa kurudi akiondoka, hakuwa na imani na serikali hiyo ya kijeshi.

Aris alifariki siku yake ya kuzaliwa tarehe 27 Machi 1999, akiwa na miaka 53. Tangu mwaka 1989, mke wake alipowekwa kizuizini nyumbani kwake, alikuwa ameona mara tano tu, ya mwisho ikiwa ni siku ya Krismasi mwaka 1995. Suu Kyi pia alitenganishwa na watoto wake, ambao wanaishi nchini Uingereza, lakini kuanzia mwaka 2011, wamekuwa wakimtembelea nchini Burma.

Kama bahati Aung San Suu Kyi aliporejea Burma mwaka 1988, kiongozi wa muda mrefu wa kijeshi nchini humo na mkuu wa chama tawala, Jenerali Ne Win, alijiuzulu. Maandamano ya umma ya kidemokrasia yalifuatia tukio hilo tarehe 8 Agusti 1988 (8-8-88, siku iliyoonekana kuwa bora), ambayo yalizimwa katika kile kilichokuja kujulikana kama Mapinduzi ya 8888. Tarehe 26 Agosti 1988, alihutunia watu nusu milioni katika mkutano wa umma katika mji mkuu, akitoa wito wa serikali ya kidemokrasia. Hata hivyo, mwezi Septemba, serikali mpya ya kijeshi ilichukua madaraka.

Akipata msukumo kutoka kwa falsafa ya Mahatma Gandhi ya siasa zisizo za vurugu na hasa dhana ya Kibuddha, Aung San Suu Kyi aliingia kwenye siasa kusaka demokrasia, alisaidia kupatikana kwa chama cha NLD Septemba 27, 1988, lakini aliwekwa kizuizi cha nyumbani tarehe 20 Julai 1989. alipewa sharti la kuachiwa uhuru kama ataondoka nchini humo, lakini alikataa.

Makala haya yameandaliwa na Bishop Hiluka kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari vya kimataifa.

No comments:

Post a Comment