Sep 28, 2011

MAHMOUD ABBAS: Je atauweza mfupa uliomshinda Yasser Arafat?

 Mahmoud Abbas

Yasser Arafat

RAMALLAH
Palestina

RAIS wa Mamlaka ya Taifa ya Palestina, Mahmoud Abbas, alipokelewa kama shujaa aliporudi nyumbani kutoka Umoja wa Mataifa, ambako alikwenda kuomba Mamlaka ya Wapalestina iwe mwanachama kamili wa Umoja wa Mataifa.

Abbas aliuambia umati uliomshangilia mjini Ramallah, kwamba hawatoshiriki kwenye mazungumzo na Israel, ikiwa hawatotambuliwa kimataifa, na kama Israel haitaacha kujenga makazi katika Ukanda wa Magharibi.

Mkuu huyo wa mamlaka ya Palestina akiwa jijini New York, Marekani alisema kwamba hawezi kuwa kigeugeu, anataka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lizungumze lolote kuhusu ombi lake la kutaka kuwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa. Kiongozi huyo aliwasilisha ombi hilo siku ya Ijumaa Septemba 23, licha ya juhudi kutoka pande mbalimbali kumtaka asifanye hivyo.

Mahmoud Abbas amesema tangu achukuwe uamuzi wa kwenda kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutaka Palestina kuwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa, amekuwa katika hali ngumu, kwani alikuwa anapokea maombi kutoka pande tofauti kumtaka aachane na mpango huo.

Historia yake

Mahmoud Abbas, ambaye pia anajulikana kama Abu Mazen, alizaliwa Machi 26, 1935, amekuwa Mwenyekiti wa Shirika la Ukombozi wa Palestina ( PLO ) tangu 11 Novemba 2004 na akawa Rais wa Mamlaka ya Palestina ya Taifa tangu alipochaguliwa kuwa rais wake mnamo Januari 2005 kwa tiketi ya Fatah.

Alichaguliwa kuongoza hadi tarehe 9 Januari 2009, aliongoza hata baada ya muda wake kwisha kwa mwaka mmoja zaidi na kuendelea hata baada ya mhula wa pili kwisha. Matokeo yake, wapinzani wakuu wa Fatah, chama cha siasa cha Hamas kilitangaza kuwa kutomtambua Abbas kama rais halali. Abbas alichaguliwa kama Rais wa Serikali ya Palestina na Halmashauri Kuu ya PLO mnamo 23 Novemba 2008, nafasi aliyoishikilia kiholela tangu Mei 8, 2005. Abbas aliwahi kuwa Waziri Mkuu wa kwanza wa Mamlaka ya Palestina Machi hadi Oktoba 2003, alipojiuzulu akitoa sababu za kukosa msaada kutoka Israeli na Marekani na "uchochezi wa ndani" dhidi ya serikali yake. Kabla ya kuwa waziri mkuu, Abbas aliiongozwa Idara ya Mambo ya Mazungumzo ya PLO.

Wasifu kabla ya kifo cha Yasser Arafat

Abbas alizaliwa katika mji wa Safed katika Galilaya. Yeye na familia yake walikimbilia Syria wakati wa vita vya Waarabu na Israel vya 1948. Alihitimu katika Chuo Kikuu cha Damascus kabla ya kwenda Misri ambako alisoma sheria.
Abbas baadaye alijiunga na masomo katika Chuo Kikuu cha Patrice Lumumba jijini Moscow, ambako alipata shahada ya Sayansi (kwa Urusi ni sawa na PhD). Maudhui ya tasnifu yake ya udaktari ilikuwa "upande wa pili: mahusiano ya siri kati ya Nazism na uongozi wa harakati wa Kizayuni" ambapo alijaribu kuthibitisha kuwa mauaji ya Kinazi kwa Wayahudi hayajawahi kutokea. Profesa wake aliyemsimamia alikuwa Yevgeny Primakov.

Amemuoa Amina Abbas na wana watoto watatu wa kiume. Mtoto mkubwa, Mazen Abbas, alikuwa anaendesha kampuni ya ujenzi jijini Doha na alifia nchini Qatar kutokana na mshtuko wa moyo mwaka 2002 akiwa na umri wa miaka 42. Abu Mazen ina maana ya "baba wa Mazen". Mtoto wao wa pili, Yasser Abbas, ni mfanyabiashara wa Canada aliyepewa jina hilo la kiongozi wa zamani wa Palestina, Yasser Arafat. Mtoto wa mwisho ni Tareq, mfanyabiashara.

Katika miaka ya 1950 katikati, Abbas alishiriki kikamilifu katika siasa za chini za Palestina, na kujiunga na idadi ya Wapalestina waliokuwa uhamishoni nchini Qatar, alikokuwa Mkurugenzi wa Utumishi wa Huduma za Kijamii wa Emirate. Akiwa bado huko, mwaka 1961, aliajiriwa na kuwa mwanachama wa Fatah, iliyoanzishwa na Yasser Arafat na Wapalestina wengine nchini Kuwait katika miaka ya 1950. Wakati huo, Arafat alianzisha msingi wa Fatah kwa kuhusisha Wapalestina matajiri walioko Qatar, Kuwait, na mataifa mengine ya Ghuba.

Waziri Mkuu

Mnamo mwaka 2003, Israeli na Marekani kwa pamoja zilionesha kukataa majadiliano na Yasser Arafat, Abbas alianza kuibuka katika ugombea wa nafasi ya uongozi. Kama mmoja wa wanachama wachache waliobakia ambao ni waanzilishi wa Fatah, alikuwa akiaminiwa ndani ya Wapalestina, na ugombea wake uliimarishwa na ukweli kwamba Wapalestina wengine waliokuwa katika ngazi za juu walikuwepo kwa sababu mbalimbali ambazo si nzuri.

Sifa ya Abbas ya kuongozwa kwa sera za kisayansi ilimsaidia kwa nchi za Magharibi na baadhi ya wabunge wa Palestina, na shinikizo lililetwa kwa Arafat kumteua waziri mkuu. Arafat akafanya hivyo tarehe 19 Machi 2003. Awali, Arafat alijaribu kuidhoofisha nafasi ya waziri mkuu, lakini hatimaye alilazimishwa kumpa Abbas baadhi ya madaraka.

Hata hivyo, muda wa Abbas kama waziri mkuu uliendelea kuwa na sifa ya migogoro kadhaa baina yake na Arafat kuhusu mgawanyo wa madaraka kati yao. Abbas mara nyingi aligusia kujiuzulu kama hakupewa mamlaka zaidi katika utawala wake. Mwanzoni mwa Septemba 2003, alikabili bunge la Palestina kuhusu suala hili. Marekani na Israeli zilimshutumu Arafat mara kwa mara kumdhoofisha Abbas na serikali yake.

Aidha, Abbas aliingia katika mgogoro na wapiganaji wa makundi ya Palestina, hasa Palestinian Islamic Jihad Movement na Hamas kwa sababu sera zake za kisayansi zilikuwa kinyume na mbinu zao. Hata hivyo, aliweka wazi kabisa kwamba alikuwa analazimishwa kuachana na matumizi ya silaha dhidi ya raia wa Israel kwa muda huo.

Kwanza, aliahidi kutotumia nguvu dhidi ya wanamgambo, ili kuepuka vita vya wenyewe kwa wenyewe, na badala yake alijaribu njia ya mazungumzo. Hii ilifanikiwa kidogo, ilisababisha kutolewa kwa ahadi kutoka makundi mawili kusitisha-mapigano kwa heshima ya nchi moja ya Palestina. Hata hivyo, kuendelea kwa vurugu na Israel "kulenga kuua" viongozi wanaojulikana kulimlazimisha Abbas kuchukua hatua ili kutekeleza upande wa Mamlaka ya Palestina katika kutafuta amani. Hii ilisababisha kugombea madaraka na Arafat juu ya udhibiti wa huduma za usalama wa Wapalestina; Arafat alikataa kutoa udhibiti kwa Abbas, hivyo kumzuia kutumia wanamgambo.

Abbas alijiuzulu uwaziri mkuu mnamo Oktoba 2003, akitoa sababu za kukosa msaada kutoka Israeli na Marekani na "uchochezi wa ndani" dhidi ya serikali yake.
Uchaguzi wa rais 2005

Baada ya kifo cha Yasser Arafat, Mahmoud Abbas alionekana, angalau kwa Fatah, kuwa mrithi wake. Tarehe 25 Novemba 2004, Abbas alipitishwa na Baraza la Mapinduzi la Fatah kama mgombea wake kwa uchaguzi wa rais, uliopangwa kufanyika Januari 9, 2005.

14 Disemba, Abbas alitoa wito wa kumalizika kwa ghasia katika Intifada ya pili na amani. Abbas aliliambia gazeti la Asharq Al-Awsat kwamba "matumizi ya silaha yamekuwa yakiharibu na lazima yakomeshwe". Hata hivyo, alikataa kupokonya silaha wanamgambo wa Palestina na matumizi ya nguvu dhidi ya makundi ambayo Israel, Marekani na Umoja wa Ulaya wanayatambua kama mashirika ya kigaidi.

Vikosi vya Israel vilikamata na kuzuia harakati za wagombea wengine, Hamas wakasusia uchaguzi, na kampeni za Abbas zikapewa asilimia 94 ya matangazo kwenye vituo vya TV katika Palestina, ushindi wa Abbas ulikuwa dhahiri, na tarehe 9 Januari, Abbas alichaguliwa kwa asilimia 62 ya kura kama Rais wa Mamlaka ya Taifa ya Palestina.

Makala hii imeandaliwa na Bishop Hiluka kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari vya kimataifa.


No comments:

Post a Comment