Sep 28, 2011

MIAKA 50 YA UHURU: Rasilimali za nchi bado hazijawanufaisha wananchi

 Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi

 Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa

 Rais Jakaya mrisho Kikwete

BISHOP J. HILUKA
Dar es Salaam

HIVI sasa inaonekana dhahiri kuwa kipaumbele kikubwa cha viongozi walio wengi katika serikali yetu kipo katika mikakati ya kuandaa sherehe za miaka 50 ya uhuru zitakazofanyika wiki chache zijazo, mnamo Disemba 9 mwaka huu, zikisindikizwa na kaulimbiu ya “Tumethubutu, Tumeweza na Tunasonga mbele”. Licha ya kaulimbiu hiyo tamu, ukweli unabaki palepale kwamba wananchi walio wengi wanaendelea kuogelea kwenye lindi la umasikini hata baada ya uhuru wao. Kila kukicha maisha yanakuwa magumu afadhali ya jana!

Wakati wa kupigania uhuru kwa nchi zilizokuwa chini ya utumwa wa kikoloni moja kati ya malengo yaliyowasukuma wapigania uhuru wa wakati huo yalikuwa ni wananchi kujiamulia mambo yao katika matumizi ya rasilimali zao. Tanganyika (kwa maana ya Tanzania Bara) ni moja kati ya nchi za Afrika zilizopata uhuru mwanzoni mwa miaka ya 1960 ikiwa na matumaini mapya ya kutumia rasilimali zake katika kujiletea maendeleo.

Wakati huu tunapojiandaa kwa sherehe za miaka 50 baada ya uhuru huo, matumaini ya wananchi wa nchi hii kutumia rasilimali zao yamepotea kabisa huku kiwango cha umasikini kwa wananchi hao kikizidi kuongezeka, na pengo kati ya walionacho na wasionacho likizidi kuongezeka kwa kuwa ni wananchi wachache sana ndiyo wanaofaidi rasilimali za nchi hii.

Tanzania imejaaliwa rasilimali nyingi; watu, ardhi yenye rutuba, maji (bahari, mito na maziwa), kuwa katika eneo la kimkakati la kijiografia kwa biashara, na maliasili ikiwemo za utalii na madini. Hata hivyo, tukiwa tunajigamba kwa kuthubutu, kuweza na kusonga mbele kama kaulimbiu yetu inavyojieleza, tunaonekana kuwa na laana ya rasilimali hizi hali ambayo inafanya wananchi walio wengi kuendelea kuwa katika lindi la umasikini na wakiendelea kusukumwa pembezoni nje ya urithi ambao taifa hili linao.

Katika Tanzania ya leo na miaka mingi ijayo, hakuna jambo lolote muhimu kwa wanajamii wa nchi hii kuliko ardhi na rasilimali zao. Kama alivyowahi kusema mwanazuoni, Profesa Issa Shivji, rasilimali ndiyo chanzo cha uhai, kielelezo cha utamaduni, utambulisho wa ubinadamu, tegemeo la kuishi maisha ya kujitegemea, ya heshima na ya kifahari.

Rasilimali ardhi ndiyo rasilimali kubwa kabisa kwa wananchi, kwa sasa rasilimali hii inamilikiwa na watu wachache wenye uwezo kifedha hasa baada ya serikali hii kupitisha sera ya uwekezaji, na kumekuwepo matukio mengi ya uporaji wa ardhi za vijiji yanayofanywa na wawekezaji wa ndani na nje – kifisadi – kwa kisingizio cha uwekezaji.

Kwa hali hii, hivi sasa tunakabiliwa na tishio kubwa la usalama na amani katika taifa letu linalotokana na migogoro hii ya kirasilimali, hasa ardhi na madini, katika maeneo mbalimbali ya nchi ambayo haina tofauti na bomu litakalotulipukia wakati wowote endapo tu kasi ya ukuaji wa uchumi wenye kutoa fursa kwa wengi itaendelea kupuuzwa na haitaongezwa.

Mbali na ardhi, kumekuwepo pia taarifa za kuporwa kwa rasilimali nyingine kama vile wanyamapori, madini, maji na misitu, ambazo kwa sasa zinamilikiwa na matajiri huku masikini walio wengi wakizipata kwa taabu. Hali hii imekuwa ikisababisha Watanzania walalahoi wa mijini na vijijini kupoteza kabisa matumaini ya maisha kutokana na kushindwa kufaidika na rasilimali zao, japo kama Taifa tunajigamba kuthubutu, kuweza na kusonga mbele.

Tukiwa tunapanga mikakati na kujiandaa katika sherehe za kuadhimisha miaka 50 ya Uhuru, Taifa bado lipo gizani kutokana na mgawo wa umeme unaoendelea, pia bado kuna idadi ndogo sana ya Watanzania waliounganishwa kwenye gridi ya taifa, ingawa tunajivunia kaulimbiu yetu ya kuthubutu, kuweza na kusonga mbele.

Tatizo hili sugu la mgawo wa umeme ambalo sasa limekomaa na kuwa janga la taifa pamoja na ahadi mbalimbali zinazotolewa mara kwa mara za kulimaliza ambazo zimegeuka ndoto za alinacha, limetokana na ufisadi na udhaifu wa kiuongozi na kiutendaji ambao umeikabili sekta ya nishati nchini kuanzia Awamu ya Pili, likaongezeka katika Awamu ya Tatu na kukomaa zaidi katika Awamu hii ya Nne ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, licha ya kuthubutu, kuweza na kusonga mbele.

Kwa Serikali yoyote makini yenye kujali watu wake isingekimbilia kuandaa sherehe kama hii na kutumia pesa za wananchi bali ingetumia fursa ya miaka hamsini kukaa chini na kuyaangalia kwa makini mapungufu yaliyopo, hasa katika katiba, ili wananchi wapewe kipaumbele katika madai na matakwa yao kuhusu ardhi na rasilimali zao.

Alamsiki


No comments:

Post a Comment