Sep 7, 2011

Kesi ya Bi Victoire Ingabire na demokrasia finyu barani Afrika

 Ramani ya Bara la Afrika

 Rais mstaafu wa Afrika kusini, Mzee Nelson Mandela

 Rais mstaafu wa Botswana, Sir ketumile Masire

Bi Victoire Ingabire

BISHOP J. HILUKA
Dar es salaam

NI nini Watanzania tunajifunza kutoka mataifa mengine ya Afrika hasa kuhusiana na hali ya demokrasia? Je, sisi pia tunatoa fundisho gani katika demokrasia kwa mataifa mengine ya Afrika, mbali ya kukataa kuwatambua waasi wa Libya na kumshinikiza balozi wa Libya nchini kushusha bendera ya waasi hao?

Vipi kuhusu demokrasia ya nchi za Zimbabwe, Uganda, Rwanda, Libya, Misri, Ethiopia na kadhalika? Kwa nini wanasiasa wa Afrika siku zote wamekuwa wa kwanza kuharibu mambo? Ni Zimbabwe ambayo miaka ya karibuni ilikuwa tegemeo kubwa la Chakula la Afrika! Sasa vipi tena haohao waliotegemewa kwa chakula ndiyo wanaosumbuliwa na njaa na mfumuko wa bei?

Ni Uganda iliyokuwa ya kwanza kuanzisha utawala wa mihula miwili ya urais! Imekuwaje tena rais wa nchi hiyohiyo aliyesimamia uanzishwaji sheria ya mihula miwili kuendelea kuwepo madarakani kwa mihula minne na wala haoneshi dalili ya kuondoka madarakani? Vipi kuhusu kesi ya Rwanda ya wale maelfu waliouwawa mwaka 1994, ilikuwaje yale mauaji yakashindwa kuepukika? Je, Tanzania na mataifa mengine jirani yalifanya nini kukomesha mauaji ya watu wasio na hatia?

Vipi kuhusu nchi ya Libya iliyojiita Jamhuri wakati ilikuwa chini ya utawala wa mfalme Gaddafi kwa miaka 42? Nani alimsikia Gaddafi alipomshauri Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda kukataa kung'atuka madarakani? Je, nchi zingine za Afrika zilisemaje kuhusu hilo? Vipi kuhusu Misri na Ethiopia, nchi ambazo ni vinara wetu wa ustaarabu na uungwana tangu miaka mingi kabla ya Kristo, sasa ubabe wa nini?

Vipi kuhusu nchi nyingine za Afrika na hata Tanzania ambayo ingawa hatuvumi lakini tumo? Kwa nini kila inapofika wakati wa uchaguzi huwa nongwa? Je, upinzani ni uhaini? Hali hii itaendelea hadi lini?

Nchini Rwanda, kesi inayomkabili kiongozi wa chama cha upinzani cha UDF imeanza tena mapema wiki hii huku upande wa mashtaka ukiomba muda zaidi wa kukusanya ushahidi. Victoire Ingabire amefikishwa mahakamani chini ya ulinzi mkali huku wanahabari wakizuiwa kuzungumza naye.

Bibi Ingabire anakabiliwa na mashtaka ya ugaidi ambapo imedaiwa kwamba amekuwa akifadhili shughuli za kundi la FDLR ambalo serikali ya Rwanda imelitaja kuwa ni la kigaidi. Ingabire amekanusha madai hayo na kuituhumu serikali ya Rais Paul Kagame kuwa inatawala kwa mkono wa chuma na kwamba imeshindwa kuvumilia mashinikizo ya wapinzani.

Victoire Ingabire alikamatwa mwanzoni mwa mwaka jana baada ya kurudi nyumbani akitokea Uholanzi alikokuwa akiishi kama mkimbizi wa kisiasa. Alikamatwa na kuzuiwa kugombea katika uchaguzi uliofanyika nchini humo Agosti mwaka jana, licha ya kupendekezwa na muungano wa vyama vya upinzani kwamba yeye ndiye asimame dhidi ya Kagame

Inashangaza kwamba Victoire aliyeamua kurudi nyumbani Rwanda, baada ya miaka 16 uhamishoni alitumia muda mwingi kujifunza, na kufanya kazi huku akiihudumia familia yake nchini Uholanzi, kisha kuchukua uzito sana katika muktadha mpana ambao watu wake wanateseka. Alikaririwa akisema kuwa alirudi nyumbani kwa sababu hakuweza tena kuvumilia kuona watu wake wa Rwanda wanateseka chini ya udikteta wa kikatili. Kwa wakati huo, Januari 2010, alijitokeza kuwa kiongozi msomi mwenye msukumo zaidi ndani na nje ya Rwanda.

Kukamatwa kwa Ingabire ni cheche kinzani za kijamii zinazoendelea kujionesha kwa kasi na kwamba, demokarasia ya kweli barani Afrika inazidi kutoweka. Afrika limekuwa bara ambalo ukijiunga katika chama cha upinzani unahesabika kama mhaini. Ni bara ambalo si ajabu kusikia chama cha siasa cha upinzani kinapigwa marufuku, licha ya Katiba kuunga mkono tamko la haki msingi za binadamu lililotolewa na Umoja wa Mataifa.

Ni bara ambalo kuna matamko ya Serikali yanayowapokonya wananchi haki zao za msingi katika masuala ya kujieleza, kukutana na kuunda vyama mbalimbali vya kisiasa na kijamii. Kutokana na msimamo huu, nchi nyingi za bara hili zinakuwa ni nchi zinazotawaliwa kwa misingi ya kijeshi. Serikali zimeendelea kuwashughulikia wapinzani na wanaharakati wanaopania kuleta mageuzi kwa kutumia sheria dhidi ya vitendo vya kigaidi.

Bara la Afrika licha ya kukabiliwa na hali ngumu ya kiuchumi na kijamii, lakini pia lina idadi kubwa ya wagonjwa wa Ukimwi. Watu wengi wanaangamia kutokana na ugumu wa maisha baada ya kuondolewa na serikali zao kwenye maeneo yao yenye utajiri wa rasilimali, madini, mbao, ardhi nzuri ya kilimo, maji safi, mafuta na gesi asilia, ili kuendeleza mfumo wa kibepari wa kimataifa.

Je, nchi hizi za Kiafrika ikiwemo Tanzania zinaichukuliaje kesi ya Ingabire ama kwa sababu anashitakiwa na Rais mwenzao, Kagame? Je, kama Ingabire anadaiwa kuwa mhaini, kwa nini serikali ya Kagame isingelimwacha agombee huku yenyewe ikipeleka ushahidi kwa wananchi kuwa hafai hivyo wasimchague?

Pamoja na mapenzi makubwa niliyonayo kwa Kagame kama rais mchapakazi na anayesimamia vyema ufisadi nchini mwake kiasi kwamba Wanyarwanda wanapiga hatua haraka sana kulinganisha na sisi, lakini kila nikifumba macho na kufumbua naona Ingabire hatendewi haki katika hili. Kuna mkono wa kisiasa hapa. 
 
Tanzania na dunia nzima kwa ujumla tunapaswa kumwambia Kagame amwachie mwanamke huyu. Ana haki ya kugombea urais. Marais mliostaafu kwa heshima mko wapi? Joachim Chisano, Nelson Mandela, Ketumile Masire, Sam Nujoma, Ali Hassan Mwinyi na wengine wengi mko wapi? Tumieni busara zenu kumwambia Kagame amwachie huru Ingabire kwa sababu mahakama nzuri kuliko zote lilikuwa sanduku la kura. Kwa nini wananchi hawakuruhusiwa kutoa hukumu kupitia sanduku hilo?


No comments:

Post a Comment