Ndesumbuka Merinyo, mwenyekiti wa kamati ya Vazi la Taifa na mjumbe wa Kamati hiyo
BISHOP HILUKA
ZIMEKUWA zikitolewa hoja mbalimbali
kuhusiana na hiki kinachoitwa vazi la taifa. Hoja ambazo zimekuwa zikiniacha na
maswali kadhaa ambayo nimejaribu kuyauliza lakini hadi leo wahusika hawajajitokeza
kuyatolea ufafanuzi, na hata pale walipofafanua walitoa hoja dhaifu ambazo
binafsi bado hazijanishawishi kukiamini kile wanachokihubiri.
Mtaniwia radhi kama nitaonekana si mzalendo, lakini mimi pia nina mtazamo wangu katika
jambo hili. Mwanzoni mwa mchakato nilidhani kinachotafutwa ni vazi la taifa,
lakini siku chache hata kabla ya mdahalo mmoja uliorushwa na kituo cha
televisheni cha ITV nilishangazwa kuanza kusikia kauli za wahusika wakuu wa
mchakato huu kuhusu mwenendo mzima wa kupata kile kinachoitwa vazi la taifa.
Wahusika hao, kwa nyakati tofauti walikuwa wakisikika kuongelea aina ya
kitambaa, ubora wake na rangi gani inafaa!
Hapa bado pana mkanganyiko
mkubwa, wanaposema eti kitambaa kitakuwa na ubora tofauti kulingana na hadhi ya
mvaaji, wakitolea mfano wa wabunge, ambao wanaweza kuchagua suti waipendayo
kutokana na kitambaa hicho! Kumbe mawazo yao yamejikita kwenye kitambaa na ubora wa kitambaa na
si vazi kama dhana nzima ilivyoelezwa mwanzo! Je, kwa wananchi
wengi, hususan vijijini ambao hawamudu bei za vitambaa madukani na kimbilio lao
kubwa ni mitumba tunawaambia nini? Pia hapa sijajua, hoja ni vazi au kitambaa
cha taifa?
Hata hivyo, vazi la taifa
halitafutwi na halijawahi kutafutwa! Wamasai walitafutiwa na nani? Au hizo nchi
zinazotolewa mfano; Ghana , Nigeria , Afrika Kusini au China hawajawahi kuwa na kamati ya kutafuta vazi. Kwanza si kweli kwamba wana mavazi ya taifa, hayo tunayodhani kuwa ni ya
taifa ni mavazi yanayovaliwa na makabila makubwa. Nina wasiwasi kwamba tutatumia
pesa nyingi katika kitu kisicho na tija kwa maana kuwa mwisho wa mchakato vazi
halitakuwepo.
Nimekuwa sikubaliani na
sababu zinatolewa eti vazi hili litazidisha uzalendo, litaleta maendeleo,
litatangaza utamaduni, vivutio na utambulisho wa nchi! Nijuavyo, vazi la taifa kama ni utamaduni basi utamaduni hauundiwi mezani kama tunavyotaka kuaminishwa.
Ieleweke kuwa lengo la
makala hii ni kutoa changamoto na kuibua mjadala zaidi katika kuangalia namna
nzuri ya kurudisha maadili, uzalendo na kuutangaza utamaduni wetu katika kazi
za sanaa na changamoto zinazotukabili juu ya namna ya kukuza au kudhibiti wimbi
la mapokeo ya sanaa zinazokiuka mila, desturi na maadili yetu ya Ki-Tanzania,
badala ya kufikiria kuwa kitambaa pekee kitatusaidia.
Hebu tujiulize ni nchi gani
duniani ambayo kuendelea au kutokuendelea kwake kumetokana na kuwa ama kutokuwa
na vazi la taifa? Je, ni kitu gani cha muhimu ambacho kama taifa tumekikosa kwa miaka 50 kwa sababu ya kutokuwa na kipande cha
nguo kinachoitwa vazi la taifa? Ni kweli uzalendo umepungua nchini kwa sababu
ya kukosa vazi la taifa? Je, vazi la taifa ni sawa na vazi la heshima ambalo
ndicho kitu cha msingi sana kama tunaangalia udumishaji wa mila?
Nafikiri tuna changamoto
nyingi ambazo hata tukileta hilo
vazi haliwezi kuziondoa, tunapaswa kukabiliana na mmomonyoko wa maadili kwenye
jamii yetu ambao unaletwa na utamaduni tunaoiga toka nje, huku wizara
inayoratibu mchakato wa kitambaa kinachoitwa cha taifa ikiwa kimya na haijawahi
kuunda kamati kuushughulikia. Tunashuhudia mmomonyoko mkubwa katika jamii hii,
kupitia nyimbo za matusi, filamu na nyimbo za mapenzi au zisizo na asili yetu
zilizonakili vitendo na maudhui ya jamii za nje. Je, wizara husika iko wapi
katika hili?
Sanaa kama nguzo muhimu ya utamaduni hukua na pia hufa. Hivi sasa sanaa zetu zipo
katika chumba cha wagonjwa mahututi na tusipochukua juhudi za ziada tutazika
uasili wa sanaa zetu tulizoachiwa na wazee wetu zilizodumu kizazi hadi kizazi.
Hili linazigusa sanaa zote kuanzia filamu, muziki, sanaa za maonesho na kazi za
mikono. Ni kweli njia tunayoenda nayo katika kazi zetu za sanaa inatupeleka
kwenye msingi wa waliotutangulia au tumepotea na wimbi la utandawazi? Je, hili
vazi litasaidiaje kuzifanya sanaa zetu zisife?
Tuna tatizo kubwa la
maadili katika sanaa na udhibiti wa kazi chafu, jambo ambalo limekuwa gumzo.
Mbona wizara haijawahi kuandaa kamati ya kutafuta alama ya muziki wetu? Mbona
haitafuti alama ya filamu au chanzo cha wasanii kuiga filamu zisizo na maadili?
Au mbona ubunifu wa mitindo yetu ya kucheza muziki wetu na sanaa nyinginezo ni
wa kuiga? Kwa nini vazi la taifa?
Nimewahi kusoma kwenye
chapisho fulani kuwa fani ya muziki inaporomoka kwani wanamuziki walio wengi
wamepotea njia kwa kutofuata miiko katika tungo zao, miundo, mitindo na maudhui
kulingana na uasili, mila, desturi, mapokeo, historia na urithi tulioachiwa.
Haya yote yakiwa yanaashiria kuporomoka kwa fani hii.
Kadri muda unavyozidi
kwenda tunawapoteza wapiga ala kama ngoma, marimba, zeze, Saxophone na kadhalika, huku
idadi lukuki ya waimbaji bandia wasio na msingi na kanuni za fani ya uimbaji na
utunzi wakiongezeka na kusababisha muziki wetu kuchuja katika muda mfupi, hapo
hapo teknolojia ikimaliza vipaji vya wapiga ala kwa kuwa kila ala siku hizi ipo
studio kwenye mashine (computer). Mbona wizara haiundi kamati kunusuru hili?
Tumekuwa mahodari wa
kushabikia sanaa za kutoka nje ya nchi. Kuanzia kwenye jamii hadi ngazi ya
taifa, jambo linalotufanya kuwa wasindikizaji kwa kupokea sanaa na mitindo toka
nje. Haya yanajitokeza katika fani za unenguaji, filamu, muziki wa injili na
hata fani nyinginezo za sanaa. Bila kujua tumekuwa tunapandikiza mbegu mbaya
katika jamii kwa kutopenda cha kwetu. Je, katika mazingira haya uzalendo na
moyo wa kuipenda nchi utabadilishwaje na kitambaa tunachoita vazi la taifa?
Mwisho, tujiulize maswali
haya; je, vipaumbele vyetu kama taifa ili kujiletea maendeleo na kudumisha maadili
ni muhimu kuwa na vazi la Taifa leo? Tunapoangalia ubora na rangi ya vitambaa
katika nchi hii ya wavaa mitumba, je, serikali kupitia wizara husika haikuona
umuhimu wa kuunda kwanza tume ya kusaidia wakulima wa pamba ili pamba yao iwe katika kiwango bora badala ya kukimbilia kuunda
tume ya kutafuta vazi la Taifa?
Je, kuna mkakati gani hadi
sasa wa kuongeza thamani ya pamba yetu ili tuiuze kama malighafi nje ya nchi? Kwa nchi ambayo haina viwanda vya nguo, leo
tunaunda tume ya kutafuta vazi la Taifa, hivi kama vazi hilo likipatikana ni kiwanda gani hapa nchini kitashona
nguo hizo za vazi linaloitwa la Taifa? Au tutaanza tena mchakato wa kutafuta
mzabuni wa kutushonea nguo katika nchi kama China , India , Pakistani na kwingineko?
Alamsiki…