Sep 7, 2011

VICTOIRE INGABIRE: Mwanamke jasiri aliyejitokeza kuwa mpinzani wa Kagame

 Victoire Ingabire

 Rais wa Rwanda, Paul kagame

KIGALI
Rwanda

JAJI wa Rwanda ameamuru kesi inayomkabili kiongozi wa upinzani, Victoire Ingabire iendelee. Victoire anatuhumiwa kwa kueneza propaganda za chuki na za kikabila na "kukana kutokea kwa mauaji ya kimbari" - mashtaka anayosema yamechochewa kisiasa.

Upande wa mashtaka ulitaka kesi hiyo iahirishwe mpaka ushahidi zaidi uwasilishwe kutoka Uholanzi, ambapo Victoire aliishi mpaka Januari 2010 alipoamua kurejea Rwanda. Alikamatwa mwezi Aprili na kuzuiwa kugombea katika uchaguzi wa Agosti mwaka jana.

Alifikishwa mahakamani akiwa na pingu, na kuvaa sare ya wafungwa wa Rwanda ya rangi ya waridi huku akiwa amenyolewa kipara. Mwandishi wa Shirika la Habari la Uingereza (BBC), Geoffrey Mutagoma, aliyeko mjini Kigali alisema ni kawaida kwa wafungwa wa Rwanda kunyolewa vipara kutokana na sababu za kiafya.

Wakili wa Victoire Ingabire anayetokea nchini Uingereza, Iain Edwards, alitaka kesi hiyo ianze kusikilizwa kama ilivyokuwa imepangwa na Jaji Alice Rulisa akakubali. "Mwendesha mashtaka alisema tangu mwanzo kwamba wako tayari kwa kesi hiyo kuanza kusikilizwa, na wana ushahidi wote wa kuweza kuanza kesi hiyo," alisema.

"Sasa wanasema wanahitaji muda zaidi." Kesi hiyo imeshacheleweshwa katika vipindi viwili tofauti.

Kiongozi huyo wa chama cha Unified Democratic Forces anatuhumiwa kula njama na aliyekuwa afisa wa jeshi la Kihutu kununua na kusambaza silaha za kutishia usalama wa taifa. Victoire amesema kuwa mashtaka hayo si ya kweli na yamechochewa kisiasa. Ikiwa atakutwa na hatia, huenda akapewa kifungo cha maisha.

Victoire ni Mhutu na wengi miongoni mwa 800,000 waliouawa kwenye ghasia za mwaka 1994 walikuwa ni Watutsi. Rais Paul Kagame, aliyekuwa kiongozi wa waasi wa chama cha Rwandan Patriotic Front (RPF) chenye Watutsi wengi alisitisha mauaji hayo ya kimbari, alishinda kwa kipindi cha pili cha urais Agosti mwaka jana kwa jumla ya asilimia 93 ya kura zote.

Ni nani huyu Victoire Ingabire?

Victoire Ingabire Umuhoza alizaliwa Oktoba 3, 1968, ni Mwenyekiti wa Unified Democratic Forces (UDF); muungano wa vyama vya upinzani nchini Rwanda. Alikuwa mgombea wa chama kwenye uchaguzi wa rais wa mwaka 2010, lakini alizuiliwa kuwania nafasi hiyo. Kwa sasa yupo chini ya ulinzi kwa madai ya ugaidi na kutishia usalama wa taifa.

Familia yake na kazi

Ameolewa na ni mama wa watoto watatu, amepata mafunzo katika sheria ya biashara na uhasibu na kufuzu katika uchumi na usimamizi wa biashara wa makampuni nchini Uholanzi. Victoire alifanya kazi kama afisa wa kampuni ya kimataifa ya uhasibu nchini Uholanzi ambapo alikuwa kiongozi wa idara ya uhasibu katika matawi 25 barani Ulaya, Asia na Afrika.

Mwezi Aprili 2009, alijiuzulu kazi na kujiingiza katika siasa na kujiandaa kurudi katika nchi yake, kama mkuu wa chama cha kisiasa, ili kuchangia katika ujenzi wa nchi yake. Januari 2010, Victoire alirejea nchini mwake, baada ya miaka 16 ya uhamishoni, kama kiongozi mkuu wa chama cha upinzani cha kisiasa nchini Rwanda.

Kazi ya siasa

Tangu mwaka 1997, Victoire amekuwa akishiriki katika mapambano ya kisiasa za upinzani nchini Rwanda akiwa uhamishoni. Amekuwa akinukuliwa kusema "Lengo langu ni kuiingiza Rwanda katika utawala wa sheria na hali ya kikatiba ambapo viwango vya kimataifa vya kidemokrasia vinaheshimiwa, ambapo uzalendo utakuwa msingi wa mwisho kwa taasisi zote za umma."

Shughuli zake za kisiasa zinazingatia wazo la haki ambapo watu binafsi watachagua vyama vyao kwa kuzingatia matarajio yao ya pamoja ya kisiasa badala ya ukabila au ukanda. Pia ameanzisha mijadala katika kutoa wito wa kuwapatia uwezo zaidi wanawake nchini Rwanda.

Mwaka 1997, alijiunga na Republican Rally for Democracy nchini Rwanda. Mwaka mmoja baadaye, akawa Rais katika tawi lake lililopo Uholanzi na mwaka 2000, aliteuliwa kuwa Rais wa RDR katika ngazi ya kimataifa. Kuanzia 2003 hadi 2006, alichukua nafasi ya Rais wa Unified Rwandan Democratic Forces (UFDR), ambao ni umoja wa vyama vya siasa vya upinzani na kuviongoza kutokea uhamishoni, ambapo RDR ni mwanachama hai.

Kupigania umoja wa kisiasa wa upinzani akiwa uhamishoni kuliongoza kazi yake ya kisiasa. Novemba 2004, jijini Amsterdam, Uholanzi aliandaa mkutano uliojulikana kama "Jukwaa la Amani, Usalama, Demokrasia na Maendeleo katika Ukanda wa Maziwa Makuu" ambalo lilifuatiwa na Mpango wa Amsterdam wenye lengo la kujenga jukwaa jipya kwa ajili ya ushirikiano.

Mnamo Oktoba 2005, Victoire alianzisha mawasiliano na vyama vingine vya upinzani na waliandaa mikutano yote ya umoja kwa ajili ya vyama vyote vya kiraia vya Rwanda na vyama vya siasa. Makubaliano ya kawaida dhidi ya utawala wa Paul Kagame hatimaye yalifikiwa.

Kuanzia Aprili 2006, alishiriki kwenye uanzishwaji wa Umoja wa vyama na alichaguliwa kuwa Rais wa ajenda ya kisiasa. Umoja huo ulikuwa na lengo la kuanzisha utawala wa sheria nchini Rwanda, kama heshima ya maadili ya kidemokrasia ilivyoainishwa katika Azimio la Haki za binadamu na haki nyingine za kimataifa zinazohusiana na demokrasia na utawala bora.

Victoire alishiriki kikamilifu katika mijadala inayoihusu Rwandaj Barcelona, ​​Hispania mwaka 2004, 2006 na mwezi Aprili - May 2009 kwa msaada wa Juan Carrero Saralegui, aliyeteuliwa kuwania tuzo ya Amani ya Nobel na Adolfo Pérez Esquivel, mshindi wa tuzo ya Amani ya Nobel, na Federico Mayor Zaragoza, Makamu wa Rais wa Muungano wa Asasi za Kiraia.

Alitoa mapendekezo yafuatayo na kutoa wito kwa mageuzi kwa ajili ya mabadiliko katika maisha ya kila siku ya Wanyarwanda wote na njia ya wao kuhusiana na siasa: Uanzishwaji wa Kamati ya Haki, Ukweli na Maridhiano kusaidia Wanyarwanda katika upatanisho wa kweli; Uanzishwaji wa tume ya mambo yasiyo ya kisiasa katika uandikwaji na kutafsiri historia halisi ya Rwanda; Kupitisha muswada wa haki ya umiliki binafsi na kwa ajili ya ulinzi wa wanachama dhaifu wa umma, kwa ajili ya dhamana ya kisheria ya fursa sawa na upatikanaji wa mikopo na ajira kwa wananchi wote.
Mwezi mmoja baada ya kuwasili Rwanda mnamo Januari 2010, pamoja na viongozi wengine wawili wa kisiasa wa upinzani nchini humo, alianzisha Baraza la Ushauri la Kudumu kwa Vyama vya Upinzani, kuweka pamoja juhudi zao za kuongeza nafasi za kisiasa kwa vyama vya upinzani na kwa kuimarisha mchakato wa kidemokrasia nchini Rwanda.

Victoire Ingabire Umuhoza ni mwanachama mwanzilishi wa vyama vingi na mashirika katika sekta ya muungano: Chama cha Mawasiliano, Dialogue et Hatua Caritatives (CODAC) ambacho kinataka kutoa maadili, ushauri wa kisheria na msaada wa vifaa kwa waathirika wa Kanda ya Maziwa Makuu nchini Uholanzi au katika maeneo yao; Chama cha URAHO cha wanawake wakimbizi kutoka Rwanda nchini Uholanzi, kinacholenga kupata wanawake wa Rwanda waliotengwa nje ya nchi na kuwaunganisha katika jamii ya Kiholanzi, kusaidia watoto na kuwatafutia hifadhi.

Chama cha PROJUSTITIA-Rwanda, kinachopigania haki sawa kwa waathirika wote wa janga la Rwanda; HARAMBE, jukwaa la vyama vya wanawake wa Afrika nchini Uholanzi kwa nia ya kukuza maendeleo ya wanawake katika bara la Afrika. Victoire pia alikuwa mwanachama wa kamati ya utendaji ya ZWALU, jukwaa linalowaleta pamoja wanawake wa kigeni nchini Uholanzi na kuendeleza ukombozi wao

Machapisho

Victoire ni mwandishi wa makala mbalimbali na machapisho ambapo yeye alionesha maoni yake juu ya masuala muhimu yanayohusiana na matukio ya sasa katika nchi yake na ile ya kanda ya Maziwa Makuu. Miongoni mwa hayo ni:
  • "What is the Outlook for Peace in Central Africa?" (2001),
  • "International Justice After the Crisis in Rwanda" (2002),
  • "Conflicts in the Great Lake region of Africa: Origins and Solution Proposals" (2003),
  • "National Reconciliation As a Requirement for Security and Sustainable Peace in Rwanda and in the Countries of the African Great Lakes" (2004),
  • "Pleading for a True National Reconciliation in Rwanda, Requirements for Sustainable Peace" (2005).

Makala hii imeandaliwa na Bishop J. hiluka kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari vya kimataifa.

 

Sep 2, 2011

DOMINIQUE STRAUSS-KAHN: Kuutaka urais wa Ufaransa kulimponza

*Hata hivyo mahakama yamfutia mashitaka

 Dominique Strauss-Kahn

PARIS

JAJI ambaye alikuwa anasikiliza kesi ya tuhuma za ubakaji iliyokuwa inamkabili Mkurugenzi wa zamani wa Shirika la Fedha Duniani IMF, Dominique Strauss-Kahn, ametupilia mbali mashtaka hayo na hivyo kumuacha huru kigogo huyo.

Jaji Michael Obus alilazimika kuitupilia mbali kesi hiyo baada ya waendesha mashtaka kuwasilisha pendekezo la kufutwa kwa mashtaka hayo wakiamini hayana ukweli wowote na yalikuwa na lengo la kumchafua tu.

Baada ya Jaji Obus kutoa uamuzi huo ndipo Mwanasheria wa Strauss-Kahn, Benjamin Brafman, akachukua nafasi hii kuzungumza na waandishi wa habari ambapo alisema umma ulikosea kutokana na kuchukua hatua ya kuhukumu.

Naye Mwanasheria wa Nafissatou Diallo, Kenneth Thompson ametoa malalamiko kwa mahakama kwa hatua yake ya kutupilia mbali ombi lake la kuletwa kwa mwendesha mashtaka mwingine ambaye angesimamia kesi hiyo.

Strauss-Kahn mwenyewe baada ya kufutiwa mashtaka yaliyokuwa yanamkabili alimshuru mkewe pamoja na familia yake kwa kuwa naye pamoja kwenye kipindi kigumu cha kukabiliwa na tuhuma.

Hata hivyo, inasemekana kuwa Wafaransa wengi wanamuheshimu sana mwanasiasa huyu mwenye mwendo wa madaha, ambaye ni mashuhuri kwa jina la mkato la DSK. Mwenyewe amewahi kusema kwamba ana udhaifu katika mambo matatu: pesa, wanawake na uyahudi wake.

Upande mmoja wa familia ya Dominiques Strauss-Kahn ni Mayahudi wenye asili ya Morocco, nchi ya Kaskazini mwa Afrika na iliyokuja kuwa miongoni mwa makoloni ya Hispania.

Dominique Gaston Andre Strauss-Kahn alizaliwa Aprili 25, 1949 katika eneo la Neuilly Sur-Sein, karibu na mji mkuu wa Paris, Ufaransa. Amekulia Morocco kabla ya kuhamia Monaco na kusomea baadaye mjini Paris.

Mara nyingi akijulikana katika vyombo vya habari kama DSK, ni Profesa wa kiuchumi wa Ufaransa, mwanasheria, na mwanasiasa, na mwanachama wa Chama cha Kisoshalisti cha mrengo wa kushoto. Amekuwa pia akiwika katika jukwaa la kisiasa nchini Ufaransa kwa miongo miwili sasa.

Strauss-Kahn alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Fedha Duniani (IMF) tangu tarehe 28 Septemba 2007, kwa msaada wa Rais Nicolas Sarkozy, na ametumikia katika nafasi hiyo hadi alipojiuzulu tarehe 18 Mei 2011.

Mei 2011, Strauss-Kahn alikamatwa katika mji wa New York na kushtakiwa kwa unyanyasaji wa kijinsia wa mfanyakazi wa hoteli aliyeingia chumbani kwake, lakini mashitaka yote yalifutwa baadaye kwa ombi la upande wa mashtaka. Strauss-Kahn alikana mashtaka yote. Mwanasheria wa Wilaya ya New York aliondoa mashtaka tarehe 22 Agosti 2011, kutokana na upande wa mlalamikaji kushindwa kuthibitisha, na mahakama ilikubali.

Strauss-Kahn au DSK, kama ulivyo umaarufu wake kwenye siasa za Ufaransa, alifuata nyayo za wazee wake na kuelemea mrengo wa kushoto. Alijiunga mapema na Chama cha Kisoshialisti ambacho mnamo mwaka 1971 kilikuwa nguvu muhimu ya mrengo wa kushoto uliokuwa ukiongozwa na Francois Mitterand.

Katika miaka ya ’80 na ’90 alikabidhiwa nyadhifa tofauti za kisiasa, hadi mnamo mwaka 1997 alipochaguliwa kuwa Waziri wa Uchumi, Fedha na Viwanda.

Yeye ndiye aliyetandika misingi ya Ufaransa kuweza kujiunga na sarafu ya euro. Wengi wanakiri kwamba Strauss-Kahn alifanikiwa kuunganisha mawazo yakinifu ya kiuchumi na yale ya ujamaa wa kidemokrasia. Kwa mfano, yeye ndiye aliyepunguza muda wa kufanya kazi kwa wiki na wakati huo huo kuanzisha utaratibu wa kubinafsishwa mashirika ya serikali.

Mnamo mwaka 1999, Strauss-Kahn alijiuzulu kwa tuhuma za kuhusika na rushwa, ingawa baadaye alitakaswa na tuhuma hizo. Baada ya kujizulu, DSK alikuwa akijishughulisha zaidi na kazi yake ya kusomesha kwenye vyuo vikuu.

Miongoni mwa mengineyo, alikabidhiwa jukumu la kusimamia chuo kikuu mashuhuri cha Institut d’Etudes Politiques (IEP), ambako binafsi ndiko alikosomea. Wakati huo huo akateuliwa kuwa mshauri wa Shirika la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo barani Ulaya (OECD).

Staruss-Kahn alirejea katika jukwaa la kisiasa mwaka 2001 na kuongoza kampeni ya uchaguzi ya Lionel Jospin mnamo mwaka 2002 alipopigania kuwa rais wa Ufaransa.

Akiwa mbunge, Strauss-Kahn alipigania sana masuala yanayohusu Ulaya na kuunga mkono ushirikiano kati ya Ujerumani na Ufaransa kama injini ya Umoja wa Ulaya. Yeye alikuwa miongoni mwa wale waliokuwa wakiunga mkono katiba ya Umoja wa Ulaya iliyokataliwa na Ufaransa mnamo mwaka 2005.

Magazeti ya Ufaransa yakiandika taarifa za kashfa ya Strauss-Kahn; baada ya kukaa kwenye upande wa upinzani kwa miaka kadhaa, Strauss-Kahn akajitokeza kutaka kupigania kiti cha rais mwaka 2006 kwa tiketi ya chama chake cha Kisoshalisti cha mrengo wa kushoto, lakini alishindwa na Ségolène Royal. Wakati huo, Strauss-Kahn alikuwa akifikiria umuhimu wa kuunda chama kipya cha mrengo wa kushoto.

Lakini kabla ya kufanya hivyo, akajikuta anateuliwa kuwa mkuu wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), akiwa amependekezwa na mpinzani wake wa kisiasa, Rais Nicolas Sarkozy.

Lakini mara tu baada ya kuchaguliwa kuongoza shirika hilo, IMF ikakafanya uchunguzi dhidi ya kiongozi wake mpya. Lengo lilikuwa kutaka kujua ikiwa bosi huyo alitumia vibaya madaraka yake na kumpendelea mtaalamu wa kike wa kiuchumi, Piroska Nagy.

Naggy, ambaye alisemekana kuwa na uhusiano na Strauss-Kahn, alikubali kupokea fidia mnamo Agusti mwaka 2008 na kuacha kazi yake kutoka IMF.

Baada ya Straúss-Kahn kuomba radhi wakati ule, baraza la shughuli za utawala likapiga kura kwa sauti moja kumruhusu kuendelea na kazi yake. Uchunguzi haukutoa ushahidi wowote wa madai ya kutumia vibaya madaraka yake.

Februari mwaka 2010, Strauss Kahn alisema katika mahojiano ya radio kwamba anaweza kuamua kutetea kiti cha rais kwa tiketi ya Chama cha Kisoshalisti dhidi ya Rais Sarkozy wa kutoka chama tawala cha UMP na, kwa hivyo, kuachana na IMF kabla ya wakati wake kumalizika.

Maisha binafsi

Strauss-Kahn amemuoa mwandishi habari na mtangazaji wa televisheni, Anne Sinclair, tangu mwaka 1991. Ana watoto wanne wa kike kutoka ndoa zake mbili za mwanzo, mmoja kati yao ni kwa mke wake wa pili, Brigitte Guillemette, aliyemuoa mwaka 1984.

Ukiacha lugha yake ya Kifaransa, anazungumza pia kwa ufasaha Kiingereza na Kijerumani na pia ana ujuzi mzuri wa Kihispania na Kiarabu.

Nafasi muhimu alizoshika

  • Waziri wa Viwanda na Biashara ya Nje, 1991-1993.
  • Waziri wa Fedha, Uchumi na Viwanda, 1997-1999 (kujiuzulu).
  • Mbunge wa Bunge la Ufaransa kupitia Val d'Oise, 1986-1991 (na waziri 1991), akachaguliwa tena 1997, kisha akawa waziri 2001-2007 (alijiuzulu baada ya kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa IMF 2007).
  • Alichaguliwa tena miaka ya 1986, 1988, 1997, 2001, 2002, 2007.
  • Diwani wa Mkoa wa Ile-de-France, 1998-2001 (kujiuzulu).
  • Meya wa Sarcelles, 1995-1997 (kujiuzulu).
  • Naibu meya wa Sarcelles, 1997-2007 (alijiuzulu baada ya kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa IMF 2007), akachaguliwa tena mwaka 2001.
  • Diwani wa manispaa ya Sarcelles, 1989-2007 (alijiuzulu baada ya kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa IMF 2007), alichaguliwa tena 1995, 2001.
  • Rais wa jamii wa Agglomeration katika Val de France, 2002-2007 (alijiuzulu baada ya kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa IMF 2007).
  • Mwanachama wa jumuiya ya Agglomeration wa Val de France, 2002-2007 (alijiuzulu baada ya kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa IMF 2007).
  • Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Fedha Duniani, 2007-2011 (alijiuzulu kwa tuhuma za shambulio la ngono).

Makala hii imeandaliwa na Bishop J. Hiluka kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari vya kimataifa

Aug 24, 2011

Kanali Gaddafi alishakosa uhalali wa kuongoza

Kanali Muammar Gaddafi

 Waasi wakikanyanga sanamu ya Gaddafi

BISHOP J. HILUKA
Dar es Salaam

WAKATI naandika makala hii (siku ya Jumatano), kulikuwepo taarifa za waasi kuyazingira na kuyadhibiti makazi ya kiongozi wa Libya, Kanali Muammar Gaddafi, mjini Tripoli, huku taarifa zingine zinasema kuwa kiongozi huyo ameapa kupigana na waasi hao hadi kifo au ushindi.

Televisheni inayomuunga mkono Kanali Gaddafi, al-Urubah, imesema kuwa kiongozi huyo ambaye bado hajulikani alipo, ametoa hotuba akisema kuwa kuondoka kutoka kwenye makazi yake kulikuwa ni “mpango”. Makazi hayo ndiyo yaliyokuwa maeneo ya mwisho chini ya udhibiti wa Kanali Gaddafi mjini Tripoli.

Waasi wamekuwa wakisheherekea mafanikio yao katika bustani ya Green Square, mjini Tripoli huku picha za televisheni zikiwaonesha wapiganaji hao wakiivunja sanamu ya kiongozi huyo na kuipiga mateke baada ya kuuteka Bab al-Aziziya siku ya Jumanne.

Akizungumza na redio moja mjini Tripoli, Kanali Gaddafi ameahidi “kifo au ushindi” katika mapigano dhidi ya majeshi ya NATO na waasi wa Libya, redio ya al-Urubah ilisema.

Siku za nyuma Kanali Gaddafi aliwahi kukaririwa kusema ameleta heshima kwa Libya, jambo ambalo siwezi kubisha kwani inaeleweka wazi kuwa Gaddafi amewasaidia sana wananchi wake katika mambo fulanifulani. Amefanikiwa sana kukuza uchumi wa Libya na kuwafanya waishi kama wapo peponi, lakini hiyo haikumpa uhalali wa kukiuka misingi ya haki za binadamu na kutaka kutawala milele pamoja na kuanzisha utawala kama wa kisultani.

Uhalali wa utawala wake uliisha pale alipoamuru jeshi kuwashambulia kwa risasi za moto wananchi waliokuwa wanaandamana na hivyo kupoteza kabisa uhalali wa kuongoza. Wengi waliokuwa wakimshangilia ilikuwa ni katika kujikomba tu, au walifanya hivyo kwa hofu ya kupoteza maisha yao.

Azimio la Umoja wa Mataifa kuhusu Haki msingi za Binadamu linatamka bayana na kusisitizia uhuru wa mawazo, hii ni dhamana ya kila Serikali kuhakikisha kwamba, watu wake wanatekelezewa uhuru huo, badala ya kuendekeza dhuluma, ubaguzi na mateso hata kama umesaidia kukua kwa uchumi wa nchi.

Kilichokuwa kinaendelea Libya kinaakisi hali halisi ya kisiasa katika bara la Afrika, nchi nyingi katika bara hili bado zina changamoto kubwa kama vile: kudumisha misingi ya haki na amani pamoja na kutetea zawadi ya maisha hasa ya wale ambao ni wanyonge zaidi ndani ya jamii.

Wakenya bado wanakumbuka kwa namna ya pekee, machafuko ya kisiasa yaliyojitokeza kunako mwaka 2007 mara baada ya uchaguzi mkuu. Si rahisi kufuta picha ya mateso na mahangaiko ya wananchi wa Kenya katika kipindi hiki, mateso ambayo hayakuwa na msingi wowote ule!

Uvunjwaji wa haki za binadamu ni tatizo kubwa barani Afrika. Sheria mbaya, mahakama zisizokuwa huru, na vyombo vya dola vinavyofanya kazi kwa kufuata matakwa binafsi ya viongozi wa serikali, badala ya katiba na sheria, vimesababisha haki za binadamu katika nchi zetu kuwa katika hali mbaya.

Kimsingi shughuli zote za mwanadamu na mahusiano ya watu hapa duniani yalipaswa kuwa ni kwa ajili ya kuboresha hali yake kimwili, kiakili, kiroho na kuongeza ubora wa mahusiano yake na viumbe wengine. Hivyo, mchakato wa kila shughuli afanyayo ulipaswa kuwa katika namna ambayo haina dhuluma, uonevu, madhalilisho, taabu, ubaguzi, wala vikwazo kwa mwanadamu awaye yeyote na kwa kiumbe hai kingine chochote.

Kilele cha uwepo wa haki ni kuzalishwa na kutunzwa kwa furaha ya jamii na ya dola. Jamii kamwe haiwezi kuwa na furaha ya kweli kama haki haitawali na wala dola haliwezi kusimama imara pasipo kutunzwa kwa kiwango kikubwa haki ndani ya mipaka ya dola husika.

Jamii zote za wanadamu zina mfumo wa kimsingi wa kijamii, kiuchumi, na taasisi za kisiasa zilizo rasmi na zisizo rasmi. Ili kutambua kama mfumo fulani unaathiri mipangilio ya kijamii na una uhalali, mtu hana budi kutazama kukubalika kwa mfumo huo miongoni mwa watu wanaoongozwa na mfumo husika.

Uhuru wa kisiasa (mfano kuwepo kwa taasisi za demokrasia ya uwakilishi, uhuru wa kujieleza, wa vyombo vya habari na wa kukusanyika) uhuru wa kujumuika na kushirikiana na wanajamii uhuru wa mtu kwenda atakako na kuchagua kazi aitakayo bila kukinzana na misingi ya uadilifu, uhuru wa kupata haki binafsi zinazolindwa na utawala wa sheria.

Alamsiki

JORGE CARLOS FONSECA: Mpinzani aliyeshinda urais wa Cape Verde

Jorge Carlos Fonseca

Cape Verde

JORGE Carlos Fonseca, mgombea wa upinzani ameshinda katika uchaguzi wa urais wa Cape Verde, dhidi ya Manuel Inocencio Sousa, kutoka chama tawala. Fonseca alipata takriban asilimia 55 ya kura zote katika duru ya pili ya uchaguzi siku ya Jumapili, ukilinganisha na Sousa aliyepata asilimia 45.

Fonseca kutoka chama cha upinzani cha Movement For Democracy (MFD), alishinda kwa zaidi ya asilimia 37 ya kura zilizopigwa katika duru la kwanza la uchaguzi, kabla ya uchaguzi wa marudio uliomwingiza madarakani.

Viongozi hao wawili wamewania nafasi hiyo baada ya Rais Pedro Pires kung'atuka kufuatia kumaliza vipindi vyake viwili.
Wachambuzi wanasema, Cape Verde ni moja ya nchi zenye demokrasia thabiti barani Afrika.

Fonseca, mwenye umri wa miaka 60, aliyekuwa waziri wa mambo ya nje alisema atalenga zaidi kuujenga uchumi wa Cape Verde. Amenukuliwa na shirika la habari la AFP akisema, "ushindi wangu ni wa kidemokrasia, kwa heshima ya watu wa Cape Verde walioamini mipango yangu."

Historia yake

Jorge Fonseca Carlos de Almeida amezaliwa 20 Oktoba 1950, ni mwanasiasa, mwanasheria na profesa wa chuo kikuu, ambaye kwa sasa ndiye mshindi wa urais wa Jamhuri ya Cape Verde, kutoka chama cha Movement for Democracy (MfD).

Jorge Fonseca alimaliza elimu yake ya msingi na ya sekondari kati ya Praia na Mindelo, na baadaye, elimu yake ya juu mjini Lisbon. Alihitimu shahada ya kwanza katika Sheria na shahada ya uzamili wa Sheria katika Kitivo cha Sayansi ya Sheria, Chuo Kikuu cha Lisbon.
Alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa uhamiaji wa Cape Verde kati ya 1975 na 1977, na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Cape Verde kati ya 1977 na 1979.

Alikuwa mkufunzi msaidizi wa Kitivo cha Sheria, Chuo Kikuu cha Lisbon kati ya 1982 na 1990, Profesa mwalikwa wa sheria ya jinai katika Taasisi ya Tiba kuchunguza mauaji ya Lisbon mwaka 1987 na mkurugenzi mkazi na profesa mwalikwa katika kozi ya Sheria na Utawala katika Chuo Kikuu cha Asia ya Mashariki, Macau mwaka 1989 na 1990. Pia alikuwa profesa msaidizi na mwenyekiti wa bodi ya Taasisi ya Sheria na Sayansi ya Jamii katika Cape Verde.

Kati ya 1991 na 1993 alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje katika serikali ya kwanza ya Jamhuri ya Pili, na mgombea wa Rais wa Jamhuri mwaka 2001, nafasi ambayo ameitumia tena katika uchaguzi wa Agosti 7, 2011, wakati huu kwa kutumia chama cha upinzani cha MfD, na kushinda katika raundi ya 1 (kwa asilimia 38 ya kura) na duru ya pili, na hivyo kuwa Rais wa nne katika historia ya uhuru wa Cape Verde.

Pia ni mwanzilishi na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa taasisi ya “Direito e Justica”, mwanzilishi na mkurugenzi wa gazeti la “Direito e Cidadania”, mshiriki wa gazeti la “Revista Portuguesa de Ciência Criminal”, na mwanachama wa bodi ya wahariri ya “Revista de Economia e Direito”.

Pia ni mwandishi wa vitabu kadhaa na makala zaidi ya hamsini za kisayansi na kiufundi katika uwanja wa sheria, na amechapisha vitabu viwili vya mashairi. Amepewa tuzo kadhaa na Serikali ya Cape Verde.

Makala hii imeandaliwa na Bishop Hiluka kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari vya kimataifa.

ANNA HAZARE: Mwanaharakati India anayeitoa jasho serikali kuhusu ufisadi

Anna Hazare

India

MWANAHARAKATI nguli nchini India, Anna Hazare, ameweka nadhiri ya kufanikisha mapinduzi nchini mwake wakati huu ambapo ameanza kutekeleza ahadi yake ya kufunga kula na kunywa kwa kipindi cha siku kumi na tano.

Mwanaharakati huyo anahurumiwa na wengi nchini India na tayari maandamano ya kumuunga mkono yanazidi kuvutia idadi kubwa ya watu kote nchini humo. Hazare anashinikiza kufanyika kwa mageuzi katika sheria za kupambana na rushwa na alikuwa amepanga kuanza kukesha bila chakula ili kushinikiza hilo lifanyike.

Watu wengi wanaomuunga mkono wamejitokeza na mabango huku wakikemea serikali wakitaka aachiwe huru. Raia hao wa India wanasema lazima serikali ichukue hatua za kukabili ufisadi uliokithiri nchini humo.

Uamuzi wa Mwanaharakati Hazare una lengo la kuishinikiza serikali nchini India kutunga sheria kali zaidi dhidi ya viongozi ambao wanajihusisha na vitendo vya ulaji rushwa vilivyotawala kwenye taifa hilo.

Hazare aliitaka serikali kushughulikia mapendekezo yake ya namna ya kushughulikia suala la rushwa siku moja baada ya kufanyika kwa sherehe za kumbukumbu ya uhuru wa nchi hiyo ambapo Waziri Mkuu, Manmohan Singh alitangaza mikakati ya kukabiliana na hali hiyo.

Hata hivyo, Singh, amemkosoa mwanaharakati huyo akisema, ingawa nia yake ni nzuri anatumia dhana potofu kulazimisha bunge lifuate matakwa yake. Mshirika wa karibu wa Hazare amesema kuwa sasa amekubali kuondoka jela baada ya polisi kuridhia kuwa anaweza kufanya mgomo huo wa kususia chakula kwa siku kumi na tano kwenye bustani moja mjini Delhi.

Hazare na wafuasi wake wapatao 1,200 walitiwa nguvuni na polisi wakiwa kwenye bustani ya JP Park saa chache kabla hawajaanza kususia chakula.

Mwezi April Hazare alivunja mgomo wake wa kususia chakula baada ya siku nne pale serikali ilipokubali kuwa anaweza kuhusika kuandaa muswada wa kupambana na ufisadi nchini humo ambapo kutakuwa ofisi maalum ya kuchunguza wanasiasa na watumishi wa serikali wanaoshukiwa kuhusika na ufisadi.

Serikali ya Waziri Mkuu Singh imekuwa ikikosolewa vikali kutokana na kushindwa kudhibiti vitendo vya ulaji rushwa ambavyo vimekuwa vikifanywa na baadhi ya mawaziri.

Historia yake

Kisan Baburao Hazare, maarufu kama ya Anna Hazare amezaliwa Juni 15, mwaka 1937 ingawa machapisho mengine yanaonesha kuwa alizaliwa Januari 15 mwaka 1940 katika eneo la Bhingar, Ahmednagar, wilaya ya Maharashtra.

Baba yake alikuwa mfanyakazi asiyekuwa na ujuzi wowote na alimiliki ekari 5 ya ardhi kwa ajili ya kilimo. Hali mbaya ya kilimo iliisukuma familia yao katika mtego wa umaskini na mwaka 1952, Hazare alihamia katika nyumba yake ya mababu huko Ralegan Siddhi. Alilelewa na mama mmoja asiye na mtoto aliyemlipia pesa kwa ajili ya elimu yake mjini Mumbai, lakini kukosekana kwa fedha kulimsukuma kuuza maua kwa ajili ya kuishi na aliacha masomo baada ya darasa la saba.

Mara baada ya kuajiriwa katika Jeshi la India na kupatiwa mafunzo ya udereva wa magari aliajiriwa mjini Punjab. Siku zake katika utumishi wa Jeshi alizitumika kusoma vitabu mbalimbali vya falsafa za wanafalsafa wakubwa kama Swami Vivekananda, Mahatma Gandhi na Acharya Vinoba Bhave. Mawazo yao ndiyo yaliyomuongoza kujitoa maisha yake kwa kazi ya jamii.

Makala hii imeandaliwa na Bishop Hiluka kwa msaada wa mashirika mbalimbali ya habari
 

Aug 17, 2011

Kukosekana kwa uzalendo halisi kunavyochangia matatizo Afrika

Rais Jakaya Kikwete

 Basil Mramba, aliyewahi kusema kuwa
bora Watanzania wale nyasi ili ndege 
ya rais inunuliwe kwa gharama yoyote

BISHOP J. HILUKA
Dar es Salaam

MAKALA zangu mbili zilizotangulia nilielezea kuhusu miaka 50 ya uhuru wetu na kugusia kwamba matatizo yetu yamesababishwa na kukosekana uzalendo, jambo ambalo limenifanya kuonekana mpinzani. Msomaji mmoja amehoji kama naelewa maana ya neno hilo, kwa kuwa nimeonekana kulitumia sana katika mambo ambayo yeye anadhani hayakupaswa.

Pia ameonesha wasiwasi wake kuwa makala zangu zilibeba ujumbe mmoja tu; kuikosoa Serikali ya Chama Cha Mapinduzi kwa mawazo ya kiupinzani. Japo hakunieleza waziwazi lakini alikusudia kuniambia kuwa mimi ni mpinzani wa serikali, kwa kupinga hata mazuri yaliyofanyika.

Ningependa kuweka wazi msimamo wangu kwake na kwa wengine kuwa mimi sina chama na wala sijawahi kuwa mwanachama wa chama chochote cha siasa katika maisha yangu. Kwa kifupi sitaki kuwa na chama, hivyo sifungwi na itikadi za chama chochote na siandiki kwa utashi wa chama au mtu mwingine, ndiyo maana nipo huru kutoa mawazo yangu.

Pia siipendi siasa kwa kuwa kwangu siasa ni “si hasa”, ila navutwa kuandika kuhusu siasa kwa kuwa napenda kutoa mchango wangu kuhusu mustakabali wa nchi yetu.

Nirudi kwenye mada husika - Uzalendo – nijuavyo neno hili maana yake ni mtu kuipenda nchi yake, uzalendo ni miongoni mwa tabia njema ambazo inatakiwa ziwe ni pambo la mtu. Tabia hii ina athari kubwa sana katika kuchochea maendeleo ya mtu binafsi na nchi yake kwa ujumla. Uzalendo humsukuma mtu kuithamini na kuionea fahari nchi yake, vitu ambavyo ni chachu na hamira ya maendeleo. Uzalendo humfanya mtu kuitakia mema nchi yake.

Kiongozi yeyote mzalendo husukumwa na mapenzi kwa nchi yake, hawezi kulazimisha kununua ndege ya rais ya mabilioni hata kama wananchi wake watakula nyasi. Kiongozi mzalendo hawezi kujilimbikizia mali haramu ambazo upatikanaji wake una utata. Je, viongozi matajiri wamefanya biashara gani madarakani hadi wakaupata utajiri walio nao kama si kukosa uzalendo kwa nchi yao? Hivi utajiri wa viongozi hawa umelipiwa kodi ya mapato? Ni kweli wana mapenzi ya dhati kwa Watanzania wenzao katika kuondokana na madhila ya umaskini yanayowasibu?

Kiongozi yeyote mzalendo hawezi kuchukua 'ten parcent' ili kupitisha mikataba ya kinyonyaji ambayo italeta maafa kwa wananchi na kumfaidisha mgeni ambaye akishapata akitakacho ataondoka zake. Leo hii pesa za kodi ya wananchi zinaishia kujenga mahekalu na kununua magari ya kifahari ya viongozi ili-hali wananchi wanaendelea kuwa masikini, wanaoishi chini ya mstari wa ufukara ambapo asilimia 80 yao wanaishi vijijini wakitegemea kilimo cha jembe la mkono.

Uzalendo ni kitu adimu sana katika serikali nyingi za Kiafrika japo watawala wawapo majukwaani huhubiri uzalendo utadhani ni nguo unayoweza kuinunua dukani au kwa machinga. Wanasahau kuwa uzalendo uko moyoni, uzalendo ni sumu ya unyonyaji, uzalendo ni sumu ya rushwa, uzalendo ni sumu ya ukandamizaji, uzalendo ni sumu ya uonevu, uzalendo ni dawa kwa wananchi.

Kukosekana kwa uzalendo huwafanya viongozi kujivua majukumu yao ya kuhakikisha wananchi wanapata fursa sawa katika kushiriki masuala ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Viongozi ambao hushirikiana na wafanyabiashara wasio waaminifu kufanya udanganyifu katika biashara kwa kuwauzia wananchi bidhaa zilizo chini ya kiwango cha ubora, kuwapunja katika mizani au kuwauzia kwa bei ya juu kupita kiasi.

Kiongozi au mwananchi mzalendo ni yule afikaye kazini mapema kwa muda utakiwao na kufanya kazi kikamilifu kwa mujibu wa taratibu za kazi, atokaye kazini kwenda nyumbani kwa muda uliopangwa. Ukosefu wa uzalendo ndiyo umefanya viwanda vingi kufa, mashirika ya umma yamekufa na kuongeza idadi ya wazururaji na wakaa vijiweni ambao walikuwa wameajiriwa kwenye mashirika hayo.

Ukosefu wa uzalendo unasababisha umasikini katika nchi nyingi za Kiafrika kuwa ni wa Kujitakia. Umasikini wa aina zote mbili: umasikini wa nchi na umasikini wa watu walio wengi katika ujumla wao. Yaani tunashindwa hata kujinasua kwenye hili moja la kuwa na umasikini wa watu tu huku nchi ikiondoka kwenye utegemezi wa wahisani, kama sasa ambapo bajeti yetu haikamiliki bila kutegemea wahisani.

Inapotokea serikali imekuwa masikini hadi kuendeshwa kwa misaada toka nje ya nchi huku ikiendeshwa na viongozi matajiri kuliko serikali yao, ndipo kunapokuwa na maswali, halafu mbaya zaidi na wananchi nao wakawa masikini hadi kufikia kiwango cha kushindwa kufanya lolote.

Umasikini umekuwa kikwazo dhidi ya demokrasia na kikwazo dhidi ya utawala bora kwa kuwa wezi wa mali za umma, walaji rushwa na mafisadi ndio wenye tabia za kuwanunua wapiga kura walalahoi kwa njaa na umasikini wa kupindukia.

Ni muhali bali uongo mweupe mtu kudai kuwa anaipenda nchi yake huku anawasahau wananchi wake ambao wamemfanya yeye awepo hapo alipo na kuneemesha kundi dogo la marafiki wake na familia yake. Kielelezo na nembo kuu ya kuonesha taswira ya uzalendo wake kwa nchi yake kiwe ni kuwahudumia wananchi wake; katika hali na mali.

Ni wajibu na jukumu la kila mmoja wetu kuipenda nchi yake. Mwanafunzi mwenye uzalendo na nchi yake ni yule anayesoma kwa hima juhudi na bidii huku akizingatia miiko na taratibu za elimu ambazo ni pamoja na kuwaheshimu walimu wake na kanuni zote za shule sambamba na kushirikiana na wenzake.

Naomba kuwasilisha...

JULIUS MALEMA: Kinda wa Afrika Kusini aliyezua utata masuala ya mashauri ya nchi za nje

Julius Malema

AFRIKA KUSINI

NI kama ilivyokuwa wakati viongozi wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) walipotoa tamko katika mkutano wa wajumbe wa Kamati ya Utekelezaji ya Baraza Kuu la Umoja huo na Jukwaa la Wahariri Tanzania, kwenye hoteli ya Peacock, mjini Dar es Salaam, kukemea bila woga, ndivyo ilivyotokea nchini Afrika Kusini kwa kiongozi mkakamavu wa tawi la vijana la chama tawala cha ANC, Julius Malema, ingawa ni kwa aina tofauti kidogo.

Julius Malema aliingilia kati masuala ya mashauri ya nchi za nje, alipotoa wito kuwa serikali ya nchi jirani ya Botswana, iliyochaguliwa kwa njia ya kidemokrasia inafaa kupinduliwa. Hata hivyo, tawi hilo la vijana la ANC, limeomba msamaha kwa chama.

Mapema mwezi huu, ANC ilililaumu vikali tawi lake la vijana, na kiongozi wake, Julius Malema, kwa matamshi hayo.

Historia yake

Julius Malema Sello amezaliwa 3 Machi 1981, katika eneo la Seshego, ni kijana mwanasiasa wa Afrika Kusini, na Rais wa Tawi la Vijana wa African National Congress (ANC). Malema yupo kwenye nafasi tata ya kisiasa nchini Afrika Kusini; akiibukia kwenye umaarufu kwa msaada wa rais wa ANC, na baadaye Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma.

Malema amekuwa akielezewa na wote, Zuma na Waziri Mkuu wa Limpopo kama "kiongozi wa baadaye" wa Afrika Kusini. Lakini pia amekuwa akitafsiriwa na wengine kama “maarufu asiyejali” mwenye uwezekano wa kuidhoofisha Afrika Kusini na cheche za ubaguzi wa rangi. Alipatikana na hatia ya kutumia lugha ya chuki mnamo Machi 2010.

Maisha ya awali na kazi

Malema alizaliwa katika eneo la Seshego, Mama yake alikuwa mfanyakazi wa ndani na mzazi pekee aliyemlea mwanaye. Alijiunga na Masupatsela ya ANC katika umri wa miaka tisa au kumi ambapo kazi yake kubwa ilikuwa ni kuyaondoa (kuyachana) mabango na matangazo yote ya chama cha National (mpinzani wa ANC) kinyume cha sheria.

Elimu

Ilimchukua Malema miaka minne kumaliza darasa la 8 na 9 la shule ya sekondari. Alimaliza darasa la 12 katika Shule ya Juu ya Mohlakaneng katika eneo la Seshego, Limpopo, akiwa na umri wa miaka 21, baada ya kuwa mtoro wa shule kwa muda wa miezi mitano katika mwaka huo. Matokeo yake ya mtihani wa darasa la 12 yaliyoonesha kupata alama mbaya yalichapishwa katika gazeti la taifa mnamao Oktoba 2008, yakionesha kumkejeli.

Kazi ya siasa

Malema alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa tawi la vijana la Seshego na mwenyekiti wa kikanda mwaka 1995. Mwaka 1997 akawa mwenyekiti wa Shirikisho la Wanafunzi wa Afrika Kusini (Cosas) wa jimbo la Limpopo, na alichaguliwa kuwa rais wa kitaifa wa shirikisho hilo mwaka 2001. Mwaka 2002, Malema aliongoza maandamano ya Cosas ya wanafunzi, katika mitaa ya Johannesburg yaliyofunikwa na matukio ya ghasia na uporaji.

Kiongozi wa Vijana wa ANC

Malema alichaguliwa kuwa rais waVijana wa ANC mwezi Aprili 2008. Uchaguzi - na mkutano – ulioelezewa na kile ambacho Malema mwenyewe alikisema baadaye kuwa "mwenendo wa yanayotokea". Uadilifu wa uchaguzi wake umekosolewa na kuhojiwa. Alichaguliwa tena bila ya kupingwa kwa awamu ya pili mnamo 17 juni 2011.

Ziara ya Zimbabwe, Aprili 2010
3 Aprili 2010, Malema alitembelea Zimbabwe, kwa kile kilichoelezwa kama ziara ya uzawa. Alitarajiwa kukutana na Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe. Alipotua Harare, Malema alisalimiwa na wafuasi wa Zanu-PF pamoja na Waziri wa Vijana na Uzawa wa Zimbabwe, Mwokozi Kasukuwere, na Mwenyekiti wa Vijana wa Zanu-PF, Absolom Sikhosana, pamoja na wafanyabiashara maarufu wa Zimbabwe.

Morgan Tsvangirai, Waziri Mkuu wa Zimbabwe, aliishutumu ziara ya Malema, baada ya Malema kukikosoa chama cha Tsvangirai, cha MDC. Wakati wa ziara hiyo, Malema alimuelezea Tsvangirai kama mshirika wa "mabeberu". Mashirikisho ya Vijana wa Zimbabwe yaliikosoa ziara ya Malema, yakitoa maelezo yake ya ubaguzi wa rangi na madai ya rushwa. Wakati wa ziara yake kulizua hofu kwamba Afrika Kusini itafuata mageuzi ya ardhi kama ya Zimbabwe. Malema pia aliilaumu MDC kwa kuanzisha ghasia za kisiasa nchini Zimbabwe, na kutetea rekodi ya kisiasa na haki za kibinadamu ya Robert Mugabe.
Baada ya Malema kurudi kutoka Zimbabwe, Vijana wa ANC walitoa taarifa kumsifu Mugabe na sera zake za kutaifisha ardhi Zimbabwe. Pia walitoa wito kwa vijana wa Afrika Kusini wa kufuata mfano wa vijana wa Zimbabwe, na kushiriki katika kilimo ili kupunguza utegemezi wao juu ya wakulima wa kizungu. Msaada wa Malema ndani ya Vijana wa ANC bado ni imara.

Kushiriki katika mikataba ya nchi

Taarifa juu ya kuhusika kwa Malema katika zabuni za nchi (mikataba) ilianza kuonekana Novemba 2009. Maswali kuhusu maisha yake binafsi yalitolewa na vyombo vya habari Afrika Kusini. Machi 2010, alijibu madai hayo katika mkutano uliofanyika kampasi ya chuo kikuu, Malema, aliimba wimbo wa mapambano "piga risasi Makaburu", na aliwakemea wanasiasa wa upinzani. Pia alimshambulia Katibu Mkuu wa COSATU, Zwelinzima Vavi.

Agosti 2010, ilitolewa ripoti iliyomsafisha Malema kushiriki kwake katika zabuni za nchini katika mkoa wa Limpopo. Hii ilipokelewa kwa wasiwasi na baadhi ya watu.

Vitisho kwa waandishi wa habari
Wiki chache baada ya utata wa zabuni kuibuka kwa mara ya kwanza, Vijana wa ANC walitoa maelezo binafsi ya Mhariri wa Uchunguzi wa City Press, Dumisane Lubisi, mke wake na watoto wake, ikiwa ni pamoja na namba zao za vitambulisho, maelezo ya benki, anuani ya makazi na maelezo ya gari zao. Lubisi alikuwa ametoa taarifa kuhusu kiwango duni cha ujenzi wa miradi katika Limpopo uliofanywa na makampuni ya Malema.

Vijana wa ANC walitoa madai kuwa walikuwa na ushahidi kuwa waandishi walikuwa wanapokea rushwa katika mambo kadhaa. Katika majibu, kundi kubwa la waandishi wa habari wa kisiasa walilalamika kwa mamlaka mbalimbali ndani ya ANC na Jukwaa la Wahariri la Afrika Kusini (SANEF) wakisema kwamba taarifa hiyo ilikuwa kama jaribio la kuwatisha wasichapishe habari zaidi, na kama tishio kwa uhuru wa vyombo vya habari.

Ufafanuzi wa vyombo vikubwa vya habari

Malema anajulikana kwa taarifa zake tata na mara kwa mara amekuwa akishutumiwa. Awali, wachora katuni, Zapiro na Jeremy Nell mara nyingi walimchora akiwa amevaa nepi. Hivi karibuni, wasifu wa Malema kwa umma umeongezeka, amekuwa akielezwa na wakosoaji katika vyombo vya habari kama "kiongozi wa kisiasa anayeshawishi watu kwa kutumia hisia badala ya fikra zao". Pia alitajwa katika orodha ya watu wasio na ushawishi ya gazeti la Time kwa mwaka 2010.

Kupatwa hatia kwa kauli za chuki

Machi 15, 2010 Malema alipatikana na hatia ya kutumia lugha ya chuki katika Mahakama ya Usawa, akatozwa faini ya R50 000 na kuamriwa kuomba msamaha, kufuatia tukio la 2009 alipowaambia kundi la wanafunzi wa Cape Town, katika Mkutano wa Wanafunzi wa Afrika Kusini (SASCO) kwamba mwanamke aliyemshitaki Rais wa ANC, Jacob Zuma kwa ubakaji alipata “wakati mzuri” kwa sababu baada ya kuamka asubuhi alipata “kifungua kinywa na fedha za teksi”. Kufuatia hukumu hiyo SASCO walionesha "furaha", na kumshambulia Malema kwa “matumizi mabaya” ya jukwaa ambalo SASCO walimpa.

Malema alitoa taarifa mbalimbali kuhusu Wachina nchini Afrika Kusini katika chakula cha jioni cha Umoja wa Wanafunzi wa Afrika Kusini na Wayahudi Aprili 2011. Aliwakebehi wawekezaji wa China ambao "hawakuleta chochote nchini" na kukosoa Uwekezaji wa China nchini Afrika Kusini, kuhoji Afrika Kusini kujihusisha na biashara ya Brazil, Russia India na China.

Makala haya yameandaliwa na Bishop J. Hiluka kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari vya kimataifa.