Jun 1, 2012

Tuwekane sawa; ni vazi au kitambaa cha taifa?


Ndesumbuka Merinyo, mwenyekiti wa kamati ya Vazi la Taifa na mjumbe wa Kamati hiyo


BISHOP HILUKA
Dar es Salaam

ZIMEKUWA zikitolewa hoja mbalimbali kuhusiana na hiki kinachoitwa vazi la taifa. Hoja ambazo zimekuwa zikiniacha na maswali kadhaa ambayo nimejaribu kuyauliza lakini hadi leo wahusika hawajajitokeza kuyatolea ufafanuzi, na hata pale walipofafanua walitoa hoja dhaifu ambazo binafsi bado hazijanishawishi kukiamini kile wanachokihubiri.

Mtaniwia radhi kama nitaonekana si mzalendo, lakini mimi pia nina mtazamo wangu katika jambo hili. Mwanzoni mwa mchakato nilidhani kinachotafutwa ni vazi la taifa, lakini siku chache hata kabla ya mdahalo mmoja uliorushwa na kituo cha televisheni cha ITV nilishangazwa kuanza kusikia kauli za wahusika wakuu wa mchakato huu kuhusu mwenendo mzima wa kupata kile kinachoitwa vazi la taifa. Wahusika hao, kwa nyakati tofauti walikuwa wakisikika kuongelea aina ya kitambaa, ubora wake na rangi gani inafaa!

Hapa bado pana mkanganyiko mkubwa, wanaposema eti kitambaa kitakuwa na ubora tofauti kulingana na hadhi ya mvaaji, wakitolea mfano wa wabunge, ambao wanaweza kuchagua suti waipendayo kutokana na kitambaa hicho! Kumbe mawazo yao yamejikita kwenye kitambaa na ubora wa kitambaa na si vazi kama dhana nzima ilivyoelezwa mwanzo! Je, kwa wananchi wengi, hususan vijijini ambao hawamudu bei za vitambaa madukani na kimbilio lao kubwa ni mitumba tunawaambia nini? Pia hapa sijajua, hoja ni vazi au kitambaa cha taifa?

Hata hivyo, vazi la taifa halitafutwi na halijawahi kutafutwa! Wamasai walitafutiwa na nani? Au hizo nchi zinazotolewa mfano; Ghana, Nigeria, Afrika Kusini au China hawajawahi kuwa na kamati ya kutafuta vazi. Kwanza si kweli kwamba wana mavazi ya taifa, hayo tunayodhani kuwa ni ya taifa ni mavazi yanayovaliwa na makabila makubwa. Nina wasiwasi kwamba tutatumia pesa nyingi katika kitu kisicho na tija kwa maana kuwa mwisho wa mchakato vazi halitakuwepo.

Nimekuwa sikubaliani na sababu zinatolewa eti vazi hili litazidisha uzalendo, litaleta maendeleo, litatangaza utamaduni, vivutio na utambulisho wa nchi! Nijuavyo, vazi la taifa kama ni utamaduni basi utamaduni hauundiwi mezani kama tunavyotaka kuaminishwa.

Ieleweke kuwa lengo la makala hii ni kutoa changamoto na kuibua mjadala zaidi katika kuangalia namna nzuri ya kurudisha maadili, uzalendo na kuutangaza utamaduni wetu katika kazi za sanaa na changamoto zinazotukabili juu ya namna ya kukuza au kudhibiti wimbi la mapokeo ya sanaa zinazokiuka mila, desturi na maadili yetu ya Ki-Tanzania, badala ya kufikiria kuwa kitambaa pekee kitatusaidia.

Hebu tujiulize ni nchi gani duniani ambayo kuendelea au kutokuendelea kwake kumetokana na kuwa ama kutokuwa na vazi la taifa? Je, ni kitu gani cha muhimu ambacho kama taifa tumekikosa kwa miaka 50 kwa sababu ya kutokuwa na kipande cha nguo kinachoitwa vazi la taifa? Ni kweli uzalendo umepungua nchini kwa sababu ya kukosa vazi la taifa? Je, vazi la taifa ni sawa na vazi la heshima ambalo ndicho kitu cha msingi sana kama tunaangalia udumishaji wa mila?

Nafikiri tuna changamoto nyingi ambazo hata tukileta hilo vazi haliwezi kuziondoa, tunapaswa kukabiliana na mmomonyoko wa maadili kwenye jamii yetu ambao unaletwa na utamaduni tunaoiga toka nje, huku wizara inayoratibu mchakato wa kitambaa kinachoitwa cha taifa ikiwa kimya na haijawahi kuunda kamati kuushughulikia. Tunashuhudia mmomonyoko mkubwa katika jamii hii, kupitia nyimbo za matusi, filamu na nyimbo za mapenzi au zisizo na asili yetu zilizonakili vitendo na maudhui ya jamii za nje. Je, wizara husika iko wapi katika hili?

Sanaa kama nguzo muhimu ya utamaduni hukua na pia hufa. Hivi sasa sanaa zetu zipo katika chumba cha wagonjwa mahututi na tusipochukua juhudi za ziada tutazika uasili wa sanaa zetu tulizoachiwa na wazee wetu zilizodumu kizazi hadi kizazi. Hili linazigusa sanaa zote kuanzia filamu, muziki, sanaa za maonesho na kazi za mikono. Ni kweli njia tunayoenda nayo katika kazi zetu za sanaa inatupeleka kwenye msingi wa waliotutangulia au tumepotea na wimbi la utandawazi? Je, hili vazi litasaidiaje kuzifanya sanaa zetu zisife?

Tuna tatizo kubwa la maadili katika sanaa na udhibiti wa kazi chafu, jambo ambalo limekuwa gumzo. Mbona wizara haijawahi kuandaa kamati ya kutafuta alama ya muziki wetu? Mbona haitafuti alama ya filamu au chanzo cha wasanii kuiga filamu zisizo na maadili? Au mbona ubunifu wa mitindo yetu ya kucheza muziki wetu na sanaa nyinginezo ni wa kuiga? Kwa nini vazi la taifa?

Nimewahi kusoma kwenye chapisho fulani kuwa fani ya muziki inaporomoka kwani wanamuziki walio wengi wamepotea njia kwa kutofuata miiko katika tungo zao, miundo, mitindo na maudhui kulingana na uasili, mila, desturi, mapokeo, historia na urithi tulioachiwa. Haya yote yakiwa yanaashiria kuporomoka kwa fani hii.

Kadri muda unavyozidi kwenda tunawapoteza wapiga ala kama ngoma, marimba, zeze, Saxophone na kadhalika, huku idadi lukuki ya waimbaji bandia wasio na msingi na kanuni za fani ya uimbaji na utunzi wakiongezeka na kusababisha muziki wetu kuchuja katika muda mfupi, hapo hapo teknolojia ikimaliza vipaji vya wapiga ala kwa kuwa kila ala siku hizi ipo studio kwenye mashine (computer). Mbona wizara haiundi kamati kunusuru hili?

Tumekuwa mahodari wa kushabikia sanaa za kutoka nje ya nchi. Kuanzia kwenye jamii hadi ngazi ya taifa, jambo linalotufanya kuwa wasindikizaji kwa kupokea sanaa na mitindo toka nje. Haya yanajitokeza katika fani za unenguaji, filamu, muziki wa injili na hata fani nyinginezo za sanaa. Bila kujua tumekuwa tunapandikiza mbegu mbaya katika jamii kwa kutopenda cha kwetu. Je, katika mazingira haya uzalendo na moyo wa kuipenda nchi utabadilishwaje na kitambaa tunachoita vazi la taifa?

Mwisho, tujiulize maswali haya; je, vipaumbele vyetu kama taifa ili kujiletea maendeleo na kudumisha maadili ni muhimu kuwa na vazi la Taifa leo? Tunapoangalia ubora na rangi ya vitambaa katika nchi hii ya wavaa mitumba, je, serikali kupitia wizara husika haikuona umuhimu wa kuunda kwanza tume ya kusaidia wakulima wa pamba ili pamba yao iwe katika kiwango bora badala ya kukimbilia kuunda tume ya kutafuta vazi la Taifa?

Je, kuna mkakati gani hadi sasa wa kuongeza thamani ya pamba yetu ili tuiuze kama malighafi nje ya nchi? Kwa nchi ambayo haina viwanda vya nguo, leo tunaunda tume ya kutafuta vazi la Taifa, hivi kama vazi hilo likipatikana ni kiwanda gani hapa nchini kitashona nguo hizo za vazi linaloitwa la Taifa? Au tutaanza tena mchakato wa kutafuta mzabuni wa kutushonea nguo katika nchi kama China, India, Pakistani na kwingineko?

Alamsiki…

AHMED SHAFIK: Kusuka au kunyoa urais wa Misri



Ahmed Shafik


CAIRO,
Misri

HALI ni tete nchini Misri kwa mgombea mmoja wa urais. Waandamanaji nchini humo wameshambulia makao makuu ya mgombea huyo wa urais, Ahmed Shafik, mjini Cairo. Ahmed Shafik anashutumiwa kuunga mkono utawala wa zamani wa Hosni Mubarak, madai ambayo yeye na wafuasi wake wanakanusha vikali.

Uvamizi huo umetokea muda mfupi baada ya tume ya uchaguzi kuthibitisha kuwa uchaguzi wa marudio utafanyika mwezi huu kati ya Ahmed Shafik, ambaye aliwahi kuwa waziri mkuu wa zamani katika utawala wa Rais Hosni Mubarak, na Mohamed Mursi wa chama cha Muslim Brotherhood.

Hakuna aliyedai kuhusika na mashambulio hayo. Mwandishi wa Shirika la Utangazaji la Uingereza, BBC, katika eneo la tukio alisema kuwa jengo liliwaka moto kidogo, lakini halikupata uharibifu mkubwa.

Waandamanaji wapatao elfu moja wanaliokuwa wanapinga matokeo ya uchaguzi huo pia walikusanyika katika medani ya Tahrir.

Wakati hayo yakijiri, wagombea urais wawili walioshindwa katika duru ya kwanza ya uchaguzi nchini humo pia wametaka baadhi ya kura zihesabiwe tena, wakidai kuwa kulitokea udanganyifu.

Afisa mmoja wa polisi aliwashutumu baadhi ya wenzake, kwamba waligawa kadi 900,000 za utambulishi, bila ya kutaja kazi yao, ili wapate kupiga kura. Inasemekana kuwa katika uchaguzi nchini humo, wanajeshi hawaruhusiwi kabisa kupiga kura.

Msemaji wa kiongozi wa mrengo wa kushoto aliyeshika nafasi ya tatu katika duru ya kwanza, Hamdeen Sabahi, alisema kuwa wangekata rufaa Jumapili, ili kuzuwia duru ya pili ya uchaguzi wa urais.

Waziri wa zamani wa mashauri ya nchi za nje, Amr Moussa, aliyemaliza akiwa wa tano, alimsihi afisa wa mashtaka kufanya uchunguzi. Kwa matokeo ya hadi sasa, duru ya pili ya uchaguzi itakuwa kati ya Ahmed Shafik, waziri mkuu wa mwisho wa Hosni Mubarak, na Mohamed Mursi wa chama cha Muslim Brotherhood.

Historia ya Shafik

Ahmed Mohamed Shafik alizaliwa Novemba 1941, ni mwanasiasa wa Misri. Aliwahi kuwa kamanda mwandamizi katika Jeshi la Anga la Misri na baadaye alifanya kazi kama Waziri Mkuu wa Misri kati ya Januari 31, 2011 na Machi 3, 2011, kipindi cha siku 33 tu.

Baada ya kazi ya anga kama rubani wa mapigano, kamanda wa tawi na kituo cha kijeshi, Ahmed Shafik alikuwa Kamanda wa Jeshi la Anga la Misri kuanzia 1996 hadi 2002, na kufikia daraja la jemadari wa anga. Baada ya hapo alifanya kazi katika serikali kwenye nafasi ya Waziri wa Usafiri wa Anga kuanzia mwaka 2002 hadi 2011.

Aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu na Rais Hosni Mubarak mnamo Januari 31, 2011, katika kukabiliana na Mapinduzi ya Misri ya mwaka 2011, na hivyo kumfanya kuwa Waziri Mkuu wa mwisho kutumikia nafasi hiyo chini ya utawala wa Hosni Mubarak. Alikaa kwenye nafasi hiyo kwa mwezi mmoja tu, akajiuzulu mnamo Machi 3, 2011, siku moja baada ya kipindi cha mahojiano kilichozua utata kwenye kituo cha televisheni ambapo alishutumiwa na mwandishi maarufu wa vitabu nchini Misri ya kuendeleza utawala wa Mubarak.

Maisha ya awali

Shafik alizaliwa katika jiji la Cairo mwezi Novemba, 1941. Baada ya kufuzu mafunzo yake katika Chuo cha Anga cha Misri mwaka 1961, alijiunga na Jeshi la Anga la Misri (EAF) akiwa na umri wa miaka 20. Baadaye katika kazi yake, alipata shahada yake ya uzamili katika Sayansi ya Jeshi, Nishani ya Juu ya Vita kutoka Chuo cha Kijeshi cha Nasser, Nishani ya Pamoja ya Kijeshi kutoka Chuo cha Juu cha Vita jijini Paris, Nishani ya ulinzi wa Taifa kutoka katika Chuo cha Kijeshi cha Nasser na shahada ya uzamivu (Ph.D.) katika "Mkakati wa Taifa wa Anga". Jemadari wa Anga, Ahmed Shafik, alipata medali za juu na uhalali wakati wa utumishi wake.

Kazi ya kijeshi

Kama afisa wa jeshi kijana, Shafik aliwahi kuwa rubani mpiganaji na baadaye aliteuliwa kuwa kamanda wa kikosi cha jeshi la anga. Wakati wa Vita ya msuguano kati ya 1967 na 1970, Shafik alijikuta akiwa anafanya zaidi kazi kama Kamanda mwenye majukumu mengi katika kikosi cha anga. Baadaye akawa kamanda wa kikosi cha jeshi la anga.

Mwaka wa vita vya Oktoba 1973, Shafik alikuwa rubani mpiganaji mwandamizi chini ya uongozi wa Hosni Mubarak. Inaaminika kwamba Shafik alizidondosha ndege mbili za Israel wakati wa vita mnamo tarehe 14 Oktoba, 1973.

Mwaka 1984 Shafik aliteuliwa kuwa mwambata wa kijeshi katika ubalozi wa Misri nchini Roma. Aliendelea katika nafasi hii hadi mwaka 1986. katika kipindi cha kuanzia 1988 hadi 1991, Shafik alifanya kazi katika nafasi kadhaa andamizi za kijeshi kabla ya kuteuliwa kuwa Kamanda wa Idara ya Uendeshaji wa Anga.

Mwezi Septemba 1991, Shafik aliteuliwa kuwa Mkuu wa Utumishi wa Jeshi la Anga, akishikilia nafasi hii hadi mwezi Aprili 1996, alipokuwa Kamanda wa Kikosi cha Anga cha jeshi la Misri. Mwaka 2002, baada ya kujiuzulu kutoka huduma za kijeshi, aliteuliwa kuwa Waziri wa Usafiri wa Anga na nafasi yake ilichukuliwa na na mkuu wake wa utumishi, Jemadari wa Anga Magdy Galali Sharawi.

Uteuzi wa Waziri Mkuu na Kujiuzulu

Katika kipindi cha vuguvugu la Mapinduzi ya Misri ya mwaka 2011, Shafik aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu mnamo Januari 29. Hata hivyo, Uwaziri Mkuu wake ulikuwa wa muda mfupi mno, ulidumu kwa kipindi cha mwezi mmoja tu na siku chache, baada ya kujiuzulu mnamo Machi 3 kutokana na shinikizo kutoka kwa waandamanaji na upinzani.

Walikuwa walipinga Shafik kuwa Waziri Mkuu, baada ya kuonekana kama mmoja wa walinzi wa zamani wa Mubarak. Shafik alidaiwa kuwa alikuwa ni mjumbe wa Baraza Kuu la Vikosi vya Jeshi ambavyo vilichukua madaraka baada ya kuondoka kwa Mubarak mnamo Februari 11, 2011. nafasi ya Shafik ilichukuliwa na Essam Sharaf baada ya kujiuzulu.

Shafik alijiuzulu nafasi ya Waziri Mkuu siku moja baada ya mahojiano yaliyozua utata kwenye kituo cha ONTV (Misri) ambapo alikuwa anakabiliwa na Alaa Al Aswany, mwandishi maarufu wa vitabu nchini Misri aliyeandika ‘The Yacoubian Building’, kwenye kipindi cha majadiliano cha Baladna bel Masry. Al Aswany alimkosoa vikali Shafik wakati matangazo hayo yakirushwa, akiwakilisha moja ya vipindi vya kwanza vya ukosoaji katika televisheni rasmi ya umma katika historia ya serikali ya Misri.

Katika hatua moja, Al Aswany alisema kuhusu Shafik, "kama mtoto wako alikuwa mmoja wa wale waliokimbia na magari ya polisi, usingeweza kubaki kimya kama hiyo." Al Aswany alimtuhumu zaidi Shafik ya kuwa bado anaendeleza utawala ambao Jihadi ya Wamisri imeupindua, na kwamba alikuwa hafai kuwakilisha Wamisri katika zama za baada ya mapinduzi.

Makala haya yameandaliwa na Bishop Hiluka kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari vya kimataifa.

Kama tunataka kuulinda muungano turuhusu mjadala wa wazi

Mwalimu Nyerere akichanganya mchanga kuashiria Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliozaa taifa jipya la Tanzania, Aprili 26, 1964

BISHOP J. HILUKA
Dar es Salaam

MUUNGANO wa nchi mbili za Tanganyika na Zanzibar uliozaa taifa jipya la Tanzania ulizaliwa Aprili 26, 1964 na hivyo Alhamisi ya Aprili 26 mwaka huu muungano wetu umetimiza miaka 48. Nilishuhudia sherehe za Muungano kupitia televisheni, na hali imeendelea kubainisha kuwa tunalazimisha kusherehekea huku kukiwa na manung’uniko kutoka kwa wananchi na hata baadhi ya viongozi wa kisiasa wakionekana ama kuupinga mfumo wa Muungano au kutoutaka kabisa Muungano huu.

Wazanzibar wanalalamika wamemezwa na Tanzania Bara, Watanzania Bara (Watanganyika) wanalalamika kuwa wameipoteza Tanganyika yao na wananyonywa kupitia mwamvuli wa Muungano wa Tanzania, lakini wachache katika serikali yetu wameapa kuwa wataulinda muungano huu kwa nguvu zote!

Ni ajabu sana kuwa kila upande unalalamika! Inashangaza sana katika vuta nikuvute hii eti kuna kundi linasema litaulinda Muungano kwa nguvu zote! Katika kuulinda huu Muungano kumekuwepo tafsiri ambayo inahitaji ufafanuzi; kuulinda kwa nguvu zote maana yake nini?

Wafuatiliaji wa masuala ya siasa wanaiona kauli ya kuulinda ni kuzuia watu wasiujadili. Kutoruhusu uvunjike. Huku wengine (nikiwemo mimi) tukijiuliza, ya nini kuwa na muungano bila kuujadili? Inafaa nini kuishi kwa mazoea? Na kwa faida ya nani? Huku Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akisema kuwa jambo pekee wanalopaswa wananchi kujadili kuhusu Muungano ni kuuboresha! Inawezekanaje watu waboreshe kitu ambacho hawajakubaliana umuhimu wake?

Rais amesahau kuwa Watanzania walio wengi leo hii ni vijana waliozaliwa baada ya Muungano. Ingawa wamesoma habari za Muungano katika vitabu vya historia lakini hawauelewi vyema, ndiyo maana hata shamrashamra za serikali na wananchi juu ya Muungano zimeshuka siku hizi. Tunachoshuhudia ni wananfunzi kulazimishwa kwenda kwenye sherehe hizi bila ridhaa yao.

Kama vijana hawaujui vyema Muungano wetu, kwa nini sasa wanataka kunyimwa fursa ya kuujadili? Fursa imejitokeza lakini viongozi wanatuzuia? Hivi kweli wanautakia mema Muungano huu?

Hapa sijui kama kweli kuna nia ya dhati ya kuuboresha. Kutoujadili? Kutorusu uvunjike? Hivi tunayafanya haya kwa faida ya nani? Wananchi ambao ndiyo wenye nchi yao wanataka kuandika upya historia yao tena kwa nyakati zao
lakini viongozi wanataka kuwaenzi waasisi kinafiki! Nani mwenye nchi? Wananchi au viongozi?

Siandiki haya kwa kuwa labda siutaki Muungano, hasha! Nautakia mema ndiyo maana napenda tukae mezani kuujadili, tuangalie kasoro zote zilizopo na kuzirekebisha ili hatimaye tuingie kwenye Muungano uliopata ridhaa za wananchi wa pande zote. Ni kufilisika kimawazo kudhani kwamba anayehoji Muungano ana nia ya kuuvunja. Badala yake, ni kuchochea mjadala mpana na wa kina kuhusu umuhimu wa Muungano. Hatutakuwa na muungano imara kama viongozi wataendelea kutulazimisha bila kusikiliza hoja na manung’uniko yetu.

Hata hivyo, kuvunjika kwa muungano si jambo la ajabu, kama hatutaruhusu mijadala ya wazi tunaweza kuishia walikoishia wengine. Tusidhani kuwa sisi tuna akili zaidi au tumebarikiwa zaidi ya wengine. Tuna kipi cha ajabu? Kumbukumbu zangu zinanieleza kuwa mojawapo ya waliokuwa nchi moja na kutengana ni Ethiopia iliyotengana na Eritrea, muungano wa Senegambia ulishindikana kwa kuwa wananchi hawakushiriki na hatimaye walitengana na kubaki nchi mbili za Senegal na Gambia, pia iliyokuwa Rwanda-Burundi ambayo sasa ni nchi mbili za Rwanda na Burundi, India iliyogawanyika na kuzaa Pakistan, na Pakistan ikazaa Bangladesh.

Inashangaza sana kuona kuwa kundi dogo linataka kubinafsisha mawazo ya walio wengi, vijana na wasomi wa taifa hili wanashindwa kuhoji mambo kwa mapana yake. Tunapaswa tujiulize, hivi kwa nini tuliungana? Huu si wakati tena wa kuleta sababu dhaifu eti tunaleta umoja au eti kwa vile sisi ni ndugu. Mbona hatuungani na Wakenya wakati nchi zote hizi zina undugu?

Kwa nini hatupewi nafasi ya kuhoji nini sababu hasa ya muungano huu? Wenye majibu wote kwa sasa hawapo na yaliyobaki ni majibu ya kufikirika tu, nafasi ya uongo ni kubwa. Bila majibu haya, ni vigumu ni bora watu wakajadili na wakaja na aina ya muungano wanaoutaka.

Hali ya mashaka inaugubika Muungano huu, inatokana na kile kinachodaiwa kuwa kuundwa kwa Muungano wetu kulikuwa siri na tangazo la kutiwa saini mkataba wa Muungano kati ya Rais wa Tanganyika, Mwalimu Julius K. Nyerere, na Rais wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume, liliwashangaza watu kutoka pande zote za muungano; Bara na Visiwani.

Habari zinazidi kupasha kuwa hali hii ilitokana na habari za Muungano kuwa za siri na watu wa pande zote mbili za Muungano hawakushauriwa utadhani hawakuwa na haki yoyote ya mustakabali wa nchi yao.

Ndiyo maana nafikiri kuendelea kudhani kuwa kujadili jambo lolote linalohusu Muungano ni uhaini au kuendelea kuyafumbia macho masuala ya Muungano tutakuwa tunajidanganya, kwani kuficha au kudharau maradhi ni ugonjwa hatari, na ipo siku mauti itatuumbua.

Ukiuangalia Muungano wetu kijuujuu utaona kuwa ni mfano mzuri sana wa maelewano kwa watu wa Bara la Afrika, lakini chini kwa chini kunafuka moshi ambao ukiachwa hivi hivi bila kutafutiwa ufumbuzi utakuja kujitokeza moto mkubwa ambao tunaweza kushindwa kuuzima na hivyo matokeo yake hayatakuwa mazuri.

Kwa kuwa tupo katika kipindi cha kuandika Katiba mpya, nadhani ni wakati mwafaka kila Mtanzania aweke maslahi ya taifa mbele bila ushabiki, viongozi nao wawe mstari wa mbele kuonesha njia na siyo kuwa na sauti ya mwisho juu ya Muungano.

Hofu za viongozi wetu zinatoka wapi? Mbona Watanzania wengi kutoka pande zote zinazohusika na Muungano, wanaonekana wazi hawapingi kuungana, kwani muungano kwao ni baraka. Ila hiki kinachoitwa Kero za Muungano.

Kero hizi ni pamoja na mfumo wa Muungano, ikiwa ni pamoja na wanaotaka muundo wa serikali mbili uendelee, lakini wapo wanaosema uwe wa serikali moja na wapo wanaopendelea mfumo wa shirikisho wa serikali tatu. Nadhani wote wanapaswa kusikilizwa, ikiwa ni pamoja na sababu wanazotoa kama kweli tunataka kuuboresha Muungano. Muundo wa Muungano, hata kama chama tawala kimekuwa kikidai kuwa sera yake ni ya serikali mbili, linatakiwa liwe jambo litakaloamliwa na wananchi wenyewe kupitia kura ya maoni.

Ukiangalia kwa makini utagundua kuwa Muungano wetu uliundwa ukiwa zaidi na sura ya kisiasa na ulikuwa wa mambo 11 kama ambavyo imekuwa ikielezwa, lakini sasa wapo wanaosema yamefika 22 na wengine hudai ni zaidi ya 30. Kumekuwa na utata juu ya kuongezeka mambo ya Muungano na viongozi wengine wanasema mengi yameongezwa kinyemela.

Hata hili la ushirikiano wa kimataifa halikuwa limejumuishwa katika orodha asili ya mambo ya Muungano na ndiyo maana Zanzibar waliamua kujiunga na Jumuiya ya Nchi za Kiislamu (OIC), kwa vile suala hili halikuwa la Muungano, hali iliyoutikisa Muungano na kusababisha mzozo mkubwa.

Kero nyingine ni kuhusu Rais wa Zanzibar aliyetakiwa moja kwa moja awe Makamu wa Rais wa serikali ya Muungano kama Rais atatoka Bara, na pale Rais atakapotoka upande wa pili, yaani Zanzibar mwenzake wa Bara awe Makamu wa Rais. Lakini hili limeondolewa bila ya kura ya maoni, kwa hofu tu zisizo na maana yoyote

Miaka ya hivi karibuni zimekuwa zinasikika kelele kutoka Zanzibar kutaka masuala ya uchimbaji na biashara ya mafuta na bahari kuu yatolewe katika orodha ya Muungano, huku Mamlaka ya Kodi ya Mapato pia ikilalamikiwa. Haya yanahitaji muungano kuhojiwa kwa uwazi ili majibu ytaolewe. Kama kutakosekana majibu ya maana, itakuwa ni kazi bure kutumia maneno makali kwani wananchi wataukataa.

DIONCOUNDA TRAORÉ: Rais wa mpito nchini Mali anayekabiliwa na shinikizo

Dioncounda Traore


BAMAKO,
Mali

WAKUU wa serikali nchini Mali wamesema kuwa Rais wa Mpito wa nchi hiyo, Dioncounda Traore, amepelekwa eneo salama baada ya kupigwa hadi kuzirai na mamia ya waandamanaji nchini humo.

Mamia ya waandamanaji walimshambulia Rais Traoure wakipinga mkataba ulioafikiwa na Tume ya kiuchumi ya nchi za Magharibi mwa Afrika, ECOWAS, ambapo Traoure ataendelea kutawala kwa hadi mwaka mmoja badala ya siku 40 pekee zilizokubaliwa miezi miwili iliyopita.

Mwandishi wa Shirika la Utangazaji la Uingereza, BBC, amesema kuwa shambulio hilo litawashtua wanadiplomasia waliokuwa wakifanya kila juhudi kurejesha amani na utangamano nchini humo. Muda wa kuongoza aliopewa kiongozi huyo, Djouncounda Traore, ulitarajiwa kukamilika Jumatatu.

Lakini viongozi wa nchi za Magharibi mwa Afrika, waliafikia mkataba na kiongozi wa mapinduzi, Kapteni Amadou Sanogo, kwamba Traore asalie mamlakani ili aweze kuongoza harakati za uchaguzi na kumaliza harakati za waasi wa Tuareg.

Mkataba huo pia ulijumuisha mpango wa kukubalia Sanogo atajwe kama kiongozi wa zamani alipwe mshahara wa rais na apewe nyumba ya kifahari.

Mapinduzi hayo pamoja na harakati za waasi kuteka maeneo ya Kaskazini mwa Mali, yamesababisha maelfu ya watu kutoroka makwao. Mashirika ya misaada wanasema wana wasiwasi mkubwa kuhusu hali ya kibinadamu nchini Mali nchi ambayo pia inakumbwa na baa la njaa.

Mwandishi wa Shirika la Utangazaji la Uingereza, BBC, mjini Bamako, Martin Vogl amesema kuwa wanajeshi waliwaruhusu baadhi ya waandamanji kuingia katika ikulu ya rais ingawa rais huyo wa mpito hakuwepo wakati huo.

Historia yake

Dioncounda Traoré amezaliwa tarehe 23 Februari, 1942, ni mwanasiasa wa Mali ambaye amekuwa Rais wa Mali katika kipicha cha muda mfupi tangu mwezi Aprili mwaka 2012.  Amekuwa Rais wa Bunge la Mali tangu mwezi Septemba 2007, na Rais wa chama cha kisiasa kinachojulikana kama Alliance for Democracy in Mali-African Party for Solidarity and Justice (ADEMA-PASJ) tangu mwaka 2000. Pia alikuwa Rais wa Alliance for Democracy and Progress (ADP), muungano wa vyama ambavyo viliunga mkono uchaguzi wa marudio wa Rais Amadou Toumani Touré mwaka 2007.

Kazi ya siasa

Traoré alizaliwa katika eneo la Kati. Baada ya kusoma nje ya nchi katika Umoja wa Kisovyeti, katika Chuo Kikuu cha Algiers, na katika Chuo Kikuu cha Nice, alifundisha nchini Mali katika Chuo cha Walimu (ENSUP) kati ya 1977 na 1980. Kisha alikamatwa kwa kujishughulisha na harakati za mambo ya muungano wa vyama vya kibiashara na kupelekwa Ménaka kaskazini mwa Mali.

Baada ya hapo, akawa mkurugenzi mkuu wa Shule ya Taifa ya Uhandisi. Alishiriki katika mapambano kwa ajili ya demokrasia ambayo yalisababisha kuangushwa kwa Rais Moussa Traoré mnamo Machi 1991. Alikuwa mwanachama mwanzilishi wa ADEMA, na katika mkutano wake wa Katiba, uliofanyika mnamo Mei 25 na 26 mwaka 1991, alichaguliwa kuwa Makamu wa Pili wa Rais wa ADEMA, wakati Alpha Oumar Konaré alichaguliwa kuwa Rais wa chama hicho na Mohamed Lamine Traoré alichaguliwa kuwa Makamu wake wa kwanza wa Rais.

Baada ya Konaré kuchaguliwa kuwa Rais wa Mali katika uchaguzi wa rais wa mwaka 1992, Traoré aliteuliwa kuwa Waziri wa Utumishi wa Umma, Kazi, na Utawala mnamo tarehe 9 Juni 1992, katika serikali ya kwanza chini ya rais wa Konaré. Baadaye aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi kwa ajili ya Ulinzi mnamao tarehe 16 Aprili 1993, ameshika nafasi hiyo hadi alipokuwa Waziri wa Nchi kwa ajili ya Mambo ya Nje mnamo tarehe 25 Oktoba 1994. Katika mkutano wa kwanza wa ADEMA wa kawaida, uliofanyika Septemba 1994, Traoré alichaguliwa kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa chama hicho, wakati Ibrahim Boubacar Keïta alichaguliwa kuwa Rais wake.

Alichaguliwa kuwa Naibu katika Bunge akitokea Nara mwaka 1997 na kujiuzulu nafasi yake ya Waziri wa Mambo ya Nje mnamo tarehe 24 Agosti 1997 ili kuchukua kiti chake cha ubunge. Katika Bunge, akawa Rais wa Kundi la Wabunge wa ADEMA, kufuatia kujiuzulu kwa Keïta katika nafasi ya Urais wa ADEMA mnamo Oktoba 2000, Traoré alichaguliwa kuwa Rais wa ADEMA kwa mara ya kwanza katika Mkutano wa chama wa dharula, uliofanyika Novemba 25 hadi 28, 2000. Katika uchaguzi wa mwaka 2002 wa bunge, Traore alishindwa katika jimbo la Nara na kupoteza kiti chake.

Katika uchaguzi wa wabunge mnamo Julai 2007, Traoré aligombea tena katika akiwemo orodha ya ADEMA katika jimbo la Nara, ambapo viti vitatu vilikuwa hatarini. Katika raundi ya kwanza, orodha yake ilishinda kwa asilimia 39.59 ya kura, na katika raundi ya pili ilishinda kwa asilimia 58.41 ya kura. Wakati Bunge jipya la taifa lilipofanya mkutano wake wa kwanza tarehe 3 Septemba 2007, Traoré alichaguliwa kuwa Rais wa Bunge, akipata kura 111 dhidi ya kura 31 za Mountaga Tall wa National Congress for Democratic Initiative (CNID), mwanachama mwingine wa ADP.

Kufuatia mapinduzi ya kijeshi mnamo Machi 2012, ambayo yalisababisha kuwekwa vikwazo vya kiuchumi na Jumuiya ya Kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) dhidi ya Mali, mpango huo, ulioandaliwa katika nchi ya Burkina Faso na Rais Blaise Compaoré chini ya mwamvuli wa ECOWAS, ulisainiwa tarehe 6 Aprili 2012 ambao ulitarajiwa kuona mkuu wa serikali hiyo ya kijeshi, Kapteni Amadou Sanogo, akiachia madaraka kwa Dioncounda Traoré ili ashikilie madaraka ya urais katika serikali ya mpito hadi uchaguzi utakapofanyika. Traoré alikuwa ameondoka nchini humo kufuatia mapinduzi ya kijeshi, lakini alirudi mnamo Aprili 7.

Traoré aliapishwa kuwa Rais katika sherehe iliyofanyika mnamo tarehe 12 Mei 2012. Aliahidi "kufanya vita" juu ya uasi wa Tuareg katika upande wa kaskazini mwa Mali isipokuwa kama wataachia udhibiti wa miji ya kaskazini mwa Mali na kutangaza kuwa ni nchi ya Azawad.

Shambulio la Mei 2012

Tarehe 21 Mei 2012, askari waliruhusu kundi la waandamanaji wanaounga mkono mapinduzi ndani ya ofisi ya Traoré katika mji wa Bamako. Waandamanaji, ambao walikuwa wamebeba jeneza likiwa limeandikwa kimasikhara jina la Traoré juu yake, wakamshambuliwa, hadi akapoteza fahamu. Alipelekwa katika Hospitali ya Point G lakini hakuwa na fahamu wakati akipelekwa hapo, inaonekana alikwa anaosumbuliwa na majeraha ya kichwa. Waandamanaji watatu waliuawa na wengine kujeruhiwa wakati wana usalama wa Traoré walipowafyatulia risasi.

Makala haya yameandaliwa na Bishop Hiluka kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari vya kimataifa.

FRANCOIS HOLLANDE: Japo ilionekana kuwa ni safari ndefu hatimaye katua Ikulu

Francois Hollande


PARIS,
Ufaransa

TAREHE 6 Mei 2012, Ufaransa imempata rais mpya kupitia chama cha kisoshalisti, Francois Hollande, ambaye amemshinda rais aliyekuwa madarakani akitarajia kupata kipindi kingine cha uongozi, Nicolas Sarkozy, katika uchaguzi wa marudio uliofanyika mwishoni wa juma lililopita.

Hollande anakuwa rais wa kwanza wa kisoshalisti nchini Ufaransa kwa kipindi cha miaka 17; na amekuwa wa kwanza kumshinda rais aliyetumika kwa muhula mmoja tu, tangu mwaka wa 1981.

Wasoshalisti wanasema kazi ya mwanzo ni kufanya majadiliano tena juu ya sera za kiuchumi za Umoja wa Ulaya. Punde baada ya kura za awali kuonesha matokeo, Rais Sarkozy alikiri kuwa ameshindwa, na alimpigia simu Hollande kumtakia heri.

Historia yake

François Gérard Georges Hollande alizaliwa Agosti 12, 1954. Aliwahi kuwa katibu wa kwanza wa chama cha Socialist cha Ufaransa kuanzia 1997 hadi 2008 na Naibu wa Bunge la Ufaransa wa Jimbo la Corrèze 1 tangu mwaka 1997, na hapo awali aliwakilisha kiti cha ubunge kuanzia 1988 hadi 1993. Alikuwa Meya wa jiji la Tulle kuanzia mwaka 2001 hadi 2008, na alikuwa Rais wa Baraza Kuu la Corrèze kuanzia 2008 hadi 2012.

Maisha ya awali

Hollande alizaliwa katika eneo la Rouen, Seine-Maritime, Upper Normandy, katika familia ya kati. Mama yake, Nicole Frédérique Marguerite Tribert (1927-2009), alikuwa mfanyakazi wa jamii, na baba yake, Georges Gustave Hollande, alikuwa daktari wa koo, pua na masikio ambaye "aliwahi mara moja kugombea katika siasa za mitaa". Ubini wa "Hollande" "unaaminika kutoka kwa mababu waliotoroka Holland (Netherlands) katika karne ya 16 na kuchukua jina la nchi yao ya zamani." Hollande alilelewa katika dhehebu la Katoliki.

Elimu

Alisoma katika shule ya Saint Jean-Baptiste de La Salle, baadaye HEC Paris, shule ya utawala ya École, na Taasisi ya Mafunzo ya Siasa ya Paris. Alimaliza mwaka 1980. Aliishi nchini Marekani katika majira ya joto ya 1974 alipokuwa mwanafunzi wa chuo kikuu. Mara baada ya kuhitimu, alifanya kazi kama Diwani wa Mahakama ya Ukaguzi.

Kazi za mwanzo za kisiasa

Baada ya kazi za kujitolea kama mwanafunzi, François Mitterrand hatimaye alishindwa katika kampeni za uchaguzi wa rais 1974, Hollande alijiunga na Chama cha Kisosholisti miaka mitano baadaye. Haraka alionwa na Jacques Attali, mshauri mwandamizi wa Mitterrand, ambaye alipanga Hollande agombee katika uchaguzi wa Bunge la Taifa la Ufaransa mwaka 1981 katika jimbo la Corrèze dhidi ya aliyekuja kuwa rais, Jacques Chirac.

Hollande alishindwa na Chirac katika raundi ya kwanza, ingawa baadaye alikuwa Mshauri Maalum wa Rais mpya Mitterrand, kabla ya kufanya kazi chini ya Max Gallo, msemaji wa serikali. Baada ya kuwa Diwani wa Manispaa wa Ussel mwaka 1983, aligombea katika jimbo la Corrèze kwa mara ya pili mwaka 1988, wakati huu alichaguliwa kuingia katika Bunge.

Katibu wa kwanza wa Chama cha Kisosholisti

Mwisho wa kipindi cha Mitterrand madarakani ulivyokaribia, Chama cha Kisoshalisti kilipasuka kutokana na mapambano ya makundi ndani ya chama, kila kundi likitaka kushawishi mwelekeo wa chama. Hollande aliomba upatanisho ili chama kiungane nyuma ya Jacques Delors, Rais wa Tume ya Ulaya, lakini Delors alitangaza nia yake ya kugombea Urais wa Ufaransa mwaka 1995, na kusababisha Lionel Jospin kuanza upya mbio za uongozi wa chama.

Jospin alimchagua Hollande kuwa msemaji rasmi wa chama, na Hollande akagombea katika jimbo la Corrèze kwa mara nyingine tena mwaka 1997, alifanikiwa kurudi katika Bunge. Mwaka huo, Jospin akawa Waziri Mkuu wa Ufaransa, na Hollande akashinda na kuwa Katibu wa Kwanza wa chama cha Socialist wa Ufaransa, nafasi ambayo alishikilia kwa miaka kumi na moja. Kwa sababu ya nafasi kubwa sana ya Chama cha kisoshalisti ndani ya Serikali ya Ufaransa wakati wa kipindi hiki, nafasi ya Hollande iliwafanya baadhi kumuona kama "Makamu wa Waziri Mkuu". Hollande alichaguliwa kuwa Meya wa Tulle mwaka 2001, alishikilia nafasi hiyo kwa miaka saba.

Kujiuzulu mara moja kwa Jospin katika siasa kufuatia mshtuko wake wa kushindwa na mgombea Jean-Marie Le Pen katika raundi ya kwanza ya uchaguzi wa rais mwaka 2002 kulimlazimisha Hollande kutizamwa na umma wa chama kwa uchaguzi wa 2002 wa wabunge, ingawa aliweza kuzuia kushindwa na alichaguliwa tena katika jimbo lake mwenyewe, Chama cha Kisoshalisti kiliopoteza ushindi kitaifa.

Ili kujiandaa kwa Mkutano wa Chama mwaka 2003 katika eneo la Dijon, alipata msaada wa watu wengi mashuhuri wa chama na alichaguliwa tena kuwa Katibu wa Kwanza dhidi ya upinzani kutoka mrengo wa kushoto. Baada ya ushindi wa kushoto katika uchaguzi wa mwaka 2004 wa kikanda, Hollande alitajwa kuwa mgombea urais, lakini chama cha kisoshalisti kiligawanyika kuhusu Katiba ya Ulaya, na nguvu ya Hollande kwa nafasi ya "ndiyo" katika kura ya maoni ya Ufaransa kwa Katiba ya Ulaya iliyosababisha msuguano ndani ya chama. Ingawa Hollande alichaguliwa tena kama Katibu wa kwanza katika mkutano wa Le Mans mwaka 2005, mamlaka yake kwenye chama yalianza kushuka.

Hatimaye mwenzi wake wa ndani, Segolene Royal, alichaguliwa kuwakilisha Chama cha Kisosholisti katika uchaguzi wa rais wa 2007, ambapo alipoteza kwa Nicolas Sarkozy. Hollande alilaumiwa sana kwa kushindwa kwa Chama cha Kisoshalisti katika uchaguzi wa 2007, na alitangaza kuwa hatagombea mhula mwingine kama Katibu wa Kwanza. Hollande alitangaza hadharani kumuunga mkono Bertrand Delanoë, Meya wa Paris, ingawa ni Martine Aubry aliyefanikiwa kushinda mwaka 2008.

Kufuatia kujiuzulu kwake kama Katibu Kwanza, Hollande mara moja alichaguliwa kuchukua nafasi ya Jean-Pierre Dupont kama Rais wa Baraza Kuu la Corrèze mwezi Aprili 2008, nafasi aliyoishika hadi anachaguliwa kuwa rais.

Kufuatia kuchaguliwa kwake tena kama Rais wa Baraza Kuu la Corrèze Machi 2011, Hollande alitangaza kwamba atagombea katika uchaguzi ujao wa awali kuchagua mgombea wa chama cha kisoshalisti wa urais. Kufuatia kukamatwa kwa Strauss-Kahn kwa tuhuma za unyanyasaji wa kijinsia jijini New York Mei 2011, Hollande alionekana kuanza kuongoza kura ya maoni. Nafasi yake kama mgombea ilianzishwa na Strauss-Kahn aliposema hatatafuta nafasi ya uteuzi katika kinyang’anyiro hicho. Baada ya mfululizo wa mijadala mwezi wote wa Septemba, Hollande aliongoza katika kura katika duru ya kwanza iliyofanyika Oktoba 9 kwa asilimia 39 ya kura, dhidi ya Martine Aubry, aliyekuwa wa pili kwa asilimia 30 ya kura.

Uchaguzi wa pili ulifanyika Oktoba 16, 2011. Hollande alishinda kwa asilimia 56 ya kura kwa 43 za Aubry na hivyo akawa mgombea rasmi wa chama cha kisoshalisti wa urais kwa mwaka 2012. Baada ya matokeo ya awali, aliungwa mkono mara moja na wagombea wengine wa chama kwa ajili ya uteuzi, ikiwa ni pamoja na Aubry, Arnaud Montebourg, Manuel Valls na mgombea wa 2007, Segolene Royal.

Kampeni za urais za Hollande zilisimamiwa na Pierre Moscovici na Stéphane Le foll, Mbunge ambaye pia ni Mbunge wa Ulaya. Hollande alizindua kampeni zake rasmi na mkutano wa hadhara na hotuba kubwa katika eneo la Le Bourget Januari 22, 2012, mbele ya watu 25,000.

Tarehe 26 Januari iliainisha orodha kamili ya sera katika ilani yenye maazimio 60, ikiwa ni pamoja na mgawanyo wa shughuli za rejareja kutoka biashara za uwekezaji za kibenki; kupandisha kodi kwa makampuni makubwa, mabenki na matajiri; kutengeneza ajira za kufundisha 60,000; kurudisha umri rasmi wa kustaafu kutoka 62 hadi 60; kuanzisha ajira za ruzuku katika maeneo ya uhaba mkubwa wa ajira kwa vijana; kukuza zaidi viwanda nchini Ufaransa kwa kujenga uwekezaji wa benki za umma; kupitisha ndoa na haki za kuasili mtoto kwa wanandoa za jinsia moja, na kuwaondoa askari wa Kifaransa nchini Afghanistan mwaka 2012. Februari 9, alielezea kwa kina sera zake hasa kuhusiana na elimu katika hotuba kubwa katika eneo la Orleans.

Tarehe 15 Februari, Rais Nicolas Sarkozy alitangaza kugombea kwa awamu ya pili na ya mwisho, akikosoa vikali mapendekezo ya Hollande na kudai kuwa ataleta "maafa ya kiuchumi ndani ya siku mbili baada ya kuchukua madaraka" kama akishinda.

Katika ziara yake ya kwanza nje ya nchi kwa ajili ya kampeni zake, alitembelea Berlin, Ujerumani, Desemba 2011 kwenye mkutano wa Shirikisho wa Chama cha Kidemokrasi cha Kijamii, ambapo alikutana na Sigmar Gabriel, Peer Steinbrueck, Frank-Walter Steinmeier na Martin Schulz; pia alisafiri hadi Ubelgiji kabla ya kwenda Uingereza mwezi Februari 2012, alikokutana na kiongozi wa upinzani, Ed Miliband, na hatimaye Tunisia mwezi Mei 2012.

Duru ya kwanza ya uchaguzi wa rais ilifanyika 22 Aprili. François Hollande aliongoza kwa asilimia 28.63 ya kura, na kumkabili Nicolas Sarkozy katika duru ya pili. Katika mzunguko wa pili Jumapili iliyopita ya Mei 6, 2012, François Hollande alichaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Ufaransa kwa asilimia 51.7 ya kura.

Makala haya yameandaliwa na Bishop Hiluka kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari vya kimataifa.

MACKY SALL: Waziri mkuu wa zamani na meneja kampeni wa rais anayeingia ikulu

Macky Sall


DAKAR,
Senegal

ALIYEKUWA rais wa Senegal, Abdoulaye Wade, amekubali kushindwa na mpinzani wake, Macky Sall, katika dura ya pili ya uchaguzi wa Urais huku hirika la habari la serikali nchini Senegal likitoa habari za kukubali kwake kushindwa.

Wade alimpigia simu mpizani wake Macky Sall, na kumuambia kuwa amekubali kushindwa. Na maelfu ya wafuasi wa Macky Sall walijitokeza katika barabara za mji wa Dakar wakisherehekea ushindi wa kiongozi wao.

Miongoni mwa waliokuwa wakisherehekea ni Bi Seynabou Seck ambaye alishindwa kuficha furaha yake kwa kusema kuwa: "Niimefurahi sana, Macky bado ni kijana na tena ni mtu mpole sana na ana heshima! Kwa hakika anastahili ushindi huu. Kila mtu alikuwa akimuombea ashinde”.

Mshindi huyo wa duru hiyo ya pili ya uchaguzi wa urais ameutaja ushindi wake kama muamko mpya kwa raia wa Senegal. Macky Sall aliyazungumza hayo mara tu baada ya mpinzani wake Abdoulaye Wade mwenye umri wa 85 kukubali kuwa ameshindwa katika duru hiyo ya pili.

Wade alikuwa anataka kuchaguliwa tena kama raia wa Senegal kwa muhula mwengine wa tatu baada ya kubadilisha katiba ya nchi hiyo. Mabadiliko hayo yalizua machafuko na vurugu kubwa nchini humo.

Machafuko hayo yalishtua ulimwengu kwani tofauti na jirani zake Senegali imekuwa tulivu na haijawahi kuwa na mapinduzi ya kijeshi kama jirani zake. Lakini upinzani ulipinga hatua ya kiongozi wao mkongwe na kwenda mahakamani. Hata hivyo, mahakama iliidhinisha hatua ya Wade ya kubadili katiba ili aweze kusimama tena kama rais.

Na baada ya duru ya kwanza kukosa kuwa na mshindi wa moja kwa moja kwani hakuna aliyepata zaidi ya asilimia 50, ikiwa ni lazima kuwe na duru ya pili ambapo viongozi wote wa upinzani walimuunga mkoni Macky Sall.

Na sasa Macky Sall ambaye zamani alikuwa Waziri mkuu katika serikali ya Abdoulaye Wade ameibuka mshindi.

Historia yake

Macky Sall amezaliwa 11 Desemba 1961. Anatarajiwa kuapishwa rasmi kuwa rais keshokutwa, Jumapili tarehe 1 Aprili 2012. Aliwahi kuwa Waziri Mkuu wa Senegal kuanzia Aprili 2004 hadi Juni 2007 na alikuwa Rais wa Bunge la Senegal kuanzia Juni 2007 hadi Novemba 2008. Alikuwa Meya wa Fatick kuanzia 2002 hadi 2008 na kushikilia tena nafasi hiyo tangu Aprili 2009.

Sall alikuwa mwanachama wa muda mrefu wa chama kilichotawala cha Senegal Democratic Party (PDS). Baada ya kuingia katika mgogoro na Rais Abdoulaye Wade, aliondolewa kutoka katika wadhifa wake kama Rais wa Bunge mwezi Novemba 2008, hivyo alianzisha chama chake mwenyewe na kujiunga na upinzani. Amejitokeza kuwa Rais wa Senegal tarehe 25 Machi 2012 baada ya kuishinda tawala katika uchaguzi wa marudio.

Sall, mhandisi wa jiolojia ki taaluma, alizaliwa katika eneo la Fatick. Alikuwa Katibu Mkuu wa PDS wa Mkoa wa Fatick mwaka 1998 na aliwahi kuwa Katibu wa Taifa wa PDS mkuu wa Madini na Viwanda. Alikuwa Mshauri Maalum wa Nishati na Madini kwa Rais Abdoulaye Wade kuanzia Aprili 6, 2000 hadi Mei 12, 2001, pamoja na kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Mafuta ya Senegal (PETROSEN) kuanzia Desemba 13, 2000 hadi Julai 5, 2001. Kisha akawa Waziri wa Madini, Nishati na Hydraulics mnamo Mei 12, 2001, na alipandishwa cheo na kuwa Waziri wa Nchi, lakini akiendelea na nafasi yake nyingine, tarehe 6 Novemba, 2002. Pia alikuwa Meya wa Fatick Juni 1, 2002.

Mnamo Agosti 27, 2003, Sall alihamishwa kutoka nafasi yake kama Waziri wa Nchi anayeshughulikia pia Madini, Nishati na Hydraulics na kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani na Jumuiya za Mitaa, wakati pia akiwa msemaji wa serikali. Kisha aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu na Rais Wade Aprili 21, 2004, wakati mtangulizi wake, Idrissa Seck, alipofukuzwa. Aprili 25, 2004, Seck akawa Makamu wa Rais wa PDS wa kamati ya uendeshaji.

Sall aliwahi kuwa mkurugenzi wa kampeni za Wade wakati wa uchaguzi katika uchaguzi wa rais wa Februari mwaka 2007, ambao Wade alishinda, akipata wingi wa kura katika raundi ya kwanza tu. Baada ya Wade kuapishwa, Sall aliwasilisha hati ya kujiuzulu kwake Aprili 10 na mara moja aliteuliwa tena.

Rais wa Bunge

Katika uchaguzi wa wabunge wa Juni 2007, Sall alichaguliwa kwenye Bunge kama mgombea katika orodha ya taifa ya Muungano wa Sopi. Baada ya uchaguzi, Wade alimteua kuwa Cheikh Hadjibou Soumaré kuwa Waziri Mkuu wa Juni 19, akichukua nafasi ya Sall, ambaye alikuwa amejiuzulu pamoja na serikali yake muda mfupi kabla. Sall alisema kuwa aliona fahari kwa kile alichokifanya wakati akiwa Waziri Mkuu.

Sall alichaguliwa kuwa Rais wa Bunge siku moja baadaye, mnamo Juni 20, 2007, alikuwa mgombea pekee na alipata kura 143 kutoka kwa manaibu 146 ya sasa. Sall na Wade wakaingia katika migogoro baadaye mwaka 2007 wakati Sall alipomuita mtoto wa Wade Karim, Rais wa Wakala wa Taifa wa Shirika la Kiislam (OIC), kwa ajili ya kusikilizwa katika Bunge kuhusu maeneo ya ujenzi jijini Dakar kwa Mkutano wa OIC uliopangwa kufanyika huko Machi 2008. Hii ilichukuliwa kama jaribio la Sall kutaka kudhoofisha nafasi ya Karim na uwezekano wa kushawishi ili kujijengea nafsi yake ya kuwania urais, kuchochea uadui wa Wade na wafuasi wake ndani ya PDS.

Mnamo Novemba 2007, Kamati ya Uendeshaji ya PDS iliifutwa nafasi ya Sall ya Naibu Katibu Mkuu, ambayo ilikuwa ya pili kwa madaraka katika chama, na hivyo kamati hiyo iliamua kuwasilisha muswada katika Bunge ambao uliomba kupunguza muda wa Rais wa Bunge wa kutoka miaka mitano hadi mwaka mmoja. Kufuatia kifo cha kiongozi wa kidini wa Mourides, Serigne Saliou Mbacké, mwishoni mwa Desemba 2007, mrithi wake, Serigne Mouhamadou Lamine Bara Mbacké, alimuomba Wade kumsamehe Sall; Wade baadaye alikutana na Sall na wawili walisemekana kupatana mwanzoni mwa Januari 2008.

Sall alibaki katika msuguano na uongozi wa PDS mwaka 2008.  Mwezi Septemba 2008, naibu wa PDS aliwasilisha muswada wa kupunguza muda wa Rais wa Bunge kwa mwaka mmoja, na baadaye katika mwezi huo, Sall aliitwa mbele ya Kamati ya Nidhamu ya PDS, ingawa hakujitokeza. Kwa jambo hili, Sall alishitakiwa kwa mipango binafsi ya kuleta mgawanyiko ndani ya chama, pia alidaiwa kufanya "kwa lengo la kudhoofisha chama na nchi", ikimaanishwa hasa kwa ziara ya Sall kwa Seneti ya Ufaransa na Mkataba wa 2008 wa chama cha Democratic nchini Marekani. Taarifa iliyotolewa na mshauri wa Sall wa kisiasa ililaani hatua ya kumuadabisha Sall kama "jaribio la kutaka kumfilisi kisiasa".

Oktoba 13, 2008, Bunge lilipiga kura ili kupunguza muda wa Rais wa Bunge kuwa mwaka mmoja, hii ilithibitishwa na Rais Wade Oktoba 21. Pamoja na jitihada za Sall kulinda nafasi yake, Bunge lilipiga kura ya kumfukuza katika nafasi hiyo ya Rais wa Bunge Novemba 9, 2008. Kulikuwa na kura 111 zilizotaka aondolewe na 22 dhidi ya kitendo hicho. Sall mara moja alitangaza kuwa anajiuzulu katika PDS; uamuzi huu ulimaanisha kwamba alikuwa anapoteza kiti chake katika Bunge, pamoja na kiti chake katika baraza la halmashauri ya manispaa ya Fatick na wadhifa wake kama Meya wa Fatick. Pia alisema kuwa angeunda chama kipya. Seck Mamadou alichaguliwa kuchukua nafasi ya Sall kama Rais wa Bunge la Novemba 16, 2008.

Katika upinzani

Sall ilianzisha chama chake mwenyewe, Alliance for the Republic–Yaakaar, mwanzoni mwa Desemba mwaka 2008. Wizara ya Mambo ya Ndani ilimtuhumiwa Sall kujihusisha na fedha haramu Januari 26, 2009; Sall alikanusha na kusema kuwa mashtaka yalikuwa ya kisiasa. Mwishoni mwa Februari 2009 iliamuliwa kutomshitaka Sall kutokana na kukosekana kwa ushahidi.

Kufuatia uchaguzi wa Machi 2009 wa halmashauri ya Fatick, Sall alichaguliwa tena katika nafasi yake ya mwanzo ya Meya mwezi Aprili 2009.  Alipata kura 44 kutoka kwa madiwani 45 wa manispaa wa wakati huo; madiwani watano wa Muungano wa Sopi hawakuwepo kupiga kura

Kampeni ya urais wa Senegal 2012

Matokeo ya awali ya uchaguzi wa rais Februari 26, 2012 yalionesha Sall kupata asilimia 26.5 ya kura dhidi ya 34.8 za Wade, na kulazimisha kurudiwa.

Katiba na uchaguzi

Sall anapenda kurejea kwenye mipaka ya awali ya muda wa urais. Katika mzunguko wa pili wa uchaguzi wa rais, Sall alitoa wito kwa wagombea wengine wote walioshiondwa kumsaidia na kumuacha Youssou N'Dour kwa sababu aliahidi kurejesha muda wa miaka mitano kutoka muhula uliopita wa miaka saba ambao Wade alitaka urejeshwe, pia alisema atahakikisha kwamba hakuna kiongozi anaweza kubaki madarakani kwa zaidi ya vipindi viwili.

Makala haya yameandaliwa na Bishop Hiluka kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari vya kimataifa.

Hii ndiyo Dini inayoenea kwa kasi kubwa nchini Tanzania


Charles Ekerege, Mkurugenzi Mkuu wa TBS

Machinjio ya ng'ombe


BISHOP HILUKA
Dar es Salaam

MAJUZI nilikutana na dokezo moja kutoka kwa Profesa Mbele alilolitoa kwenye blogu yake, kuwa ufisadi ndiyo dini inayoenea kwa kasi nchini Tanzania. Kwangu mimi hii ilikuwa ni habari kubwa mno. Japo ilikuwa ni kama dokezo tu (fupi mno) la kawaida, lakini ilinifanya kufikiria kwa kina huku nikilinganisha na hiki kinachoendelea kutokea nchini mwetu. Kwa kifupi nakubaliana na Profesa Mbele kuhusu hilo.

Profesa Mbele aliandika hivi: “Mara kwa mara ninawasikia watu wakiongelea suala la dini inayoenea kwa kasi kuliko zote Tanzania, Afrika au duniani kwa ujumla. Kila mtu ana mtazamo wake. Wengine wanatoa pia takwimu, ambazo sijui kama ni za kweli au ndoto. Ni mchezo wa kuringiana nani zaidi kwa kutumia takwimu, wakati dini ni suala la mtu binafsi. Wala hutaingia ahera kwa msingi kuwa dini yako hapa duniani ilikuwa na wafuasi wengi kuliko dini nyingine.

“Kwa mtazamo wangu, dini inayoenea kwa kasi kuliko zote Tanzania ni ufisadi na ushirikina. Ufisadi na ushirikina huo unaendelea kushamiri kiasi kwamba unajitokeza hata kwenye nyumba za ibada za dini mbalimbali. Hebu tutafakari hilo.”

Ni maneno machache lakini yaliyobeba ujumbe mkubwa mno na unaweza kuyaelezea kwa kurasa zaidi ya elfu moja. Binafsi nadhani kuenea kwa dini (ufisadi) hii kumesababishwa na nchi hii kuitupa misingi iliyoongozwa na Azimio la Arusha, kufumbia macho vitendo vya rushwa na kukubali wafanyabiashara ambao wengi wao historia zao binafsi katika suala zima la uadilifu zinafahamika waziwazi ndani ya jamii na zimekuwa zinatiliwa shaka sana kupewa nafasi kwenye vyama vya siasa, hasa chama tawala.

Wafanyabiashara hawa wakubwa wenye kashfa mbalimbali za kuhujumu Taifa wamekuwa wakijitokeza kugombania nafasi mbalimbali za kisiasa, wanapokosa huwa wanaamua kupandikiza watu wao katika uongozi ili kuhakikisha dili zao na biashara zao zinakaa sawa.

Kinyume na ilivyokuwa katika awamu ya kwanza na kipindi cha kwanza (1985-90) cha awamu ya pili ya uongozi wa nchi hii, uongozi wa Tanzania kwa sasa si dhamana tena kama tulivyokuwa tukifundishwa shuleni kwamba 'cheo ni dhamana'. Uongozi sasa hivi umegeuka kuwa njia ya kumfanya mtu mambo yake yamnyookee, uongozi umekuwa biashara 'bab kubwa' isiyo na hasara. Zamani uongozi ulikuwa ni mzigo lakini siku hizi uongozi ni ‘kuula’ kwa maana ya dhiki kutoweka kabisa.

Kuenea kwa dini hii ni matokeo ya wimbi la wafanyabiashara kujiingiza kwenye siasa na kuviteka vyama huku wakipandikiza watu wao kwenye uongozi. Inashangaa hata pale wataalamu wa fani tofauti wanapoacha fani zao na kukimbilia kwenye siasa. Hebu fikiria maprofesa, madaktari, wahandisi, na wataalamu wa fani mbalimbali wanaacha kazi zao walizosomea na kupigania kwenda kusinzia bungeni au kwenye mikutano ya halmashauri!

Wafanyabiashara hawa wana nguvu kubwa sana ndani ya vyama na hata serikalini, ndiyo maana sasa tunashuhudia wakisamehewa kodi kila mwaka huku ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2009/10 aliyoitoa hivi karibuni ikionesha kwamba katika kipindi hicho misamaha ilifikia shilingi trilioni 1.2 (asilimia 18 ya bajeti yote ya serikali).

Kibaya zaidi, mawaziri na wabunge wetu ni miongoni mwa vigogo wanaojinufaisha na Sheria ya Msamaha wa Kodi kinyume cha taratibu. Orodha ya majina ya watu waliosamahewa kodi na Serikali katika mwaka wa fedha 2009/2010 inaonesha majina ya baadhi ya mawaziri, wabunge na wakuu wa taasisi za Serikali wakiwa wamenufaika na misamaha hiyo.

Viongozi hawa wameshiriki katika kuidhinisha shilingi bilioni 31 kununua bidhaa kwa matumizi ya Serikali pasipo kutolewa ufafanuzi, shilingi bilioni 8 kutumika bila kufuata utaratibu maalumu na shilingi milioni 143 kutumiwa na serikali kulipa mishahara kwa wafanyakazi hewa, watoro na waliostaafu! Yaliyomo kwenye ripoti hiyo yanasikitisha na kutisha sana.

Matokeo ya kushamiri kwa dini hii yamesababisha wataalamu wa wanyama, afisa afya na watendaji wa majinchio ya Vingunguti jijini Dar es Salaam kuruhusu kuletwa utumbo na nyama iliyooza na kuuzwa kwa wananchi, kitendo kilichovuka hata mipaka ya ubinadamu!

Ni nani atabisha kwamba dini hii haina nguvu na haijaenea nchini? Hata kama nchi inanuka rushwa na ufisadi, lakini ndiyo iwe kwa kiwango cha namna hii? Kwa hali ya kawaida, haihitaji kuwa msomi sana kubaini kuwa bidhaa ya kuoza kama ile italeta madhara makubwa sana kwa watu na pengine hata ndugu wa karibu wa wahusika.

Hii pia haina tofauti na ile habari Shirika la Viwango Nchini (TBS) kuruhusu bidhaa feki zitumike nchini. Tukubali au tukatae, hii ni dini inayoenea kwa kasi kutokana na kukumbatia rushwa, kuruhusu wafanyabiashara watawale mfumo wa uongozi kwa kupandikiza watu wao, na kutochukuliwa hatua thabiti kwa wanaobainika kufanya ‘madudu’.

Kushamiri kwa dini hii kumesababisha pia kuwapo habari kuwa vibali bandia 480 vimetolewa na kuidhinishwa na kigogo mmoja wa Idara ya uhamiaji mkoani Kilimanjaro. Vibali hivyo vimeisababishia Serikali hasara ya Sh 231 milioni. Serikali pia ilipata hasara ya Sh 86 milioni kutokana na vibali vingine bandia 84 vilivyokamatwa mwaka jana katika kiwanda kimoja wilayani Mwanga, huku kinara mkuu akidaiwa kuwa uraiani.

Hayo na mengine mengi yanatufanya tuamini kuwa sasa hii ndiyo dini iliyoshamiri nchini. Ni kipi kitatufanya tusiamini kuwa dini hii ndiyo inayoenea kwa kasi nchini?

ABDULLAH SENUSSI: Jasusi na shemeji wa Kanali Gaddafi anayehusishwa na uhalifu wa kivita

Abdullah Sanussi


Mauritania

TAARIFA za vyombo vya habari vya kimataifa imeikariri Serikali ya Libya kusisitiza kuwa ina uwezo wa kumfanyia kesi mkuu wa zamani wa usalama, Abdullah Sanussi, na imeomba arejeshwe nyumbani. Kumetolewa wito kuwa Sanussi apelekwe Mahakama ya Jinai ya Kimataifa, ICC, mjini Hague au Ufaransa, ambako ameshtakiwa kwa ugaidi.

Ingawa hakuna picha zilotolewa za Abdullah Sanussi tangu kuarifiwa kuwa amekamatwa nchini Mauritania, wakuu wa Libya wanasema wana hakika kuwa ametekwa, na wameomba kuwa arejeshwe nyumbani.

Mkuu huyo wa ujasusi wa Kanali Gaddafi, anakabiliwa na mashtaka kadhaa, pamoja na yale yanayohusu mauaji. Serikali ya mpito ya Libya ina hamu kuwa arejeshwe nyumbani kufikishwa mahakamani haraka.

Lakini kuna wasiwasi, kwa sababu serikali kuu ya Libya bado haina nguvu, na bado hakuna mfumo wa sheria unaoweza kufanya kesi ya al-Sanussi au viongozi wengine wa zamani wa utawala wa Gaddafi.

Ufaransa imeshasema kuwa itapenda kumpata al Sanussi kwa sababu ya kuhusika kwake na shambulio la bomu kwenye ndege ya Ufaransa mwaka wa 1989.

Pia kuna wito mwengine kuwa mwanasiasa huyo apelekwe ICC, ambako anakabiliwa na mashtaka ya kushiriki kwenye shughuli za kufyeka upinzani wa Libya mwaka jana.

Wakuu wa Mauritania bado hawakusema vipi watajibu maombi hayo, na inaweza kuchukua muda kabla ya afisa huyo kurejeshwa nyumbani - afisa aliyechukiwa na kuogopwa kabisa nchini mwake.

Historia yake

Abdullah Senussi amezaliwa tarehe 5 Desemba, mwaka 1949. Raia huyu wa Libya alikuwa mkuu wa upelelezi na shemeji wa aliyekuwa rais wa Libya, Kanali Muammar Gaddafi. Alikuwa amemuowa shemeji wa Kanali Gaddafi.

Maafisa wa polisi wa Kiskochi wana mpango wa kumhoji al-Senussi kuhusu uhusiano wake na mabomu yaliyoripua Lockerbie, wakiongeza matarajio ya kuibua kesi ya pili kuhusu shambulio la Lockerbie.

Kwa mujibu wa gazeti la The Guardian la Uigereza, al-Senussi alikuwa na sifa ya ukatili tangu miaka ya 1970. Katika miaka ya 1980 alikuwa mkuu wa usalama wa ndani nchini Libya, katika kipindi ambacho wapinzani wengi wa Gaddafi waliuawa. Baadaye, alielezewa kama mkuu wa upelelezi wa kijeshi, lakini haijawekwa wazi kama kweli aliwahi kuwa na cheo hicho.

Mwaka 1999 alikutwa na hatia wakati akiwa hayupo mahakamani nchini Ufaransa kwa kushiriki kwake katika shambulio la bomu 1989 katika ndege ya abiria iliyokuwa ikiruka Niger ambalo lilisababisha vifo vya watu 170. Walibya wanaamini kuwa hawezi kukwepa tuhuma za mauaji ya wafungwa 1,200 katika jela ya Abu Salim mwaka 1996. Pia anadhaniwa kuwa nyuma ya mauaji ya mwaka 2003 ya mrithi wa ufalme wa Saudi Arabia, Prince Abdullah.

Mtandao wa Ubalozi wa Marekani umemuelezea al-Senussi kama msiri wa Gaddafi ambaye alifanya "mipango yake mingi ya matibabu". Wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Libya vya 2011, al-Senussi alilaumiwa kwa kuchochea mauaji katika mji wa Benghazi na kuajiri mamluki wa kigeni. Aliaminika kuwa na maslahi makubwa ya kibiashara katika Libya.

Tarehe 1 Machi 2011, gazeti la Libya la Quryna lilitoa taarifa kwamba Gaddafi alimfukuza kazi al-Senussi.

Tarehe 16 Mei 2011, mwendesha mashitaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai alitangaza kuwa anatafuta kibali cha kukamatwa kwa Abdullah Senussi kwa madai ya uhalifu dhidi ya binadamu.

Tarehe 21 Julai 2011, vyanzo vya upinzani nchini Libya vilidai kuwa Senussi alikuwa ameuawa katika shambulizi lililofanywa na waasi wenye silaha katika jiji la Tripoli, hata hivyo, saa chache baadaye vyanzo hivyo kukanusha madai yao yaliyotolewa kabla na hata baadhi wakasema kuwa huenda alikuwa amejeruhiwa tu.

Tarehe 30 Agosti 2011, kulikuwa na taarifa kuwa watoto wote wawili; wa Senussi, Mohammed Abdullah al-Senussi, na wa Kanali Muammar Gaddafi, Khamis, waliuawa wakati wa mapigano na vikosi vya NATO na NTC katika eneo la Tarhuna. Mnamo mwezi Oktoba, kituo cha televisheni cha Arrai, mtandao uliokuwa ukimuunga mkono Kanali Gaddafi nchini Syria ulithibitisha kuwa Mohammed Senussi na Khamis Gaddafi walikuwa wameuawa tarehe 29 Agosti.

Tarehe 20 Oktoba, Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Niger, Mohammad Bazoum, aliliambia shirika la habari la Reuters kwamba alikuwa kakimbilia Niger. Hata hivyo, mpiganaji wa Libya baadaye aliliambia gazeti la The Guardian kwamba waasi walikuwa wanashikilia watu wengine watatu ambao walikuwa katika msafara wa Gaddafi wakati alipouawa na kwamba aliamini kuwa mmoja wao alikuwa Senussi.

Watu wengine wawili walitambuliwa kama mwana wa Gaddafi aliyeuawa, Mutassim na mmoja wa makamanda wake wa kijeshi, Mansour Dhao, ambaye alikuwa bado hai na kuthibitisha utambulisho wake, pamoja na maelezo ya kifo cha mtoto wa Gaddafi, kwa shirika la Haki za Binadamu wakati wakiwa katika hospitali hiyo; Dhao awali alidhaniwa kuwa alikuwa kakimbilia Niger.

Hata hivyo, baadaye zilisikika taarifa kwamba Senussi katoka katika maficho yake nchini Niger kumsaidia Saif al-Islam Gaddafi ili atoroke kutoka nchini Libya. Senussi aliripotiwa kuwa alitekwa nyara tarehe 20 Novemba karibu na mji wa Sabha. Baadaye ilitolewa taarifa ya kwamba angeweza kuchukuliwa hadi Tripoli kujibu mashtaka ya uhalifu dhidi ya binadamu, kwa mujibu wa Baraza la Mpito la Taifa.

Hata hivyo, mwendesha mashitaka mkuu wa ICC, Luis Moreno Ocampo, alionesha wazi kuwa na shaka kama kweli Senussi alikuwa kakamatwa. Waziri wa Ulinzi wa Libya, Osama Jweli, pia alisema kuwa hakuna ushahidi wa Senussi kuwa alikuwa katekwa. Mnamo tarehe 4 Desemba 2011, Abdullah Nakir, afisa wa Libya, alikiambia chombo cha habari cha Al Arabiya kwamba Senussi alikamatwa na alikuwa akihojiwa kuhusu kituo cha siri cha nyuklia ambacho Gaddafi alikuwa akikiendesha, lakini alikiri kwamba serikali ya Libya haikuweza kutoa picha yoyote ya yeye akiwa chini ya ulinzi.

Tarehe 17 Machi 2012, taarifa za vyombo vya habari zilisema kuwa Senussi ametiwa mbaroni katika uwanja wa ndege wa Nouakchott katika nchi ya Mauritania. Serikali ya Libya inaelezwa kutoa ombi la kumtaka al-Senussi apelekwe nchini Libya kwa mahojiano.

Makala haya yameandaliwa na Bishop Hiluka kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari vya kimataifa.

KIPSANG NA KEITANY: Wakenya wanaoitangaza vyema nchi yao katika riadha

Mary Keitany

Wilson Kipsang

LONDON,
Uingereza

WILSON Kipsang na Mary Keitany kutoka Kenya walichukua ushindi kwa kishindo katika mashindano ya Jumapili ya iliyopita katika mbio za London Marathon mwaka 2012. Katika mbio za wanaume, Kipsang aliweza kuongoza katika maili saba za mwisho, na ilikuwa nusra avunje rekodi ya mashindano ya London.

Alimaliza kwa muda usiokuwa rasmi wa saa 2:04.44. Mkenya mwenzake Martin Lel alifanikiwa kumpita mwanariadha wa Ethiopia, Tsegaye Kebede, na ambaye ameshawahi kuwa mshindi wa mashindano ya London, na kumaliza katika nafasi ya pili, ikiwa ni kasi ya juu mno katika kumalizia mashindano.

Kebede, aliyemaliza wa tatu, alifanikiwa kuwazuia Wakenya kuzoa nafasi zote tatu za mwanzo kwa upande wa mbio za wanaume, lakini kwa upande wa kina dada juhudi za Waethiopia hazikufanikiwa kwani mkenya mwingine, Mary Keitany alifanikiwa kuhifadhi ubingwa wake kwa mwaka wa pili mfululizo, kwa kushinda katika muda wa 2:18.37.

Historia ya Wilson Kipsang Kiprotich

Wilson Kipsang Kiprotich amezaliwa tarehe 15 Machi 1982. Ni mkimbiaji wa mbio ndefu, anayetoa ushindani katika mbio za kuanzia km 10 hadi marathon kamili.

Anashikilia nafasi sita kwa kasi zaidi katika mbio za nusu marathon (dakika 58:59). Nafasi yake bora katika marathoni ni saa 2:03:42 aliyoiweka mwaka 2011 katika Frankfurt Marathon iliyomfanya kuwa wa pili kwa kasi katika muda wote nyuma ya Mkenya mwenziye, Patrick Makau (aliyekimbia kwa 2:03:38). Ni mshindi mara mbili wa mashindano ya Frankfurt (2010 na 2011) na pia alishinda katika mashindano ya Lake Biwa Marathon na London Marathon (2012).

Kipsang anatoka Wilaya ya Keiyo nchini Kenya, alianza ushindani wa mbio katika Polisi, na kumaliza wa pili katika kilomita 10 za Tegla Loroupe Peace. Akaanza mbio za kimataifa mwaka 2007 na mwaka huo alichukua nafasi ya pili katika mbio za Tilburg, akiweka rekodi ya muda wa 46:27, na alishinda mbio za Hem (kwa muda wa 27:51 akiwa wa nne kwa kasi katika mbio za km 10 mwaka huo). Pia alichukua nafasi ya tatu katika michuano ya Jeshi la Polisi nchini Kenya, na kumaliza nyuma ya Richard Mateelong.

Katika mashindano Bora ya Dunia ya kilomita 10, alishika nafasi ya tatu kwa muda wa 28:09, akishindwa na Deriba Merga na Sila Kipruto.

Alirudi katika mbio za Tilburg mwaka 2008, na kumaliza tena akiwa wa pili kwa sekunde mbili tu nyuma ya mshindi, Abiyote Guta. Kilele chake kwa mwaka huo kilikuwa katika Nusu Marathon za Delhi. Kipsang alimsukuma Merga, mshindi wa World Road Champion mwaka 2006, karibu kabisa na mstari wa kumalizia lakini alimaliza wa pili nyuma yake. Pamoja na kumaliza nafasi ya pili, Kipsang alifurahishwa na ubora wake kwa zaidi ya dakika 59:16. Pia alikuwa wa tatu kwa kasi katika nusu marathon kwa kwa mwaka huo, Merga na Haile Gebrselassie wakiwa mbele yake.

Kipsang alianza kwa nguvu 2009, kwa kushinda Nusu Marathon za Egmond katika hali ya baridi. Kazi nzuri nyingine ni pale alipotwaa nafasi ya pili katika mbio za Nusu Marathoni za Ras Al Khaimah - muda wake ni 58:59 uliomfanya kushika nafasi ya pili na akawa wa nne kukimbia chini ya dakika 59. Pamoja na kuwa bora mwaka 2009 katika Nusu Marathon ya Berlin, aliishia katika nafasi ya tatu ambayo ilikuwa ni mara ya kwanza, ambapo wakimbiaji wote wanne wa juu kumaliza chini ya saa moja.

Alishiriki katika mashindano ya World 10k ya Bangalore Mei 2009, na kumaliza wa nne. Alimaliza wa kwanza katika Nusu Marathoni ya Mabingwa ya IAAF mwishoni mwa mwaka huo, na kuchukua nafasi ya nne kwa muda wa 01:00:08.

Mwaka 2010 alishiriki mara ya kwanza katika mbio za Marathoni za Paris mnamo Aprili 2010, na alishika nafasi ya tatu katika muda wa saa 2:07:13, nusu dakika nyuma ya mshindi, Tadesse Tola. Alishinda katika marathoni za Frankfurt mwezi Oktoba katika rekodi mpya ya saa 02:04:57, akimshinda Tadesse kwa zaidi ya dakika. Ubora wake mpya ulimfanya kuwa wa nane kwa kasi katika muda wote. Alishinda mbio zake za tatu za Lake Biwa Marathon mwaka 2011, akimshinda Deriba Merga katika rekodi ya saa 2:06:13. Alitetea taji lake katika mbio za Frankfurt, alijitokeza ndani ya sekunde nne, kabla ya kuvuka mstari wa mwisho kwa saa 2:03:42, na kuwa mtu wa pili kwa kasi katika marathon kwa muda wote.

Mwaka 2012 alianza na kumaliza katika nafasi ya tatu katika mbio za Nusu Marathoni za RAK.

Historia ya Mary Jepkosgei Keitany

Mary Jepkosgei Keitany amezaliwa Januari 17, 1982 katika eneo la Kisok, wilaya ya Baringo. Ni mwanariadha kutoka Kenya wa mbio ndefu. Alishinda medali ya fedha mwaka 2007 katika Mbio za Dunia za Mabingwa za IAAF na akawa bingwa wa dunia katika Nusu Marathon miaka miwili baadaye. Alishinda mbio za London Marathon za 2011 kwa saa 2:19:19 zikimfanya kuwa wa nne kwa kasi kwa upande wa wanawake katika muda wote.

Rekodi yake ya muda wa saa 1:05:50 katika mbio za nusu marathoni ndiyo rekodi ya dunia kwa wanawake. Pia anashikilia rekodi ya dunia katika maili 10 kwa wanawake (dakika 50:05), kilomita 20 (62:36), na km 25 (1:19:53).

Alianza kushiriki mbio alipokuwa shule ya msingi. Mwaka 2002, alijiunga na Hidden Talent Academy. Januari 2006 alikuwa katika nafasi ya 21 katika mbio zake za kwanza (Mbio za Wanawake za Shoe4Africa, baada ya mafanikio kadhaa katika mashindano ya kitaifa, alishiriki nje ya nchi kwa mara ya kwanza, akashinda katika baadhi ya mbio za barabarani barani Ulaya).

Alishinda medali ya fedha katika Mbio za Mabingwa za Dunia za IAAF mwaka 2007, akimaliza wa pili nyuma ya Lornah Kiplagat aliyevunja rekodi ya dunia. Ameolewa na Mkenya mwenzake mwanamichezo, Charles Koech, mwishoni mwa mwaka 2007 na walipata mtoto, Jared Kipchumba 2008. Baada ya mwaka kuwa nje, alirudi katika mashindano ya Dunia ya 10k Bangalore Mei 2009. Alimaliza wa pili nyuma ya mshindi, Aselefech Mergia, lakini akaweka rekodi mpya ya ubora ya 32:09 katika km 10. Septemba mwaka huo, alimaliza kwa 1:07:00 katika mashindano ya 2009 ya Nusu Marathoni ya Lille, ambayo ilikuwa ni alama ya ushindi na akawa wa saba kwa kasi katika muda wote.

Mashindano ya Lille ilimaanisha kuwa alifuzu kwa Mashindano ya Dunia ya Mabingwa ya Nusu Marathoni ya IAAF 2009 mjini Birmingham. Alimshinda Aberu Kebede katika ushindi wake wa kwanza wa michuano ya Dunia, akaweka rekodi mpya ya ubora ya saa 1:06:36 na kuvunja rekodi ya michuano. Pia alichukua medali ya dhahabu ya pili kama sehemu ya kikosi cha ushindi cha Kenya katika mashindano ya timu. Muda wake wa km 15 wa dakika 46:51, ni bora zaidi kuliko rekodi ya dunia iliyowekwa na Kayoko Fukushi wa Japan ya 46:55. Muda wake ulikuwa wa pili kwa kasi kwa muda wote katika nusu marathon (baada ya Lornah Kiplagat) na mkurugenzi wa New York City Marathon, Maria Wittenberg, alitabiri kwamba Keitany anaweza kuwa bora ulimwenguni katika marathon katika miaka ijayo. Nusu marathon ilikuwa rekodi mpya ya Afrika, rekodi ya awali ya saa 1:06:44, iliwekwa na Elana Meyer wa Afrika Kusini mwaka 1999. Pia aliishinda rekodi ya bingwa aliyemtangulia wa Kenya ya saa 1:06:48 aliyoiweka huko Udine miaka miwili kabla.

Alishinda mbio za 2010 za Nusu Marathon za Abu Dhabi. Pia alishinda mbio za 2010 za Berlin 25K, akiweka rekodi mpya ya dunia kwa saa 01:19:53. Rekodi ya awali ilikuwa inashikiliwa na Mizuki Noguchi wa Japan tangu mwaka 2005. Alitumia mbio za Nusu Marathon za Ureno mwezi Septemba kama maandalizi kwa mbio za New York na kuongoza kuanzia mwanzo na kushinda kwa muda wa saa 1:08:46. Katika ukimbiaji wake wa kwanza katika Marathon za 2010 NYC alikuwa miongoni mwa watu watatu walioongoza lakini alishindwa katika hatua za mwisho kukamilisha katika saa 2:29:01 na kushika nafasi ya tatu.

Keitany aliuanza 2011 kwa kuvunja rekodi aliposhinda Nusu Marathon za Ras Al Khaimah na kuweka rekodi ya dunia ya 01:05:50. Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa mwanamke kukimbia kwa chini ya dakika 66 na kuweka rekodi kadhaa zingine baadaye, ikiwa ni pamoja na rekodi ya dunia ya 1:02:36 kwa km 20 na ile ya km 8 na maili 10. Kisha alishinda katika marathoni za 2011 za London katika muda wa saa 02:19:17, na kuwa wa nne kwa kasi katika muda wote kwa wanawake. Alishinda kwa mara ya pili katika mbio za Nusu Marathoni za Ureno na kuboresha rekodi yake mwenyewe kwa saa 1:07:54.

Alikusudia kuboresha rekodi yake ya dunia ya Nusu Marathoni ya 2012 RAK, lakini hali ya upepo ilimfanya kutumia muda wa saa 1:06:49 akishinda kwa muda zaidi kuliko mwaka uliopita.

Makala haya yameandaliwa na Bishop Hiluka kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari.