Feb 15, 2012

BASHAR AL-ASSAD: Sasa akalia kuti kavu nchini Syria

Rais wa Syria, Bashar al-Assad

DAMASCUS

Syria



MUUNGANO wa nchi za Kiarabu unaendelea kutoa wito kwa Assad kukabidhi madaraka kwa naibu wake ambaye ataunda serikali ya muungano wa kitaifa na sasa unaungwa mkono na Marekani, Uingereza na Ufaransa. Lakini Moscow imesema kuwa mpango huo "hauna usawa" na "utatoa mwanya'' wa uingiliaji wa masuala ya ndani ya Syria.



Marekani imetoa wito kwa mataifa yote kutoa msimamo wao kuhusiana na kile ilichokitaja kuwa udhalimu serikali ya Syria. Imesema kuwa mataifa ya kirafiki yanayoitakia Syria utawala wa Kidemokrasia yanapaswa kuungana katika kumshutumu kiongozi wa taifa hilo Rais Assad. Waziri wa mashauri ya Kigeni wa Marekani, Hillary Clinton, alisema ni jambo la kusikitisha kuwa Urusi na China zilipiga kura za turufu kupinga azimio la kuikosoa Syria katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.



Alitoa wito kwa jamii ya kimataifa iunge mkono makundi ya upinzani nchini Syria. Ni wazi kwamba Marekani pamoja na wanadiplomasia wa mataifa mengine ya Magharibi wameghadhabishwa mno na hatua ya Urusi na China kupinga azimio la kuikosoa Syria.



Clinton alizungumza akiwa Bulgaria ambako amesema Marekani pamoja na mataifa mengine zitashinikiza Rais Assad aondoke madarakani. Alizungumzia kuhusu kuwekwa vikwazo zaidi pamoja na kuwataja watu ambao wanafadhili na kuipa silaha serikali ya Syria.



Mataifa ya magharibi yanajiandaa kupigia debe azimio kali kwenye mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusiana na mgogoro uliopo nchini Syria. Katibu mkuu wa muungano wa Mataifa ya Kiarabu Nabil al-Arabi anatarajiwa kutoa ombi kwa Baraza la Usalama kuunga mkono mpango mpya wa muungano huo unaotaka rais wa Syria Bashar al-Assad ajiuzulu.



Historia ya Assad



Bashar al-Assad alizaliwa Septemba 11, 1965, mbai na urais pia ni Katibu wa Mkoa wa Chama cha Ba'ath.  Baba yake Hafez al-Assad alitawala Syria kwa miaka 29 hadi kifo chake mwaka 2000. Al-Assad alichaguliwa mwaka 2000, na kuchaguliwa tena mwaka 2007, bila kupingwa.



Maisha ya awali



Bashar al-Assad alizaliwa katika Dameski, ni mtoto wa Aniseh (nee Makhluf) na Hafez al-Assad. Nyumba aliyokulia ilikuwa na vuguvugu la siasa chini ya kivuli cha baba yake, Hafez Assad, ambaye alichukua madaraka ya urais wa Syria katika Mapinduzi ya 1970. Tofauti na ndugu zake, Basil na Maher, dada zake Bushra, Bashar, alikuwa kimya na hakupenda siasa au kazi ya kijeshi.



Alipata elimu yake ya msingi na sekondari katika shule ya mchepuo wa Kiarabu-Kifaransa ya al-Hurriya, Damascus na alikuwa mwanafunzi mfano bora aliyefanya vizuri sana kimasomo. Mwaka 1982, alihitimu shule ya sekondari na kwenda kusomea tiba katika Chuo Kikuu cha Damascus. Mwaka 1988, Bashar Assad alihitimu masomo ya tiba na kufanya kazi kama daktari katika hospitali kubwa ya kijeshi, "Tishrin", nje kidogo ya Damascus.



Miaka minne baadaye, alikwenda Uingereza kuanza mafunzo ya Udaktari bingwa wa macho (Ophthalmology) katika Western Eye Hospital, sehemu ya makampuni ya mafunzo ya St Mary jijini London. Wakati huo Bashar hakuwa na matarajio ya kisiasa. Baba yake alimwandaa kaka wa Bashar, Basil al-Assad, kuwa rais wa baadaye. Hata hivyo, Bashar aliitwa mwaka 1994 kujiunga na jeshi, baada ya kifo cha Basil kisichotarajiwa katika ajali ya gari.



Kifo cha Basil



Muda mfupi baada ya kifo cha Basil, Hafez Assad alifanya uamuzi wa kumfanya Bashar kuwa mrithi wake mpya. Katika kipindi cha miaka sita na nusu iliyofuata, hadi kifo chake mwaka 2000, Hafez aliandaa utaratibu kwa ajili ya Bashar kuchukua madaraka. Maandalizi kwa ajili ya kipindi cha mpito yalifanywa katika ngazi tatu. Kwanza, alijengwa ndani ya jeshi na vyombo vya usalama. Pili, picha ya Bashar ilijengwa ili afahamike zaidi kwa umma. Na mwisho, Bashar alifanywa kuzoea taratibu za kuendesha nchi kabla.



Kupata sifa ya kijeshi, mwaka 1994 Bashar alijiunga katika chuo cha kijeshi cha Homs, Kaskazini mwa Dameski, na alipitia safu haraka hadi nafasi ya Kanali Januari 1999. Ili kuandaa msingi imara kwa Bashar katika jeshi, makamanda wakongwe walitakiwa kustaafu, na damu changa, maafisa vijana watiifu kwake walichukua nafasi zao. Sambamba na kazi yake ya kijeshi, Bashar alishiriki katika masuala ya umma. Alipewa mamlaka makubwa na akawa mshauri wa kisiasa kwa Rais Hafez al-Assad, mkuu wa ofisi ya kupokea malalamiko ya rufaa ya wananchi, na aliongoza kampeni dhidi ya rushwa. Kama mkuu wa kampeni dhidi ya rushwa, Bashar alipata uwezo wa kuondoa wapinzani wake wenye uwezekano wa kuwania urais.



Mwaka 1998, Bashar alichukua mamlaka ya faili la masuala ya Syria-Lebanon, ambalo lilikuwa linashikiliwa na aliyekuwa Makamu wa Rais, Abdul Khaddam tangu miaka ya 1970, mmoja wa viongozi wachache wa Sunni katika serikali ya Assad, ambaye hadi wakati huo alikuwa na uwezekano wa kuwa rais. Kwa kuchukua mamlaka ya masuala ya Syria nchini Lebanon, Bashar alikuwa na uwezo wa kushinikiza Khaddam akae kando na kusimika nguvu zake katika Lebanon.



Katika mwaka huo huo baada ya mashauriano madogo na wanasiasa wa Lebanon, Bashar alimweka Emile Lahoud, mshirika wake mwaminifu, kama Rais wa Lebanon na kumuweka kando Waziri Mkuu wa zamani wa Lebanon, Rafic Hariri, kwa kutolipa uzito jina lake katika nafasi ya waziri mkuu. Ili kudhoofisha zaidi mkakati wa zamani wa Syria nchini Lebanon, Bashar alimbadilisha balozi wa mrefu wa Syria nchini Lebanon, Ghazi Kanaan, na mshirika mwaminifu, Rustum Ghazali. Chini ya Bashar, rushwa ya Syria nchini Lebanon, ambayo tayari ilikuwa inakadiriwa kufikia dola bilioni 2.0 kwa mwaka katika miaka ya 1990, na kushindwa kudhibitiwa kulikosababisha kuanguka kwa benki ya Lebanon Al-Madina mwaka 2003.



Al-Madina ilitumiwa kuchukua fedha katika michezo ya kubahatisha (kamari) kinyume cha sheria ya mpango wa Umoja wa Mataifa wa mafuta-kwa-chakula nchini Iraq. Vyanzo vilisema kuwa kiasi kilichohamishwa kwa njia ya benki ya al-Madina ni zaidi ya dola 1 bilioni, na asilimia 25 kwenda kwa viongozi wa Syria na washirika wao wa Lebanon, miongoni mwa wapokeaji wa fedha hizi alikuwa ndugu wa Bashar Assad, Maher, mkwe wa Emile Lahoud, Elias Murr, na Ghazali.



Urais



Wakati Assad mkubwa alipokufa mwaka 2000, Bashar aliteuliwa kuwa kiongozi wa chama cha Ba'ath na Jeshi, na alichaguliwa kuwa rais bila kupingwa katika kile serikali ilichodai kuwa kuungwa mkono kwa wingi (asilimia 97.2 ya kura), baada ya Al Majlis Sha'ab (Bunge) kupunguza umri wa chini kwa mtu anayetaka kugombea kutoka 40 hadi 34 (umri Assad alipochaguliwa). Mei 27, 2007, Bashar alipitishwa tena kuwa rais kwa kipindi kingine cha miaka saba, pamoja na matokeo rasmi ya asilimia 97.6 ya kura katika kura ya maoni bila ya mgombea mwingine.



Katika sera yake ya ndani, amekuwa akikosolewa kwa kupuuza haki za binadamu, kushuka kwa uchumi, na rushwa. Katika sera zake za kigeni, Al-Assad ni mkosoaji mkubwa wa Marekani na Israeli. Chama cha Ba'ath kinabakia katika udhibiti wa bunge, na kikatiba ni "chama kinachoongoza" serikali.



Hadi anakuwa rais, Bashar al-Assad hakuwa akishiriki sana katika siasa; jukumu lake kwa umma lilikuwa ukuu wa Chama cha Kompyuta cha Syria, ambacho kilianzisha huduma ya Internet nchini Syria mwaka 2001. Al-Assad alithibitishwa kuwa rais kwa kura ya maoni bila kupingwa mwaka 2000.



Alitarajiwa kufuata njia huru zaidi kuliko baba yake. Katika mahojiano alisema kuwa aliona demokrasia nchini Syria kama 'chombo cha maisha bora' lakini baadaye alisema kuwa itachukua muda kwa demokrasia kukomaa na kwamba isiharakishwe.



Kisiasa na kiuchumi, maisha ya raia wa Syria yamebadilika kidogo tangu mwaka 2000. Mara baada ya kuchukua madaraka harakati za mageuzi zimefanywa kwa tahadhari katika Dameski, ambayo yalisababisha al-Assad kufunga gereza la Mezzeh na mamia ya wafungwa wa kisiasa kutolewa.



Makala haya yameandaliwa na Bishop Hiluka kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari vya kimataifa.

Kwa kudharau Kiswahili tutaendelea kuwa wasindikizaji

Mwalimu Julius Nyerere, alikipigania Kiswahili ambacho kwa sasa kinapuuzwa

BISHOP HILUKA
Dar es Salaam

“VIONGOZI wamekuwa wakitupiga fiksi miaka yoote, ooh Kiswahili lugha ya taifa, ooh tujivunie Kiswahili, ooh tukienzi… Haya sasa nimejifunza Kiswahili kwa bidii na cheti nimekipata. Nakaa nasubiri kazi, matangazo yote kwenye magazeti yetu yanatoka kwa Kimombo. Kina fulani wanapata kazi, mimi naambiwa …we need English!...” Kijana mmoja anawaeleza wenzake walipokuwa kijiweni.

“Acha mambo yako, Wabongo ndivyo mlivyo, mnapenda kulalamika wakati nyinyi wenyewe hamtaki hata kujishughulisha! Nafasi zipo lakini hamzitumii matokeo yake mnalalamikia Kiswahili, kinahusiana nini na hayo?” kijana mwingine anaingilia kati.

“Hivi wewe uko nchi gani?” anajibu kwa ghadhabu yule kijana wa kwanza, “Tujishughulishe vipi? Ina maana huoni kinachoendelea nchini? Wamekuwa wanatuongopea eti Kiswahili ndiyo lugha ya taifa wakati wao wanapeleka watoto wao Ulaya na kwenye shule za English Medium, si hivyo tu hata tenda zote nzito nzito kwenye magazeti zinaandikwa kwa Kiingereza. Nasikia hata Kanumba alipokwenda kule Big Brother alienda huku akiwa anajivunia lugha yake ya Kiswahili, unajua nini kilichotokea? Akaambiwa …we need English”

“Kweli bradha, Watanzania sasa tumeshtuka, tena tumeshtuka ile mbaya. Hizi fiksi tumegundua zinatulostisha kabisa. Wengi wameshtuka sasa, ndiyo maana hata huku Uswahilini sasa hivi shule zenye majina kama Tujitegemee, Tuungane, Umoja au Mwongozo huzikuti. Na ukizikuta ujue hazina tena soko. Usishangae siku hizi kusikia shule kama Santa Paul ya Manzese, New World Academy ya Gongolamboto, Galaxy International School ya Kiwalani na nyingine kibao… tumeshtuka!” Alidakia kijana mwingine.

Haya ni baadhi ya mazungumzo kwenye kijiwe kimoja huku mtaani kwetu niliyobahatika kuyanasa wakati nikipita eneo hilo. Ingawa niliyachukulia kama mzaha tu wa vijana wasio na kazi wanaopenda kulalamika, lakini yameendelea kujirudia akilini mwangu kiasi kwamba nadhani ni muhimu ikawekwa wazi ili Watanzania tuufahamu ukweli.

Inaeleweka kabisa kuwa kila nchi ina lugha yake ya taifa, lugha ambayo inatumika katika shughuli zote za kiserikali. Mfano mzuri ukienda Kenya, lugha yao ya taifa ni Kiswahili na Kiingereza na ndio maana katika shughuli zote za mambo ya serikali, wanatumia lugha hizo za Kiingereza na Kiswahili. Ukienda hospitali, mahakamani, shule na hata katika vyuo vya elimu ya juu, lugha inayotumika ni Kiingereza tu.

Hebu tujiulize hapa kwetu Tanzania ni ipi ni lugha ya taifa? Kila mara napata wakati mgumu, ninapoona viongozi wakichanganya lugha - yaani Kiswahili na Kingereza (Kiswanglish au Kiswakinge)!

Lugha ni utambulisho wa jamii na kwa kutumia lugha watu hupashana habari, hujenga uhusiano kwa kufahamiana, kuelimishana na kupatana au kufarakana. Lugha ndiyo njia kuu ya mawasiliano. Ni sehemu ya utamaduni, ni amali ya jamii inayoizungumza na ina alama ya umoja wa kitaifa. Kwa kweli suala la mila na utamaduni wetu huwa linachanganya kidogo. Tunapoongelea utamaduni na mila za Watanzania katika Tanzania yenye zaidi ya makabila 120 ambayo kila moja lina mila na utamaduni wake, tujiulize utamaduni na mila za Watanzania ni zipi?

Hapa ndipo Serikali na Watanzania wote kwa ujumla wetu tunapokuwa na jukumu la kuhakikisha tunalinda tamaduni zetu na kuwa urithi bora kwa vizazi vijavyo nao wataposherekea miaka mia moja ya uhuru wawe na vitu cha kujivunia kutoka kwenye jamii yao ya asili. moja ya vitu hivi ni lugha ya Kiswahili.

Ieleweke kuwa maendeleo ya sekta zote, yawe ni maendeleo ya kiuchumi, kisiasa, kijamii na kitamaduni yanahusisha lugha katika utekelezaji wa majukumu yake ya kila siku. Hivyo sekta zote zinapaswa kuhimiza matumizi ya Kiswahili, iwe ni kwa mazungumzo au kwa maandishi.

Kwa njia ya lugha, maisha ya jamii yanaakisiwa na kuifanya kuwa kioo cha jamii, bila lugha ingekuwa vigumu kuurithisha utamaduni wa kizazi kimoja hadi kingine. Kwa maana hiyo, Kiswahili kitaendelea kuwa kielelezo cha utamaduni wa Watanzania na njia kuu ya mawasiliano ya wanajamii wa Tanzania. Tunapaswa tukitunze na kukienzi badala ya kuendelea kupiga porojo kuwa ni lugha ya taifa wakati hatukithamini.

Kiswahili ni lugha ambayo ni kielelezo cha ndani cha jamii ya Watanzania, kimekuwa kikitumika kuelezea mila na desturi ambazo ni nguzo muhimu za utamaduni wa Tanzania. Utamaduni (kupitia lugha) ni kielelezo cha uhai na utashi wa taifa na ni mama na baba wa sekta nyingine za jamii; siasa na uchumi. Lugha ni nyenzo muhimu sana katika kuuelezea utamaduni wa Taifa kwani haiwezi kuwa utambulisho wa taifa bila kuelezea utamaduni wake.

Ni ukweli ulio dhahiri kuwa lugha ya taifa hapa nchini ni Kiswahili, lakini cha ajabu watu hawakitumii inavyostahili, kutokana na madai eti wakiongea Kiswahili, wataonekana si wasomi! Hii imedhihirishwa hat kwa watunga sera wetu kwa kuandaa sera na mambo muhimu (sheria, kanuni) yanayomgusa mwananchi wa kawaida kwa Kingereza badala ya Kiswahili.

Kama walivyokuwa wakisema vijana wa kijiweni huku mtaani kwetu, Kiswahili kimekuwa hakipewi umuhimu, ingawa ndio lugha ya taifa; na badala yake hata viongozi wamekuwa na tabia ya kuchanganya Kiswahili na Kingereza! Hali hii imeigwa na wasanii wa filamu ambako sasa kuchanganya Kingereza na Kiswahili limekuwa jambo la kawaida.

Wasomi wetu, imekuwa ni jambo la kawaida kuchanganya Kiswahili na Kingereza, Wakiamini kufanya hivyo ni kujitambulisha katika jamii, kuwa wao ni wasomi wa elimu ya juu! Wakisahau kuwa Kiingereza ni kama lugha zingine tu, na kujua Kingereza haimaanishi kuwa wewe ni msomi, kwani Kingereza ni lugha kama Kijita, Kingoni au Kizaramo, tofauti yake ni kwamba lugha hii inazungumzwa na Wazungu! Kwa nini hatutaki kujifunza toka nchi za dunia ya kwanza kama China ambao lugha yao imewasaidia katika maendeleo? Unapokwenda kusoma China ni lazima ufahamu lugha ya Kichina na utafundishwa kwa lugha hiyo.

ABDOULAYE WADE: Akiuka katiba aliyoiasisi mwaka 2001 ili agombee ngwe ya tatu

Rais  wa Senegal, Abdoulaye Wade

DAKAR,
Senegal

RAIS wa Senegal, Abdoulaye Wade, mwenye umri wa miaka 85 sasa na akiendelea kuongoza taifa hilo kwa miongo kadhaa anajiandaa kugombea tena kwa kipindi cha tatu baada ya uamuzi wa Mahakama Kuu kutolewa. Hukumu hiyo imesababisha vyama vikuu vya upinzani kufanya maandamano makubwa ya kupinga hatua ya Rais Wade kugombea nafasi yake kwa kipindi cha tatu mfululizo.

Jopo la Majaji watano ndilo lililoamua hatima ya Rais Wade kwenye harakati za kusaka kuwania kiti hicho kwa mara nyingine huku shinikizo kubwa likitaka kiongozi huyo asuruhusiwe kuvunja katiba.

Rais Wade amewasihi wananchi ambao wameonekana kukerwa na kitendo chake cha kuendelea kutaka kusalia madarakani, wawe watulivu baada ya maandamano ya ghasia kuzuka kufuatia uamuzi wa mahakama kutoa uamuzi wake. Rais Wade alisema kuonesha hasira kwa fujo hakutaleta tija yoyote.

Alitokeza kwenye televisheni huku ghasia zikiwa zinatapakaa katika miji kadhaa ya Senegal. Katika mji mkuu, Dakar, vizuizi viliwekwa, magari yalipinduliwa na maduka kadhaa yalichomwa moto. Kuna taarifa za askari polisi kuuawa.

Mpinzani maarufu wa Wade, mwimbaji Youssou N'Dour, ameonya kuwa hukumu ya Mahakama ya Katiba haitakubalika. Mahakama hayo yalitupilia mbali ombi la Youssou N'Dour kutaka kugombea urais katika uchaguzi wa mwezi ujao. Uchaguzi wa Senegal unatarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu ambapo ndiyo hatima ya uongozi nchini humo utabainika.

Historia yake

Abdoulaye Wade amezaliwa Mei 29, 1926, ingawa baadhi wanadai alizaliwa miaka kadhaa nyuma. Ni rais wa tatu wa Senegal, aliyeingia madarakani mwaka 2000. Pia ni Katibu Mkuu wa Chama cha Kidemokrasia cha Senegal (PDS) alichokiongoza tangu kilipoanzishwa mwaka 1974. Amekuwa kiongozi wa muda mrefu wa upinzani, akiwa amewania urais mara nne, kuanzia 1978, kabla ya kuchaguliwa mwaka 2000.

Maisha kabla ya siasa

Wade alizaliwa katika eneo la Kebemer nchini humo. Alisoma na kufundisha sheria katika Shule ya Lycee Condorcet nchini Ufaransa. Ana shahada mbili za udaktari katika sheria na uchumi. Alikuwa pia Mkuu wa Kitivo cha sheria na uchumi katika Chuo Kikuu cha Dakar nchini Senegal. Amemuoa Viviane Wade mwenye asili ya Uzungu.

Mtoto wao wa kiume, Karim Wade, alikuwa mkuu wa zamani wa wakala wa Taasisi ya Kitaifa ya Kiislam na alifanya kazi tangu Mei 2009 kama Waziri wa Ushirikiano wa Kimataifa, Mipango Miji na Mikoa, Usafiri wa Anga, na Miundombinu. Binti yao, Sindjely Wade, ni Msaidizi Maalum wa Rais ambaye alishiriki katika mikutano ya kampeni mingi ikifanyika Paris na Dakar.

Kazi ya siasa

Katika mkutano wa kilele wa Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika (OAU) mjini Mogadishu, mwaka 1974, Wade alimwambia Rais Leopold Senghor Sedar kwamba alitaka kuanzisha chama kipya, na Senghor alikubali. PDS ilianzishwa tarehe 31 Julai 1974. Chama ambacho awali kilikuwa na lengo la Uliberali mwaka 1976 kutokana na kuanzishwa kwa sheria ya kuruhusu kuwepo kwa vyama vitatu tu na itikadi tofauti tatu, mbili zilichukuliwa na vyama vingine (uliberali ndo' chaguo pekee lililobakia).

Wade aliwania urais mwezi Februari 1978 dhidi ya Senghor, na kupata asilimia 17.38 ya kura. Pia mwaka huo, Wade alichaguliwa kuwa mbunge, alioutumikia hadi 1980. Aliwania pia urais katika uchaguzi wa 1983 na 1988 na kuchukua nafasi ya pili kila wakati, nyuma ya mrithi wa Senghor wakati huo, Abdou Diouf. Kufuatia uchaguzi wa 1988, alikamatwa kutokana na maandamano na alisimamishwa asigombee. Baada ya hapo alikwenda Ufaransa na kurudi mwaka 1990.

Mwezi Aprili 1991, Wade na wanachama wengine wanne wa PDS walijiunga na serikali ya umoja wa kitaifa pamoja na chama tawala cha Kisoshalisti (PS); Wade akawa Waziri wa Nchi asiye na wazara maalum. Oktoba 1992, yeye na mawaziri wengine wa PDS walijiondoa serikalini kutokana na malalamiko kuhusu namna ambayo PS ilikuwa ikiidhibiti serikali. Katika uchaguzi wa rais wa Februari 1993, Wade alikuwa wa pili tena, akiwa na asilimia 32 ya kura, nyuma ya Diouf, aliyeshinda kwa asilimia 58.
 
Kufuatia mauaji ya Makamu wa Rais wa Baraza la Katiba Mei 1993, Babacar Seye, Wade, pamoja na viongozi wengine wa PDS, walihojiwa na polisi. Oktoba 1, Wade, mke wake, na wabunge wawili wa PDS (Abdoulaye Faye na Ousmane Ngom), walishtakiwa kwa makosa ya mauaji, ingawa hawakuwa chini ya ulinzi au kufunguliwa kesi. Kufuatia maandamano mwezi Februari 1994, Wade alikamatwa pamoja na wengine wengi kwa tuhuma za kutishia usalama wa serikali. Mashtaka ya kushiriki katika mauaji ya Sèye yakafutwa Mei 1994, na Wade na washitakiwa wenzake walianza mgomo wa kutokula mnamo Juni 30. Yeye na washitakiwa wenzake waliachiwa Julai 4, na mashtaka yaliyosalia yalifutwa mnamo Agosti 30, 1994.

Wade alijiunga tena na serikali kama Waziri wa Nchi mwezi Machi 1995, lakini yeye na mawaziri wengine wa PDS walijiondoa tena Machi 1998. Ingawa alichaguliwa katika Bunge la Taifa katika uchaguzi wa Februari 1998 wa bunge, alitangaza kujiuzulu katika Bunge la Taifa mwishoni mwa Julai 1998, akisema kuwa kulikuwa na "wasaidizi wa kutosha kufanya kazi katika nafasi yangu".

Uchaguzi wa 2000 na muhula wa kwanza

Wade aliishi kipindi cha mwaka nchini Ufaransa, na kurejea tena Senegal tarehe 27 Oktoba, 1999. Katika duru ya kwanza ya uchaguzi wa rais 2000, uliofanyika Februari 27, alikuwa katika nafasi ya pili tena, kwa kupata asilimia 31 ya kura, lakini kwa mara ya kwanza, Diouf hakuwa amefikia asilimia zinazomfanya atangazwe mshindi katika raundi ya kwanza, hivyo mzunguko wa pili ulifanyika Machi 19. Wade alishinda kwa asilimia 58.49 ya kura, baada ya kuungwa mkono na wagombea kutoka duru ya kwanza, ikiwa ni pamoja na mgombea aliyeshika nafasi ya tatu, Moustapha Niasse. Wade akawa Rais tarehe 1 Aprili, 2000, na kumteua Niasse kuwa Waziri Mkuu wake muda mfupi baadaye.

Katiba mpya ilipitishwa mwaka 2001, na kupunguza kipindi cha urais kuwa miaka mitano baada ya Wade kukamilisha muda wake wa miaka saba mwaka 2007.

Uchaguzi wa 2007 na awamu ya pili

Oktoba 15, 2006, Wade aliteuliwa kuwa mgombea urais wa PDS kwa uchaguzi wa urais wa Februari 2007. Mmoja kati ya wapinzani wa Wade katika uchaguzi huu alikuwa waziri mkuu wake wa zamani, Idrissa Seck, ambaye mwanzoni alichukuliwa kuwa mfuasi wa Wade, lakini alikamatwa mwaka 2005. Matokeo ya mwisho yaliyotolewa Machi 11, 2007, yalionesha Wade kashinda katika raundi ya kwanza kwa asilimia 55.9 ya kura, kwa mbali dhidi ya wapinzani wake wa karibu, Seck asilimia 15 na kiongozi wa Socialist Party, Ousmane Tanor Dieng, asilimia 13.6. Dieng na mgombea mwingine wa upinzani, Abdoulaye Bathily, walikata rufaa kuhusu uchaguzi, lakini ilikataliwa na Baraza la Katiba. Wade aliapishwa kwa kipindi chake cha pili mnamo Aprili 3 katika Uwanja wa Leopold Sedar Senghor jijini Dakar, na viongozi wengi wa Afrika na watazamaji 60,000 walihudhuria.

Vyama vikuu vya upinzani havikukubali ushindi wa Wade wa mwaka 2007 na kuhoji uhalali wake kama Rais; waligomea uchaguzi wa Bunge la Taifa na Seneti baadaye mwaka huo. Wade alihitimisha kwa kusema katika mahojiano yaliyochapishwa na ‘Le Soleil’ mnamo Mei 19, 2008, kwamba hakukuwa tena na uwezekano wa mazungumzo na upinzani isipokuwa kwanza atambuliwe kama Rais halali. "Waacheni wafanye wanachotaka, hainisumbui," alisema, "mradi tu waheshimu sheria na utaratibu."

Julai 2007, Umoja wa Afrika katika mkutano wa kilele mjini Accra, Ghana, Wade aliunga mkono kuundwa haraka kwa mapendekezo ya Umoja wa Afrika na alisema: "Kama tunashindwa kuungana, tutakuwa dhaifu, tukiishi kila nchi pekee yake katika nchi ambazo zimegawanywa, tutakabiliwa na hatari ya kuangukia katika nchi kubwa zilizoungana kiuchumi".

Uchaguzi wa 2012 na awamu ya tatu

Julai 2008, Bunge la Taifa lilipitisha mabadiliko ya katiba na kuongeza muda wa urais kwa miaka saba, kama ilivyokuwa kabla ya kupitishwa kwa katiba ya mwaka 2001. muda huu hautahusu kipindi cha uongozi wa Wade cha 2007-2012, lakini Waziri wa Sheria, Madické Niang, alisisitiza kuwa Wade ana uwezekano wa kugombea uchaguzi wa mwaka 2012 kama bado ana afya. Baadaye, Septemba 17, 2009 Wade alithibitisha kuwa alipanga kugombea awamu ya tatu mwaka 2012 "kama Mungu atanipa maisha marefu". Wade, katika hotuba ya 14 Julai 2011 kwa wafuasi, alitumia lugha ya Wolof “Ma waxoon waxeet” (nilisema, naweza kugombea tena) katika kueleza uamuzi wake wa 2007 wa kutogombea kwa kipindi kingine.

Januari 27, 2012 Abdoulaye Wade alipitishwa rasmi na Baraza la Katiba (linalojumuisha majaji wakuu watano) kugombea kwa muhula mwingine wenye utata wa tatu na wa mwisho. Kufuatia tamko hili, hasira za umma ziliwatuma kushiriki katika maandamano. Pia kumekuwepo na taarifa kuwa Wade ni mwanachama wa Freemason.

Makala haya yameandaliwa na Bishop Hiluka kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari vya kimataifa.

Jan 27, 2012

Kinachotafutwa ni vazi la taifa au kitambaa cha taifa?

Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Emmanuel Nchimbi akiwa na wajumbe wa kamati ya kutafuta vazi la taifa, ofisini kwake jijini Dar es Salaam

 Wa-Nigeria wanaopigiwa mfano


Wanawake wa Kimasai wakiwa katika mavazi rasmi ya kabila lao

BISHOP HILUKA

Dar es Salaam



WIKI iliyopita katika kituo kimoja cha televisheni nilishuhudia mdahalo kuhusu vazi la taifa, mdahalo ulinivutia kiasi cha kuamua kuandika makala hii. Hoja zilizotolewa katika mdahalo huo na nyingine ambazo nimekuwa nikizisikia zimeshindwa kunishawishi kukubaliana na hiki kinachoitwa vazi la taifa. Hoja hizo zimeniacha na maswali kadhaa ambayo ningependa wahusika wajitokeza kuyatolea ufafanuzi ili kutushawishi wote wenye mashaka kama yangu.



Mtaniwia radhi kama nitaonekana si mzalendo, lakini mimi pia nina mtazamo wangu katika jambo hili. Mwanzoni nilidhani kinachotafutwa ni vazi la taifa, lakini siku chache hata kabla ya mdahalo huo nilishangazwa na kauli za wahusika wakuu wa mchakato huu kuhusu mwenendo mzima wa kupata kile kinachoitwa vazi la taifa. Wahusika hao, kwa nyakati tofauti nimewasikia wakiongelea aina ya kitambaa, ubora wake na rangi gani inafaa!



Hapa pana mkanganyiko, wanaposema eti kitambaa kitakuwa na ubora tofauti kulingana na hadhi ya mvaaji, wakitolea mfano wa wabunge, ambao wanaweza kuchagua suti waipendayo kutokana na kitambaa hicho! Kumbe mawazo yao yamejikita kwenye kitambaa na ubora wa kitambaa na si vazi kama dhana nzima ilivyoelezwa mwanzo! Je, kwa wananchi wengi, hususan vijijini ambao hawamudu bei za vitambaa madukani na kimbilio lao kubwa ni mitumba tunawaambia nini? Pia hapa sijajua, hoja ni vazi au kitambaa cha taifa?



Hata hivyo, vazi la taifa halitafutwi na halijawahi kutafutwa! Wamasai walitafutiwa na nani? Au hizo nchi zinazotolewa mfano; Ghana, Nigeria, Afrika Kusini au China hawajawahi kuwa na kamati ya kutafuta vazi. Kwanza si kweli kwamba wana mavazi ya taifa, hayo tunayodhani kuwa ni ya taifa ni mavazi yanayovaliwa na makabila makubwa. Nina wasiwasi kwamba tutatumia pesa nyingi katika kitu kisicho na tija kwa maana kuwa mwisho wa mchakato vazi halitakuwepo.



Sikubaliani na sababu zinatolewa eti vazi hili litazidisha uzalendo, litaleta maendeleo, litatangaza utamaduni, vivutio na utambulisho wa nchi! Nijuavyo, vazi la taifa kama ni utamaduni basi utamaduni hauundiwi mezani kama tunavyotaka kuaminishwa.



Ieleweke kuwa lengo la makala hii ni kutoa changamoto na kuibua mjadala zaidi katika kuangalia namna nzuri ya kurudisha maadili, uzalendo na kuutangaza utamaduni wetu katika kazi za sanaa na changamoto zinazotukabili juu ya namna ya kukuza au kudhibiti wimbi la mapokeo ya sanaa zinazokiuka mila, desturi na maadili yetu ya Ki-Tanzania, badala ya kufikiria kuwa kitambaa pekee kitatusaidia.



Hebu tujiulize ni nchi gani duniani ambayo kuendelea au kutokuendelea kwake kumetokana na kuwa ama kutokuwa na vazi la taifa? Je, ni kitu gani cha muhimu ambacho kama taifa tumekikosa kwa miaka 50 kwa sababu ya kutokuwa na kipande cha nguo kinachoitwa vazi la taifa? Ni kweli uzalendo umepungua nchini kwa sababu ya kukosa vazi la taifa? Je, vazi la taifa ni sawa na vazi la heshima ambalo ndicho kitu cha msingi sana kama tunaangalia udumishaji wa mila?



Nafikiri tuna changamoto nyingi ambazo hata tukileta hilo vazi haliwezi kuziondoa, tunapaswa kukabiliana na mmomonyoko wa maadili kwenye jamii yetu ambao unaletwa na utamaduni tunaoiga toka nje, huku wizara inayoratibu mchakato wa kitambaa kinachoitwa cha taifa ikiwa kimya na haijawahi kuunda kamati kuushughulikia. Tunashuhudia mmomonyoko mkubwa katika jamii hii, kupitia nyimbo za matusi, filamu na nyimbo za mapenzi au zisizo na asili yetu zilizonakili vitendo na maudhui ya jamii za nje. Je, wizara husika iko wapi katika hili?



Sanaa kama nguzo muhimu ya utamaduni hukua na pia hufa. Hivi sasa sanaa zetu zipo katika chumba cha wagonjwa mahututi na tusipochukua juhudi za ziada tutazika uasili wa sanaa zetu tulizoachiwa na wazee wetu zilizodumu kizazi hadi kizazi. Hili linazigusa sanaa zote kuanzia filamu, muziki, sanaa za maonesho na kazi za mikono. Ni kweli njia tunayoenda nayo katika kazi zetu za sanaa inatupeleka kwenye msingi wa waliotutangulia au tumepotea na wimbi la utandawazi? Je, hili vazi litasaidiaje kuzifanya sanaa zetu zisife?



Tuna tatizo kubwa la maadili katika sanaa na udhibiti wa kazi chafu, jambo ambalo limekuwa gumzo. Mbona wizara haijawahi kuandaa kamati ya kutafuta alama ya muziki wetu? Mbona haitafuti alama ya filamu au chanzo cha wasanii kuiga filamu zisizo na maadili? Au mbona ubunifu wa mitindo yetu ya kucheza muziki wetu na sanaa nyinginezo ni wa kuiga? Kwa nini vazi la taifa?



Nimewahi kusoma kuwa fani ya muziki inaporomoka kwani wanamuziki walio wengi wamepotea njia kwa kutofuata miiko katika tungo zao, miundo, mitindo na maudhui kulingana na uasili, mila, desturi, mapokeo, historia na urithi tulioachiwa. Haya yote yakiwa yanaashiria kuporomoka kwa fani hii.



Kadri muda unavyozidi kwenda tunawapoteza wapiga ala kama ngoma, marimba, zeze, Saxophone na kadhalika, huku idadi lukuki ya waimbaji bandia wasio na msingi na kanuni za fani ya uimbaji na utunzi wakiongezeka na kusababisha muziki wetu kuchuja katika muda mfupi, hapo hapo teknolojia ikimaliza vipaji vya wapiga ala kwa kuwa kila ala siku hizi ipo studio kwenye mashine (computer). Mbona wizara haiundi kamati kunusuru hili?



Tumekuwa mahodari wa kushabikia sanaa za kutoka nje ya nchi. Kuanzia kwenye jamii hadi ngazi ya taifa, jambo linalotufanya kuwa wasindikizaji kwa kupokea sanaa na mitindo toka nje. Haya yanajitokeza katika fani za unenguaji, filamu, muziki wa injili na hata fani nyinginezo za sanaa. Bila kujua tumekuwa tunapandikiza mbegu mbaya katika jamii kwa kutopenda cha kwetu. Je, katika mazingira haya uzalendo na moyo wa kuipenda nchi utabadilishwaje na kitambaa tunachoita vazi la taifa?



Mwisho, tujiulize maswali haya; je, vipaumbele vyetu kama taifa ili kujiletea maendeleo na kudumisha maadili ni muhimu kuwa na vazi la Taifa leo? Tunapoangalia ubora na rangi ya vitambaa katika nchi hii ya wavaa mitumba, je, serikali kupitia wizara husika haikuona umuhimu wa kuunda kwanza tume ya kusaidia wakulima wa pamba ili pamba yao iwe katika kiwango bora badala ya kukimbilia kuunda tume ya kutafuta vazi la Taifa?



Je, kuna mkakati gani hadi sasa wa kuongeza thamani ya pamba yetu ili tuiuze kama malighafi nje ya nchi? Kwa nchi ambayo haina viwanda vya nguo, leo tunaunda tume ya kutafuta vazi la Taifa, hivi kama vazi hilo likipatikana ni kiwanda gani hapa nchini kitashona nguo hizo za vazi linaloitwa la Taifa? Au tutaanza tena mchakato wa kutafuta mzabuni wa kutushonea nguo katika nchi kama China, India, Pakistani na kwingineko?


Naomba kuwasilisha…


LEON MUGESERA: Mtuhumiwa wa mauji ya kimbari aliyerudishwa Rwanda baada ya kukwepa kwa zaidi ya miaka 16

Leon Mugesera

QUEBEC
Canada

MTUHUMIWA wa mauji ya kimbari, Leon Mugesera, aliyekuwa anahitajika sana nchini Rwanda kwa madai ya kuchochea mauaji ya halaiki na uhalifu dhidi ya binadamu yenye uhusiano na mauaji ya kimbari ya mwaka 1994, ambayo yalishuhudia ukatili mkubwa ulioongozwa na Wahutu kwa mamia ya maelfu ya watu, hasa wa kabila la Watutsi.

Madai ya uchochezi yanahuswa na hotuba ya Mugesera aliyoitoa mwaka 1992 akitoa wito kwa Wahutu kuwaondoa nchini Rwanda Watutsi, aliowaita "mende."

Serikali ya Canada imeamua kumrudisha Rwanda mtuhumiwa huyo wa mauji ya kimbari. Mahakama hiyo ya Canadian imekataa ombi la rufaa kutoka kwa mshukiwa huyo aliyepinga kurudishwa nchini Rwanda akisema kuwa hatapata haki nchini huko.

Mugesera ambaye anakabiliwa na mashtaka hayo ya kutoa matamshi ya kuchochea mauaji ya halaiki na uhalifu dhidi ya binadamu, inasemekana alitoa hotuba ya kichochezi mwaka 1992, mbele ya wanachama wa kilichokuwa chama tawala cha wahutu (MRND), na anadaiwa kusema kwamba Watutsi wanapaswa wauawe huku akiwaita 'mende'.

Mwenyewe amekanusha madai hayo akisema kuwa matamshi yake yametafsiriwa vibaya. Mugesera, mwanataaluma na mwanaharakati wa kisiasa ambaye alikuwa akiishi katika jiji la Quebec, alipigania bila mafanikio kwa muda wa miaka 16 katika mahakama kadhaa - ikiwa ni pamoja na Mahakama Kuu ya Canada mwaka 2005 - ili kuepuka kurejeshwa nchini Rwanda.

Kufuatia hukumu, ambayo mahakama ilisema kuwa kuna ushahidi wa kutosha kuonesha kuwa Mugesera ndiye alichochea mauaji dhidi ya Watutsi, hatimaye serikali ya Canada mnamo Novemba mwaka jana ilipitisha uamuzi wa kufukuzwa kwa Mugesera.

Wakili wa Mugesera alikuwa ameomba apewe muda zaidi ili Kamati ya Umoja wa Mataifa inayopinga vitendo vya unyanyasaji na mateso ichunguze kwanza na itoe hakikisho kuwa hatapatwa na kadhia hiyo akiwa Rwanda lakini mahakama ilitupilia mbali ombi hilo. Mugesera na wanasheria wake walisema kuwa atateswa au kuuawa kama atarudishwa Rwanda na kupambana na kesi hiyo, kwa vile yeye ni adui wa Rais Paul Kagame. Wameonesha shaka katika utawala wa nchi hiyo wa sheria au uwezo wa Mugesera wa kupata hukumu ya haki mbele ya mahakama nchini humo.

Serikali ya Rwanda imefurahishwa na uamuzi huo.

Historia yake

Leon Mugesera amezaliwa mwaka 1952, ni mzaliwa wa Rwanda, ambaye alikuwa anaishi katika jiji la Quebec, Canada tangu mwaka 1992, kabla hajatakiwa kuondoka nchini Canada kwa sababu ya kesi inayomkabili ya uchochezi dhidi ya Watutsi kutokana na hotuba yake ambayo wakosoaji wanadai ndiyo iliyochochea mauaji ya kimbari nchini Rwanda ya 1994.

Akiwa Rwanda

Mugesera wa kabila la Kihutu, amekuwa mwanachama wa chama kikubwa cha Kihutu cha MRND, ambacho kilikuwa na mahusiano ya karibu zaidi na jeshi la nchi hiyo. Alikuwa Makamu Mwenyekiti wa MRND katika mkoa wa Gisenyi.

Katika hotuba yake iliyotolewa Novemba 22, 1992 nchini Rwanda, inadaiwa Mugesera aliwaambia wanachama 1000 wa chama chake kwamba "sisi watu wa Kabila la Hutu tuna wajibu wa kuchukua jukumu wenyewe na kufuta hili povu" na kwamba wanapaswa kuwaua Watutsi na "kuitupa miili yao katika mito ya Rwanda". Kauli hii haipo katika tafsiri rasmi ya hotuba, kama iliyotolewa katika hati ya kisheria mbele ya Waziri wa Uraia na Uhamiaji wa Canada tarehe 8 Agosti 2003.

Kufuatia hotuba hii, Waziri wa Sheria wa Rwanda wakati huo, Stanislas Mbonampeka, alitoa kibali cha kukamatwa dhidi ya Mugesera kwa kuchochea chuki za kikabila. Mugesera alikimbia na familia yake, kwanza katika jeshi la Rwanda na kisha katika jiji la Quebec, Canada. Muda mfupi baadaye, Mbonampeka alijiuzulu nafasi ya Waziri wa Sheria kufuatia maandamano.

Canada

Nchini Canada, Mugesera na familia yake waliwasili kama wakimbizi, na walipatiwa haraka nyaraka za ukazi wa kudumu. Mugesera akapata kazi ya kufundisha katika Chuo Kikuu cha Laval.

Mashtaka ya uhalifu wa kivita

Philip Gourevitch, mwandishi wa “We Wish to Inform You That Tomorrow We Will Be Killed With Our Families”, alidai kwamba hotuba ya Mugesera ya mwaka 1992 ilisababisha kasi na mhemko wa watu wasio wa kabila la Watutsi ambayo ndiyo ilisababisha mauaji ya kimbari, akisema kuwa "(Mugesera) alikuwa mmoja wa watu wa kwanza kabisa kwenda kwenye vyombo vya habari kutoa hotuba kwa umma na kusema, ‘Angalieni, makosa yetu katika siku za nyuma yanavyotugharimu kuruhusu Watusi wachache kuendelea kuishi. Lazima tuwamalize’”. Kauli hii haipo katika tafsiri rasmi ya hotuba, kama iliyotolewa katika hati ya kisheria mbele ya Waziri wa Uraia na Uhamiaji wa Canada tarehe 8 Agosti 2003.

Mchakato wa kufukuzwa

Mwaka 1995, wanasheria wa serikali ya Canada walianza kusikiliza shauri dhidi ya Mugesera. Mahakama mbili za uhamiaji ziliamuru kuondoshwa kwake na kurudishwa Rwanda, hata hivyo, Mahakama ya Rufaa ya Shirikisho la Canada ilitengua hukumu hizi. Jaji Robert Décary, aliiandikia Mahakama, kwamba kulikuwa hakuna ushahidi wa kutosha kuunganisha hotuba ya mwaka 1992 na mauaji ya kimbari ambayo yalitokea miaka miwili baadaye. Katika kesi zote, Mugesera aliwakilishwa na mwanasheria wa Quebec, Guy Bertrand.

Tarehe 1 Agosti, 2001, Mugesera alitoa taarifa, na kuomba kesi ifutwe chini ya Sheria mpya za Canada dhidi ya ubinadamu na uhalifu wa kivita.

Mahakama ya Rufaa ya Shirikisho baadaye ilitoa uamuzi wa 8-0 kuhusiana na Mahakama Kuu ya Canada mnamo Juni 28, 2005, ambayo awali iliidhinisha kufukuzwa nchini humo kwa Mugesera.

Kufukuzwa kwa Mugesera kulicheleweshwa kwa sababu ya wasiwasi juu ya uwezekano wa kukabiliwa na adhabu ya kifo nchini Rwanda. Hata hivyo Rwanda ilipiga marufuku adhabu ya kifo mwaka 2007. Mugesera ndipo akaanza kupigania asihamishwe Canada kutokana na hofu kuwa atateswa akiwa nchini Rwanda. Serikali ya Canada ilisita kumfukuza nchini mtu ambaye angeweza kukabiliwa na mateso, lakini Kigali waliihakikishia Canada "dhamana ya kidiplomasia" kuhusu hali ya baadaye ya Mugesera.

Uamuzi wa Jaji wa Mahakama ya Juu, Michel Delorme, wa kukubali hoja zilizotolewa na serikali ya shirikisho, ambayo ilisema ni Mahakama Kuu tu ndiyo ina mamlaka katika masuala ya uhamiaji. Delorme aliendelea zaidi kwa kusema kuwa Kamati ya Umoja wa Mataifa haina nguvu kisheria kuilazimisha serikali katika maamuzi yoyote.

Wanasheria wa Idara ya Sheria pia walisema kuwa tayari walishafanya utafiti wa muda mrefu na kugundua kuwa hakuna hatari yoyote wala mateso katika kesi ya Mugesera awapo nchini Rwanda na kwamba hali nchini Rwanda kwa sasa ni salama.

Jumatatu ya Januari 23, 2012, Jaji wa Mahakama Kuu ya Quebec alikataa jitihada za Leon Mugesera za kuzuia kufukuzwa nchini humo. Mugesera aliondolewa nchini humo kupitia uwanja wa ndege wa kimataifa wa Montreal siku hiyo hiyo ya Jumatatu, saa 10 jioni.

Makala haya yameandaliwa na Bishop Hiluka kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari vya kimataifa.