Jan 19, 2012

Kuna maisha bora kwa kila Mtanzania kwa gharama hizi?

  Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), Harun Masebu, akizungumza na waandishi wa habari

Makao Makuu ya Shirika la Ugavi wa Umeme (Tanesco)
yaliyopo Ubungo jijini Dar es Salaama

BISHOP J. HILUKA
Dar es Salaam

MAMLAKA ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) imetangaza tena kupanda kwa gharama za umeme. Mwaka jana ilitangaza ongezeko la bei ya umeme kwa asilimia 18.5. Mwaka huu imeongeza bei ya umeme kwa zaidi ya asilimia 40 kuanzia Januari 15 huku mgao wa umeme ukiendelea ingawa hata huo upatikanaji wa umeme ni wa mashaka, huku chini ya asilimia 15 ya Watanzania wote ndiyo wanaopata umeme! Kupanda kwa bei ya umeme hakika kunazidisha ugumu wa maisha ambao upo hasa kwa wananchi walio wengi ambao ni wenye kipato cha chini.

Pamoja na Tanesco kupandisha gharama ya umeme, lakini shirika hilo bado halijafanya maboresho ya mitambo kwa kuwa umeme umekuwa ukikatika mara kwa mara na kuleta madhara makubwa ikiwemo kuunguza vitu majumbani na maofisini.

Hatua ya kupandisha gharama hizi inazidi kuwaongezea umaskini Watanzania ambao tayari wana maisha magumu mno kwa sababu hata bei ya awali wengi walikuwa hawaimudu. Jumatano asubuhi kwenye kipindi cha asubuhi cha moja ya vituo vyetu vya televisheni nilimsikia mbunge wa zamani wa Tabora Mjini, Siraji Kaboyonga akitetea ongezeko hili la bei, lakini haikuniingia akilini kutokana na sababu alizozitaja.

Kupandisha bei bado hakuwezi kuwa suluhisho au kuifanya Tanesco ijiendeshe kwa ufanisi kwani kinachotakiwa ni mbinu za kiutendaji na ubunifu katika kuliendesha shirika. Mbona mapato Tanesco yako mengi, isipokuwa imekosa mbinu na mikakati ya kuzuia wizi wa umeme unaofanywa na watumiaji wengi wa umeme.

Mfano eneo ninaloishi na hata maeneo mengi ninayotembelea, wezi wanaotumia umeme wa wizi bila malipo ni wengi, tena wanashirikiana na wafanyakazi wa Tanesco na wala hakuna jitihada za makusudi kuwazuia vishoka. wanapandisha bei ya umeme wakati hata huduma zenyewe hazijaboreshwa!

Kupanda kwa bei hakika kunapunguza watumiaji wa umeme na kuwarudisha watu katika utumiaji wa vibatari na mishumaa kwa sababu ya kuogopa gharama ya umeme. Hali hii imefika hapo ilipo kutokana na mfumo wa nchi hii kuegemea zaidi kwenye siasa kuliko kujali utaalamu. Siyo siri kuwa wananchi wa Tanzania kwa sasa wanaishi kwenye kiza kinene baada ya kujitokeza jinai ya kugawiwa umeme wakati huu.

Ni aibu kuendelea kutegemea chanzo cha maji kuzalisha umeme wakati tuna vyanzo mbadala. Uchumi wa Tanzania unaporomoka kwa kasi kubwa kutokana na ukosefu wa nguvu ya umeme wa uhakika pamoja na kuwa madini ya Uranium yanayotengeneza nishati ya nyuklia yanapatikana kwa wingi Tanzania. Madini ambayo kwa nchi kama Iran na Korea yanatumika kwenye uzalishaji nguvu za umeme kwa njia ya nyuklia.

Moja ya tatizo ambalo tumekuwa nalo kipindi kirefu sasa, Watanzania wengi tunategemea nishati hii kutoka kwenye vyanzo vya mabwawa ya maji. Miundombinu bado haijaboreshwa halafu linakuja suala la kuongeza bei ambalo ni kumwongezea mwananchi mzigo mkubwa usiobebeka na hiyo ni hatari kwa taifa, kwani itashusha hata uzalishaji na uchumi wa taifa utashuka.

Kwa nini tusiachane na vyanzo hivi na kuangalia vyanzo mbadala, kwani siku zote ambazo mabwawa hayo hupungua kina cha maji au kukauka, tumekuwa tukishuhudia mgao mkali, jambo ambalo tunaamini sasa umefika wakati wa serikali kutafuta njia mbadala ya kukabiliana na hali hii.

Hebu fikria ni biashara ngapi zinaathirika kutokana na mgao huu wa umeme. Hata kama ni biashara ya mwananchi wa kawaida ya kuuza barafu au juisi bado ina mchango katika ujenzi wa taifa changa
kama Tanzania. Kukosekana umeme wa uhakika katika mgao wa siku ni pigo kubwa kwa taifa kwani shughuli nyingi za uzalishaji zinasimama.

Mgao huu wa umeme licha ya kudhoofisha uchumi wa taifa na wa mtu mmoja mmoja unasababisha uharibifu na uchafuzi wa mazingira. Majenereta yanayofanya kazi mchana kutwa mijini yamekuwa yanachafua mazingira kwa moshi na hata kelele. Mgao wa umeme mbali na kusababisha kuparaganyika kwa uchumi pia ni chanzo cha rushwa. Mara nyingi sehemu za wenye pesa na vigogo serikalini huwa haziathiriki na kadhia kama hizi. Hii ni kwa vile ama wenye nazo wanahonga watendaji wa Tanesco, au wenye madaraka wanapendelewa kwa vile wameshikilia kila kitu katika nchi hii.

Inaposemwa eti ongezeko hili haliwagusi wenye kipato kidogo naona kama kuwafanya Watanzania mbumbumbu. Kwani ongezeko linapovikumba viwanda basi hata bidhaa zitapanda bei na watumiaji ni hawa hawa walalahoi.

Gharama hizi za umeme ni kama muendelezo na mzigo mkubwa wanaotwishwa wananchi baada ya matatizo mengi yanayowakabili, huku ikisemwa kuwa serikali ndiye mdaiwa sugu lakini sidhani kama inaguswa. Kwa gharama hizi hakika ile kaulimbiu ya Rais Kikwete ya maisha bora kwa kila Mtanzania itabaki kuwa ndoto nzuri ya mchana.

Alamsiki…

MUKESH KAPILA: Ailaumu Sudan baada ya kufukuzwa nchini Chad

Mukesh Kapila

N'DJAMENA
Chad

WIKI hii kulikuwa na habari za afisa misaada mwandamizi wa Uingereza kufukuzwa nchini Chad wakati alipojaribu kutembelea kambi ya wakimbizi ambao bado wanaishi mashariki mwa nchi hiyo.

Afisa huyo, Mukesh Kapila, alikuwa mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan aliyezungumza wazi wakati mgogoro wa Darfur ulipoanza miaka tisa iliyopita. Waziri wa mambo ya ndani wa Chad alimuamuru afisa huyo kuondoka nchini humo.

Kapila mwenyewe amesema sababu za kufukuzwa kwake kunahusiana na ushirikiano wa karibu uliopo kati ya serikali ya Sudan na Chad ambao amewatuhumu kuhusika na mauaji ya kimbari.

Hii ilikuwa ni ziara ya kwanza ya Kapila kuzuru eneo hilo tangu alipoondolewa katika nafasi yake mwaka 2004 akiwa amechanganyikiwa na kushindwa kuwashawishi jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua kwa hali iliyokuwepo wakati huo Darfur, aliamua kuzungumza kwa umma alipozungumza na Shirika la Habari la Uingereza, BBC. Kapila anatishiwa na kivuli chake mwenyewe baada ya kushindwa kuzuia mauaji Darfur.

Kapila alitembelea makambi ya wakimbizi mashariki mwa nchi ambako watu 200,000 bado wanaishi. "Nilichanganyikiwa, nimehuzunishwa sana na kukasirishwa mno," aliiambia BBC alipojua kuwa amefukuzwa nchini humo.

Mukesh Kapila amefanya kazi sana na alishauri katika mgogoro na usimamizi wa migogoro, masuala ya kibinadamu, ahueni baada ya vita na maendeleo, na VVU na UKIMWI. Kapila bado anafanya kazi Chini ya Katibu Mkuu wa Taifa wa Maendeleo ya Jamii na Maarifa katika Shirikisho la Kimataifa la Msalaba na Mwezi Mwekundu (IFRC).

Historia ya Kapila imejikita katika tiba, afya ya umma na, hatimaye, maendeleo ya kimataifa na masuala ya kibinadamu.  amehitimu kutoka Vyuo vya Oxford na London.

Akiwa mtumishi wa umma wa ngazi ya kati mwaka 1994, alikuwa sehemu ya timu ya kwanza ya Uingereza kuangalia matokeo ya baada ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda hasa baada ya Rwanda Patriotic Front kuidhibiti Kigali.

Alikuwa Naibu Mkurugenzi wa programu ya Taifa ya UKIMWI nchini Uingereza katika miaka ya 1990.

Aliwahi kuwa Mkuu wa Migogoro na Mambo ya Kibinadamu wa Uingereza kitengo cha Idara ya Maendeleo ya Kimataifa kuanzia 1998 hadi 2002. Kuanzia 2002 hadi 2003, Kapila alikuwa Mshauri Maalum wa Umoja wa Mataifa, kwanza kwa Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu nchini Afghanistan na kisha kwa Kamishna wa Haki za Binadamu. Mwaka 2003 hadi 2004 Kapila alikuwa Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa wa Kibinadamu, na Mwakilishi Mkazi wa Programu ya Maendeleo ya Umoja wa Mataifa kwa Sudan.

Alipokuwa Sudan, alishutumu vikali ukiukwaji wa haki za binadamu uliofanywa katika jimbo la Magharibi la Darfur. Harakati yake ilianza baada ya mwanamke wa Darfur aliyekuja ofisini kwake kumwambia jinsi gani yeye, binti yake na wanawake wengine 200 katika kijiji cha Tawilla walivyobakwa na makundi na wengi kuuawa na askari wa serikali na wanamgambo. Ripoti yake juu ya vita ya Darfur wakati huo ilifutwa na Serikali ya Sudan kwa madai kuwa "ni ya uongo", ingawa walifanikiwa kuileta Darfur katika sura ya vyombo vya habari vya dunia kwa mara ya kwanza. Kapila hatimaye alihamishiwa nje ya Sudan mwezi Aprili 2004, miezi 13 tu katika miezi 24 ya mkataba wake.

Akizungumza mwaka 2006 katika kipindi cha BBC, Kapila alisema:
“Kuna mjadala kuhusu kama tuliwahi kuwa na mauaji ya halaiki katika jimbo la Darfur au la, lakini kwa hakika katika akili yangu, na mawazo ya watu wengi, wengi, nadhani kuna shaka kidogo sana kwamba kile kilichotokea katika jimbo la Darfur mwaka 2003 na mwanzoni mwa 2004 hakika kilikuwa ni mauaji ya kimbari. Tunaweza kusema maneno, lakini ambayo hayatakuwa na faraja kwa watu wote ambao wameathirika.
Hivyo hatimaye niliendelea kusema kuhusu hilo hadharani, baada ya kujaribu njia mbalimbali za kidiplomasia na ustawi, na nilijikuta haraka  nikikokotwa kwenye ndege na kutupwa nje ya Khartoum. Na nilipotazama yaliyojitokeza nyuma, nilijiuliza kwamba kulikuwa na mauaji ya kwanza ya karne ya 21 - ni mahali katika historia ambapo hutotaka kuwepo.”

Kapila ameshinda tuzo kadhaa kwa kazi yake ya kibinadamu na maendeleo. Mwaka 2003, alitunukiwa tuzo na Malkia Elizabeth II na kutajwa kuwa Kamanda wa Order wa Dola ya Uingereza kwa huduma yake ya kimataifa. Mwaka 2007 alipokea Tuzo Kimataifa ya ijulikanayo kama Dk Jean Mayer Global Citizenship Award of the Institute for Global Leadership.

Aliwahi kuwa Mkurugenzi katika Idara ya Afya inayohusiana na migogoro ya Shirika la Afya Duniani kuanzia 2004 hadi 2006. Mfanyakazi wa Serikali ya Uingereza, alikuwa ameazimwa kufanya kazi kwenye ofisi za Umoja wa Mataifa. Alikuwa mshauri wa Benki ya Dunia juu ya masuala ya mabadiliko ya hali ya hewa, amewahi kuushauri Umoja wa Mataifa katika Mkakati wa Kimataifa wa Kupunguza Maafa (UN /ISDR), na Shirika la Kimataifa la Kazi Duniani. Alikuwa mtendaji mkuu wa PHG Foundation katika Cambridge, Uingereza kuanzia Septemba 2003 hadi Agosti 2004.

Kabla ya kuteuliwa kuwa chini ya Katibu Mkuu kwa kazi ya Maendeleo ya Taifa ya Jamii na Maarifa, Kapila aliwahi kuwa Mwakilishi Maalum wa VVU na UKIMWI, na hatimaye kama Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa IFRC. Wakati akiwa IFRC, Kapila alikuwa chombo katika maendeleo duniani kote "ushirikiano wa kimataifa" ya Msalaba Mwekundu na Mwezi Mwekundu kama vile VVU na kupunguza hatari ya maafa, ambapo mafanikio kidogo yamekuwa na mafanikio. Hivi karibuni, amekuwa na wajibu wa kuandaa Mkakati wa mwaka 2020 – visheni ya Shirikisho la Kimataifa kwa muongo ujao.

Aliwahi kutumikia nafasi ya Mshauri wa Bodi wa Kituo cha Geneva kwa ajili ya Udhibiti ya Kidemokrasia wa Vikosi vya Jeshi (Democratic Control of Armed Forces), na wa Minority Rights Group International, na Mjumbe Mtendaji wa Kamati ya Utekelezaji ya Muungano wa moja kwa moja dhidi ya ubakaji katika Migogoro na migongano (AllianceDARC).  Amekuwa mjumbe wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya Umoja wa Mataifa ya Mafunzo na Utafiti (UNITAR), Kituo cha Amani cha Kimataifa na Mratibu wa mfumo wa Tathmini ya Majanga Umoja wa Mataifa.
Dk Kapila kwa sasa ni mjumbe mwandamizi wa Hughes Hall College, Chuo Kikuu cha Cambridge, nchini Uingereza. Pia ni Mshiriki Mweza katika Taasisi ya kukabiliana na Migogoro ya Kibinadamu, katika Chuo Kikuu cha Manchester, Uingereza.

Kapila anaishi Uingereza na Uswisi.  Ameoa na ana watoto watatu.

Makala haya yameandaliwa na Bishop Hiluka kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari.

Jan 11, 2012

ANWAR IBRAHIM: Upinzani dhidi ya serikali wamfanya kubambikwa mashtaka ya ulawiti

Anwar Ibrahim

KUALA LUMPAR
Malaysia

KIONGOZI wa upinzani nchini Malaysia, Anwar Ibrahim ameondolewa makosa ya ulawiti katika kesi iliyochukua karibu miaka miwili. Mwanasiasa huyo alituhumiwa kufanya ngono na aliyekuwa msaidizi wake wa kiume. Hata hivyo jaji wa mahakama hiyo alisema uchunguzi wa DNA haukutoa ushahidi wowote.

Punde baada ya mahakama kutangaza uamuzi huo, jamaa wa Anwar walionekana kububujikwa na machozi ya furaha huku wafuasi wake wakishangilia uwamuzi huo. Wafuasi wa mwanasiasa huyo waliokusanyika nje ya mahakama mjini Kuala Lumpar wamekuwa wakisisitiza kwamba kesi hiyo haikufaa kufunguliwa tangu kuwasilishwa kwa tuhuma za ulawiti.

Hii ni mara ya pili Anwar ameshtakiwa kwa kufanya ulawiti. Kesi dhidi yake zimesababisha kuwepo na msisimko mkubwa wa kisiasa nchini Malaysia kwa zaidi ya muongo mmoja. Anwar Ibrahim ametaja kesi hiyo kama iliyochochewa kisiasa japo serikali imekanusha kuhusika kwa vyovyote.

Huku uchaguzi mkuu ukitarajiwa karibuni, chama tawala ambacho kimekuwa madarakani kwa zaidi ya nusu karne kinakabiliwa na upinzani mkali kutoka mrengo wa upinzani unaoongozwa na Anwar.

Historia yake

Anwar Ibrahim amezaliwa 10 Agosti 1947 ni mwanasiasa wa Malaysia ambaye aliwahi kuwa Naibu Waziri Mkuu wa Malaysia 1993 hadi1998. Mapema katika kazi yake, Anwar alikuwa mshirika wa karibu wa Waziri Mkuu, Mahathir Mohamad, lakini baadaye alijitokeza kama mkosoaji maarufu wa serikali ya Mahathir.

Mwaka 1999, alihukumiwa kifungo cha miaka sita jela kwa rushwa, na mwaka 2000, miaka mingine tisa kwa kulawiti. Mwaka 2004, Mahakama Kuu iliipindua hukumu yake ya pili na kumuachia. Julai 2008, alikamatwa kwa madai ya kumlawiti mmoja wa wasaidizi wake wa kiume, lakini aliachiwa huru mwaka 2012.

Tarehe 26 Agosti 2008, Anwar alishinda tena uchaguzi wa Pauh Permatang na kurejea Bungeni kama kiongozi wa upinzani wa Malaysia. Amesema ipo haja ya kuwepo uhuru, ikiwa ni pamoja na mahakama huru na vyombo vya habari huru, ili kupambana na rushwa iliyotapakaa ambayo anaona inaisukuma Malaysia kwenye umasikini.

Kuanzia 1968 hadi 1971, akiwa mwanafunzi, Anwar alikuwa rais wa chama cha wanafunzi wa Kiislamu. Alikuwa pia mmoja wa waasisi wa kamati ya Vuguvugu la Vijana wa Kiislamu wa Malaysia, ambayo ilianzishwa mwaka 1971. Pia alichaguliwa kuwa Rais wa Baraza la Vijana wa Malaysia. Mwaka 1974, Anwar alikamatwa wakati wa maandamano ya wanafunzi dhidi ya umaskini na njaa vijijini. Hii ilitokana na tetesi kuwa familia ilikufa kutokana na njaa katika kijiji cha Baling, katika jimbo la Kedah, pamoja na ukweli kwamba haikuwahi kutokea. Alifungwa jela chini ya Sheria ya Usalama wa Ndani, inayoruhusu kuwekwa kizuizini bila kufunguliwa mashitaka, na alikaa kizuizini kwa miezi 20 katika Kituo cha Kamunting.

Mwaka 1968-1971, alilelewa katika Umoja wa Kitaifa wa Wanafunzi wa Kiislamu wa Malaysia ​​akiwa rais wa Muungano. Mwaka 1982, Anwar, aliyekuwa kiongozi mwanzilishi na rais wa pili wa chama cha vijana wa Kiislamu, aliwashangaza wafuasi wake kwa kujiunga na United Malays National Organisation (UMNO), iliyoongozwa na Mahathir Mohamad, aliyekuwa waziri mkuu mwaka 1981. Alipanda safu ya kisiasa haraka: kazi yake ya kwanza ilikuwa ni Waziri wa Vijana, Utamaduni na Michezo mwaka 1983, baadaye, aliongoza wizara ya kilimo mwaka 1984 kabla ya kuwa Waziri wa Elimu mwaka 1986. Kwa wakati huo, uvumi ulienea kuwa Anwar kupanda hadi nafasi ya Naibu Waziri Mkuu kitu kilichokuwa jambo la kawaida nchini Malaysia kwa Waziri wa Elimu kushika nafasi ya Naibu Waziri Mkuu.

Kipindi cha uongozi wake kama Waziri wa Elimu, Anwar alianzisha sera mbalimbali katika mitaala ya shule kitaifa. Moja ya mabadiliko makubwa aliyofanya ni kuipa jina jipya lugha ya taifa kutoka Bahasa Malaysia na kuwa Bahasa Melayu, moja ya makabila nchini Malaysia kitendo kilichokosolewa na wasio wa kabila hilo.

Mwaka 1991 aliteuliwa kuwa Waziri wa Fedha. Mwaka 1993, akawa Naibu Waziri Mkuu wa Mahathir baada ya kushinda Unaibu Rais wa UMNO dhidi Ghafar Baba. Kuna taarifa Anwar alitumia fedha nyingi ili kuungwa mkono. Ilidaiwa pia alitumia fedha za siasa ili kupata nafasi yake kama makamu wa rais wa UMNO.

Mwishoni mwa miaka ya 1990, hata hivyo, uhusiano wake na Mahathir ulianza kuzorota, ulisababishwa na kutofautiana juu ya utawala. Wakati Mahathir hayupo, Anwar alijichukulia hatua kali za kuboresha mifumo ya uongozi wa nchi hiyo ambayo ilikuwa tofauti na sera za Mahathir za kibepari.

Matarajio ya Kisiasa

Novemba 2006, Anwar alitangaza mpango wa kugombea ubunge mwaka 2008. Anwar amekuwa mkosoaji wa sera za serikali tangu kuachiliwa kwake kutoka gerezani, hasa utata wa Sera Mpya ya Uchumi, ambayo inatoa usawa wa kijinsia kwa Bumiputras. Sera zinazoweka idadi maalum ambayo lazima ifikiwe. Pia ni Mshauri wa Parti Keadilan Rakyat, chama ambacho mke wake, Dk Wan Azizah ni rais.

Tarehe ya uchaguzi wa 2008, hata hivyo, ilipangwa kuwa Machi 8, 2008, na kuzua mzozo ambapo chama cha Barisan Nasional kilitoa wito wa kufanyika uchaguzi huo mapema kwa nia ya kuzima mipango ya Anwar kutaka kurudi Bungeni. Mke wa Anwar, Wan Azizah Wan Ismail, alitangaza kuwa angejiuzulu ili kurejesha kiti chake cha ubunge wa Permatang Pauh ili kulazimisha uchaguzi ambao Anwar atagombea. Alipoulizwa kuhusu uwezekano wa Anwar kuwa Waziri Mkuu ajaye, kiongozi wa zamani, Tun Dr Mahathir, alijibu kwa vijembe, "Labda awe Waziri Mkuu wa Israel".

Madai ya ngono

Katika Baraza Kuu la UMNO, kitabu, "Sababu 50 Kwanini Anwar Hawezi Kuwa Waziri Mkuu" kilisambazwa chenye picha pamoja na shutuma za rushwa dhidi ya Anwar. Kitabu kimeandikwa na Khalid Jafri, mhariri wa zamani wa gazeti la serikali, ‘Utusan Malaysia’ na aliyekuwa mhariri mkuu wa gazeti wa jarida lililoshindwa la Harian National. Anwar aliomba amri ya mahakama kuzuia usambazaji zaidi ya kitabu na kufungua kesi dhidi ya mwandishi kwa kashfa. Polisi walimshtakiwa mwandishi wa kitabu kwa kuchapisha habari za uongo. Miongoni mwa madai katika kitabu ni kwamba Anwar ni shoga. Polisi waliamuriwa kuchunguza ukweli wa madai hayo. Katika kile gazeti la Sydney Morning Herald liliita "ukweli wa kisiasa uliopangwa", Anwar alishtakiwa kwa kulawiti, alikutwa na hatia na kuhukumiwa miaka 15 jela.

Mwaka 1999, Anwar alifungua kesi dhidi ya Waziri Mkuu Mahathir ya kashfa, kwa madai ya kutamka shutuma za vitendo kinyume na maadili na kumwita Anwar shoga katika mkutano wa waandishi habari nchini Malaysia. Hukumu hii iligeuzwa mwaka 2004, na Anwar akatoka gerezani. Mwandishi wa kitabu alikufa mwaka 2005 kwa ugonjwa wa kisukari, lakini si kabla ya Mahakama Kuu kumkuta na hatia ya kashfa na kutakiwa kulipa fidia ya mamilioni. Mahakama Kuu, Machi 8, 2010 ilitoa uamuzi kuwa kutimuliwa kwa Anwar mwaka 1998 kutoka Baraza la Mawaziri kulikofanywa na Mahathir kulikuwa halali kikatiba.

Tarehe 29 Juni 2008, iliripotiwa kuwa msaidizi wa Anwar Ibrahim alitoa ripoti polisi ya madai kuwa alilawitiwa na Anwar. Anwar alisema kuwa uwezekano wa hukumu ya kifungo jela kutokana na madai inaweza kuwa jaribio la kumuondoa kwenye nafasi ya kiongozi wa upinzani kufuatia kuongezeka kwa wafuasi wake na ushindi katika uchaguzi. Pia alisaini kuwa hana hatia na alitoa ushahidi katika mfumo wa taarifa za matibabu.

Kesi hii imefutwa tarehe 9 Januari 2012, karibu miaka miwili baada ya kesi kuanza, baada ya Jaji Mohamad Zabidin Mohd Diah, kumuona Anwar hana hatia ya kulawiti. Jaji aligundua kuwa ushahidi wa DNA uliowasilishwa na upande wa mashtaka haukuwa sahihi, na kumwachia huru Anwar.

Madai ya mkanda wa ngono uliofichwa

Machi 21, 2011 video ya ngono ilionekana ambayo ilidaiwa kumshirikisha Anwar Ibrahim. Siku moja baadaye, Anwar Ibrahim alifungua malalamiko polisi. Polisi kwa sasa wanafanya uchunguzi dhidi ya watu watatu ambao waliionesha video hiyo. Watu hao ni waziri kiongozi wa zamani wa Malacca, Tan Sri Abdul Rahim Thamby Chik, mfanyabiashara Datuk Shazryl Eskay Abdullah na mweka hazina wa zamani wa Perkasa, Datuk Shuaib Lazim.

Makala haya yameandaliwa na Bishop Hiluka kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari.


Jan 4, 2012

Mambo haya yanachangia mimba zisizotarajiwa

*Yachunguze kwa binti yako, chukua hatua


 Mtoto mwenye mtoto



BISHOP HILUKA

Dar es Salaam



KUNA siku chapisho moja la makala lilinivutia sana kuhusu vijana kujiingiza katika tabia za hatari. Makala ile ilieleza mambo yanayoweza kuwachelewesha au kuwakwaza vijana kutofikia malengo yao ya maisha kama: Dawa za kulevya, Ulevi, VVU/Ukimwi, Mimba kabla ya wakati n.k.



Katika makala hiyo, zilielezwa sababu zinazowafanya vijana (wasichana) kupata mimba kabla ya wakati, mwandishi alipendekeza namna ya kuwasaidia ili wasijikute katika mtego huu na pia waweze kufikia malengo yao katika maisha yao. Ingawa sababu hizi ziliwalenga wasichana moja kwa moja, hata hivyo, zinaweza kutumika kwa wavulana pia, kwa vile wavulana wanajiingiza katika mambo haya kirahisi kuliko wasichana.



Bibi Tricia M. Davis alifanya utafiti kati ya wasichana wapatao 500 wenye umri wa miaka chini ya 19, waliowahi kupata mimba zaidi ya mara moja. Katika utafiti wake ameeleza sababu saba zilizojitokeza na kuchangia katika hawa kupata mimba zaidi ya mara moja. Katika makala yake, “An Examination of Repeat Pregnancies Using Problem Behaviour Theory”, iliyochapishwa katika Jarida la Journal of Youth Studies (Vol. 5, no.3, 2002, pp.337-351), amefafanua kwa kina juu ya tatizo hili. Mimi nitajaribu kugusia tu kwa kadri ninavyoweza.



Imeelezwa kuwa sababu ya kwanza ni kutokuwa na malengo maalum katika maisha. Vijana wenye malengo endelevu katika maisha huwa wanachelewesha tendo la ndoa na hivyo kutopata mimba kabla ya wakati. Kijana anapokuwa amejiwekea malengo makubwa katika maisha yake, hakika atakuwa makini zaidi na daima atajiepusha na tabia zinazoweza kumfanya kutofikia malengo yake. Kwa mfano, ikiwa kijana fulani aliye katika kidato cha kwanza (Form I) na ana lengo la kuwa rubani wa ndege au kiongozi mashuhuri katika nchi au mtu yeyote maarufu, ni wazi atajishugulisha zaidi na mambo ya masomo.



Kutojithamini ambapo kijana kujiona hafai kwa chochote katika familia anamotoka au katika jamii ya watu inayomzunguka. Hisia hii inamfanya kujichukia na kupata msukumo wa kutaka kutafuta thamani ya nafsi yake kirahisi. Njia mojawapo ya kufanya hivi ni kujaribu mambo ya mapenzi. Kwa msichana wa hali hii ni rahisi kufikiri thamani yake inatokana na tendo hili la ngono kwani linaambatana na lugha nzuri wanazotumia wavulana na ahadi au zawadi anazoweza kupewa. Wasichana wanaotoka katika familia zisizo na upendo wa kweli kati ya wazazi ni rahisi kudanganyika na kutafuta thamani zao nje ya familia.



Kutowajibika humsababisha kijana kupata mimba kirahisi. Kutowajibika kuna maana ya mtu anavyoeleza matukio mbalimbali ya maisha yake na jinsi gani anavyojiepusha na tukio lile. Tabia hizi zaweza kuonekana hata katika mambo madogo madogo. Kwa mfano, kijana akidondosha kitu fulani na kusema, “Kitu hiki kimedondoka”, yeye anajaribu kutafsiri tukio lile kuwa hakuhusika nalo kabisa. Au mwingine anapovunja glasi na kusema, “Glasi imevunjika” anajaribu kutowajibika na tukio hilo. Sote tunatambua jinsi Adamu alivyotaka kujiepusha na kutokuwajibika kwa kosa alilofanya katika bustani ya Edeni. Mungu alipomuuliza, “Umefanya nini?” Adamu alimjibu Mungu, “Mwanamke uliyenipa ndiye alinidanganya nami nikala…” Adamu hakutaka kuwajibika na tendo lake. Hali kadhalika kijana mwenye mazoea ya kutowajibika katika mambo madogo madogo, ni rahisi kwake kujiingiza katika ngono na hatimaye kupata mimba bila kujali au kuwajibika. Wasichana wenye tabia ya kusema, “Shetani alinidanganya” au “Tulikuwa tunajaribu,” wanaonyesha dalili za kutowajibika na tendo walilofanya.



Ukosefu wa uchaji Mungu ambayo ni ile hali ya kijana kutojali mambo ya kiimani. Vijana wanaokuwa na hali hii ya kutojali mambo ya kidini na imani kwa ujumla wanajiweka katika mazingira rahisi zaidi ya kujiingiza katika tabia za hatari. Hii ni kwa sababu wanakuwa wamezamisha dhamiri zao zisiwasumbue wanapokuwa wamekosea. Kwa upande mwingine, vijana wanaojihusisha na vikundi mbalimbali vya kukuza imani, wanapata malezi mazuri juu ya dhamiri zao na hivyo hata kama wakikosa ni rahisi kwao kurudi katika msingi mzuri wa maadili.



Mazingira duni nyumbani pia huwafanya vijana kujiingiza katika tabia za hatari. Kama msichana anaishi na mzazi mmoja, kuna uwezekano wa binti kupata mimba mapema kutokana na kuathiriwa na mfano wa muundo wa familia anayoishi. Pia kwa wale wanaotoka katika familia ambazo mume na mke si waaminifu, kuna uwezekano mkubwa wa kijana kushawishika na kuanza mambo ya mapenzi mapema.



Mshinikizo wa rika unaweza kuwalazimisha vijana lakini si kwa sehemu kubwa! Vijana wanaweza kushawishika kufanya ngono au kujiingiza katika tabia za hatari kutokana na hadithi zinazosimuliwa na wenzao. Kila mmoja hujidai kuwa alijaribu mambo haya na kuelezea jinsi alivyojisikia. Hali hii inaweza kuchochea hamu ya kutaka kujaribu mambo ya hatari. Kama kijana tayari ana malengo na anajithamini si rahisi sana kupeperushwa na upepo huu wa masimulizi haya. Lakini kama kijana hana malengo maalum katika maisha na hajui thamani yake, basi ni wazi mshinikizo wa rika una nafasi kubwa ya kumpotosha.



Vijana wenye tabia ya kupenda kujaribu ili kujua ladha yake hata bila kujali madhara yake wanaweza kuingia katika mtego kirahisi. Kwa kufikiri kuwa wanaweza kujaribu tendo lolote la hatari mara moja tu na kuacha, kumbe kunaweza kuwa mtego wa kudumu.

YOUSSOU N'DOUR: Msanii na mwanaharakati anayeutaka urais wa Senegal

Youssou N'dour

DAKAR
Senegal

MWANAMUZIKI mashuhuri nchini Senegal na mwanaharakati wa kisiasa, Youssou N'dour, ametangaza kuwa atawania kiti cha urais katika uchaguzi wa mwezi Februari nchini humo.

Mwanamuziki huyo amesema kuwa anaitikia wito wa kumtaka agombee kiti hicho dhidi ya rais wa sasa Abdoulaye Wade, ambaye anapania kuwania kiti hicho kwa muhula wa tatu.

Youssou N'dour amekuwa akijihusisha na masuala ya kibinadamu kwa siku nyingi na pia ni balozi wa shirika la umoja wa mataifa kuhusu masuala ya watoto (UNICEF).

Mwandishi wa BBC mjini Dakar, Thomas Fessy, amesema kuwa hatua ya Youssou N'dour kutangaza kuwa atawania kiti cha urais, haijawashangaza wengi. Hii ni kufuatia tangazo alilotoa mwisho wa mwaka uliopita kuwa atajitosa katika ulingo wa kisiasa.

Katika hotuba iliyorushwa kupitia kituo chake cha redio na televisheni, mwanamuziki huyo ambaye pia ni mfanyabiashata mwenye mafanikio amesema atapunguza matumizi ya serikali na kuahidi kuzalisha chakula na umeme kwa wote iwapo atachaguliwa kuwa rais wa Senegal.

Youssou N'dour anakubali kuwa yeye sio msomi lakini anaelezea wadhifa wa urais kuwa ni ''kazi na sio taaluma''.

Youssou N'dour alikuwa rafiki wa karibu wa Rais Abdoulaye Wade, lakini baada ya Wade kutangaza nia ya kuwania kiti cha urais kwa muhula wa tatu, aligeuka na kuwa mpinzani wake mkuu.

Na amekuwa akisema kwamba Wade anatakiwa kutogombea mhula mwingine wa tatu kwa sababu anavunja katiba.

Lakini haitakuwa kazi rahisi kwa Youssou Ndour kuwabadili maelfu ya wafuasi wake wa muziki kumpigia kura. Aidha, Youssou N'dour amewahi kuwashutumu viongozi wa nchi za Afrika kuhusu jinsi walivyoshughulikia janga la njaa nchini Somalia.

Historia yake

Youssou N'Dour (tamka Yusuu nduu) alizaliwa Oktoba 1, 1959, ni mwanamuziki wa Senegal na mwigizaji. Mwaka 2004, Rolling Stone alimuelezea kuwa, katika Senegal na sehemu kubwa ya Afrika, "ndiye mwimbaji maarufu kati ya walio hai." Amesaidia sana kuutangaza na kuuendeleza mtindo wa muziki maarufu nchini Senegal, unaojulikana kwa lugha ya Serer kama mbalax, aina ya muziki  ambao huelezea mbinu na mitindo yake mingi kutoka mapokeo ya kihafidhina ya muziki wa Serer wa "Njuup".

Amesaidia sana kuleta mafanikio makubwa na tuzo kwa filamu ya “Return to Goree” aliyoshiriki kuiongoza kwa kushirikiana na Pierre-Yves Borgeaud, na “I Bring What I Love” ilivyoongozwa na Elizabeth Chai Vasarhelyi, zilizotolewa na kuoneshwa katika majumba ya sinema duniani kote.

Maisha na kazi

Youssou N'Dour alizaliwa mjini Dakar kwa baba ambaye ni wa kabila la Serer. Alianza kuimba katika umri wa miaka 12. Ndani ya miaka michache alikuwa akiimba mara kwa mara na Star Band, kundi maarufu zaidi mjini Dakar katika miaka ya 1970. wanamuziki kadhaa wa Star Band walijiunga na Orchestre Baobab katika wakati huo.

Ingawa Youssou N'Dour ana uhusiano wa tamaduni za griot kwa upande wa mama yake, lakini hakulelewa katika utamaduni huo, ila alijifunza kutoka kwa ndugu zake. Wazazi wake walimtia moyo wa kutazama mambo kwa njia za kisasa zaidi, wakiacha kuzizoea tamaduni zote mbili, matokeo yake alijichukulia mwenyewe kama mtu wa kisasa katika jamii ya griot.

Mwaka 1979, alianzisha kundi lake mwenyewe, Etoile de Dakar. Kazi yake ya mwanzo na Etoile de Dakar ilikuwa katika mtindo wa kawaida wa Kilatini maarufu kote Afrika wakati huo, lakini katika miaka ya 1980 alianzisha sauti ya kipekee wakati alipoanzisha kundi lake sasa, Super Etoile de Dakar akishirikiana na Jimi Mbaye kwenye gitaa, mpiga besi Habib Faye, na Tama (mpiga ngoma) na mchezaji Assane Thiam.

Youssou N'Dour ni mmoja kati ya wanamuziki maarufu sana wa Afrika katika historia. Mwimbaji mashuhuri, mwandishi wa nyimbo, na mtunzi, mchanganyiko wa tamaduni. Ana mvuto usioegemea upande wowote kuanzia Samba ya Cuba hadi hip hop, jazz na soul zimempatia mamilioni ya mashabiki kimataifa. Katika nchi za Magharibi, Youssou ameshirikiana na wanamuziki kama Peter Gabriel, Red Axelle, Sting, Alan Stivell, Bran Van 3000, Neneh Cherry, Wyclef Jean, Paul Simon, Bruce Springsteen, Tracy Chapman, Branford Marsalis, Ryuichi Sakamoto, Dido na wengineo. Nchini Senegal, Youssou ni nyota mwenye nguvu ya utamaduni anayeshiriki kikamilifu katika masuala ya kijamii.

Amejaaliwa kuwa na vipaji mbalimbali vya ajabu, mtunzi wa nyimbo, kiongozi wa bendi, na mtayarishaji na mwenye uwezo mkubwa katika muziki. Gazeti la New York Times liliielezea sauti yake kama "Sauti nyembamba yenye kukamata, silaha nyumbufu iliyotumika kwenye mapambano na yenye mamlaka ya kinabii". Youssou N'Dour anauteka wigo wa muziki wote wa Senegal katika kazi yake.

Mwezi Julai 1993, mchezo wa kuigiza wa Kiafrika uliotungwa na Youssou N'Dour ulioneshwa katika tamasha jijini Paris nchini Ufaransa. Aliandika na kutumbuiza wimbo rasmi wa Kombe la Dunia 1998 akiwa na Axelle Red "La Cour des Grands". Youssou N'Dour aliteuliwa Balozi wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) tarehe 16 Oktoba 2000.

Rasilimali kubwa ya Youssou N'Dour ni kwamba ana ufahamu mkubwa sana katika utamaduni wake. Hata kama aliamua kutafiti mahali pengine, mizizi yake ni imara. Baadhi wamekwenda mbali wakimuelezea kama Msanii wa Afrika wa Karne (jarida la Folk Roots). Ameshafanya ziara za kimataifa kwa miaka thelathini. Alishinda tuzo yake ya kwanza ya American Grammy Award (best contemporary world music album) kwa CD yake ya Egypt mwaka 2005.

Mwaka 1991 alifungua studio yake ya kurekodia, Xippi, na mwaka 1995 lebo yake mwenyewe, Jololi. Pia ni mmiliki wa L'Observateur, moja ya magazeti makubwa nchini Senegal, na kituo cha redio RFM (Radio Future Medias).

Youssou N'Doura amekuwa akijihusisha na masuala kadhaa ya kijamii na kisiasa. Mwaka 1985, aliandaa tamasha kwa ajili ya kutolewa kwa Nelson Mandela. Alishirikiswa kuimba katika matamasha ya Haki za Binadamu yalilojulikana kama Amnesty International Human Rights Now mwaka 1988, duniani kote. Ziara iliyomshirikiana Lou Reed kuchangia toleo la wimbo wa Peter Gabriel uliotolewa na Richard James Burgess na kushirikishwa kwenye albamu ya Amnesty International.

Pia amewahi kufanya kazi Umoja wa Mataifa na UNICEF na alianzisha Mradi wa Joko kwa kufungua migahawa ya intaneti katika Afrika na kuunganisha jamii ya Senegal duniani kote. Amewahi kutumbuiza katika tamasha maarufu la Live 8 (katika tamasha la Live 8, London, tamasha la Live 8, Paris na katika tamasha la Live 8, Mradi wa Edeni katika Cornwall) tarehe 2 Julai 2005, akiwa na Dido.

Mwaka 2006, Youssou N'Dour alicheza katika filamu ya kustaajabisha ya Wafrika-Waingereza (African-British abolitionist Olaudah Equiano), iliyoelezea juhudi za William Wilberforce kumaliza utumwa katika Dola ya Uingereza.

Alishiriki katika "Jealous Guy" ya John Lennon kwa CD ya 2007 Karma Instant: Kampeni ya Amnesty International Kuiokoa Darfur. Pia alishiriki katika kampeni ya pamoja ya Hispania na Senegal dhidi ya wahamiaji haramu. Youssou N'Dour alishiriki katika Soko la Hisa la mradi wa Visions mwaka 2007. Tangu mwaka 2007 amekuwa mwanachama wa baraza la World Future Council.

Mwaka 2008, Youssou N'Dour alitoa kama zawadi moja ya nyimbo zake: bebe, kwa mwimbaji wa Kifaransa, Cynthia Brown.

Mwaka 2009, aliachia wimbo wake "Wake Up (It's Africa Calling)" chini ya leseni ya Creative Commons ili kusaidia afya kimataifa katika kampeni ya IntraHealth Open ili kuleta chanzo cha maombi ya wazi ya afya kwa Afrika. Wimbo uliorudiwa ukichanganya wasanii mbalimbali ikiwa ni pamoja na Nas, Peter Buck wa R.E.M., na Duncan Sheik kusaidia kutafuta fedha kwa ajili ya kampeni.

Mwaka 2011, N'Dour ilitunukiwa shahada ya udaktari wa heshima katika Muziki kutoka Chuo Kikuu cha Yale.

Makala haya yameandaliwa na Bishop Hiluka kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari vya kimataifa.