Aug 10, 2011

Miaka 50 ya uhuru uchumi unakua, huku umasikini ukizidi kuongezeka!

Baba wa Taifa, mwalimu Julius Nyerere

Abeid Aman Karume, Rais wa Kwanza wa Zanzibar

BISHOP J. HILUKA
Dar es Salaam

WIKI iliyopita niliandika makala yenye kichwa cha habari “Miaka 50 ya uhuru, kiwango cha elimu mmh”, iliyoibua hisia tofauti kwa wasomaji, baadhi wakikubaliana nami na wengine wakionesha kunishangaa eti kwa kutoyaona mazuri ya nchi hii.

Walionishangaa walinilaumu kwa kuandika mambo ambayo kwa mtazamo wao ni ya kupotosha huku wakiniuliza endapo ningechaguliwa kuwa rais au waziri ningefanya nini? Msomaji mmoja alinipigia simu kuonesha jinsi alivyokerwa na jinsi nilivyowasilisha suala la kukosekana kwa uzalendo kwa viongozi wetu.

Naomba niweke bayana kwamba kila mtu ana mitazamo yake katika mambo mbalimbali, nilichoandika ulikuwa mtazamo wangu binafsi na wala sitaandika anavyofikiri mwingine au kwa utashi wa mtu mwingine. Lakini nitazidi kusisitiza kuwa hapa tulipofika ni kwa sababu ya kukosekana uzalendo.

Nchi hii imeingiwa na ugonjwa mbaya sana wa mmong'onyoko wa misingi ya utawala bora, umoja na mshikamano wa kitaifa; maadili na utu wema, jambo linalowatumbukiza walio wengi katika umaskini.

Huko nyuma tulizoea kuambiwa kuwa ‘cheo ni dhamana’ na kwamba ‘uongozi ni utumishi’, lakini siku hizi kupata cheo ni kuula! Neno 'kuula' limeanza kama lugha ya mtaani ambayo ina tafsiri pana kidogo. Moja ya tafsiri ni 'mambo kuwa mazuri (kunyooka)'.

Bahati mbaya tumefika mahala tumejisahau kabisa, wala hatukumbuki tena kwamba cheo ni dhamana. Kwa miaka ya hivi karibuni wazo la cheo ni dhamana limepotelea mbali na kusahauliwa kama lilivyosahauliwa Azimio la Arusha. Tunawezaje kupata viongozi wazuri kama kila mmoja anafikiri nafasi aliyonayo ni haki yake, ni mali yake, na ni stahili yake?

Zama hizi mtu anaruhusiwa kuwa na kampuni na akajipa tenda ya kutoa huduma ofisini kwake, anaruhusiwa kutembea dunia nzima kwenye makongamano na warsha kwa kutumia hela za wananchi, ukiwa na cheo kikubwa utawapa ajira watoto na dugu zako wote ofisi waipendayo.

Zama hizi mtumishi wa umma anajengewa nyumba ya kuishi ya thamani ya mabilioni ya shilingi na akikaribia kustaafu anakopeshwa kwa vimilioni vichache, pia ni zama ambazo kufikishwa mahakamani kwa ubadhirifu inategemea umekwapua kiasi gani, kama ni kikubwa, dola yenyewe inatamka kuwa hukamatiki!

Ni zama ambazo ukiwa mtumishi wa umma mwenye cheo kikubwa unaweza kusomesha mwanao nchi yoyote uitakayo bila mawazo ya karo, si hivyo tu kutibiwa nje si kwa magonjwa ya moyo tu bali hata mafua, muhimu cheo kizuri cha kuhudumia umma.

Wakati tukijiandaa kwa maadhimisho ya miaka hamsini tangu kupata uhuru wa kisiasa, inasikitisha kuona kwamba, sehemu kubwa ya utajiri na rasilimali ya Tanzania iliyopaswa kuwa ni kwa ajili ya mafao ya wengi, inaendelea kuwanufaisha watu wachache ndani ya jamii, kinyume kabisa na mipango na mikakati iliyowekwa na waasisi wa Taifa hili, wakati wa kupigania uhuru; misingi ya uadilifu, uzalendo na umoja wa kitaifa inazidi kumong'onyoka siku hadi siku, hali ambayo inasababisha kustawi kwa ubinafsi, ufisadi na kinzani za kijamii.

Kumong'onyoka kwa misingi ya utawala bora; umoja na mshikamano wa kitaifa, maadili na utu wema; uzalendo, utu na heshima ya kila Mtanzania na wala si mali anayomiliki, kumesababisha Watanzania wachache kuendelea kufaidika na rasilimali ya nchi, wakati kundi kubwa la watu likiendelea kuogelea katika dimbwi la umaskini, ujinga na maradhi.

Yote haya yamesababishwa na kukosekana kwa uzalendo, jambo linalofanya kundi dogo la watu kufaidi utajiri wa rasilimali na madini wa nchi hii, wakati kuna mamilioni ya watu wanakufa kwa njaa, magonjwa na umaskini katika nchi yenye utajiri wa maliasili na madini ambazo, kimsingi zinapaswa kuwa ni kwa ajili ya mafao ya wengi.

Tanzania kadiri ya vigezo vya Mashirika ya Fedha ya Kimataifa ni kati ya nchi masikini zaidi duniani, lakini imekuwa na mvuto mkubwa kwa wawekezaji kutoka sehemu mbalimbali za dunia, wanaokimbilia nchini kutafuta madini.

Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Tanzania imefanikiwa kuuza dhahabu yenye thamani ya zaidi ya dola bilioni mbili nukta tano, lakini, cha kushangaza imeambulia dola millioni mbili nukta saba, hali inayoonesha kimsingi, ukosefu wa haki na usawa katika soko la kimataifa. Matajiri wanaendelea kufaidika na mikataba ya madini, wakati kuna mamillioni ya watu wanaokufa kwa baa la njaa, umaskini na magonjwa, katika maeneo haya yenye rasilimali na utajiri mkubwa kiasi hiki.

Kukosekana kwa uzalendo kumesababisha hata ndani ya nyumba za ibada; kwa maana ya Makanisa na Misikiti, harufu ya ufisadi inasikika hali ambayo inadunisha mchakato mzima wa kutafuta haki na usawa katika soko la kimataifa, kwa ajili ya mafao ya wengi.

Baadhi ya watu wanaendekeza rushwa na ufisadi; maadui wakuu wa haki na usawa kama alivyobainisha Mwalimu Nyerere wakati fulani. Masuala haya yameleta mpasuko wa kijamii ambao kwa sasa ni hatari kubwa kwa ustawi na maendeleo ya Watanzania.

Mikataba ya madini, imeendelea kuwanufaisha wawekezaji kutoka nje ya nchi na wananchi wa Tanzania kuendelea kuogelea katika umasikini wa kipato, licha ya kuzungukwa na utajiri wa rasilimali. Uchumi wa Tanzania utaendelea kudidimia, ikiwa kama hatutarudisha uzalendo wa kuipenda nchi yetu.

Rushwa na ufisadi vinaendelea kuota mizizi katika mioyo ya watu, jambo ambalo itakuwa vigumu kulifuta kwa kipindi kifupi, kama ilivyo dhana ya udini, iliyoibuliwa na baadhi ya wanasiasa kwa mafao yao binafsi.


No comments:

Post a Comment