Aug 3, 2011

Miaka 50 ya uhuru wetu, kiwango cha elimu mmh!

 Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, 
Dk. Shukuru Kawambwa

 Minara pacha ya Benki Kuu (BOT)

Ndege ya Rais aina ya Gulfstream 550

BISHOP J. HILUKA
Dar es Salaam

KUMBE wewe ndiyo Bishop? Ninasoma sana makala zako... una upeo mkubwa mwanangu, siyo huyu rafiki yako hana akili! Kakosa hata nafasi ya ualimu?” ananiambia mama Beka, mkazi wa Kinondoni, mara baada ya kutambulishwa kwake na mwanaye ambaye ni rafiki yangu.

Kauli yake imenifanya kuandika makala nyingine kuhusu elimu. Nimewahi kuandika makala kadhaa kuhusu mfumo wetu wa elimu na sikuwa na sababu ya kuendelea kuandika kuhusu elimu. Ikizingatiwa kuwa hivi karibuni ilitolewa ripoti ya utafiti kuhusu elimu na Shirika la Utafiti la Uwezo, ambapo Tanzania tunazidiwa na jirani zetu, Kenya na Uganda.

Naamini wengi wameisoma ripoti hiyo, binafsi sikupata nafasi ya kuisoma na sielewi wametoa sababu zipi za kudorora elimu yetu, lakini kwa kauli kama ya mama Beka, naamini sababu zipo wazi kabisa.

Kwanza nakubaliana na wanaosema kuna tofauti kubwa sana ya wasomi wa sasa na wa zamani, hasa waliosoma enzi za utawala wa kikoloni na miaka michache baada ya uhuru. Katika kipindi hicho, japo elimu ilikuwa bidhaa adimu kwa wananchi wazawa, waliobahatika kusoma walisomesheka na kuwa watu muhimu sio tu katika ulingo wa ajira lakini hata katika jamii zao.

Kwa kweli huwezi kumlinganisha mhitimu wa darasa la saba wa leo na yule wa wakati huo kwa kuwa mfumo wa elimu uliopo sasa umechakachuliwa sana. Tumefika mahala mtu aliyekosa kuchaguliwa kwenye chaguzi zingine ndio anayejiunga na ualimu! Ndio maana hata mama Beka anamshangaa mwanaye kukosa hata nafasi ya ualimu?

Imesemwa kuwa athari ya mwalimu aliyefeli inajidhihirisha hata kwa wale anaowafundisha, kwa kuwa hawatokuwa na upeo mkubwa, matarajio yao yatakuwa madogo, na nchi itazidi kuwa masikini kwani itakuwa na idadi kubwa ya watu wasiojiweza na wenye uwezo mdogo wa kujikwamua kimaisha. Mwalimu aliyefeli hawezi kujiamini anapofundisha na aghlabu hawezi kukidhi mahitaji ya wanafunzi hasa wale wenye uwezo mkubwa wa kuhoji mambo ambao mara nyingi huitwa wasumbufu na walimu wasiojimudu.

Kwa muda mrefu, vyuo vya ualimu nchini vimekuwa vikidahili wanafunzi wenye alama za chini kusomea ualimu ikiwa ni mojawapo ya mikakati ya serikali kukabiliana na uhaba wa walimu shuleni. Na hivi karibuni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, alikiri bungeni kuwa ili kupunguza tatizo la uhaba wa walimu, vyuo hivyo vimekuwa vikiwapokea hata wanafunzi waliopata daraja la nne!

Mi' nadhani, utaratibu wa kudahili wanafunzi wasio na sifa stahiki kwa kisingizio cha kukabiliana na uhaba wa walimu shuleni una athari zaidi kuliko manufaa. Kwanini taaluma ya ualimu iendelee kuwa kapu la kuwapokea watu wasio na uwezo? Walimu wa aina hii tunaowaamini kufundisha wanetu, ni kweli wanawajengea ufahamu wanafunzi kuhusu rasilimali zao?

Takwimu zilizomo katika kitabu cha Takwimu za Msingi za Elimu Tanzania (BEST) kilichotolewa mwaka 2007 zinaonesha kuwa hadi mwaka huo, Tanzania ilikuwa na walimu 2663 tu waliothibitishwa kati ya walimu 18,463 waliokuwa wakifundisha!

Hivi kweli wanafunzi wanaohitimu katika ngazi mbalimbali za elimu wanafahamu kuwa wamekwenda shule ili wazifahamu rasilimali zao na matumizi yake? Mi' nadhani tatizo liko kwa viongozi wa sasa kukosa uzalendo na kupenda kujilimbikizia mali! Kwani hadi miaka ya tisini kiwango cha elimu kilikuwa bora japo nafasi zilikuwa chache!

Viongozi wabinafsi hushindwa hata kupanga vipaumbele kwa maslahi ya taifa. Sidhani kama ununuzi wa ndege ya rais na rada lilikuwa jambo muhimu zaidi kuliko kujenga vituo vya afya, madarasa ya kutosha, maabara na kadhalika. Siamini kama ujenzi na baadaye ukarabati wa ukumbi mpya wa Bunge ulikuwa muhimu kuliko kuweka madawati kwenye shule zote za msingi nchi nzima! Au ujenzi wa minara pacha ya BOT ulikuwa muhimu kuliko kuboresha mazingira ya kazi kwa walimu na askari wanaoishi kwenye nyumba ambazo hazijakarabatiwa tangu alipoziacha mkoloni!

Kufifia kwa utaifa, uzalendo na uwajibikaji ndiyo chanzo kikuu cha mambo kwenda ovyoovyo katika nchi hii japo tunajisifu kufikia miaka hamsini ya uhuru huku tukiwa tumefanikiwa kuanzisha sekondari katika kila kata, shule ambazo hazina walimu wala maabara na hakuna kiongozi yeyote ambaye anasomesha watoto wake huko!

Enzi zile tulikuwa tunasoma na watoto wa viongozi wa juu serikalini, wakiwemo watoto wa marais! Siku hizi hakuna kitu kama hicho! Viongozi wote wanasomesha watoto wao katika shule bora za binafsi, zenye walimu wazuri. Unategema kutakuwa na walimu bora kwenye shule za walalahoi?

Sawa tumefanikiwa kuongeza shule za sekondari zinazoingiza wanafunzi wengi kidato cha kwanza, lakini vipi kuhusu ubora wa elimu? Mi' nadhani kujisifu kwa kujenga sekondari nyingi zinazopokea wanafunzi wengi bila kujali ubora wa elimu wanayoipata ni kufilisika kimawazo.

Kama ulikuwa na wanafunzi 10 wakashinda 2, hapa hakuna sifa ya ubora. Na mwaka unaofuatia ukawa na wanafuzi 30 wakashinda 5 bado hakuna Ubora. Wanaohesabu ushindi wa watoto toka wawili kwenda watano kuwa ni ongezeko basi tumefilisika kwa sababu kuna watoto ishirini na tano wameshindwa kwenda mbele!

Unapokuwa 'bachela' utapika chakula kwa kiwango cha kukutosha wewe na upimaji wa shibe lazima uwe kwa mtu mmoja, lakini huwezi kuhesabu mafanikio kwa kupika chakula kingi wakati hali halisi inasema umepika chakula hicho kwa sababu ya ongezeko la wageni. Jambo la msingi ni kupima malengo ya ongezeko lenyewe kama watu wote wamekula na kushiba.

0755 666964
bjhiluka@yahoo.com

No comments:

Post a Comment