Jul 1, 2011

Kudhani muungano hauna matatizo ni kujidaganya


Mchanga wa nchi hizo mbili ukichanganywa 
kuonesha muungano, mwaka 1964
 
 Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na 
Hayati Abeid Amani Karume wakisaini hati 
za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar
mwaka 1964

BISHOP J. HILUKA
Dar es Salaam

MUUNGANO wa nchi mbili za Tanganyika na Zanzibar uliozaa taifa jipya la Tanzania hadi sasa umeshapitia misukosuko na dhoruba za kila aina, lakini bado unaendelea kuwepo hata kama kuna hali ya mashaka, huku nchi nyingi za Kiafrika, Kiarabu na hata Asia zilizokuwa zimeungana kama sisi miaka ya nyuma zikishindwa kuuendeleza.

Hali ya mashaka ninayoizungumzia hapa inatokana na kile kinachodaiwa kuwa kuundwa kwa Muungano wetu kulikuwa siri na tangazo la kutiwa saini mkataba wa Muungano kati ya Rais wa Tanganyika, Mwalimu Julius K. Nyerere, na Rais wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume, liliwashangaza watu kutoka pande zote za muungano; Bara na Visiwani.

Habari zinazidi kupasha kuwa hali hii ilitokana na habari za Muungano kuwa za siri na watu wa pande zote mbili za Muungano hawakushauriwa utadhani hawakuwa na haki yoyote ya mustakabali wa nchi yao.

Ndiyo maana nasema kuendelea kudhani kuwa kuujadili Muungano ni uhaini au kuendelea kuyafumbia macho masuala ya Muungano tutakuwa tunajidanganya, kwani kuficha au kudharau maradhi ni ugonjwa hatari, na ipo siku mauti itatuumbua.

Hoja za wabunge wa Zanzibar kuanzisha tena mjadila wa muundo wa Muungano zimeendelea kulitikisa Bunge baada ya wiki hii wabunge kutoka Zanzibar kuonekana kuushambulia muungano huu huku mbunge mwingine kuibuka na kutaka uvunjwe na kuundwa upya ili kumaliza malalamiko yasiyokwisha kuhusu kuwapo kwake.

Mbunge aliyetoa hoja ya kutaka muungano huo kuangaliwa upya na ikibidi kuvunjwa ni Haji Khatib Kai (Micheweni-CUF), aliyekuwa akichangia katika mjadala wa Hotuba ya Makadirio na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mbunge mwingine wa Mgogoni, Kombo Khamisi Kombo (CUF), alisema suala hilo limewafikisha Wazanzibari pabaya hali ambayo inawafanya kuiona serikali hiyo ya Muungano kuwa inayowadhalilisha. Alisema wapo wanajeshi, polisi na wafanyakazi wengine Zanzibar ambao wanapata huduma zote muhimu visiwani humo, ingawa hawalipi kodi kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) na badala yake kodi zao zimekuwa zikichukuliwa na Serikali ya Muungano.

Mbunge huyo alisema masuala ya namna hiyo yamekuwa yakisababisha watu wa visiwani kuuangalia muungano katika jicho la kuutilia shaka.

Akitoa mfano, mbunge huyo alisema, Zanzibar ina jumla ya mabalozi wanne tu nje ya nchi ambao wote wanaiwakilisha nchi hii katika mataifa ya Kiarabu isipokuwa Omar Ramadhani Mapuri ambaye ni balozi nchini China.

Wazanzibari mbalimbali wameendelea kulalamika kuwa Katiba ya Tanganyika imelindwa na ilipaswa kuwepo na Serikali yake, pamoja na viongozi wake kuwepo na kusimamia mambo yasiyo ya Muungano. Katiba na sheria za Tanganyika ndizo zilizotakiwa zitumike katika eneo la Tanganyika kwa yale mambo yaliyokuwa hayamo kwenye Muungano kama ambavyo Katiba na sheria za Zanzibar zinavyotumika katika eneo la Zanzibar kwa yale mambo ambayo si ya Muungano.

Imekuwa ikisemwa kwamba Serikali ya Tanganyika imefutwa kwa makusudi na Bunge la Tanganyika kinyume na Makubaliano ya Muungano ili kujipa nafasi kuitumia Serikali ya Muungano, kama kwamba ndio Serikali ya Tanganyika. Lengo ni hatimaye kuiua Serikali ya Zanzibar na kufanya Tanganyika mpya ikiwa na jina jipya la Tanzania lenye mipaka mipya, yaani kuwa nchi moja yenye Serikali Moja.

Kimtazamo hapa, malalamiko ya Wazanzibari kunadai uwepo wa serikali ya Tanganyika yana mantiki kwa kuwa pamoja na hatua ya kuifuta Katiba ya Tanganyika, lakini kule kuendelea kutambua kuwepo kwa sheria zisizo za muungano ni kutambua kuwepo kwa mamlaka ya Tanganyika ambako sheria hizo kwa mambo yote yasiyo ya Muungano ziliendelea na zinaendelea kutumika hadi leo.

Manung'uniko ya Wazanzibari yameenda mbali zaidi wanapodai kuwa miongoni mwa mambo yaliyodhihirisha kuwa hakukuwa na nia njema katika Muungano huu tokea awali ni pale wafanyakazi wa Serikali ya Tanganyika wote walipopandishwa vyeo kwa pamoja na kuwa wafanyakazi wa Muungano kama kifungu cha 3 (1) cha Provisional Transitional Decree.

Vivyo hivyo, kifungu cha 6 (i) cha Decree kinasema mara tu baada kuanza Muungano, Mahakama ya Tanganyika na Majaji wake wote nao watakuwa ndio Mahakama na Majaji wa Jamhuri ya Muungano kinyume na Makubaliano ya Muungano. Mpaka leo Katiba zote mbili hazitambuwi Mahakama kama ni suala la Muungano. Nembo ya Tanganyika inatumika kama nembo ya Serikali ya Muungano na Idara ya Mwanasheria Mkuu wa Tanganyika inachukuliwa kama Idara ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Muungano.

Ukiuangalia Muungano wetu kijuujuu utaona kuwa ni mfano mzuri sana wa maelewano kwa watu wa Bara la Afrika, lakini chini kwa chini kunafuka moshi ambao ukiachwa hivi hivi bila kutafutiwa ufumbuzi utakuja kujitokeza moto mkubwa ambao tunaweza kushindwa kuuzima.

Kwa kuwa tupo katika kipindi cha kuelekea kwenye mchakato wa kupata Katiba mpya, nadhani ni wakati mwafaka kila Mtanzania aweke maslahi ya taifa mbele bila ushabiki, viongozi nao wawe mstari wa mbele kuonesha njia na siyo kuwa na sauti ya mwisho juu ya Muungano. 

Kwa Watanzania wengi kutoka pande zote zinazohusika na Muungano, inaonekana wazi hawapingi kuungana, kwani muungano kwao ni baraka. Ila hiki kinachoitwa Kero za Muungano. 

Mojawapo ya mambo yaliyoibuliwa wiki hii na wabunge ni kuhusu Rais wa Zanzibar aliyetakiwa moja kwa moja awe Makamu wa Rais wa serikali ya Muungano kama Rais atatoka Bara, na pale Rais atakapotoka upande wa pili, yaani Zanzibar mwenzake wa Bara awe Makamu wa Rais.

No comments:

Post a Comment