Jul 1, 2011

ABDOULLAYE WADE: Mgawo wa umeme watia doa mpango wake wa kung’ngania madarakani

Rais wa Senegal, Abdoulaye Wade


DAKAR
Senegal

RAIS wa Senegal, Abdoulaye Wade, amesalimu amri kuhusu pendekezo la kutaka kufanya mabadiliko ya sheria za uchaguzi, na kuuondoa kabisa muswada ambao ulizua vurugu kubwa baina ya polisi na waandamanaji katika mji mkuu Dakar hivi karibuni.

Mahasimu wa Wade walisema kwamba pendekezo hilo lingeruhusu kuchaguliwa kwake tena dhidi ya upinzani usio na nguvu katika uchaguzi ujao utakaofanyika mwezi Februari mwakani na pia lilitishia kuzuka kwa maandamano ya mapinduzi katika nchi hiyo ambayo kwa muda mrefu ni imara katika Afrika Magharibi.

Wakosoaji wamesema marekebisho hayo ya katiba yalilenga kuhakikisha Rais Wade, ambaye ana umri wa miaka 85, anachaguliwa tena mwakani. Wade aliingia madarakani katika uchaguzi wa kidemokrasia, lakini sasa anakabiliwa na ongezeko la hasira kutoka kwa wananchi kutokana na matatizo ya umeme ya kila siku na kupanda kwa gharama za maisha.

Wanaharakati, vyama vya upinzani, waangalizi wa haki za binadamu na wananchi kwa ujumla waliandamana kupinga hatua ya Rais Wade kutaka kubadili katiba ya nchi hiyo na kumuwezesha makamu wa rais kuwa mgombea mwenza katika uchaguzi mkuu ujao.

Mbali na kutaka kubadili kipengele hicho cha katiba, Rais Wade pia alitaka kubadili mfumo wa ushindi wa kura za urais kutoka ushindi wa asilimia 50 hadi asilimia 25 ambazo ndizo zitawezesha mshindi kutangazwa, hatua inayopingwa na wanaharakati wakisema kingemhakikishia ushindi wa mkondo wa kwanza dhidi ya upinzani wake hata kama ni dhaifu.

Rais Wade aliwasilisha mapendekezo yake ya kutaka kubadilishwa kwa katiba ya nchi hiyo kwenye kikao cha bunge kinachoendelea ikiwa imebaki miezi nane tu kupisha uchaguzi mkuu wa nchi hiyo.

Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa hatua hiyo ya Rais Wade kutaka kubadili katiba ya nchi hiyo ina lengo la kumuwezesha kiongozi huyo kuwania urais kwa kipindi kingine cha tatu huku akimpa nafasi ya uwaziri mtoto wake wa kwanza wa kiume ili kuja kurithi nafasi hiyo.

Wachambuzi hao wameongeza kuwa haiwezekani rais kupatikana kwa ushindi wa asilimia 25 pekee badala yake ni muhimu kwa rais kupata ushindi wa asilimia 50, hali hiyo inaelezwa ni mkakati wa rais Wade kutaka kuepusha uchaguzi mkuu kurudiwa kwa mara ya pili.

Lakini vipengele vingine vilisalia, na licha ya kukubali huko, waandamanaji na wanachama wa vikosi vya usalama, wakitumia mabomu ya kutoa machozi, waliendelea kukabiliana katika maeneo yaliyo karibu na afisi za rais na bunge.

Kipengele kilichosalia chenye utata zaidi ni kile cha kuunda wadhifa wa makamu wa rais. Mahasimu wake wanasema jukumu hilo linapendekezwa ili amkabidhi mamlaka mwanawe wa kiume Karim, ambaye tayari ni waziri mashuhuri anayesimamia robo ya bajeti ya kitaifa, lakini serikali ilisema nafasi hiyo sio lazima.

Hadi kufikia usiku wa Alhamisi wiki iliyopita ghasia zilikuwa zimepungua lakini katikati mwa mji taswira ilikuwa ni mawe na mabaki ya magari yaliyochomwa moto. Askari polisi wapatao 12 walikuwa miongoni mwa zaidi ya watu 100 waliojeruhiwa wakati wa mapambano hayo.

Watu wawili wamethibitishwa kufa na wengine zaidi ya mia moja wamejeruhiwa kufuatia maandamano hayo ya kupinga hatua ya Rais Abdoulaye Wade kubadili katiba ya nchi hiyo. Polisi nchini humo wamesema kuwa mpaka sasa wamefanikiwa kupata idadi ya watu 120 ambao wamejeruhiwa katika maandamano hayo na kuongeza kuwa watu wawili waliuawa kwa kupigwa risasi.

Polisi mjini Dakar walilazimika kutumia mabomu ya machozi na risasi za mpira kutawanya maelfu ya wananchi waliokusanyika nje ya ukumbi wa bunge la nchi hiyo wakiwa na mabango yanayoshutumu utawala wa Rais Wade.

Haya yanakuwa ni maandamano ya kwanza makubwa kuwahi kufanyika nchini humo katika kipindi cha miaka kumi tangu Rais Abdoulay Wade achukue madaraka mwaka 2000.

Wachambuzi wanasema hali hiyo pia ilionesha jinsi upinzani pamoja na makundi ya kiraia yanavyoweza kupanga shughuli za kumpinga Wade wakati ambapo kuna hofu za kijamii nchini humo. Waziri wa sheria, Cheikh Tidiane Sy, aliliambia bunge la nchi hiyo kuwa rais Wade alipokea jumbe kutoka mbali hasa kutoka viongozi wa kidini, na hapo ndipo akamtaka aondoe sheria hiyo.

Ibrahima Sene, afisa wa ngazi ya juu wa muungano wa upinzani wa Benno Siggil nchini Senegal, aliwasifu waandamanaji kwa kujitolea kwao lakini akasema walifanya kazi nusu tu. Amesema bado kuna kazi ya kumwondoa Wade madarakani, na huo ndio mwito wanaotoa. 
 
Senegal imetambulika kwa muda mrefu kama taifa lililo imara zaidi na lenye demokrasia Afrika Magharibi na limeshuhudia chaguzi kadhaa zenye amani kwa miaka 50 iliyopita tangu ilipopata uhuru wake kutoka Ufaransa. Lakini kuna ongezeko la wasiwasi kuhusu kupewa madaraka mengi washirika wa karibu wa Rais Wade, pamoja na raia kukata tamaa kutokana na kuzorota kwa huduma za umma na kupanda kwa bei za bidhaa muhimu.

Pia Senegal imeshuhudia maandamano mengine katika mji mkuu, Dakar na katika jiji la Kusini la Mbour, yakihusishwa na ukosefu wa umeme, ambapo jijini Dakar, majengo kadhaa ya serikali yalichomwa moto, zikiwemo ofisi za shirika la umeme la serikali - Senelec.

Majeshi ya usalama katika mji wa Mbour yalipiga mabomu ya machozi kutawanya maelfu ya waandamanaji. Tatizo la ukatikaji wa umeme, ambao umedumu kwa saa 48 katika maeneo kadhaa, limekuja wiki moja tu baada ya kutokea maandamano dhidi ya rais. Chupa zilizovunjwa, mabaki ya majengo na matairi yaliyochomwa moto vimetapakaa mitaani.

Mjini Mbour, karibu kilomita 80 kusini mashariki mwa Dakar, ofisi za shirika la umeme pia zilishambuliwa. Watu walioshuhudia walisema ofisi za Senelec zilivunjwa na magari yaliyoegeshwa nje kushambuliwa pia. Senelec imeshindwa kutoa huduma ya umeme ya kuridhisha kwa miaka mingi.

Hata hivvyo Rais Wade ameahidi kuondoka madarakani iwapo wananchi wataendelea kumpinga, lakini amesisitiza kuwa yeye si mzee sana wa kushindwa kugombea katika uchaguzi wa mwaka ujao ili kuiongoza nchi hiyo kwa mara ya tatu. Amesema kuwa, tofauti kati ya nchi hiyo na Tunisia au Misri ni kuwa, yeye binafsi anataka wananchi waandamane.

Historia yake
Abdoulaye Wade amezaliwa 29 Mei 1926, ingawa baadhi wanadai alizaliwa miaka kadhaa hapo nyuma. Ni rais wa tatu wa Senegal, aliyeingia madarakani mwaka 2000. Pia ni Katibu Mkuu wa Chama cha Kidemokrasia cha Senegal (PDS) alichokiongoza tangu kilipoanzishwa mwaka 1974. Amekuwa kiongozi wa muda mrefu wa upinzani, akiwa amewania urais mara nne, kuanzia 1978 , kabla ya kuchaguliwa mwaka 2000.

Maisha kabla ya siasa
Wade alizaliwa katika eneo la Kebemer nchini humo. Alisoma na kufundisha sheria katika Shule ya Lycee Condorcet nchini Ufaransa. Ana shahada mbili za udaktari katika sheria na uchumi. Alikuwa pia Mkuu wa Kitivo cha sheria na uchumi katika Chuo Kikuu cha Dakar nchini Senegal. Amemuoa Viviane Wade ambaye ni mzungu.
Mtoto wao wa kiume, Karim Wade, ni mkuu wa zamani wa wakala wa shirika la taifa la Kiislam na alifanya kazi tangu Mei 2009 kama Waziri wa Ushirikiano wa Kimataifa, Mipango Miji na Mikoa, Usafiri wa Anga, na Miundombinu. Binti yao, Sindjely Wade, ni Msaidizi Maalum wa Rais ambaye alishiriki katika mikutano ya kampeni mingi ikifanyika Paris na Dakar.

Kazi ya siasa
Katika mkutano wa kilele wa Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika (OAU) mjini Mogadishu, mwaka 1974, Wade alimwambia Rais Leopold Senghor Sedar kwamba alitaka kuanzisha chama kipya, na Senghor ilikubali. PDS ilianzishwa tarehe 31 Julai 1974. Chama ambacho awali kilikuwa na lengo la Uliberali mwaka 1976 kutokana na kuanzishwa kwa sheria ya kuruhusu kuwepo kwa vyama vitatu tu na itikadi tofauti tatu, mbili zilichukuliwa na vyama vingine (uliberali ndo' chaguo pekee lililobakia).

Wade aliwania urais mwezi Februari 1978 dhidi ya Senghor, na kupata asilimia 17.38 ya kura. Pia mwaka huo, Wade alichaguliwa kuwa mbunge, alioutumikia hadi 1980. Aliwania pia urais katika uchaguzi wa 1983 na 1988 na kuchukua nafasi ya pili kila wakati, nyuma ya mrithi wa Senghor wakati huo, Abdou Diouf. Kufuatia uchaguzi wa 1988, alikamatwa kutokana na maandamano dhidi ya matokeo na alisimamishwa asigombee. Baada ya hapo alikwenda Ufaransa na kurudi mwaka 1990.

Mwezi Aprili 1991, Wade na wanachama wengine wanne wa PDS walijiunga na serikali ya umoja wa kitaifa pamoja na chama tawala cha Kisoshalisti (PS); Wade akawa Waziri wa Nchi asiye na wazara maalum. Oktoba 1992, yeye na mawaziri wengine wa PDS walijiondoa serikalini kutokana na malalamiko kuhusu namna ambayo PS ilikuwa ikiidhibiti serikali. Katika uchaguzi wa rais wa Februari 1993, Wade alikuwa wa pili tena, akiwa na asilimia 32 ya kura, nyuma Diouf, aliyeshinda kwa asilimia 58. 
 
Kufuatia mauaji ya Makamu wa Rais wa Baraza la Katiba Mei 1993, Babacar Seye, Wade, pamoja na viongozi wengine wa PDS, walihojiwa na polisi. Oktoba 1, Wade, mke wake, na wabunge wawili wa PDS (Abdoulaye Faye na Ousmane Ngom), walishtakiwa kwa makosa ya mauaji, ingawa hawakuwa chini ya ulinzi au kufunguliwa kesi. Kufuatia maandamano mwezi Februari 1994, Wade alikamatwa pamoja na wengine wengi kwa tuhuma za kutishia usalama wa serikali.

Makala haya yameandaliwa na Bishop J. Hiluka kwa msaada wa mashirika mbalimbali ya habari ya kimataifa.

No comments:

Post a Comment