Jul 27, 2011

Hili la samaki wa sumu, wahusika wawajibike

 Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na 
Ustawi wa Jamii, Blandina Nyoni


 Samaki aina ya Mackerel

BISHOP J. HILUKA
Dar es Salaam

HII taarifa kuhusu samaki wenye sumu imetushtua na kutuogofya watu wengi. Kwanza niliposikia kwa mara ya kwanza nilidhani ni mzaha, lakini baada ya kusikia tangazo la tahadhari likitolewa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, kuwataka wananchi washiriki msako kuhusu kusambazwa kwa zaidi ya kilo 1,000 za samaki wenye sumu sehemu mbalimbali za nchi, nilijikuta nikichanganyikiwa.

Ndiyo nilichanganyikiwa! Nilichanganyikiwa kwa kuwa familia yangu wanapenda sana kula samaki, si hivyo tu bali hata hii taarifa ya wizara iliyotolewa Jumatatu wiki hii jijini Dar es Salaam, imeeleza kuwa samaki hao ni sehemu tu ya tani takriban 125 (kilo 124,992) zilizoingizwa nchini kutoka Japan, na kwamba Serikali imeanza msako mkali kuwatafuta samaki hao, lakini ikaonesha wasiwasi kwamba juhudi hizo huenda zisizae matunda kwa kuwa sehemu ya shehena hiyo imeshaingia sokoni!

Mpaka hapa tayari kila atakayesoma makala yangu ataelewa kwa nini nilichanganyikiwa. Hapa ninajaribu kuyaangalia majaaliwa ya Watanzania waliokwishakula na watakaokula samaki hawa. Uchunguzi wa awali unaonesha kuwa samaki hao tayari wameingizwa katika masoko ya Dar es Salaam na Morogoro.

Taarifa hiyo ilisema kuwa athari za sumu inayohofiwa kuwapo kwenye samaki hao ni ya mionzi ya nyuklia ambayo kimsingi hujitokeza taratibu katika mwili wa binadamu.

Taarifa hiyo iliendelea kueleza kuwa samaki hao aina ya 'Mackerel' waliingizwa nchini na kampuni ya
Alphakrust Ltd ya Dar es Salaam kutoka kampuni ya Kaneyama Corporation ya Chiba, Japan. Samaki hao walisafirishwa kupitia Bandari ya Yokohama, Japan na kuingia nchini kupitia Bandari ya Dar es Salaam, na inaonesha waliingizwa baada ya kukidhi masharti ya kisheria na taratibu zilizowekwa!

Hapa kuna maswali ya kujiuliza; masharti ya kisheria na taratibu zipi zilizozingatiwa katika kuingiza samaki hao? Hivi hadi lini nchi yetu itaendelea kufanywa dampo la bidhaa mbovu? Eti samaki hao waliruhusiwa kuingizwa nchini kwa kibali cha TFDA namba TFDA11/F/IPER/0896, cha Julai 11 2011. Je, ni kweli hakuna viashiria vya rushwa katika sakata hili?

Inaeleweka wazi kuwa samaki na mboga zitokazo Japan zimechafuliwa na mionzi ya nyuklia, na inasikitisha sana kuona watu wanaagiza vyakula 'vya baharini' kutoka Japan kwa wakati huu, huku Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) ikiruhusu ziingizwe nchini. Inamaana tumeshindwa hata kutumia busara tu ya binadamu wa kawaida?

Hapa sielewi, hili ombi la Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kuwaomba wananchi kutoa ushirikiano kwa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Idara za Afya za Mikoa ya Dar es Salaam na Morogoro na Jeshi la Polisi, ili samaki waliobaki wapatikane ni nini kama si kiini macho? Ushirikiano upi inautaka mamlaka iliyosababisha uzembe na wala hatuoni wahusika kuwajibika? Kwa nini wahusika wasiwajibike kwanza?

Taarifa ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Blandina Nyoni, ilisema kuwa hadi kufikia Jumapili asubuhi, kiasi cha samaki wenye uzito wa tani 123.673, kati ya tani 124.992 walioingizwa nchini, walipatikana na kuzuiliwa katika maghala ya kampuni ya Alphakrust Ltd. Nyoni alisema wizara yake iliiagiza TFDA kuchukua hatua za haraka za kuzuia usambazaji wa samaki hao hadi uchunguzi utakapokamilika.

Hivi kama Japan yenyewe imepiga marufuku samaki hao kusambazwa kwenye maeneo mengine ya nchi yao, iweje sisi bila hata wasiwasi tunaingiza bidhaa kutoka mji huo? Kama balaa hilo la mionzi lingetokea nchini mwetu hata pini tusingeweza kuuza nje, hivi tunawaogopa hawa wakubwa mpaka kiasi cha kuweka rehani maisha yetu kiasi hiki? Haya yamefanywa kwa maslahi ya nani ili kuwaua Watanzania?

Kama wahusika hawatawajibika na serikali haitachukua hatua katika kuwawajibisha waliohusika na sakata hili sisi wananchi hatutaielewa kabisa serikali yetu! Itabidi tuelezwe serikali ipo kwa maslahi ya raia wa nchi ipi kama si raia wake; Watanzania?

Kwa mujibu wa nyaraka za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), mzigo huo ulifika Bandari ya Dar es Salaam tarehe 18 Julai, 2011. Wizara ilipata taarifa siku ya Jumamosi kwamba samaki hao wanahisiwa kuchafuliwa na mionzi ya nyuklia iliyotokea huko Japan, mwezi Machi, 2011.

Hakuna asiyejua kuwa mionzi ya nyuklia ina athari kubwa sana kwa afya ya jamii. Dalili za awali zinafanana na za mtu anayefanyiwa tiba ya mionzi kwa kansa: kichefuchefu na uchovu, kisha kutapika. Baada ya hapo mtu hupoteza nywele na kuharisha.

Lakini kama mfiduo (exposure) ni mkubwa, hatua ya pili kwa ujumla ni uharibifu wa utando wa matumbo, kuhara sana kunakosababisha upungufu wa maji mwilini, baadaye uharibifu kwenye mfumo wa neva kunakosababisha kupoteza fahamu, na hatimaye kifo.

Je, tuliowaamini kutuongoza haya ndiyo malipo yao kwetu? Kwa nini wahusika wasiwajibike kwa (uzembe?) walioufanya kama si kitu kidogo kimetumika kuruhusu samaki hawa waingizwe nchini?

Mungu ibariki Tanzania...

No comments:

Post a Comment