Jul 20, 2011

Miaka 50 ya uhuru na nadharia ya Mkukuta ya kupunguza umasikini

 Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo (kulia), 
akichati na Katibu Mkuu wake, Ramadhan Khijah (katikati) 
pamoja na Naibu Katibu Ofisi ya Rais Tume ya Mipango, 
Clifford Tandari mara baada ya uzinduzi wa mchakato 
wa majadiliano ya Mpango wa Kukuza Uchumi na Kuondoa 
Umaskini Tanzania (Mkukuta).
 
 
 Rais Jakaya Kikwete
 
BISHOP J. HILUKA
Dar es Salaam

MKUKUTA ni neno lililojipatia umaarufu mkubwa katika jamii ya Tanzania toka mpango huo ulipozinduliwa mwaka 2005. Ni neno maarufu ingawa Watanzania wengi hata hawajui ni kitu gani au kirefu chake, na limekuzwa zaidi na wanasiasa, hasa wa chama tawala, CCM.

Hata hivyo kirefu cha Mkukuta ambacho ni Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini Tanzania, bado kinatuwia vigumu wengi wetu kuelewa mkakati huo unatekelezwa namna gani. Mkakati wa kwanza wa kupunguza umasikini ulizinduliwa mnamo Oktoba 2000 na kutekelezwa kuanzia 2005 hadi 2010. Hivi sasa tuna Mkukuta Awamu ya Pili.
Mojawapo ya eneo ambalo Mkukuta ulipaswa kujikita ni kwenye ukuaji wa uchumi na kupunguza umasikini wa kipato kwa wanawake na wanaume wa maeneo ya vijijini wanaoishi chini ya mstari wa umasikini wapungue toka asilimia 38.6 hadi asilimia 14.

Kupungua kwa umasikini kutatokana tu na wakazi wa maeneo ya vijijini ambao wengi wao ni wakulima wadogo endapo watajengewa uwezo wa kuongeza tija na kupata faida ndani na nje ya sekta ya kilimo. Kuwezesha kutafuta masoko ya uhakika ya bidhaa za kilimo. Kuwajengea uwezo wa kuongeza thamani mazao wazalishayo ili waweze kupata faida.

Tukiwa tunaelekea miaka 50 tangu tujipatie uhuru toka kwa Waingereza, huku tukiwa kwenye awamu ya pili ya mpango huu wa Mkukuta baada ya awamu yake ya kwanza kufika mwisho wake mwaka jana 2010, umasikini wa Watanzania bado uko pale pale na umeendelea kukita mizizi hasa maeneo ya vijijini, ingawa serikali inajigamba kuwa uchumi wa nchi unakua.

Umasikini wa kipato vijijini unachangiwa na wakulima kuendesha kilimo cha kujikimu kwa kutegemea mvua, uzalishaji duni, nguvukazi haba na vitendea kazi duni ingawaje huduma za kilimo cha umwagiliaji zinaonesha kuanza kukua lakini wananchi wengi hawatumii kutokana na ubunifu mdogo.

Mitaji na fursa finyu ya kupata mikopo ni changamoto kwa wakazi wengi wa vijijini. Hata maeneo ya mijini ambayo tatizo lilionekana sio kubwa sana ukilinganisha na maeneo ya vijijini hali ni mbaya vilevile.

Nakubali kuwa yapo maeneo ambayo wananchi wake hawahitaji fedha kwa ajili ya mitaji ya kuongeza kipato lakini wanakabiliwa na umasikini wa kipato kutokana na sheria ambazo kama zingerekebishwa zingeweza kuwajengea mazingira mazuri ya kuinua hali za maisha yao.

Nadhani kila kitu kipo wazi kuwa malengo ya serikali ya kupunguza umaskini hadi kufikia mwaka huu ambapo nchi yetu itaadhimisha miaka hamsini ya uhuru, kupitia mpango huu wa Mkukuta yameonesha kushindwa kabisa na maisha ya Watanzania yanazidi kuwa magumu.

Ingawa takwimu zinaonesha kuwa uchumi umekuwa ukikua kwa wastani wa asilimia saba miaka ya karibuni (nadhani kwa kanuni ya 'Head in the oven and legs in the freeze, the average is comfortable'), lakini hakuna unafuu wowote kwa wananchi wa kawaida.

Hata Malengo ya Mpango wa Milenia (MDGs) kupunguza umaskini kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2015 hayatafikiwa kwa kuwa uchumi wetu bado umeendelea kuwa tegemezi kwa kiwango kikubwa, na sasa tuna hili balaa kubwa lisiloonesha dalili zozote za kumalizika pamoja na serikali kujigamba kupata tiba yake; janga la umeme ambalo mimi hupenda kuliita 'mgawo wa giza'.

Ni aibu kubwa kwa nchi hii inayojisifu kufikia miaka 50 ya uhuru huku ikiwa bado inashindwa kujitegemea kwenye bajeti yake, ikikumbwa na janga la mgawo wa giza na matatizo lukuki. Bajeti yetu kila mara imekuwa haina jipya kwa kuwa haijabainisha njia za kutengeneza utajiri mpya kama vile kuongeza viwanda vya uzalishaji mali na kuwekeza nguvu kubwa kwenye kilimo ili kiwe na tija.

Vipaumbele vya serikali kila mara vinaonekana ni vya bajeti dhaifu na ya kivivu ambayo hata mimi nisiye mchumi naweza kuiandika hata nikikurupushwa usingizini.

Sioni kabisa kipaumbele cha uhakika katika sekta ya elimu ambayo ndiyo inaweza kuwa njia kuu ya kukuza uchumi na serikali yetu imeishia kujenga shule za kata, ambazo ukijaribu kuzikosoa utaiona hasira ya watawala watakaokuona kama msaliti wa maendeleo.

Shule hizi nyingi hazina walimu na zimeishia kuwa vijiwe vya wasichana kupata mimba kwa kuwa wanafika shuleni na kukaa bila kufundishwa.

Pia kwa hili la wabunge bila kujali itikadi zao kuikataa bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini ni uthibitisho tosha kuwa miaka hamsini baada ya uhuru, bila nishati ya uhakika Mkukuta ni sawa na porojo kwa kuwa hakuna kinachoweza kufanyika. Ukosefu wa nishati ya uhakika ni kiashirio kwamba Watanzania wasitarajie faraja yoyote.

Tanzania ingefanikiwa katika mpango huu endapo kama ingeharakisha kutekeleza mpango wa kuanzisha vitambulisho vya taifa, baada ya sheria hiyo kupitishwa na Bunge mwaka 1986.

Vitambulisho hivyo vingesaidia katika mfumo wa utambuzi wa wananchi wake na kurahisisha kazi ya kuwajua walipa kodi wote na hivyo mzigo huo kubebwa na wachache kiasi kwamba lazima nchi kama hiyo itembeze bakuli katika kutekeleza bajeti yake.

Mungu ibariki Tanzania

No comments:

Post a Comment