Jul 6, 2011

Takwimu za unywaji maziwa na madhara ya uchakachuaji

 Baadhi ya wanafunzi wa shule mbalimbali za msingi 
za Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam 
wakiandamana kwenye barabara ya Kawawa 
kuadhimisha kilele cha wiki ya uhamasishaji 
unywaji wa maziwa.
 
BISHOP J. HILUKA
Dar es Salaam

WIKI hii nimesoma habari kuhusu taarifa ya Bodi ya Maziwa nchini (TDB), kwamba wastani wa Watanzania kunywa maziwa unaongezeka na imewaomba kujenga utamaduni wa kunywa maziwa kwa wingi ili kujenga afya zao.

Akizungumza kwenye maonesho ya kimataifa ya Sabasaba katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam, Meneja Masoko wa bodi hiyo, Dk. Mayasa Simba, alisema bodi hiyo imeendelea kuhamasisha unywaji wa maziwa na hadi sasa wastani wa mtu mmoja kunywa maziwa umefikia lita 43 kwa mwaka ingawa Shirika la Afya duniani (WHO) linapendekeza wastani wa lita 200 kila mwaka kwa kila mtu.

Alisema kuwa bodi hiyo imeendelea na mikakati ya kuhamasisha unywaji wa maziwa kuanzia shuleni, kwenye maonesho kama Sabasaba na Wiki ya Maziwa ambapo bidhaa mbalimbali zitokanazo na maziwa zimekuwa zikioneshwa.

Na kaulimbiu ya bodi hiyo ni “Maziwa ya Tanzania kwa afya na utajiri”, hivyo itaendelea kuwaeleza Watanzania kuwa kuna bidhaa nyingi zitokanazo na maziwa tofauti na mtazamo wa baadhi ya watu.

Taarifa hiyo iliendelea kusema kuwa kwenye maziwa kunapatikana bidhaa nyingi kama vile jibini, yoghurt, siagi na samli na maziwa yanaweza kutumika kupikia wali na vyakula mbalimbali na kujenga afya za Watanzania.

Na mwisho habari hizo zilibainisha kuwa Bodi ya Maziwa kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo na wadau mbalimbali wanaandaa andiko kwa ajili ya mpango wa unywaji wa maziwa shuleni, hali ambayo itajenga utamaduni wa watoto kupenda kunywa maziwa.

Hivi karibuni niliandika makala kuhusu unywaji wa maziwa na jinsi Watanzania wanavyokatishwa tamaa na mambo fulanifulani. Imekuwa ikisemwa kuwa Watanzania hatuna utamaduni wa kunywa maziwa, huku wenzetu wa Kenya ndio wanaosemwa kuongoza kwa kunywa maziwa wakifuatiwa na Uganda na Rwanda ingawaje sisi tumejaaliwa kuwa na mifugo wengi ambao wangetosheleza mahitaji yetu ya vyakula hivyo.

Napenda nisisitize tena kuwa mimi ni mmoja wa watu wanaopenda sana wanywe maziwa, lakini kutokunywa maziwa hakumaanishi kwambwa hatupendi bali kinachotukatisha tamaa ni kwamba maziwa mengi yanayouzwa si maziwa halisi, kwa kuwa wafugaji tayari huwa wamekwishayachakachua kwa kuongeza maji ili yawe mengi.

Na haiishii hapo tu kwani yakishafika kwa wafanyabiashara nao hupenda kuchukua maziwa hayo kiasi kidogo na kuchanganya na maziwa ya unga au wakati mwingine hata unga wa ngano, kisha wanatia mafuta kidogo ili kupata utando wa mafuta juu yake.

Maziwa ya moto yanayouzwa kwenye vibanda vingi jijini Dar es Salaam, pindi ukiyatia mdomoni huwezi kuisikia ile radha ya maziwa, na pia huwa yana utando wa mafuta ambao si wa kawaida hasa kwa mtu anayeyafahamu vizuri maziwa halisi.

Lengo la wafanyabiashara kuamua kuchakachua maziwa ni ili wapate faida kubwa bila kujua kwamba wanajiharibia soko na wakati huohuo kuhatarisha afya za watumiaji kwani hata hayo maji wanayotumia kuchakachua sidhani kama ni maji salama.

Sababu nyingine inayosababisha Watanzania kuonekana kuwa hawapendi kunywa maziwa ni kutokana na kuendelea kwa umasikini na hali ngumu ya kiuchumi katika ngazi za kifamilia na kitaifa, hali hii imefanya afya za wananchi ziendelee kuwa hatarini kutokana na ugumu wa maisha na hivyo kufanya hata baadhi ya vyakula muhimu ikiwemo maziwa kuwa anasa kwa Mtanzania wa kawaida.

Kauli mbalimbali zinazotolewa na baadhi ya viongozi na watafiti kwamba eti Watanzania wafundishwe (waelimishwe) kuhusu umuhimu wa kula nyama, mayai na kunywa maziwa, kwangu mimi nahisi kama hiki ni kichekesho cha mwaka!

Ni kichekesho kwa kuwa sidhani kama kuna Mtanzania asiyejua umuhimu wa vyakula hivyo kwa mwili wa binadamu au asiyependa kula na kunywa vizuri!

Wanapodai kuwa tuelimishwe, wanatuelimisha katika lipi wakati tuna kliniki zimejaa nchini takriban kila kijiji, ni nani ambaye hajawahi kufundishwa au ambaye mama yake hajafundishwa umuhimu wa vyakula hivyo?

Inaposemwa kuwa Watanzania hawanywi maziwa, hawali nyama na mayai sio kwa sababu hawana elimu ya umuhimu wa lishe hiyo bali hawana imani na maziwa yanayouzwa na wafanyabiashara wetu na pia hali ya kiuchumi haiwaruhusu kufanya hivyo!

Maziwa pekee yanayoonekana kuaminika miongoni mwa jamii zetu au kuwa halisi ni yale yanayosindikwa viwandani ambayo hata hivyo kwa hali halisi ya kiuchumi ya Watanzania wengi ni sawa na anasa kuyanunua.

Nawashauri wahusika hawa wangeangalia njia nzuri ya kujirekebisha kwa kunyoosheana kidole kwa kujiharibia soko kwa kuchakachua maziwa. Lakini pia ni jukumu la Serikali kupitia Bodi ya Maziwa na Wizara ya Mifugo kuchukua hatua na kuangalia jinsi ya kudhibiti uchakachuaji huu ili kulinda afya za Watanzania na kwa kufanya hivyo, biashara hiyo itakuwa kubwa na hata Serikali itapata mapato kupitia kodi.

Alamsiki.

No comments:

Post a Comment